Hadithi ya kusisimua: Mirathi ya Kaka

Hadithi ya kusisimua: Mirathi ya Kaka

MIRATHI YA KAKA sehemu ya 34
ILIPOISHIA TOLEO LILLOPITA...
“Tuendelee!” niliropoka mara baada ya kugutuka kutoka kwenye kuwaza kwa kina.
“Huo ulikuwa ni utangulizi tu, hivyo kama unataka kuwa mmoja kati ya matajiri wa dunia hii yakubali nitakayokuambia.” Aliongea Sharifa kisha akanyosha mkono wake kuichukua brificase iliyokuwa mezani.

SASA ENDELEA..........

Aliifungua brificase na kuniambia niangalie. Naam! Ilikuwa imesheheni fedha za kigeni, fedha ambazo zilikuwa zimebanwa katika maburungutu. Nilijikuta nikimeza mate baada ya kuviona vitita hivyo.

“Kama utakubaliana na ninachoenda kusema basi matumizi yako kwa siku yatakuwa ya pesa kama hizi.” Mwanadada huyo alizidi kunitamanisha japokuwa nilikuwa sijajua atakachokitaka kutoka kwangu.

Nilishusha pumzi huku nikiongeza umakini wa kumsikiliza. Nilizidi kuwa katika wakati mgumu kwa kujua kwamba kama nitamuendekeza sana msichana huyo basi pepo ya Mwenyezi Mungu nitakuwa nimeipa kisogo.

Hata hivyo nilijiambia ngoja kwanza nimsikilize, uamuzi si ulikuwa ni wangu bwana, kama ningetaka kukubali basi ningekubali na kama ningetaka kukataa basi ningekataa.

“Najua mwanzo ulikuwa ukinichukia sana, hasa hasa pale niliposimama mbele ya mahakama kutoa ushahidi juu ya kesi yako. Lakini sasa hivi hunichukii tena, hasa baada ya kukuokoa kutoka kwenye kunyongwa, uongo?”
“Ni kweli.”
“Mateso yote uliyokuwa ukiyapata tangu kifo cha marehemu kaka yako ulikuwa ukitumikia adhabu.”
Maneno hayo yalinishtua na kunifanya nigutuke.
“Adhabu! Adhabu kwa kosa lipi? Na kosa hilo nilikuwa nimemkosea nani?” Niliuliza.
“Kosa hukutenda wewe bali ni kaka yako James.”
“Alitenda kosa gani kaka yangu?”
“Usiwe na pupa, nipo hapa kukufunulia kila kitu hivyo nitakueleza siri nzito aliyokuwa nayo kaka yako.”
Hilo nalo lilikuwa neno; kujua kile kilichokuwa kimejificha nyuma ya pazia wakati wa uhai wa kaka James, nilizidi kuongeza umakini. Kikao chetu kilizidi kutia fora, sasa nikawa na shauku ya mambo matatu. Jambo la kwanza ni shauku ya kujua siri nzito iliyokuwepo kwa kaka James.

Jambo la pili lilikuwa ni shauku ya kujua masharti ambayo nilikuwa nimeambiwa nitapewa wakati natoroshwa gerezani. Jambi la tatu ni shauku ya kutaka kujua madhara yatakayonipata endapo ningeshindwa kutekeleza masharti hayo.

Sharifa alianza kunieleza habari ya kaka James. Habari ambayo iliyaamsha machungu ya moyo wangu, nikahisi maumivu makali yakipenya barabara kunako mtima wa moyo wangu.

Kaka James alipokuwa anamalizia masomo yake ya kidato cha nne aliambiwa na rafiki yake mmoja kuwa kuna mganga wa kikongo aliyekuwa kaingia nchini. Mganga huyo alikuwa akiwatengenezea watu dawa ya kupata utajiri.
Kutokana na tamaa za kutaka kupata utajiri, kaka James alimtaka rafiki yake huyo ampeleke kwa mganga huyo ili akatengenezewe dawa ya kuwa tajiri. Ndipo alipopelekwa.

Alipofika kwa mganga huyo aliambiwa kuwa masharti ya kupata utajiri ni lazima uingie maagano na majini. Maagano hayo yalikuwa ni maagano ya kafara za damu huku yakiwa katika madaraja matatu.

Daraja la kwanza lilikuwa ni kuwatoa kafara wazazi wako wote pamoja na ndugu yako mmoja wa damu. Ndugu aliyetakiwa katika daraja hili ni mdogo wako, kaka yako ama dada yako. Kama wote hao huna basi mjomba ama shangazi hutakiwa.

