Hadithi ya kusisimua: Mirathi ya Kaka

Hadithi ya kusisimua: Mirathi ya Kaka

MIRATHI YA KAKA sehemu ya 12



ILIPOISHIA SEHEMU ILIYOPITA......
“Afande, kama vipi richukue maerezo maana tayari rimeshazinduka.” Alisikika afande aliyekuwa ameshikilia bunduki akimwambia mwenzake ambaye alikuwa kashika faili mkononi.
“Hamna tabu afande, hata mimi nilikuwa ninalifikiria hilo kichwani mwangu.” Alijibu afande huyo.


SASA ENDELEA.......

Mara nilimuona afande huyo aliyekuwa kashikilia faili mkononi akivuta kiti chake na kusogea karibu kabisa na pale nilipokuwa nimelaza kichwa changu. Alifungua faili lake huku akiwa kashikilia kalamu mkononi.

Alianza kunihoji maswali kuhusiana na tukio zima la mauaji ya Kishoka, kila aliponiuliza nilimjibu, kila nilipomjibu aliandika kwenye karatasi iliyopo kwenye faili lake.

“Mnaishi wangapi katika hiyo nyumba?” lilikuwa ni baadhi tu ya maswali niliyokumbana nayo kutoka kwa kachero huyo. Swali hilo nililijibu kwa kusema kuwa tunaishi wawili tu katika hiyo nyumba, yaani mimi na Kishoka.

Mara aliniuliza uhusiano wangu na Kishoka, nami nilimjibu kuwa Kishoka ni mpangaji wangu katika nyumba yangu niliyorithi kutoka kwa marehemu kaka yangu, kaka James ambaye alikufa kifo cha kujiua mwenyewe kwa kujifyatulia risasi kichwani baada ya kumuua aliyekuwa mpenzi wake pamoja na jamaa aliyemfuma akilamba asali ya mapenzi kwa mpenzi wake huyo..

“Sasa kwa nini umeamua kumuua Kishoka?” Askari huyo alinifyatulia swali jingine. Nami nilimjibu bila kusita wala kujing’atang’ata kwamba mimi sijaua.

“Kama wewe hujaua, ni nani aliyemchinja Kishoka ilhali mnaishi wawili tu katika hiyo nyumba?”
Nilijitahidi kuwa makini sana katika maelezo yangu ili nisijikanganyekanganye halafu nikaonekana nimeua kweli. Niliamua kumtaja muuaji, nikasema kuwa ni msichana fulani ambaye alianza kunifanyia vioja tangu juzi nilipokutana naye ufukweni. Nilieleza jinsi mambo yalivyokuwa kati yangu na mwanadada huyo kule ufukweni.

Nilipoulizwa jina lake na mahali alipokuwa anaishi niliishia kusema sina nijualo juu yake. Nilijaribu kurudia tena kutoa maelezo jinsi nilivyokutana na msichana huyo, sikuwa namfahamu hata kidogo, lakini yeye alidai kuwa ananifahamu na kwa kunithibitishia hilo alinitajia hadi jina langu. Hakuishia hapo tu, aliongeza kuwa mpaka kwangu alikuwa anapajua hivyo akaniahidi atanitembelea kesho yake asubuhi.

“Ilipofika kesho yake asubuhi kweli alikuja?” Aliendelea kuhoji askari huyo huku akionekana kunisikiliza kwa makini sana.
“Ndiyo alikuja lakini vilikuwa ni vioja vitupu!”
“Uliweza kuonana naye na mkaongea nini?” Aliniuliza afande nami nikaanza kumdadavulia vile ilivyojitokeza tangu msichana huyo anafika pale getini, akakaribishwa na Kishoka lakini akakataa kuingia ndani.

Niliendelea kueleza jinsi msichana huyo alivyopotea kimazingara tusimuone alikoelekea. Nilizidi kuweka wazi kila kilichojitokeza mpaka wakati nilipokikuta kichwa cha Kishoka kikiwa kimetenganishwa na kiwiliwili chake. Nilimalizia kwa kusema kuwa muuaji si mimi bali ni huyo msichana ambaye kwa vyovyote vile si binadamu wa kawaida.

Askari huyo aliyakataa katukatu maelezo yangu na kuniambia kuwa mimi ni muongo na hayo maelezo yangu hayawezi yakanifikisha kokote, akasema jeshi la polisi haliamini ushirikina wala mazingazi. Akanitaka nieleze ukweli ili aone ni jinsi gani ataweza kunisaidia. Nilimwambia ukweli wangu ndiyo huo na sikuwa na maelezo mengine zaidi ya hayo.

Afande huyo nilimuona akifunga faili lake na kuniambia nijiandae kwenda kuozea jela. Alichodai ni kwamba laiti kama ningeeleza ukweli basi angeweza kunisaidia.

Nikiwa rumande machozi yalizidi kunitiririka bila kukauka utadhani chemichemi za mto Naili, chemichemi ambazo hutiririka bila kukauka misimu yote; iwe masika ama kiangazi. Mifereji ya machozi ilikuwa inatiririka kutoka machoni ikipitia mashavuni mpaka kwenye kidevu.
Harufu mbaya ya humo kwenye ‘gheto’ la watuhumiwa ilinifanya nipige chafya mara kwa mara. Nilijaribu kujikaza kiume nijizuie kulia lakini cha ajabu machozi yalizidi kunitoka. Nilikuwa sijawahi kuswekwa rumande hata siku moja tangu kuumbwa kwa misingi ya dunia.

Siku niliiona kama haiendi, masaa nayo yalikuwa kama yamesimama. Tangu saa tano za asubuhi baada ya kuruhusiwa hospitali niliingia humo, mpaka muda huu ambao nilikuwa nauhisi ni kama saa tisa za jioni nilikuwa nimeiva sawasawa. Kwa muda mchache huu ambao nilikuwa nimekaa ndani nilikuwa najiona kama nimekaa mwezi mzima.

Mawazo kibao yalikuwa yametawala kichwa changu; niliwaza biashara zangu zitasimamiwa na nani, zaidi ya yote kilichokuwa kinaniumiza kichwa ni hatima ya kesi yangu iliyokuwa inanikabili, kesi ya mauaji.

Ilipofika usiku nilizidi kuipata freshi, tena ni freshi ya mwaka. Sulubu iliyokuwemo kwenye ‘gheto’ la watuhumiwa haielezeki, yaani ni sulubu ya kufa mtu. Hapo ndiyo nilianza kuamini kuwa kweli rumande siyo kanisani ama msikitini.

Mbu walinishambulia si mchezo, nilijaribu kuwaua mmoja baada ya mwingine lakini wakawa hawaishi wala kupungua, suala la kupata usingizi walau dakika moja lilikuwa ni ndoto; tena ndoto yenyewe ni ndoto ya kuota mchana kweupe.

Siyo mbu peke yao walionipa kero usiku huo, kunguni na viroboto nao walizidi kuleta adha katika mwili wangu.
‘Kama rumande ya polisi tu hali ndiyo hii, kule gerezani sasa hali ikowaje?’ Nilizidi kutafakari huku nikiwa ‘buzy’ kupambana na wadudu hao wasiyokuwa na chembe ya adabu hata kidogo.

Niliwatumbua kwa hasira kila nilipowabahatisha wakigema damu yangu, lakini nao ndiyo kwanza walizidi kuongezeka utadhani walikuwa wakialikana.
‘Kwa mtindo kama huu kufikia asubuhi nitakuwa nimepoteza lita kadhaa za damu katika mwili wangu. Lakini chanzo cha mateso haya yote ni yule msichana aliyemuua mpangaji wangu Kishoka.’ Niliendelea kunung’unika peke yangu. Manung’uniko ambayo hayakuzaa matunda ya wokovu wa kesi yangu hata kidogo.

Hayawi hayawi mwisho yakawa, jogoo la kwanza nililisikia likiruka ‘bonanza’ kuashiria alfajiri inawadia. Mara nilisikia jogoo la pili na hatimaye la tatu. Kulionekana kupambazuka huku nikiumaliza usiku kwa kuutoboa, yaani namaanisha sikusinzia hata sekunde moja zaidi ya kupepesa macho pale ilipobidi.

Ikawa asubuhi, siku ambayo sikujua itaishaje. Nilitegemea kupandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza ili kusomewa shauri lililokuwa linanikabiri. Lakini mambo yakawa sivyo.

Mara mlango ulipofunguliwa niliwaona askari wawili waliokuwa wameshikilia bunduki kila mmoja wamesimama mlangoni kisha wakanitaka nitoke. Nilipotoka walinifunga pingu mikononi kisha wakanitanguliza mbele mpaka kwenye chumba kimoja katika kituo hicho kisha mahojiano yakaanza upya.


JE, NINI KITATOKEA HUKO KATIKA MAHOJIANO? MUUAJI ATAJULIKANA? FUATILIA BAADAYE...
 
MIRATHI YA KAKA sehemu ya 14

Mara mlango ulipofunguliwa niliwaona askari wawili waliokuwa wameshikilia bunduki kila mmoja wamesimama mlangoni kisha wakanitaka nitoke. Nilipotoka walinifunga pingu mikononi kisha wakanitanguliza mbele mpaka kwenye chumba kimoja katika kituo hicho kisha mahojiano yakaanza upya.

SASA ENDELEA.......

