MIRATHI YA KAKA sehemu ya 33
ILIPOISHIA TOLEO LILLOPITA...
Nilipomaliza kula mazungumzo yalianza. Shauku yangu kubwa ilikuwa ni kusikia habari za Mapara. Hata hivyo kwa wakati huo nilikuwa na uhakika wa kusikia habari zote za Mapara kutoka kwa Benja kwani ukaribu wao ulikuwa ni kama pete na chanda.
SASA ENDELEA..........
Alianza kwa kunipa pole kwa matatizo yote yaliyokuwa yamenisibu. Baada ya hapo alianza kunieleza habari niliyokuwa naingijea kwa hamu kubwa.
“Tangu upatwe na matatizo Mapara alikuwa akijitahidi sana kuisimamia miradi yako. Tena ilikuwa ikiendelea vizuri kila kukicha.” Alinieleza Benja.
Wakati huo nilikuwa makini kusikiliza; hatua kwa hatua, neno kwa neno huku nikiwa na maswali tele kichwani juu ya hatima ya mali zangu baada ya kudokezwa kuwa niliyekuwa nimemwachia dhamana ya kuziangalia na kuzitunza alikuwa katimkia ughaibuni.
Benja aliendelea kunieleza kuwa baada ya hukumu yangu Mapara alianza kujitapa kuwa mali zote hizo nilikuwa nimemkabidhi. Akawa na jeuri ya pesa kupindukia, si unajua tena baadhi ya watu wanapopata pesa kirahisi rahisi huwa hawana machungu nazo!
Akawa ni mtu wa ahasa. Wanawake na yeye, tena akawa anawabadilisha kama nguo. Mchana yupo na huyu, asubuhi alikuwa na yule na usiku utamuona na mwingine. Pombe na yeye kila wakati.
Baada ya kutapanya mali kwa miezi kadhaa uchumi wa miradi yangu ulianza kushuka. Ndipo alipoanza kuuza kila kitu ili atimkie Bondeni kwa mzee Madiba, yaani Afrika ya kusini.
Alimalizia kwa kuuza nyumba yangu akamuuzia kigogo mmoja ambaye alikuwa ni mbunge. Baada ya kukamilisha uuzaji wa nyumba yangu Mapara alikwea ‘pipa’ na kuishia ‘Sauzi’. Huo ndiyo ulikuwa mwisho wa habari ya Mapara kwa mujibu wa maelezo ya Benja.
Kichwa changu kilizidi kuwa kizito utadhani kilikuwa kimeng’atwa na manyigu. Sikutegemea kabisa kama Mapara angefanya utumbo kama ule.
Mpaka hapo mipango yangu yote ilikuwa imechemka, kwa msemo wa vijana wa kileo ilikuwa ‘imebuma’. Niliendelea kupiga miayo mfululizo utadhani sijala siku tatu wakati ndiyo nilikuwa nimemaliza kushindilia sahani ya ubwabwa..
“Sasa utanisaidiaje rafiki yangu, maana sitaki kabisa kuendelea kuishi kwenye mji huu kwani watu wanaweza wakasanua ishu kuwa nimetoroka jela.” Nilimuuliza Benja kwa sauti ya huruma.
“Kwa hiyo unataka ukaishi mji upi?”
“Mji wowote ule ilmradi uwe upo mbali na huu, nchi yetu ina miji mingi tu ambayo shughuli za kiuchumi zinapatikana. Nina imani nikifika sehemu na kutulia baada ya muda fulani mambo yangu yatakaa sawa.” Nilizidi kumweleza Benja.
Pamoja na kuwa nilikuwa nipo mikononi mwake nikiamini kabisa kuwa shida yangu itafanikiwa, mambo yalizidi kuwa si mambo. Msaada wake ulikuwa si zaidi ya kunihifadhi kwa siku kadhaa ambazo ningekaa kwake. Kuhusu suala la pesa alikuwa ni mtupu.
Sikushangaa kusikia hivyo kwa kijana huyo kwani tangu sijaenda jela maisha yake yalikuwa yapo vilevile. Pamoja na kukaa miaka lukuki jela bado nilimkuta hajaongeza hata stuli kwenye chumba chake hicho zaidi ya godoro la kulalia na redio kaseti aliyokuwa nayo.
Hii yote ilitokana na kutojishughulisha katika maisha yake. Si yeye peke yake bali kulikuwa na vijana wengi tu katika mji huo waliokuwa na kasumba ya kukusanyikana kwenye masikani zao tu na kuanza kucheza kamali kutwa nzima.
Baada ya kukosa msaada kwa mwenyeji wangu huyo nilikaa kimya kama dakika kumi hivi nikitafakari la kufanya ili kukimbilia kujificha kwenye mji mwingine tofauti na huo. Mapara alikuwa kashaniponza kwa kuyapeleka kombo mambo yangu yote.