Baada ya hapo utajiri unaanza kwa kasi ya kawaida. Ukishakaa miaka mitano unatakiwa kutoa tena kafara ya mtoto wako wa kwanza pamoja na mama yake kama wewe ni mwanaume. Lakini kama ni mwanamke basi unatakiwa kumtoa mtoto wako wa kwanza pamoja na baba yake.

Ukishakamilisha kafara za daraja la kwanza na la pili unatakiwa sasa kuhamia kwenye daraja la tatu ambalo kafara yake huendelea mwaka hadi mwaka. Kafara katika daraja hili ni ya mtu yeyote ama awe mfanyakazi wako au anayetumia vitu vyako mfano abiria katika magari yako, mpangaji katika nyumba yako na kadhalika.

Masharti hayo ndiyo aliyopewa James naye akakubaliana nayo. Siku chake baada ya kuingia kwenye maagano yale ya kishetani wazazi wetu walikufa wote kwa mkupuo katika ajali ya kutisha.

Habari hii ndiyo iliyonitonesha majeraha yaliyokuwa yamejengeka ndani ya moyo wangu mithili ya donda ndugu. Kuanzia hapo nilianza kumchukia James na kumuona ni shetani mkubwa ambaye alikuwa anastahili kutupwa kwenye moto wa jehanamu.

Nilijikuta nahukumu wakati maandiko ya Mungu yanatuambia tusikuhumu ili na sisi tusije tukahukumiwa. Niliumia sana nilipoambiwa hiyo habari.

‘Ndiyo maana mambo ya kaka James yalianza kuwa safi mara baada ya vifo vya wazazi wetu.’ Niliwaza.
Wakati huo huo nikakumbuka swali, nikaona nimuulize huyo huyo Sharifa kwani hata yeye alikuwa ni mdau wa kafara hizo.

“Umesema kafara ya daraja la kwanza inahusisha wazazi wote wawili na ndugu mmoja wa damu, mbona sasa baba yangu alikufa wakati hakuwa baba wa kumzaa James?”
“Kwa kuwa alikuwa kamuoa mama mzazi wa James na pia alikuwa na mapenzi ya baba kwake, basi kafara yake ilifana.” Alijibu Sharifa.

Akaendelea kunieleza kosa la James lilikuja kutokea baada ya kutakiwa kutoa kafara nyingine ili kukamilisha kafara za kwenye daraja la kwanza. Hapo alitakiwa ndugu yake wa karibu; mdogo mtu, kaka mtu, shangazi ama mjomba.
Kwa bahati mbaya sana ndugu wa damu aliyekuwa yu ngali hai nilikuwa ni mimi peke yangu. Aliamua kukaidi kunitoa kafara kutokana na mambo mawili.

Jambo la kwanza ni upendo uliokuwepo baina yangu na yeye. Kusema kweli kaka James alikuwa ananipenda kupita kiasi, na ndiyo maana hakuwa tayari kunitoa kafara.

Jambo lingine lililomsababisha kaka James agome kunitoa kafara ni kwamba hapakuwa na ndungu mwingine wa karibu zaidi yangu mimi. Kama angenitoa kafara basi angebaki bila ndugu wa karibu katika dunia hii. Sasa kubaki bila ndugu wa karibu lilikuwa ni jambo gumu sana kwake.

Nadhani hata wewe mpenzi msomaji usingepata fursa ya kusimuliwa simulizi hii nzuri iliyojaa vitisho vya lejaleja na yenye kusisimua kwani ningekuwa tayari nimeshalala mauti.

Baada ya kuona kunitoa kafara haiwezekani, James aliacha kabisa kwenda kwa mganga aliyekuwa amemfanyia dawa ya kumpa utajiri huo wakati alitakiwa awe anaenda mara moja kwa mwezi kufanya ibada. Muda wa kukamilisha kafara ya daraja la kwanza ulipita huku akiwa hajakamilisha, akaongezwa muda wa ziada nao ukawa umepita.

Mganga alipoona James kapuuzia agano hilo aliamua kumripoti kwa wataalamu wake ambao ndiyo waliokuwa wanamwezesha kufanya uganga huo.

Wataalamu hao walikasirishwa sana na kitendo chake cha kujifanya mjanja na mwenye akili kuzidi wao waliokuwa wamempa maagizo yale. Ndipo walipoamua kumtoa duniani kwa staili ya kujiua mwenyewe ili akaonekane ana dhambi hata mbele za mwenyezi Mungu.