Mahojiano hayo yalichukua takribani masaa mawili na nusu, hata hivyo hapakuwa na kipya zaidi ya kurudia kuulizwa maswali niliyokuwa nimeulizwa hata kule hospitali. Pia katika mahohjiano hayo yaliambatana na vitisho lukuki vya kunitaka nikiri kuwa nilimuua Kishoka. Hata hivyo niliendelea kushikilia msimamo ya kuwa sijaua.

“Wewe ni muuaji ila unajifanya ni mbishi, mbona ripoti ya postimotamu imeonyesha kuwa wewe ndiyo umeua?”
“Hapana afande, mimi sijamuua Kishoka. Maelezo niliyoyatoa ndiyo yana ukweli wote.”

“Mbona kwenye kisu kilichotumika kumuulia marehemu tumeona alama za vidole vyako, vilevile kwenye mwili wa marehemu alama za vidole vyako zipo?”

Hilo nalo lilikuwa ni neno. Nilishtuka sana kusikia hivyo. Ukweli ni kwamba wakati naingia chumbani kwangu sikujaribu hata kukigusa kisu kilichotumika kumchinja Kishoka. Isitoshe hata mwili wake sikuugusa; sasa jambo la alama zangu za vidole kuonekana kwenye kisu hicho na kwenye mwili wa marehemu lilizidi kunichanganya. Wakati mwingine nilihisi huenda ni mitego tu ya makachero hao ili kumfanya mtu aropoke kama kweli katenda kitendo hicho.

“Hilo ni jambo geni kwangu, kile kisu sikuwahi hata kukigusa zaidi ya kukitumbulia macho. Hata mwili wa Kishoka sikuwahi kuugusa zaidi ya kuukodolea macho, sasa alama za vidole vyangu zilifikafikaje kwenye kisu na maiti ya Kishoka?”

“Unatuuliza tena sisi! Naona wewe huna jipya ila ni ubishi tu unaokusumbua. Kesho faili lako tunalipeleka mahakamani kwani uchunguzi wetu sisi umeshakamilika.” Alimalizia kuongea askari huyo aliyekuwa amevaa nguo za kiraia kisha akaamuru nirudishwe rumande.

Baada ya mahojiano hayo nilirudishwa tena rumande. Kilichokuwa kinasubiriwa pale ni kufika asubuhi nyingine kisha nipelekwe mahakamani kujibu shauri lililokuwa likinikabili.

Nilisweka tena ndani na kuanza kuburudika na adha ya humo. Joto la kufa mtu nilikuwa linanisumbua kwa wakati huo. Hamkuwa na mkeka wala busati hivyo nililazimika kujilaza kwenye sakafu.

Ilipofika jioni mbu walicharuka tena. Ikawa tafrani mtindo mmoja, usiombe mbu wa rumande ndugu msomaji, wanauma mpaka kwenye nyayo. Nahivi sikuwa na shuka wala blanketi, heheee, nakwambia nilikoma kuringa.

Asubuhi nyingine ilifika japokuwa kwa shida sana. Mbavu zote zilikuwa zikiniuma kutokana na kulala kwenye sakafu usiku kucha. Mikononi na niguuni vilikuwa vimejitokeza vipele vingi kutokana na kutafunwa na mbu usiku mzima.

Mara mlango wa selo ulifunguliwa kisha nikawaona askari watatu wakinitaka nitoke. Nami bila ubishi nilitoka. Nilipotoka tu hawakunichelewesha, wakanifunga pingu kisha wakanipeleka sehemu ambako kulikuwa na karandinga.

Waliniamru nipande nami nikajitoma bila ya ubishi. Safari ya kuelekea mahakamani ilianza. Gari lilitoka mbio utadhani lipo katika mashindano, tulitumia takribani dakika kumi kufika mahakamani.

Tulipofika mahakamani tuliwakuta watu kibao, baadhi yao niliwatambua, walikuwa ni wakazi wa mtaani kwetu. Nilianza kuhisi kuwa taarifa za kesi yangu zilikuwa zimetapakaa sana huko mtaani.

Kamera za mapaparazi nazo zilizidi kunisonga wakati naingia mahakamani. Nilijaribu kujifunika usoni ili nisipigwe picha lakini haikusaidia chochote. Nilipelekwa mpaka sehemu ya kukaa watuhumiwa wakati wanasubiri kupandishwa kizimbani.

Mara ilisikika sauti... ‘koooort!’, sauti hiyo iliashiria kufunguliwa kwa mahakama. Watu wote walisimama ili kutoa heshima katika mahakama kama ilivovyo ada, muda mfupi waliketi na kesi zikaanza kusikilizwa.

Kesi yangu ndiyo ilikuwa ya kwanza kutajwa. Nilipandishwa kwenye kizimba kisha nikaulizwa dini yangu. Nilipotaja dini yangu nikapewa kitabu kitakatifu cha dini husika na kuanza kuapishwa.

Baada ya kuapishwa nilisomewa shitaka langu na kuambiwa sitakiwi kujibu chochote kwani mahakama hiyo ilikuwa haina uwezo wa kuendesha kesi ya mauaji. Baada ya hapo nilitolewa kizimbani na kurudishwa rumande nikasubiri jalada la kesi yangu lipelekwe mahakama kuu. Lakini rumande niliyopelekwa kwa mara hii haikuwa ile ya kule kituoni bali ni rumande ya magereza.

Nilikaa mahabusu katika rumande hiyo kwa siku kadhaa nikisubiri tarehe ya kutajwa kwa kesi yangu kwa mara ya pili ambayo ilitakiwa kuhamishiwa mahakama kuu, mahakama ambayo huwa na uwezo wa kuendesha kesi za mauaji.

Kawaida ya sheria za nchi yetu ni kwamba, mshtakiwa yeyote wa kesi ya mauaji hutafutiwa wakili na serikali kama hana uwezo wa kumlipa wakili. Wakili huyo humsaidia kusimamia kesi yake mpaka mwisho.
Hicho ndicho kilichotokea kwenye kesi yangu hiyo. Nilitafutiwa wakili ambaye alikuwa ni wakili kutoka kwenye taasisi moja inayosimamia haki za binadamu.

Nikiwa nasota kwenye rumande ya magereza nilipokuwa nimepelekwa baada ya kutoka mahakamani, wakili alinifuata na kuanza kujadiliana nami jinsi ya kunisaidia katika kunitetea kwenye kesi iliyokuwa ikinikabili.
“Hebu nieleze ukweli wako wote ili nijue ni jinsi gani nitakusaidia.” Alisikika wakili Jonas Mlyanyama kwa sauti iliyokuwa imejaa upole na yenye kubembeleza.

“Kusema kweli sikuhusika kabisa na kifo cha Kishoka.”

“Ilikuwaje, hebu niambia A mpaka Z bila kuficha kitu chochote.”

Nilianza kumweleza tukio zima lilivyokuwa. Nikamweleza jinsi msichana wa kule ufukweni nilivyokutana naye na kuweka miadi ya kunitembelea kesho yake nyumbani kwangu.
Sikuishia hapo, niliendelea kusimulia jinsi mauzauza yalivyoanza kujitokeza kwa mwanadada huyo pale alipokuja nyumbani na kukatalia getini baada ya kwenda kuambiwa na Kishoka apite ndani. Hata Kishoka alipokuja kuniambia kuwa mgeni huyo kakataa kuingia ndani bali ananitaka niende kulekule getini, nilienda lakini sikumkuta.

Niliendelea kumhadithia kizaazaa hicho wakili Jonas Mlyanyama huku akiwa kanisikiliza kwa makini kabisa. Hatimaye nilimaliza maelezo yangu kwa kueleza jinsi nilivyoikuta maiti ya Kishoka ikiwa imelazwa juu ya kitanda changu.

“Nimeambiwa kwamba alama za vidole vyako zilionekana kwenye mwili wa marehemu na kwenye kisu kilichotumika kumuua marehemu, ulikigusa kisu au ile maiti?”

“Hapana wakili sikugusa chochote hapo, na ndiyo maana nakuambia kwamba kesi hii ipo kimazingara. Hata mimi nashangaa kuonekana alama za vidole vyangu.”

Wakili Jonas Mlyanyama alivuta pumzi kisha akazishusha. Wakati natoa maelezo wakili huyo alikuwa ‘busy’ kuandika maelezo yangu kwenye kitabu alichokuwa amekuja nacho.

Pamoja na kuwa ‘busy’ wakili huyo alionekana kuwa makini sana kunisikiliza kila nilichokuwa nakinena. Pia hakuacha kuhoji maswali pale ilipolazimu. Alikuwa na maswali mengi utadhani mgambo wa kata.

Alinipa moyo na kuniambia kuwa kwa vile nilikuwa sijafanya kosa hilo kama nilivyokuwa nimeshtakiwa, Mungu angetusaidia na mwisho wa siku tungeibuka kidedea.


JE, WAKILI JONAS MLYANYAMA ATAFANIKIWA KUMTETEA BRIGHTON KATIKA KESI YA MAUAJI YA KISHOKA? USIKOSE!
 
MIRATHI YA KAKA sehemu ya 15

ILIPOISHIA SEHEMU ILIYOPITA......

Alinipa moyo na kuniambia kuwa kwa vile nilikuwa sijafanya kosa hilo kama nilivyokuwa nimeshtakiwa, Mungu angetusaidia na mwisho wa siku tungeibuka kidedea.

SASA ENDELEA.......