Kabla hatujafikia muafaka juu ya sakata langu, mlango wa chumba cha Benja uligongwa. Moyo wangu ulilipuka ‘lipu’ huku hofu ya kukamatwa ikitanda katika mawazo yangu.
Naye Benja aliinuka taratibu na kwenda kufungua mlango kidogo kidogo kisha akatoka kumsikiliza aliyekuwa anagonga.
Sauti ya msichana niliisikia ikimsalimia Benja kisha kumhoji ikimuuliza kama nilikuwemo ndani. Mapigo ya moyo yalizidi kwenda kasi baada ya kusikia jina la Brighton likitajwa, yaani jina langu.
Ilikuwa hainipi kabisa akilini kwa mtu mwingine yeyote katika mtaa huo au mji kwa ujumla kujua kuwa nilikuwa nimetoka jela. Sasa kitendo cha mtu kuja moja kwa moja na kugonga nilipokuwa nimefikia kisha kuniuliza kilikuwa kimenikosesha kabisa amani moyoni.
Nilibaki nikiomba kimungu mungu wasije wakawa askari polisi ama wana usalama. Nilijikuta nikiogopa hata kupumua kwa kuhofia mihemo yangu kusikika huko nje ya chumba.
Mara nilimsikia Benja akimhoji mtu aliyekuwa akiniulizia kuwa ni nani na alikuwa akinitafutia nini. Hata hivyo majibu ya msichana huyo sikuyasikia kwani alikuwa akiongea polepole sana.
“Huyo Brighton unayemuulizia haishi hapa wala mimi simjui. Kwanza hilo jina ni geni kabisa katika mtaa wetu, kama vipi endelea kuulizia kwa wengine.” Nilimsikia Benja akijibu hivyo.
Moyo wangu ulifurahi sana kusikia Benja akijaribu kupapatua ili kuokoa maisha ya uhai wangu uliokuwa umebaki. Hata hivyo mabishano makali yaliibuka baina ya mwanadada huyo na Benja.
Mwanadada huyo alikuwa akidai kuwa ana uhakika wa asilimia mia moja kuwa nilikuwemo chumbani humo huku Benja yeye akikanusha vikali.
Alirudi ndani haraka huku akiwa na hasira kisha akaufunga mlango kwa kuukomea ili kumkomoa mtu aliyekuwa akileta ubishi pale mlangoni. Sikutaka kumuuliza chochote kwani kama ningeongea basi sauti yangu ingesikika na kisha mpango wetu kubumbuluka.
Alijitupia kitandani huku akimlaumu mwanamke huyo kwa kuwa mbishi bila sababu. Huku akiwa bado analalama, tuliuona mlango ukifunguka licha ya kukomea wakati anaufunga.
Pamoja na ubabe aliokuwa nao Benja alijikuta akinywea baada ya kuona mlango unafunguka. Hakuendelea tena kubwabwaja badala yake alibaki mdomo wazi huku hofu na woga vikimjaa.
Baada ya mlango kufunguka msichana aliyekuwa anabishana na Benja mlangoni aliingia mpaka chumbani. Kumbe alikuwa ni Sharifa, msichana aliyekuwa kanisababishia kufungwa kisha kuniokoa dakika chache kabla ya kunyongwa kitanzini.
Sasa nilikuwa nimeshaanza kumzoea msichana huyo.
“Ooh! Sharifa, kumbe ni wewe, samahani kwa yote yaliyojitokeza kwani mwenzio nalazimika kuishi kama digidigi.” Nilimwambia huku nikimlaki kwa kumkumbatia.
Wakati huo Benja alikuwa aking’aang’aa sharubu tu, nikamtambulisha kwa Sharifa huku tukiwa bado tumekumbatiana. Alishusha pumzi kwa nguvu na kurudi katika hali yake ya kawaida.
“Mbona unaishi kwa woga na wasiwasi hivi?” Sharifa alinitwanga swali hilo.
“Naogopa kugundulika kuwa nimetoroka jela, maana jambo hilo tulilifanya tu kwa uwezo wako ila ni la hatari mno.” Nilijibu vile.
“Wasiwasi wako tu. Hakuna mtu yeyote atakayekuuliza juu ya hilo hata kama uende gerezani hapo hapo.” Aliongea tena Sharifa kunitoa wasiwasi.
Hata hivyo maneno yake sikuyasadiki hata kidogo ila nilikubali ili yaishe. Nilipomuomba tukae japo pale kwenye godoro ili anisaidie ushauri juu ya suala lililokuwa linaumiza kichwa changu alikataa. Akasema alikuwa amekuja kunichukua ili tuende kumalizia maongezi yetu tuliyokuwa tumeyabakisha kule gerezani kabla ya kutoroka.