Japo kabla ya kutoa adhabu hiyo walitoa muda wa kutosha kwake wakitegemea labda angejirudi na kukamilisha agano lao, siku zilizidi kwenda bila ya mabadiliko yoyote ya kutaka kujirudi kwa James.

Tena alipoona kakaa muda mrefu bila kupatwa na matatizo yoyote ilhali alikuwa hajakamilisha kutoa kafara alijua kuwa huenda zile zote zilikuwa ni danganya toto tu na vitisho visivyokuwa na misingi yoyote. Baada ya muda wa nyongeza kuisha uhai wa James ukawa ni halali ya wataalamu hao.

Hayo ndiyo mambo yaliyosababisha kifo cha wazazi wangu pamoja na kaka yangu. Tamaa ya kaka yangu kupata mali nyingi kwa njia ya mkato ndiyo iliyagharimu maisha yake na ya wazazi wetu kwa ujumla. Habari hiyo yote mimi nilikuwa siijui ila Sharifa ndiye aliyekuja kuning’amua.

NINI KITAFUATIA? USIKOSE............!!!
 
MIRATHI YA KAKA sehemu ya 34

ILIPOISHIA TOLEO LILLOPITA...
Hayo ndiyo mambo yaliyosababisha kifo cha wazazi wangu pamoja na kaka yangu. Tamaa ya kaka yangu kupata mali nyingi kwa njia ya mkato ndiyo iliyagharimu maisha yake na ya wazazi wetu kwa ujumla. Habari hiyo yote mimi nilikuwa siijui ila Sharifa ndiye aliyekuja kuning’amua
.

SASA ENDELEA..........

Pamoja na maelezo hayo kuhusu kifo cha kaka James nilikuwa bado na maswali mengi sana kichwani mwangu. Maswali menyewe ni pamoja na yeye Sharifa anahusika vipi na kafara hiyo ama ana uhusiano upi na mganga wa kaka James?
Pia swali jingine lililokuwa limetanda kwenye ubongo wangu ni kwamba mimi kosa langu lilikuwa ni lipi hapo wakati aliyefanya maagano na mganga ni kaka yangu tu? Sikuwa na majibu yake ila niliamini kuwa maswali hayo yangejibika kwa Sharifa.

Sikusita kumuuliza kwani mpaka wakati huo nilikuwa nimemzoea na kumuona kama alikuwa ni mtu wa kawaida wakati alikuwa si wa kawaida.

Nilianza na kutaka kujua hao wataalamu hasa ni kina nani na wanapatikana wapi? Swali lilijibiwa. Nikaambiwa kuwa wataalamu ni wale viumbe waliokuwa wamemuweka mganga huyo ili aweze kufanya mawasilo nao katika kumpatia mtu utajiri aombapo. Sikutaka kuendelea tena kudodosa juu ya swali hilo kwani tayari niling’amua kuwa wataalamu hao ni majini ama pepo wachafu.

Nikahamia kwenye swali la pili ambalo ni kutaka kujua Sharifa anahusikanaje na huyo mganga. Alichonijibu wala sikukitila shaka, nikaachana na swali hilo mara baada ya kupewa jibu.

“Na wewe una shirika gani na yule mganga?”
“Ni mmoja kati ya wataalamu wake. Na mimi ndiye nilichaguliwa kuhakikisha James anaaga dunia pamoja na kukuandama wewe ili tukutie adabu, na ukiwa mgumu wa kuelewa utamfuata kaka yako aliko.”

Sikutaka hata kuendelea kudodosa kwani majibu yenyewe yalikuwa yanajitosheleza. Tangu mwanzo wa kuniandama mpaka kunitoa jela nilikuwa nimeshabaini kuwa Sharifa hakuwa kiumbe wa kawaida. Alikuwa ni jini.
Hofu ilizidi kujengeka alipotamka kauli ya kwamba hata mimi nikileta za kuleta atanitia adabu ya kumfuata kaka James alikokuwa. Tafsiri ya maneno hayo ilikuwa ni kwamba ataniua kwani James hakuwa Marekani wala Dubai bali alikuwa kuzimu.