Baada ya maongezi hayo yaliyochukua takribani saa moja wakili huyo aliondoka zake na kuniacha nikirudishwa rumande kusubiri siku yingine ya kusomwa kesi yangu.

Niliendelea na msoto wa rumande. Kila siku mlo mmoja kwa siku huku chakula chenyewe kikiwa ni ugali wa dona na maharage yenye uozo. Maisha hayo nilikuwa sijawahi kuishi hivyo ilikuwa ni vigumu sana kuyazoea.

Hata hivyo sikuwa na jinsi, nililazimika kujikaza kisabuni huku nikisubiri kudura za Wahidi ziniokoe katika hilo janga. Ilikuwa inauma sana hasa pale nilipofikiria jinsi uhusiano wangu ulivyokuwa na mpangaji wangu Kishoka ambaye nilikuwa natuhumiwa kumuua.
Tuliisha kwa ushirikiano mkubwa kama ndugu wa damu ilhali tulikuwa tumekutana ukubwani tu huku kila mmoja akiwa na meno thelathini na mbili; yaani akiwa mtu mzima.

Sikuhusika na kifo chake, lakini nilikuwa nikishtumiwa ya kwamba nilimuua. Kwa mtindo huo kwa nini sasa roho isiniume? Ilikuwa ni zaidi ya uchungu.

Siku ya kupandishwa kizimbani kwa mara nyingine tena iliwadia. Asubuhi asubuhi mimi na mahabusu kadhaa tulisweka kwenye karandinga la askari magereza huku ulinzi ukiwa umeimarishwa. Safari ya kuelekea mahakamani ilianza.

Mara baada ya kufikishwa mahakamani tulishushwa huku tukilindwa kwa silaha za moto, siraha nzito nzito za kivita. Mapaparazi nao walikuwepo kama kawaida yao, wakaanza kutusonga ili wapate picha za kwenda kutuuzisha sura runingani na magazetini.

Licha ya kukaripiwa na askari magereza waliokuwa wametutanguliza, mapaparazi hao walizidi kukomaa ‘kutufotoa’ na kamera zao. Tukaingia mpaka mahakamani tayari kabisa kwa kuanza kusomewa mashtaka yetu kila mmoja kwa awamu.

Mimi ndiyo nilianzia kupandishwa kwenye jukwaa la watuhumiwa kisha nikaapishwa kama zilivyo taratibu za mahakama kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Baada ya kuapishwa kizimbani kesi yangu ilitajwa. Hata hivyo jaji Aneth Mwalukwa aliiahirisha tena kesi ili kusubiri jalada la kesi kutoka kwa mkurugenzi wa mashtaka. Kesi yangu ilipelekwa mbele kwa muda wa majuma matatu.

Niliteremshwa kizimbani na kurudishwa kwenye sello ya hapo mahakamani kusubiri mahabusu wengine wamalize kusomewa mashtaka yao kisha turudishwe rumande.

Baada ya mahabusu wengine kumaliza kusomewa mashtaka yao tulirudishwa rumande ya magereza huku gari tulilokuwa tumepakizwa likikimbia kwa kasi.

Watu walikuwa wamefurika kusikiliza kesi mbalimbali zilizokuwa zikiunguruma katika mahakama kuu ikiwemo kesi yangu. Kesi nyingi zilizokuwa zikitajwa siku hiyo zilikuwa ni za mauaji.

Wakati huo nilikuwa nipo kwenye kizimba cha washtakiwa nikiapishwa. Mara baada ya kuapishwa, kesi ilisomwa.

“Ni kweli au si kweli?” Lilikuwa ni swali la mwendesha mashitaka Charles Ngonyani ambaye alikuwa ni wakili wa serikari.
Hata hivyo wakili wangu bwana Jonas Mlyanyama aliniambia nikane, nami nikatikisa kichwa kukataa kisha nikasema, “si kweli”

Baada ya hapo kesi iliahirishwa tena kwa muda wa wiki moja ili upande wa mashtaka uanze kupeleka mashahidi wake.
Nilirudishwa tena gerezani nikiwa bado mahabusu. Mpaka hapo nilikuwa nimeshaipata freshi ya kwenda na kurudi mahakamani, kesi yenyewe ilikuwa haijaanza hata kusomwa.

Niliendelea kukaa rumande mpaka siku ya kesi yangu ikawadia tena. Siku ilipofika kama kawaida karandinga la magereza lilitusomba mpaka mahakamani mahabusu ambao kesi zetu zilikuwa zinasomwa siku hiyo.

Shahidi aliyeanza kutoa ushahidi kutoka upande wa mashitaka alikuwa ni Sajenti Bakari Mlongo ambaye ndiye alikuwa amelibeba jukumu la kuipeleleza kesi yangu.

Huku akiongozwa na wakili wa serikali, Sajenti Bakari Mlongo alieleza kuwa siku ya tukio akiwa kazini kwake kwenye kituo cha polisi cha kati alipigiwa simu kupitia simu ya kazini na mwanamke mmoja ambaye alijitambulisha kuwa ni ndugu yake na Kishoka.

“Baada ya mpigaji kujitambulisha hivyo aliwaambia nini?” Aliuliza wakili wa serikali bwana Charles Ngonyani.

“Mtu huyo alieleza kuwa kuna mauaji ya kutisha yaliyokuwa yamefanyika kwenye nyumba ya bwana Brighton David.” Alisikika Sajenti Mlongo akijibu.
“Mtu huyo alieleza kuwa nani kauawa?”
“Ndiyo alieleza. Alisema kuwa aliyekuwa ameuawa ni ndugu yake aitwaye kishoka.”
Sajenti Mlongo aliendelea kueleza kuwa baada ya kuambiwa hivyo alitoka yeye na askari wengine wanne na kuelekea kunako eneo la tukio.
“Mlifika mpaka eneo la tukio?”
“Ndiyo tulifika.”
“Ikawaje?”
“Kwanza tulilikuta geti la ngome ya nyumba hiyo lipo wazi, tulipofika kwenye mlango wa kuingilia wa nyumba ya mtuhumiwa tuliuona uko wazi. Ndipo tulipoingia kwa tahadhari kubwa. Hata hivyo pale ukumbini hakukuwa na mtu zaidi ya runinga iliyokuwa imewashwa.”
“Baada ya kuona hapana mtu sebuleni mlichukua uamzi gani?”
“Tulijaribu kuangaza na kubaini kuwa mlango wa chumba kimojawapo kwenye hiyo nyumba ulikuwa wazi na taa ilikuwa ikiwaka. Ndipo mimi na afande mmoja tuliingia kwenye chumba hicho.”
“Endelea kuieleza mahakama mlichokikuta baada ya kuingia kwenye chumba hicho!”
“Tulimkuta mtuhumiwa ambaye ni bwana Brighton akizunguka zunguka humo chumbani huku mwili wa Kishoka ukiwa kitandani huku kichwa kikiwa mbali na kiwiliwili chake. Vile vile kisu ambacho tulishuku kutumika katika kutekeleza mauaji hayo kilikuwa kikiambaa ambaa sakafuni.”
“Baada ya kuona hivyo mlichukua uamuzi gani?”
“Tulimuweka chini ya ulinzi mtuhumiwa, lakini kabla hatujamfunga pingu alianguka ghafla na kupoteza fahamu.” Aliongea Sajenti Mlongo.
“Huyo mtuhumiwa mliyemkamata siku hiyo ukimuona unaweza kumtambua?” Aliuliza wakili Charles Ngonyani.
“Ndiyo ninaweza.”
“Hebu ionyeshe mahakama tukufu mtu huyo kama yumo humu!”
“Yule pale kwenye kizimba.” Sajenti Mlongo aliongea huku akinisonta pale nilipokuwa.

Wakili wa serikali bwana Charles Ngonyani alimtazama hakimu na kumwambia, “Nimemaliza!” aliongea na kwenda kuketi.


KESI HII ITAISHAJE? USIKOSE SEHEMU IJAYO.............
 
MIRATHI YA KAKA sehemu ya 15


ILIPOISHIA SEHEMU ILIYOPITA....
Wakili wa serikali bwana Charles Ngonyani alimtazama hakimu na kumwambia,
“Nimemaliza!” aliongea na kwenda kuketi.

SASA ENDELEA.......

Ilifika zamu ya wakili wa upande wa utetezi kumuhoji shahidi aliyekuwa kizimbani. Wakili huyo bwana Jonas Mlyanyama alisimama na kusogea karibu na kizimba cha shahidi wa upande wa mashitaka sajenti Bakari Mlongo.

“Umesema mlipoingia chumbani mlimkuta mtuhumiwa anazunguka zunguka huku kisu kikiwa kinaambaa ambaa sakafuni, si ndiyo?” Mlyanyama alimhoji shahidi huyo.