Nilipomuuliza tunaenda kuongelea wapi aliniambia anajua yeye, nilichokuwa natakiwa kufanya ni kumfuata kokote ambako ataniambia tuende.
Nilimuaga Benja kisha tukaondoka na Sharifa. Sikuwa na nijualo juu ya safari hiyo. Tulipotoka nje ya nyumba alimokuwa kapanga Benja tuliingia kwenye gari moja la kifahari ambalo alikuwa amekuja nalo msichana huyo. Safari ya kuelekea nisikokujua ilianza huku dreva akiwa ni yeye.
Baada kama ya nusu saa tulikuwa tupo kwenye hoteli moja mashuhuri sana mjini hapo. Hoteli hiyo ilikuwa siyo ngeni kwangu japokuwa nilikuwa sijawahi kuingia ndani zaidi ya kuliona jengo lake kwa nje nikiwa napita karibu nayo.
Wakati tunashuka kwenye gari hiyo mara baada ya kufika hotelini hapo, Sharifa alichukua ‘brificase’ na kushuka nayo akiwa kaishikilia mkononi.
Sikuelewa kama tayari alikuwa kashalipia chumba au vipi kwa sababu tulipapita mapokezi bila kusimama, tukaenda moja kwa moja kwenye lift. Tulipofika lift ikatupandisha mpaka ghorofa ya saba, tukatembea kwenye korido mpaka kwenye chumba namba 138.
Tulipofika kwenye chumba hicho Sharifa alifungua mlango kwa kadi maalumu nao ukafunguka kisha tukazama ndani. Chumba kilikuwa matawi ya juu kweli kweli, kila huduma inayopatikana kwenye vyumba vya hoteli kubwa kubwa basi hata humo ilikuwepo.
Kimawazo nilikuwa mbali sana wakati huo. Akili yangu ilikuwa inazunguka kuwaza ni masharti gani nitapewa na msichana huyo ikiwa ni malipo ya kuniokoa kutoka kwenye kunyongwa kwa kitanzi.
Mwili wangu ulikuwa umezizima mithili ya mtu aliyetota kwa kunyeshewa mvua. Nilikuwa mdogo kama pilton.
Tulipoingia tulikaa kwenye sofa za nguvu, ndipo mazungumzo yetu yalipoanza.
“Brighton mwana wa David!” Sharifa alichokoza mada kwa kuanza kuniita.
“Naam!” Niliitikia na kukaa kimya kusikilizia kitachachoongewa.
“Bila shaka unapenda sana kuwa tajiri, maana umekuwa ni mtu mwenye kujituma na kujishughulisha ukiwa na lengo la kuusaka utajiri! Kweli ama si kweli?”
“Ni kweli, lakini utajiri ninaopenda mimi ni ule wa kuupata kwa njia za halali zenye kumpendeza Mungu.”
Baada ya kujibu hivyo nilimuona Sharifa akiangua kicheko cha dharau kisha akaendelea kusema,
“hayo ni mawazo finyu ambayo hayataleta tija katika maisha yako. Utajiri hauji kwa njia za halali hata siku moja na Mungu hawezi akakuletea utajiri. Tangu lini kitu haramu kikaja kwa njia halali?”
Kauli hiyo iliniacha njiapanda kidogo. Ikanifanya nirejee kwenye mafundisho ya dini niliyoyapata nikiwa bado kinda wakati huo, mafundisho yaliyozungumzia matajiri wa kale ambao miongoni mwao ni kina Ibrahim na kina Ayubu, mbona wao walikuwa ni wacha Mungu wazuri tu?
Nikakumbuka tena maneno ya Yesu kristo alipokuwa akiwaambia wanafunzi wake kuwa ni vigumu kwa tajiri kuingia kwenye ufalme wa Mungu kuliko hata kwa ngamia kupenya katika tundu la sindano.
‘Je, maneno haya huenda ndiyo yanaashiria anachokisema Sharifa?’ nilimalizia tafakuli yangu kisha nikatoa jibu kuwa si matajiri wote wanaoupata utajiri kwa njia za mkato.
“Tuendelee!” niliropoka mara baada ya kugutuka kutoka kwenye kuwaza kwa kina.
“Huo ulikuwa ni utangulizi tu, hivyo kama unataka kuwa mmoja kati ya matajiri wa dunia hii yakubali nitakayokuambia.” Aliongea Sharifa kisha akanyosha mkono wake kuichukua brificase iliyokuwa mezani.
JE, NI MAMBO GANI BRIGHTON ATAAMBIWA NA SHARIFA AMBAYO YATAMFANYA AWE TAJIRI? USIKOSE ..........