“Kosa langu hapo mimi ni lipi mpaka uniandame hivi?”
“Mirathi ya kaka yako.” Alijibu kwa mkato kisha akafunga bakuli lake, yaani namanisha akanyamaza kimya.
Bado kichwa changu kilikuwa na maswali ya kumhoji Sharifa. Mirathi ya kaka ilikuwa imefanya nini? Nilizidi kuwaza kabla sijalitupia swali hilo kwa Sharifa.
Nilipomuuliza alinijibu kuwa mali ya aina hiyo huwa haitakiwi kurithiwa na mtu yeyote yule. Nilifanya kosa kubwa sana kurithi mali alizokuwa ameziacha kaka James wakati zilikuwa ni za maagano.
Mpaka hapo niliweza kuelewa kiini cha matatizo yangu. Nilijikuta nikianza kujuta kurithi hizo mali pamoja na kuzaliwa pia. Niliweza kubashiri hatari iliyokuwa inaninyemelea mbele yangu huku chanzo chote kikiwa ni mirathi ya kaka James.
“Kumbe chanzo cha misukosuko yote hii ni hicho, sasa utanisaidiaje ili nijinasue kwenye hili balaa?” Niliamua kumuuliza hivyo ili nijue hatima yangu.
“Dawa ya hapo ni moja tu”
“Ipi hiyo?”
“Kufanya yale yote tunayokutaka uyafanye, zaidi ya hapo anza kujihesabu kuwa ni marehemu mtarajiwa.”
Hakuna anayependa kufa jamani. Sikujua nifanye nini ili kujinasua kwenye urimbo niliokuwa nimenasa. Kuendelea kuishi nako nilikuwa bado nakutamani. Sasa nilizidi kuwa katika wakati mgumu.

Maelezo ya mwanadada huyo hayakuwa na chembe ya utani ndani yake hata kidogo. Alichokuwa anakisema alikuwa anakimaanisha. Uwezo wa kufanya hivyo alikuwa nao.

Tulibaki tukiwa tumetumbuliana macho, mimi nikiwaza yangu kutokana na uzito wa jambo ulivyokuwa. Nilikuwa najiona dhahiri ninavyodumbukia kwenye shimo lenye kina kirefu nisiloweza kutoka tena.

Wakati nikiwa katika lindi la mawazo niligutushwa na sauti ya Sharifa. Alianza kwa kuniita jina langu.
“Brighton!”
“Naam!” Nami nilimwitikia.

“Usiwaze sana kwani kazi nzito ilishafanywa na kaka yako, unachotakiwa wewe ni kuikamilisha tu na utakuwa bilionea wa kuogopeka.” Alinyamaza kidogo kisha akaendelea.

“Daraja la kwanza utakuwa umeshalivuka kwani wazazi wa James ni wazazi wako, pia kufa kwake kutachukua nafasi ya ndugu wa karibu, kafara ambayo ilikuwa utolewe wewe. Kitakachohitajika kwako ni kuoa mke kisha mkishazaa mtoto unamtoa kafara akifuatiwa na mama yake, hapo utakuwa tayari umeshakamilisha daraja la pili.” Alipozi kidogo.

Wakati wote huo nilikuwa nimemsikiliza kwa makini. Baada ya kupozi kidogo aliendelea kuniambia kuwa nikishaimaliza daraja la pili lile lililokuwa linafuata ni mteremko. Daraja hilo ambalo ni daraja la tatu lilikuwa ni kumtoa kafara mtu mmoja kila mwaka, mtu huyo anaweza kuwa ni mfanya kazi wako ama ni mteja wako. Hiyo hatua ndiyo ilikuwa ni nyepesi kuliko zote kwani pale unamtoa mtu ambaye siyo ndugu wa karibu.

Hata hivyo bado ulikuwa ni mzigo mzito moyoni mwangu. Dhambi ya kuua nilikuwa naichukia na nilikuwa sitegemei kabisa kuitenda katika maisha yangu.

Nilivuta kumbukumbu ya maneno ya marehemu kipenzi changu Anna aliyoniambia kwenye ile ndoto niliyoota, ndoto ya kutisha. Katika maneno yake alinisisitiza sana nisiue wala kujiua kwani adhabu yake huwa ni kubwa mno.
Alinisisitiza nizidi kutenda mema huku nikiongeza upendo kwa watu wote wanaonizunguka ili siku zangu zikiisha duniani nikapumzike kwa amani na siyo kwa mateso.

Sasa mwanamke aliyekuwa mbele yangu alikuwa ananishawishi nianze kuua kwa ajili ya kupata utajiri, tena siyo kuua mara moja bali ni kuua kila mwaka mpaka pale maisha yangu yatakapofika kikomo duniani. Niliogopa sana.