“Ndiyo!” alijibu na kumsikiliza wakili wangu aendeleee kuongea
“Nikiiambia mahakama tukufu ya kwamba mteja wangu alikuwa katika kustaajabu baada ya kulikuta tukio hilo limefanyika katika chumba chake nitakuwa nakosea?”
“Ndiyo utakuwa unakosea kwa vile alama za vidole zilionekana kwa mtuhumiwa baada ya kuchukua vipimo, yote hayo yatakuja kuelezewa na mtaalamu wetu wa mambo ya picha na alama za vidole ambaye tulikuwa tumeambatana naye siku hiyo.”
“Na ikiwa labda mtuhumiwa alikishika kisu pamoja na mwili wa marehemu wakati tukio limeshafanyika ikiwa kwa kutokujua au kutokana na kuchanganyikiwa na hali ya tukio lilivyokuwa?”
“Kwenye vipimo hatukuona alama zingine zaidi ya alama za mtuhumiwa tu.”
“Huyo aliyewapigia simu kituoni kuwapasha taarifa za tukio alikuja kituoni?”
“Hapana!”
“Mlichukua namba yake ya simu baada ya kumaliza kuongea naye?”
“Hatukuweza kuchukua namba yake ya simu kwa sababu alipiga kwenye simu ya mezani.”
“Mpaka jalada la upelelezi wa kesi hii linakamilika mtu huyo aliwahi kufika kituoni japo mara moja nanyi mkapata kumfanyia mahojiano juu ya tukio hilo?” Wakili Jonas Mlyanyama alimtwanga swali hilo tena shahidi wa upande wa mashitaka.
“Hapana!”
“Sasa mimi naiambia mahakama kuwa mteja wangu hakuua bali mwanamke huyo ndiye mbaya na huenda ndiye aliyeua au anafahamu mwanzo mpaka mwisho juu ya mauaji ya Kishoka.”
“Siyo hivyo, mtuhumiwa ni yule pale kizimbani kwa sababu hata alama zake zilionekana kwenye mwili wa marehemu na kwenye kisu kinachosadikika kutumika kumchinja marehemu.”
“Sasa kwa nini mtoa taarifa wa awali asijitokeze kituoni kutoa maelezo na kuwa tayari kuja kutoa ushahidi mbele ya mahakama?”
“Kwa kweli hilo siwezi kujua ni kwa nini hajaonekana kituoni.”
“Basi kubaliana na mimi ya kuwa yule ndiyo mhalifu.”
Sajenti Bakari Mlongo alionekana kuwa na kigugumizi hatimaye akaganda mithili ya cd kongwe iliyochakaa. Wakili wangu bwana Jonas Mlyanyama alimwambia hakimu hana la zaidi la kumuuliza shahidi huyo.

Hatimaye shahidi wa pili kutoa ushahidi aliwadia. Shahidi aliyefuatia alikuwa ni Sajenti Majaliwa Mbogo, askari ambaye yupo katika kitengo cha kupima alama za vidole ambaye pia alikuwa ameambatana na kikosi kilichokuja kwangu siku ya tukio.

Sajenti Mbogo baada ya kuapishwa alikumbushwa saa na siku ya tukio na mwendesha mashtaka bwana Charles Ngonyani.
Sajenti Mbogo alieleza kuwa siku hiyo alikuwa kwenye kituo chake cha kazi kama ilivyo ada. Ndipo alipopata wito kutoka kwa mkuu wa kituo hicho na kuambiwa kuna mauaji yametokea kwenye nyumba yangu.

“Tueleze ilikuwaje baada ya kuambiwa hivyo na mkuu wako wa kituo.”
“Agizo lililokuwa limetolewa pale ni kwenda kunako eneo la tukio, na ndicho kilichofuata.”
“Mlipofika eneo la tukio mlikuta nini?” Mwendesha mashitaka aliendelea kuuliza maswali ya kuweza kumuongoza shahidi huyo aendelee kutoa ushahidi.

Maelezo ya Sajenti Mbogo hayakutofautiana sana na yale ya shahidi aliyekuwa ametangulia. Mwisho shahidi huyo alieleza jinsi matokeo ya vipimo vya alama za vidole yalivyonihusisha kuwa nilimuua Kishoka.
Hatimaye mwendesha mashitaka alimaliza kutoa muongozo kwa shahidi huyo kisha akamwambia mheshimiwa Jaji kuwa amemaliza na akaenda kuketi.

Wakili wangu aliinuka tena na kusogea kwenye kizimba ambacho shahidi huyo alikuwa amesimama. Alipofika akaanza kumuuliza maswali kama ilivyoada.
“Natumaini wewe upo kwenye kitengo cha kupiga picha na kupima alama za vidole kwa muda mrefu katika jeshi la polisi?”
“ Ndiyo.”
“Kama mimi nikishika kitu kisha mkaja kupima alama zangu za vidole si zitaonekana?”
“Ndiyo.”
“Nikiiambia mahakama kwamba mteja wangu alishika mwili wa marehemu pamoja na kisu baada ya kukuta tukio limeshatokea chumbani kwake kwa kutokujua madhara yake ama kutokana na kuchanganyikiwa unaweza ukakubaliana na mimi?”
“Hapana sitakubaliana na wewe.”
“Kwa nini?”
“Kwa sababu hatukuona alama za vidole vya mtu mwingine zaidi.”
“Mimi nitaiambia mahakama tukufu kwamba mteja wangu alishika sehemu hiyo hiyo aliyokuwa ameshika muuaji na ndiyo maana hazikuonekana alama za mtu mwingine.?”
“Haiwezekani, siyo rahisi kumshika mtu mpaka kumuua usimguse sehemu kubwa ya mwili. Ingekuwa mtuhumiwa aliyepo kizimbani hajafanya hilo tukio basi alama za vidole za mtu wa kwanza zingetapakaa mwili mzima wa marehemu.”
“Je, mtu kama kavaa ‘groves’ mikononi alama zake huonekana akishika sehemu?”
“Hapana.”
“Basi muuaji alikuwa kavaa groves wakati anaua na ndo maana alama za vidole hazikuonekana!”
“Hapana, muuaji ni yule pale kizimbani maana ndiyo tulimkuta eneo la tukio.”
“Shahidi aliyekutangulia amesema kwamba mtu aliyetoa taarifa za awali juu ya kifo cha kishoka hakujitokeza hata kidogo zaidi ya kupiga simu tu kituoni, unaweza kuniambia kwa nini hakutaka kujitokeza?”
“Kwa kweli siwezi kujua.”
“Nikikwambia kuwa hajajitokeza kwa kuwa alikuwa ni mharifu na huenda aliogopa kuja kuumbuka utakubaliana na mimi?”
“Hapo siwezi kusema chochote kwa sababu sijui sababu zilizomfanya asijitokeze kituoni.”
“Basi huyo akipatikana na kufanyia mahojiano kikamilifu huenda akawa na maelezo ya kutosha kuwasaidia katika upelelezi wa kesi hii na huenda mtambaini muuaji halali wa Kishoka na siyo mteja wangu.” Aliunguruma bwana Mlyanyama.

Mpaka hapo Sajenti Majaliwa Mbogo hakuwa na la kuongea. Wakili wangu alimtazama jaji na kumwambia kamaliza maswali ya kumuuliza shahidi huyo. Baada ya kusema hivyo akaenda kuketi.

Jaji aliiahirisha kesi na kutaja tarehe nyingine ambayo ingeendelea kusikilizwa. Nilitolewa kizimbani na kupelekwa kwenye karandinga la magereza tayari kabisa kwa kurudishwa mahabusu.


JE, KESI HII ITAISHAJE? USIKOSE ..........
 
MIRATHI YA KAKA sehemu ya 16
ILIPOISHIA SEHEMU ILIYOPITA....

Jaji aliiahirisha kesi na kutaja tarehe nyingine ambayo ingeendelea kusikilizwa. Nilitolewa kizimbani na kupelekwa kwenye karandinga la magereza tayari kabisa kwa kurudishwa mahabusu.

SASA ENDELEA.......

Ilikuwa ni kesi iliyonipa wakati mgumu sana kwa kipindi chote nilichokuwa mahabusu nikisubiri hatima yake. Kila wakati nilikuwa siishi kuwa na wasiwasi mithili ya mbuzi wa shughuli.

Wasiwasi pamoja na kuwaza huko kulizidi kuifanya afya yangu izidi kuwa mgogoro zaidi ya vile ilivyokuwa awali. Niliiona kesi inapelekwa polepole sana, nikawa natamani bora nihukumiwe ili nijue moja, kama kusubiri kunyongwa ama kuponea kwenye wokovu wa ngamia kupenya kwenye tundu la sindano.

Pamoja na maneno ya wakili wangu bwana Jonas Mlyanyama ya kunitia moyo na kunihakikishia kuibuka kidedea katika kesi hiyo, bado nilikuwa naona kama ananikebehi na kunipa faraja za kijinga kwa vile niliamini kabisa kuwa hata yeye alikuwa anauona ugumu wa kesi yangu ulivyokuwa.

Kibaya zaidi sikuwa hata na shahidi ambaye angesimama kizimbani na kujaribu kunitetea. Kesi yenyewe ilikuwa imejaa utata mtupu. Hata wewe mpenzi msomaji uliona wapi alama za vidole zionekane kwenye kitu ambacho hukuwahi hata kukishika? Huo ni utata, kama siyo kubambikiwa basi ni kiini macho.

Tarehe ya kusikilizwa tena kesi yangu iliwadia. Siku hiyo tena upande wa mashitaka ulitakiwa kupeleka mashahidi wake wawili. Shahidi wa kwanza kupanda kizimbani kutoa ushahidi alikuwa ni Daktari aliyeufanyia uchunguzi mwili wa marehemu Kishoka.

Akiwa kizimbani huku akiongozwa na mwendesha mashitaka, daktari huyo alieleza jinsi alivyoupokea mwili wa marehemu Kishoka na kuufanyia uchunguzi. Baada ya hapo alitoa maelezo ya ripoti ya postimotam kabla ya kuwasilisha nakala ya ripoti hiyo kwa Jaji.
Wakili wangu hakuwa na maswali mengi sana ya kumuuliza shahidi huyu hivyo hakutumia muda mrefu sana kumhoji alipokuwa kwenye kizimba cha kutolea ushahidi.

Ripoti ya daktari huyo ilikiri kuwa kweli Kishoka aliuawa kwa kukatwa na kitu chenye ncha kali mpaka akapoteza uhai wake.
Baada ya shahidi huyo kutoa ushahidi, upande wa mashitaka ulitakiwa kupeleka shahidi mwingine. Shahidi aliyekuwa ameandaliwa ni mmoja wa askari waliokuwa wamekuja nyumbani kwangu kuja kunikamata baada ya kupewa taarifa za kifo cha Kishoka.

Nilimuona mwendesha mashtaka ambaye ni wakili wa serikali akisimama na kumwambia jaji kuwa shahidi aliyetakiwa kupanda kizimbani haonekani na huku alikuwepo wakati mahakama inaanza.

“Hata hivyo kuna shahidi mwingine kajitokeza ambaye ni muhimu sana katika kesi hii. Mtu mwenyewe ni yule mwanamke aliyetoa taarifa za awali kituo cha polisi kuhusiana na kifo cha Kishoka.” Nilimsikia mwendesha mashtaka akimwambia jaji.

Moyo ulinilipuka puu baada ya kusikia kauli hiyo. Tumbo langu likachemka ghafla huku maswali mia mia nikijiuliza ya kuwa huyo mtu aliyetoa taarifa kituoni akinisingizia kuua ni nani.

Hata hivyo kwa upande mwingine nilifurahi ili nimuone mtu huyo mwenye moyo wa kinyama na roho ya kishetani kwa kunisakizia kwesi ya mauaji ilhali sikuua.

Baada ya jaji kuruhusu shahidi huyo apande kizimbani, nilimuona dada mmoja akiinuka na kuanza kutembea mwendo wa maringo kuelekea kwenye kizimba cha kutolea ushahidi.

Kitendo cha kumuona mwanadada huyo kilinifanya nianze kuhisi kupumua kwa shida huku mwili wangu ukianza kuishiwa nguvu. Pumzi zilizidi kubana, ghafla nilijiona nikianguka mzima mzima huku macho yangu yakipoteza upeo wa kuona. Kabla sijafika chini niliacha kujitambua na kupoteza fahamu ghafla.


JE NINI KITAENDELEA? HUYU MWANADADA NI NANI? USIKOSE KUFUATILIA....
 
MIRATHI YA KAKA sehemu ya 17



ILIPOISHIA SEHEMU ILIYOPITA....
Pumzi zilizidi kubana, ghafla nilijiona nikianguka mzima mzima huku macho yangu yakipoteza upeo wa kuona. Kabla sijafika chini niliacha kujitambua na kupoteza fahamu ghafla.

SASA ENDELEA.......


“Brighton, unajisikiaje?” Ilikuwa ni sauti ya wakili wangu bwana Jonas Mlyanyama aliyekuwa kaketi pembeni mwa kitanda nilichokuwa nimelala.

“Mh! Wakili, hapa nipo wapi?” Nilijikuta nikiuliza swali na siyo kutoa jibu baada ya kumfahamu mtu niliyekuwa naongea naye.
“Hapa upo kwenye hospitali ya magereza, ulianguka ghafla leo asubuhi wakati ukiwa kizimbani.” Alinijibu bwana Mlyanyama.
Baada ya kuniambia hivyo kumbukumbu zilinijia kwa kinagaubaga. Hapo ndiyo nilikumbuka tukio zima lilivyokuwa, hata hivyo nikapata shauku kubwa ya kumuuliza wakili wangu jinsi mambo yalivyokuwa kule mahakamani.

Wakati mimi ninashauku hiyo, yeye naye alikuwa na shauku ya kujua ni kitu gani kilinifanya nipoteze fahamu nilipokuwa pale kizimbani. Kila mmoja akawa na hamu ya kusikia maelezo kutoka kwa mwenzake.

Nilishusha pumzi ndeefu kisha nikamwambia bwana Mlyanyama,
“hivi nilianguka mpaka chini kabisa?”
“Ndiyo! Kwani ilikuwaje?”
“Kaka, ni mambo ya ajabu niliyoyaona mle mahakamani!”
“Mambo gani hayo?” Aliniuliza wakili huyo kwa upole kabisa huku akikaa mkao wa kula kisikia kilichonifanya nianguke na kuzua gumzo mahakamani hapo.
Ndipo nilipoamua kumpasulia kile nichokuwa nimekiona mahakamani.
“Yule msichana aliyeinuka kutoa ushahidi ndiyo muuaji kaka.” Nilimwambia wakili wangu kwa sauti ya kunong’ona.
“Muuaji ki vipi?” Naye alihoji kwani somo lilikuwa bado halijamwingia akilini.
“Yule ndiyo msichana mwenye mauzauza niliyekusimulia.”
“Yule uliyeonana naye ufukweni kisha kesho yake akawa anagonga geti lakini mkienda kumfungulia mnakosa?” Alizidi kuhoji wakili Jonas Mlyanyama.
“Haswaah! Wala hjakosea kaka. Sasa kitendo cha kumuona msichana huyo moyo wangu ulishtuka ghafla mpaka nikaanza kujihisi napata shida kupumua. Baada ya hapo sikujitambua tena.”
Mpaka hapo wakili wangu akawa ameshakifahamu kilichonifanya nizirai huku nikiwa kwenye kizimba. Nilipotupia jicho kwa wakili Mlyanyama nilimuona kajishika tama huku akionekana kuwaza kwa kina, baada ya hapo akashusha pumzi ndeefu iliyoashiria mtu kuchoka ama kukata tamaa.
“Kwa kweli hii kesi inautata sana. Tangu niwe wakili sijawahi kukutana na kesi yenye kizaazaa kiasi hiki. Pamoja na kukaa katika kazi hii kwa miaka zaidi ya kumi na mitano hii ndiyo mala ya kwanza kukumbana na kesi ngumu kama hii. Ama kweli hii ni kali, tena ni kali ya karne.” Alisikika bwana Jonas Mlyanyama.

“Ehe, baada ya kuanguka nini kiliendelea?” Nikazidi kudodosa.
“Kesi yako imeahirishwa, itapangwa tena pale afya yako itakapoimarika.”
“Na yule mwanamke alielekea wapi baada ya hapo?”
“Hata sikumfuatilia.” Alinijibu na kuonekana tena kuzama kwenye lindi la mawazo.
“ Sasa subiri nikaandae hoja za kisheria za kuja kumkabili siku ya kusikilizwa tena kesi yako, labda asije.”
“Yule ni mchawi kaka sidhani kama utamuweza.”
“Pamoja na uchawi wake hapa kagonga mwamba.” Aliongea Mlyanyama huku akijipigapiga kifuani kuonyesha kujigamba fulani hivi.
“Yangu macho na masikio siku hiyo, lakini mimi nimeshamnyanyulia mikono huyo ibilisi. Nashangaa sijui kwa nini kaniandama sana na kunisababishia ndege mbaya katia maisha yangu, kanipotezea dira ya maisha kabisa, isitoshe hata hatima yangu haijulikani.” Nilijikuta nikiongea kwa uchungu huku nikionyesha kukata tamaa kwa hali zote.

“Tatizo lako wewe ni mwepesi mno wa kukata tamaa. Hebu hakikisha unapambana mpaka dakika ya mwisho.”
“Nitapambana vipi kaka wakati hali ninavyoiona inazidi kuelekea kubaya tu. Hebu jiulize hizo alama za vidole vyangu zimeonekanaje kwenye mwili wa marehemu na kwenye kisu wakati sikuwahi hata kugusa?”
“Huenda ulishika bila kijielewa kutokana na kuchanganyikiwa na tukio.”
“Hakuna kitu kama hicho kaka, mimi hata nichanganyikiwe vipi lakini huwa najielewa.”
“Basi yote hayo tumwachie Mungu, yeye ndiye atakayeamua kuwa tushindwe au tushinde hii kesi.”
“Mimi nahisi hata Mungu kashanipa kisogo, haya siyo matatizo ya kwanza kwangu, walianza wazazi wangu wakafariki, kipenzi changu Ana naye akanitoka kimzahamzaha. Haikuishia hapo tu, kaka James ambaye alikuwa ndiyo nguzo yangu ya pekee iliyokuwa imebakia, naye akafariki dunia, tena kifo cha ghafla ghafla tu.” Nilijikuta nikimshtakia Mungu kwa wakili huku machozi yakianza kunibubujika kwenye mifereji ya mashavu yangu.

Ndipo mlango ulipofunguliwa kisha askari magereza akaingia na kumtaka wakili aondoke kwani muda wa kuendelea kuongea na mimi ulikuwa umefikia kikomo.

Wakili aliniaga na kuniambia atakuja kunipa taarifa pale tarehe ya kesi yangu itakapopangwa. Aliondoka na kuniacha nikifutafuta machozi ambayo yalikuwa yameshaanza kukolea kutokana na kuyaamsha machungu yaliyokuwa yamejilaza moyoni; machungu ya kuondokewa na watu wangu muhimu katika hii dunia ambao ni wazazi wangu, kaka James na kipenzi changu Anna.