Kibaya zaidi jambo lilikuwa limekaa kwenye njia panda, kama nisingefanya hivyo basi ningeuliwa mimi. Kweli maisha ni matamu sana mithili ya asali mwitu japokuwa ni mafupi zaidi ya watu wa Uturuki.

Hapo ndipo nilizidi kuumiza kichwa. Lakini kumbukumbu ya maneno ya marehemu Anna ilionekana kunipa nguvu. Nikajisemea kimoyomoyo kuwa ni bora nife kuliko kubeba dhambi mbaya na nzito kama hiyo, dhambi ya kuua.

Nikiwa katika kuwaza wazo lilinijia, nikaliona linafaa kulifanyia kazi. Nikataka kufumbua kinywa changu ili nieleze msimamo wangu juu ya jambo lililokuwa lipo mbele yangu. Kabla sijaongea chochote nilimuona Sharifa akisimama na kuniwekea mkono wake kichwani. Mwili wote ulisisimka, nikajihisi kama nimepigwa shoti ya umeme.

Alipotoa mkono wake juu ya kichwa changu aliniambia gari tuliyokuwa tumeenda nayo hotelini hapo imekuwa yangu kuanzia wakati huo. Pia akaniambia pesa zote zilizokuwemo kwenye brificase iliyokuwa mezani zote ni zangu.

Mara baada ya kuongea hivyo alinikabidhi funguo za gari zilizokuwa mezani. Kufumba na kufumbua alipotea ghafla, nikabaki peke yangu kwenye chumba hicho. Niliogopa sana.

**************************

“JE, HUO NDIO UTAKUWA MWANZO WA UTAJIRI WA BRIGHTON???. ITAENDELEA..........
 
Nice ila mkuu umetuacha ukiwa sana leo weka hapa episode tatu aiseeh
 
MIRATHI YA KAKA sehemu ya 35

ILIPOISHIA TOLEO LILLOPITA...

Mara baada ya kuongea hivyo alinikabidhi funguo za gari zilizokuwa mezani. Kufumba na kufumbua alipotea ghafla, nikabaki peke yangu kwenye chumba hicho. Niliogopa sana.

**************************
SASA ENDELEA..........
Asubuhi ilifika, ilikuwa ni asubuhi ya kwanza kuiona nikiwa uraiani baada ya kukaa rumande na hatimaye gerezani kwa miaka mingi. Niliamkia kwenye hoteli hiyo hiyo niliyokuwa nimepelekwa na Sharifa jana yake.

Mara baada ya kuamka nilitupia jicho langu kitandani kuiangalia brificase iliyokuwa imejaa mapesa niliyokuwa nimeachiwa na Sharifa. Niliiona imetulia. Nikajiinua kisha nikaifungua na kuiona minoti imejaa tele.

Nilipoangalia mezani niliziona funguo za gari niliyokuwa nimeachiwa. Kwa bahati nzuri chumba nilichokuwa kilikuwa kipo upande tuliokuwa tumeegesha gari. Nikaamua kuchungulia nje ili kujiridhisha kama gari hilo lilikuwepo kweli. Nikaliona limetulia.

Wazo nililokuwa nalo usiku wakati Sharifa hajaondoka ni kukataa katakata kufuata masharti yote niliyokuwa nikishinikizwa kuyafanya; masharti ya kuoa mwanamke kisha akishanizalia mtoto nimtoe kafara pamoja na mtoto aliyemzaa, na baada ya hapo niwe natoa kafara mtu mmoja kila mwaka ambaye ni mfanyakazi wangu ama mteja wangu wa aina yoyote ile.
Hata hivyo baada ya Sharifa kunishika kichwani muda mfupi kabla ya kuyeyuka ghafla wazo hilo nalo liliyeyuka kabisa kichwani mwangu. Nikaanza kujiona kama mtu anayechezea shilingi kwenye tundu la msala.

Nililipima jambo hilo usiku kucha kwa mapana na marefu, nikaona hakuna sababu yoyote ya kulipiga teke debe la bahati kama hilo. Kitu kilichonipa moyo ni kwamba sikutakiwa kumtoa kafara ndugu yangu yeyote wa karibu zaidi ya mke ambaye nitamuoa kwa ajili hiyo pamoja mtoto nitakayemzaa kwa ajili hiyo.