Mawazo juu ya msichana huyo ambaye nilikuwa nimembatiza jina la Ibilisi yalianza kuzunguka kunako kichwa changu. Hata hivyo sikuweza kupata jibu ni kwa nini msichana huyo alikuwa ameniandama kiasi kile.

Niliendelea na maisha ya gerezani ingawa nilikuwa ni mahabusu. Mpaka muda huo nilikuwa bado sijayazoea kabisa maisha ya huko, ilikuwa ni ngumu sana kwangu kuyazoea maisha ya huko.

Siku moja kabla ya kesi yangu kuendelea wakili alikuja kunipa taarifa. Hata hivyo alipokuja aliniambia habari nyingine ambayo ilizidi kunichanganya zaidi.

Alisema kuwa siku aliyotoka kuongea na mimi kwenye hospitali ya magereza alikutana na msichana aliyekuwa akitusumbua katika kesi hiyo. Msichana aliyekuwa amenisingizia kuwa nimeua wakati sijaua.


MH! HAYA SASA, WAKILI WA BRIGHTON ANAKUTANA NA YULE MSICHANA HATARI. JE, ALIAMBIWA NINI? USIKOSE KUFUATILIA!
 
MIRATHI YA KAKA sehemu ya 18



ILIPOISHIA SEHEMU ILIYOPITA....
Alisema kuwa siku aliyotoka kuongea na mimi kwenye hospitali ya magereza alikutana na msichana aliyekuwa akitusumbua katika kesi hiyo. Msichana aliyekuwa amenisingizika kuwa nimeua wakati sijaua.


SASA ENDELEA.......

“Nilikutana naye sokoni niliposimama kununua matunda, ndipo akaniita wakati naingia kwenye gari niondoke zangu sokoni hapo. Kusema kweli nilikuwa sijamfahamu ila alipofika kwangu alijitambulisha.” Alieleza wakili Mlyanyama.

“Akakuambia vipi?” Nikamuuliza huku nikikaa makini kusikia alichomwambia wakili wangu.
“Eti kanionya niachane na kesi yako kwa sababu hainihusu, akadai vinginevyo nitapata matatizo makubwa.”
Taarifa hiyo ilininyong’onyeza na kunifanya niishiwe nguvu.
“Hivyi huyu mwanamke ananitafuta nini mimi?” Nilimaka kwa machungu.
“Hata hivyo nilimwambia sitishiki na nikamtaka ajipange kujibu maswali yangu yangu siku atakayosimama kutoa ushahidi.”
“Lakini yule ni mtu hatari sana kaka, bora uachane tu na kesi yangu nisije nikakusababishia matatizo.” Nilimwambia wakili Mlyanyama.
“Hapana, hayo ni maneno ya vitisho tu, ameona hana hoja za kunikabili na huenda kashaambiwa jinsi ninavyowakaba maswali mashahidi wengini au huwa anakuja kinyemela na kashashuhudia.”
“Kaka mimi nimekuambia, yule msichana ni mchawi, hii kesi achana nayo tu wanihukumu yaishe.” Nilimwambia wakili huyo.

Hata hivyo wakili huyo alikataa katakata kuiachia njiani kesi yangu. Aliapa kuwa na mimi bege kwa bega mpaka pale ambapo kingeeleweka. Alikuwa na kiu ya haki kwangu mithili ya mzee Toboa katika Kiu ya Haki.

Tuliagana na kuachana huku tukisubiri kesho yake ifike ili nipande tena kizimbani kuendelea na kesi yangu. Nilizidi kupata wasiwasi juu ya hiyo kesi yangu. Kama mpaka yule wakili alikuwa kapewa vitisho na yule msichana, niliwaza bila kupata jibu ni kipi hasa alichokuwa akikitafuta msichana yule kutoka kwangu.

Kwa kweli nilikuwa na mtihani, tena mzito. Nilitamani nikutane naye uso kwa macho kisha nimuulize kinagaubaga ni nini hasa nilichokuwa nimemkosea ama ni kipi alichokuwa anahitaji kutoka kwangu.

Kesho yake asubuhi tulisombwa tena na karandinga la magereza kuelekea mahakamani. Tulipofika mahakamani mimi nilipelekwa moja kwa moja mpaka ndani kwani kesi yangu ndiyo ilikuwa inaanzia kusikilizwa.

Jaji alipoingia watu wote walisimama wakati sauti ya “kooort” iliposikika. Baada ya kutoa heshima ya mahakama watu wote waliketi, kesi yangu ikaendelea.

Upande wa mashtaka uliendelea kuleta mashahidi wake ambapo baadhi ya polisi waliokuwa wamekuja kunikamata nyumbani siku ya tukio walisimama mmoja baada ya mwingine kutoa ushahidi.

Wakili wangu hakuwa na maswali mengi sana ya kuwahoji. Yeye alichodai ni kwamba anamsubiri kwa hamu shahidi ambaye alitoa taarifa za tukio hilo kwenye kituo cha polisi. Shahidi huyo hakuwa mwingine bali ni yuleyule msichana mwenye kiinimacho.
Baada ya polisi hao kuisha wote kutoa ushahidi, msichana huyo ambaye nilikuwa simjui hata jina aliinuka na kwenda kwenye kizimba cha upande wa pili kutoa ushahidi wake.

Kama ilivyo ada, mwendesha mashtaka alimuongoza kutoa maelezo hatua kwa hatua.
“Mimi naitwa Sharifa Abdul.” Alitaja jina lake baada ya kuulizwa na mwendesha mashtaka.
“Sharifa, hebu ieleze mahakama ulikuwa wapi mnamo tarehe ishirini na moja mwezi wa kumi na moja mwaka jana muda wa jioni?” Ilikuwa ni sauti ya mwendesha mashtaka bwana Charles Ngonyani.
“Nakumbuka siku hiyo nilikuwa nyumbani kwangu Majengo mapya, ndipo nilipoamua kwenda kumtembelea kaka yangu ambaye ni marehemu Kishoka.”

“Endelea..,”
“Nilipofika alipokuwa akiishi kaka yangu huyo nilikuta milango ipo wazi.”
“Huyo kaka yako alikuwa akiishi wapi?” Mwendesha mashtaka aliuliza.
“Alikuwa akiishi mtaa wa Tumaini.”
“Alikuwa akiishi na nani?”
“Alikuwa amepanga na alikuwa akiishi na mmiliki wa nyumba hiyo.”
“Ehe, ulipokuta mlango upo wazi ulichukua uamuzi gani?”
“Kabla sijagonga nilisikia sauti ya kilio na makelele mle ndani ambapo sauti ya mtu aliyekuwa akitoa kilio niliitambua.”
“Ilikuwa ni sauti ya nani?”
“Ilikuwa ni sauti ya kaka yangu Kishoka.”
“Uliposikia hivyo ulifanyaje?”
“Niliamua kuingia mpaka sebuleni, hata hivyo makelele hayo yalikuwa yakitokea chumbani.”
“Chumba hicho kilikuwa ni cha nani?”
“Kilikuwa ni cha mmiliki wa nyumba hiyo.”
“Baada ya hapo ulifanyaje?”

“Baada ya kuuona hata mlango wa chumbani haujafungwa, nilianza kwenda kwa tahadhari kubwa kuchungulia kilichokuwa kinaendelea ndani ya chumba hicho.”
“Uliweza kuchungulia humo ndani?”
“Ndiyo!”
“Ulipochungulia uliona nini?”
“Nilichokiona sikuamini kwa macho yangu. Nilimuona kijana mwenye nyumba akimchinja Kishoka kama mbuzi wa sherehe achinjwavyo huku kamfunga kamba miguuni na mikononi.”
“Ulipoona hivyo uliamua nini?”
“Kwanza niliongopa kuongea chochote kwa kuhofia usalama wangu. Kwa bahati nzuri nilikuwa na kamera kwenye mkoba wangu, nikaitoa na kuanza kupiga picha.”

“Baada ya hapo afanyaje?”
“Nilitoka na kuondoka mbio kurudi nyumbani, wakati nikiwa njiani nilipiga simu kituoni na kutoa taarifa hizo.”
“Hizo picha ulizozipiga siku ya tukio unazo?”
“Ndiyo zimo kwenye kamera yangu hii.” Aliongea Sharifa huku akiionyesha mahakama kamera ndogo ya digitali.
“Huyo mtu aliyefanya hayo mauaji ukimuona unaweza ukamfahamu?”
“Bila shaka!”
“Hebu tuonyeshe kama mtu huyo yumo humu ndani ya mahakama!”
“Ni yule pale kwenye kizimba.” Aliongea msichana huyo huku akinisonta.


JE, WAKILI WA BRIGHTON ATAWEZA KUMKABILI KWA MASWALI MSICHANA ALIYEMUONYA AACHANE NA HIYO KESI? NA NI MADHARA YAPI ATAYAPATA KWA KUKAIDI ONYO LA MSICHANA HUYO? USIKOSE KUFUATILIA......!
 
MIRATHI YA KAKA sehemu ya 19



ILIPOISHIA SEHEMU ILIYOPITA....
“Hebu tuonyeshe kama mtu huyo yumo humu ndani ya mahakama!”
“Ni yule pale kwenye kizimba.” Aliongea msichana huyo huku akinisonta.

SASA ENDELEA.......

Mwendesha mashtaka aliichukua kamera na kuipeleka kwa jaji kisha akasema amemaliza muongozo wake kwa shahidi.
Akili yangu ilizidi kuchanganyikiwa. Ushahidi wa picha uliokuwa umetolewa na msichana huyo ulizidi kuivuruga akili yangu. Japokuwa nilikuwa bado sijaziona hizo picha lakini niliamini kabisa kuwa msichana huyo hawezi kupeleka kitu ambacho siyo cha kweli mbele ya mahakama.

“Lazima kweli kuna picha zangu kwenye kamera hiyo, lakini sasa hizo picha kazitoa wapi wakati mimi sikumuua Kishoka?” Niliwaza na kuwazua bila kupata jibu.

Wakati nikiwaza hivyo wakili wangu aliinuka na kuomba auone ushahidi wa vielelezo vya picha uliokuwa umetolewa na shahidi huyo.

Alipoletewa kamera hiyo alibaini kuwa picha hizo zilikuwa ni zangu kweli.

Naye alizidi kuchanganyikiwa. Akaomba nionyeshwe na mimi kisha akaruhusiwa. Nilipoonyeshwa nilizidi kupigwa na butwaa baada ya kuona picha zikionyesha namchinja Kishoka. Sikuamini kwa macho yangu.

Zilikuwa ni picha kama saba hivi ambazo zilikuwa katika mapozi tofauti, yote yakiwa yanaonyesha nikiwa katika hekaheka ya kumchinja Kishoka kama kuku. Nilizidi kuchanganyikiwa.

Wakili wangu aliniangalia huku akiwa amenywea kisha akatikisa kichwa. Aliondoka na kwenda karibu kabisa na kizimba cha shahidi kisha akakaa mkao wa kuanza kumhoji maswali shahidi aliyekuwa kizimbani ambaye ni Sharifa.

Hata hivyo alishikwa na kigugumizi ghafla na kushindwa kabisa kuongea. Kila alipojaribu kuongea alijikuta akigugumia na kushindwa kuyatamka maneno waziwazi.

Hali hiyo ilileta taflani kubwa ndani ya mahakama hiyo. Kila mtu akaanza kushangaa ni kwa nini wakili huyo amekuwa namna ile. Hali hiyo ilimfanya jaji aiahirishe tena kesi na kuipangia singu nyingine.

Kwa upande wangu sikushangaa sana kuona vioja hivyo kwani nilikuwa najua fika kuwa mwanamke yule ambaye alikuwa amejitambulisha kwa jina la Sharifa alikuwa anatumia nguvu za giza.

Nilirudishwa mahabusu kama kawaida, rumande sasa ikawa ni makazi yangu ya siku nyingi. Mahabusu wengine walikuwa wananikuta na kuniacha kutokana na kesi zao kufikia muafaka, wengine walikuwa wanahukumiwa vifungo na wengine waliokuwa wakishinda waliachiwa huru.

Kwangu mimi ilikuwa kila siku danadana, limeisha hili linaingia lile. Ilifikia kipindi nikachoka kabisa na maisha ya huko rumande, nikawa natamani hata kujiua lakini niliyakumbuka maneno mazito ya marehemu Anna aliyoniambia nikiwa ndotoni ya kuwa adhabu ya mtu anayejiua ni babu kubwa.

Kabla siku ya kusikilizwa kesi yangu haijafika nililetewa taarifa kuwa wakili wangu kafariki dunia. Tangu alipotoka mahakamani siku ile hakuweza tena kuongea, hata kile kigugumizi alichokuwa akipapatua siku hiyo kilibadilika akawa haongei kabisa. alikuwa ni zaidi ya bubu.

Taarifa hizo ziliendelea kueleza kwamba zilipopita siku mbili alianza kuumwa sana hatimaye akawa ameaga dunia. Habari hizo za tanzia ziliniuma sana; kumpoteza wakili Jonas Mlyanyama, mtu ambaye alikuwa makini katika kazi yake.

‘Nilimwambia aiache kesi yangu naye akang’ang’ania kuendelea kuisimamia, ona sasa yaliyomfika. Laita kama angenisikia na kuachana na hii kesi asingekufa, huyu mwanamke ni hatari sana.’ Nilijiwazia huku moyo wangu ukiwa na simanzi kubwa kutokana na kifo cha wakili Mlyanyama.

Taarifa hizo ambazo zilitoka serikalini ziliendelea kunijuza kuwa kwa wakati huo nilikuwa natafutiwa wakili mwingine tena ambaye angeendelea kunitetea katika kesi yangu hiyo. Hata hivyo niliwaambia wasihangaike kunitafutia wakili mwingine kwani yangeweza kumtokea kama yaliyomtokea Jonas Mlyanyama.

“Hii kesi ina utata mkubwa mno kwani tangu mwanzo wake ni mauzauza matupu. Mimi nawaomba msinitafutie wakili yeyote, nitaimalizia mwenyewe.” Nilimwambia mtu aliyekuwa kaniletea taarifa hizo.

“Lakini una haki kisheria kutafutiwa wakili wa kukutetea?”
“Ndiyo nina haki, lakini kwa hali ilivyo katika kesi hii sioni maana yoyote ya kusababisha watu kupoteza maisha yao kwa ajili yangu, kesi yenyewe haina hata mwelekeo mzuri.”
“Haya bwana wewe wasema, mimi nitapeleka taarifa kama ulivyotaka.” Alimalizia mjumbe huyo na kuondoka zake.



MASKINI, WAKILI WA BRIGHTON ALIONYWA ILA AKAPUUZA, SASA YAMEMKUTA MAKUBWA! NINI HATIMA YA BRIGHTON? NA NI KWA NN MSICHANA HUYO KAMUANDAMA! USIKOSE KUFUATILIA SIMULIZI HII!
 
MIRATHI YA KAKA sehemu ya 20



ILIPOISHIA SEHEMU ILIYOPITA....
“Haya bwana wewe wasema, mimi nitapeleka taarifa kama ulivyotaka.” Alimalizia mjumbe huyo na kuondoka zake.

SASA ENDELEA.......

Siku ayami zilipita, ukakaribia kuisha mwezi bila kupata taarifa zozote za kuendelea kwa kesi yangu kutoka mahakamani. Kadri siku zilivyozidi kwenda nilizidi kuingiwa na ujasiri wa kuja kukabiliana na mwanamke huyo siku tutakayokuwa kizimbani. Tena nikawa na shauku kubwa ya kumbana na kumhoji maswali, ukizingatia kauzoefu kakuhoji maswali nilikuwa nimeshaanza kukapatapata.

Nilijikuta napania kumkaba maswali ya kufa mtu mwanadada yule. Japokuwa nilijua fika kuwa uwezekano wa kuwa bubu kama ilivyokuwa kwa wakili Mlyanyama ulikuwepo. Lakini sikujali kutokana na kuchoka na vimbwanga vya mwanamke huyo.

Nikiwa mahabusu nilizidi kujipanga kwa maswali ya kwenda kumkabili huku pointi zangu nikizipangilia kiuanasheria. Nikawa nimeandaa maswali mithili ya gwiji la mawakili.

Siku moja nikiwa sina hili wala lile nilipewa taarifa kuwa kesi yangu ingesikilizwa tena wiki moja mbele. Niliingojea kwa hamu siku hiyo huku nikiamini kuja kuushangaza umati wa watu wote watakaohudhuria siku hiyo mahakamani kwa kuuliza maswali yenye mantiki na yaliyosimama kisheria.

Wiki moja haikukawia, nilitinga ndani ya kizimba cha mshtakiwa huku upande wa mashtaka ukimpandisha mwanadada Sharifa kuendelea kutoa ushahidi.

“Kwa vile shahidi alitoa maelezo siku tuliyomalizia kusikiliza kesi hii, sasa upande wa utetezi utaendelea kumuuliza maswali.” Ilikuwa ni sauti ya jaji.

Bila kuchelewa wala kuzubaa nikakohoa kidogo kuisafisha sauti yangu, na baada ya hapo nikamfakamia kwa maswali shahidi huyo.