Nikaona ni bora nikubaliane na shinikizo la Sharifa ili nitengeneze maisha yangu, niwe mmoja kati ya matajiri wakubwa nchini na duniani pia. Moyo wangu uliridhia kabisa kutajirika kwa njia hiyo, njia ya nguvu za giza na ya kishetani huku nikiwa tayari kuendelea kuteketeza watu kila mwaka kwa kuwatoa kafara ili nizidi kuulinda utajiri wangu huo.

Pesa nilizokuwa nimeachiwa na Sharifa zilizidi kunipa jeuri, jeuri ya kwenda kununua nyumba sehemu yoyote katika nchi hiyo. Jambo la kuendelea kuishi kwenye mji huo sikuwa nalo kabisa akilini mwangu, hivyo nikaamua kuondoka asubuhi hiyo kwenda mji mwingine uliokuwa mbali na mji huo.

Niliinuka na kwenda maliwatoni kujimwagia maji mwilini mwangu. Nilipotoka nilivaa nguo zangu kisha nikainua simu ya mezani iliyokuwemo hotelini humo kuangiza kifungua kinywa.

Haukupia muda sana mlango ukagongwa, nami nilifungua na kumuona dada aliyekuwa amebeba trei (chano) iliyokuwa imesheheni mazagazaga kwa ajili ya kifungua kinywa.

Kabla hajaondoka nilichukua noti moja iliyokuwa na rangi ya kaki na kumpa ikiwa ni malipo ya kifungua kinywa hicho.
“Haina haja ya kulipa maana kila kitu kimelipiwa.” Aliniambia mwanadada huyo.

Hata hivyo ili kumuonyesha kuwa nilikuwa ni bilionea mtarajiwa kwa wakati huo, nilimwambia achukue tu hiyo pesa kwani nilikuwa nimeshaitoa kwenye mahesabu. Naye bila kuvunga aliipokea, si alikuwa kapewa!

“Samahani dada yangu kama nitakukwaza, ningependa kulijua jina lako.” Nilijikuta namchombeza zikiwa ni harakati za kutaka kutangaza nia katika suala zima la mapenzi.

Bila kinyongo wala malingo msichana huyo alinionyesha jina lake kwenye kitambulisho chake cha kazi alichokuwa amekining’iniza shingoni.

Nililisoma jina na kujikuta naachia tabasamu.

“Kumbe unaitwa Anna, jina lako lina historia ndefu sana katika maisha yangu.”
“Historia gani tena kaka yangu?”
“Kwanza mama yangu mzazi alikuwa akiitwa jina hilo, pili kuna msichana ambaye nilitokea kumpenda kupita kiasi naye alikuwa akiitwa Anna, ni jina muhimu sana katika maisha yangu.”
“Kumbe! Basi na mimi naitwa hivyo!”
“Natabiri na wewe utakuwa na historia ndefu sana katika maisha yangu,”
“Yaweza kuwa!” Aliongea Anna na kuanza kunipa mgongo ili aondoke.
Bila kufikiri wala kuwaza nilijikuta naropoka kumuomba namba ya simu ama mawasiliano yoyote. Pale pale alinitolea kadi yake ya biashara (business card) iliyokuwa na kila aina ya mawasiliano aliyokuwa akitumia.
“Asante sana mrembo!”
“Usijali!” Alimalizia maneno hayo huku akifungua mlango na kuondoka zake.
Taratiibu kabisa nilijongea kwenye kimeza kilipokuwepo chano cha mapochopocho ya chakula cha asubuhi. Pasipo kuvunga nilikaa na kuanza kujichana kwa raha zangu. Kilikuwa ni kifungua kinywa cha haja, waswahili wa siku hizi wanakwambia ‘msosi draft’ulioenda shule.

Muda mfupi baada ya kumaliza kushambulia kifungua kinywa niliondoka kwa mwendo wa madaha mpaka kwenye mchuma wangu huku nikiwa nimening’iniza kibrificase changu mithili ya kibosile ama fisadi aliyefutuka tumbo kwa kuchakachua fedha za umma.

Mpaka nafika nje sikumuona Anna, nilitamani sana japo tupungiane mkono wa kuagana ili nimringishie gari langu la kifahari, lakini haikuwezekana. Nadhani alikuwa kwenye majukumu yake mengine hotelini hapo.
 
Samahani naomba tuishie hapa; natafuta uhondo mwingine......

Shukrani kwa wote, na pia samahani sana kwa wale niliowakwaza....
 
Back
Top Bottom