“Ulisema jina lako unaitwa nani vile?”
“Sharifa.”
“Sharifa unaweza ukaeleza mbele ya mahakama ulikuwa na uhusiano gani na Kishoka?”
“Ni ndugu yangu.”
“Ndugu yako kivipi?”
“Kaka yangu!”
“Kabla ya hii kesi mimi ulikuwa unanifahamu?”
“Ndiyo!”
“Ulikuwa unanifahamu ki vipi?”
“Nilikuwa nakufahamu kama mmiliki wa nyumba alipokuwa amepanga kaka yangu.”
“Siku ya tukio ilikuwa ni mara yako ya ngapi kufika hapo kwangu?”
“Ilikuwa ni mara ya kwanza?”
“Sasa mimi ulinijulia wapi wakati ilikuwa ni mara yako ya kwanza kuja kwangu?”
“Nilikujulia mitaani.”
“Wakati unaniona mitaani nilikuwa na nani?”
“Ulikuwa peke yako?”
“Sasa ukajuaje kuwa mimi ni mwenye nyumba wa pale anapoishi kaka yako?”
“Nilijua tu!”
“Sharifa, nikikuambia kuwa wewe unajaribu kutunga uongo uwe ukweli nitakuwa nadanganya?”
“Ndiyo utakuwa unadanganya.”
“Ngoja nikwambie kitu, mimi Kishoka nilikuwa namjua kuliko mtu mwingie hapa, siri zake zote alikuwa akiniambia, na kati ya siri alizoniambia ni kwamba hana ndugu hata mmoja katika nchi, sasa wewe unadai kuwa ni ndugu yake kutoka wapi?”
“Labda alikudanganya, lakini mimi ni ndugu yake.” Alijibu Sharifa.
“Wewe unajishughulisha na nini?”
“Mimi ni fundi cherehani!”
“Siyo mpiga picha?”
“Siyo!”
“Siyo mwandishi wa habari?”
“Siyo!”
“Na wala siyo mtalii?”
“Nimekwambia mimi ni fundi cherehani?” Alitamka Sharifa kwa ukali.
“Usiwe mkali Sharifa. Sasa ilikuwaje siku hiyo utembee na kamera? Au ulikuwa unajua kwamba ukifika kwa Kishoka utakuta tukio kama hilo upige picha za ushahidi?”
“Mimi huwa na kawaida ya kutembea na kamera ili kuchukua matukio muhimu pale inapobidi.”
“Tulipoonana na wewe kule ufukweni siku moja kabla ya tukio la kuuawa kwa Kishoka ulikuwa na kamera?”
“Sijawahi kuonana na wewe ufukweni?”
“Kwa nini kesho yake asubuhi ulikuwa unatusumbua na Kishoka ukigonga geti na kupotea kimiujiza?”
“Sikuwa mimi?”
“Alikuwa nani?”
“Mimi sijui.”

JE, MAHAKAMA ITAMUELEWA BRIGHTON YA KUWA SIYO MUUAJI??
ENDELEA KUFUATILIA.......
 
MIRATHI YA KAKA sehemu ya 21



ILIPOISHIA SEHEMU ILIYOPITA....
“Kwa nini kesho yake asubuhi ulikuwa unatusumbua na Kishoka ukigonga geti na kupotea kimiujiza?”
“Sikuwa mimi?”
“Alikuwa nani?”
“Mimi sijui.”


SASA ENDELEA.......


Baada ya kuona msichana huyo anakikataa kila nilichomuuliza hasira zilianza kuniingia. Ghafla likaniijia swali ambalo nilijikuta namuuliza kwa mtindo wa kuropoka vile.

“Wewe ni mchawi?”
“Hapana mimi siyo mchawi.”
“Wewe ni jini?”
“Hapana mimi siyo jini.”
“Kama kweli wewe siyo jini hebu apa kwa Mungu ukisema kuwa wewe siyo jini?”
“Sasa niape ili iweje?” Aliongea Sharifa huku naye akionekana kuanza kuhamaki.
“A-aaah! Wewe hebu apa na kama siyo jini kweli hautadhurika na chochote.”
Huku nikiwa nimechachamaa kumlazimisha Sharifa akiri kwa ulimi wake kuwa yeye siyo jini, nilisikia sauti ya jaji akiingilia kati mahojiano yetu.

“Naona mshtakiwa umekosa maswali ya msingi ya kumuuliza shahidi. Kama huna swali jingine sema ili nimruhusu shahidi atoke kizimbani.”

“Mheshimiwa jaji huyu mwanamke siyo mtu wa kawaida kabisa, na sielewi ni kwa nini kaniandama mimi tu katika dunia hii. Amini nakwambia alianza kunifanyia mauzauza siku moja kabla ya kifo cha Kishoka kutokea, hata wakili aliyekuwa akinitetea kayaona mauzauza na ndiyo maana alishindwa kabisa kuongea siku ile. Alianza kwa kumuonya aachane na kesi hii na kumuonya kuwa atamfanya kitu kibaya lakini wakili huyo hakutishika.

Alipoona vile akaamua kumuua kabisa kwa kuona kwamba kakaidi, hebu muache aape kama kweli ni binadamu wa kaida, na endapo atakuwa siyo binadamu wa kawaida Mungu anaenda kumuumbua hapahapa!” Nilijaribu kujitetea kwa jaji.

“Unaswali jingine zaidi ya hilo?”
“Endapo ataapa maswali yatapatikana.”
“Shahidi, unaweza ukashuka kizimbani maana mshtakiwa hana jipya.” Alitamka jaji na kunifanya niishiwe nguvu.

Nilipotupia jicho kwenye kizimba cha mashahidi nilimuona Sharifa akiondoka kizimbani hapo na kwenda kuketi. Kitendo cha kuondoka msichana huyo bila kufanya nilichokuwa nimemtaka akifanye kiliniumiza sana moyoni.
Baada ya Sharifa kushuka kizimbani upande wa mashtaka ulimpandisa shahidi mwingine ambaye alikuwa ni miongoni mwa askari waliokuwa wamekuja kunikamata siku ya tukio.

Mpaka anapanda kizimbani na kuapishwa kisha kutoa ushahidi wake, akili yangu haikuwa katika ushahidi wake bali ilikuwa ikimfikiria Sharifa tu. Tena kichwa changu kilikuwa kimevurugika vibaya vibaya kutokana na jaji kunikatalia ombi langu kwani niliamini kuwa endapo angekuwa ni jini kweli basi angeumbuka.

Alipomaliza kutoa ushahidi wake ambao haukuwa na tofauti kubwa sana na ule uliotolewa na askari wenzake aliokuja nao kwangu siku ya tukio, jaji aliniuliza kama nina swali kwa shahidi.

Kusema kweli nilikuwa sijasikia hata neno moja alilokuwa ameongea shahidi huyo wakati anatoa ushahidi wake kwa vile nilikuwa nimezama katika lindi la mawazo juu ya Sharifa. Sasa ningeuliza nini ilhali nilikuwa sijayanyaka maelezo yake hata kidogo!

Ili kukata mzizi wa fitina nilifumbua kinywa changu na kusema kwa mkato kwamba sina swali lolote kwa shahidi huyo. Ndipo jaji alipomruhusu aende kuketi.

Baada ya hapo mwendesha mashtaka aliinuka na kumwambia jaji kuwa upande wa mashtaka ulikuwa umekamilisha mashahidi wake. Baada ya jaji kuambiwa hivyo aliniuliza kama nina mashahidi ili baraza lijalo nianze kuwaleta.

Nilichomjibu ni kwamba sina mashahidi kwani kesi yenyewe ilikuwa imeghubikwa na utata mkubwa, pia kutokana na mazingira yake jinsi yalivyokuwa.

Baada ya kumwambia hivyo jaji aliutaka upande wa mashtaka kuandaa maelezo ya mashtaka kuonyesha ni kwanini unamuona mshtakiwa anahatia kwa mujbu wa ushahidi uliotolewa. Shauri hilo liliahirishwa tena kwa mwezi mmoja.

*************************
NINI KITAENDELEA??, USIKOSE KUFUATILIA.......
 
MIRATHI YA KAKA sehemu ya 22




ILIPOISHIA SEHEMU ILIYOPITA....
Baada ya kumwambia hivyo jaji aliutaka upande wa mashtaka kuandaa maelezo ya mashtaka kuonyesha ni kwanini unamuona mshtakiwa anahatia kwa mujbu wa ushahidi uliotolewa. Shauri hilo liliahirishwa tena kwa mwezi mmoja.

*************************
SASA ENDELEA.......

Siku zilipita. Tarehe ya kesi iliwadia. Siku hiyo ilikuwa ni siku ambayo upande wa mashtaka ulitakiwa kutoa maelezo ya uchambuzi wa kisheria ya kueleza ni kwa jinsi gani inaniona mshtakiwa nina hatia kwa mujibu wa ushahidi uliotolewa.

Tayari nilikuwa nimeshapandishwa kizimbani. Ndipo nilipomuona mwendesha mashtaka amesimama kisha akaanza kutoa maelezo mbele ya mahakama ya kuwa upande wa mashtaka umeleta mashahidi walioweza kuthibitisha ya kwamba nilikuwa nimetenda kosa la kumuua Kishoka Mpoto kwa kukusudia, kitendo ambacho ni kinyume cha sheria.

Akaendelea kueleza kwamba ushahidi uliotolewa umeonyesha dhahiri kuwa nilimchinja Kishoka kwa mikono yangu nikitumia kisu kilichokutwa karibu na mlango kama ushahidi ulivyokuwa umeeleza.

Akaendelea kusema kuwa licha ya mshtakiwa kudai kuwa aliyetoa taarifa za awali hakutaka kujitokeza kituoni mara baada ya kutoa taarifa hizo, shahidi huyo ambaye alikuwa ni mwanadada huenda aliogopa kwenda kituo cha polisi kutokana na kuchanganyikiwa baada ya kushuhudia ndugu yake akiuawa kikatili ama kutokana na desturi iliyojengeka miongoni mwa waafrika wengi ya kukiogopa kituo cha polisi hata kama hawana hatia.

“Hata hivyo shahidi huyo alifanya jambo kubwa na la maana kwa kutoa taarifa kituo cha polisi.” Alizidi kueleza mwendesha mashtaka huyo ambaye ni bwana Charles Ngonyani.

Halikadhalika kuhusu madai yangu ya kudai kuwa msichana huyo alikuwa ni mshirikina au jini, mwendesha mashtaka huyo alisema kwamba hayo yalikuwa ni madai yasiyokuwa ya msingi na mantiki hivyo shahidi huyo alikuwa na haki ya kunifungulia kesi nyingine kwa kumzushia ya kwamba ni mchawi na ni jini. Pia aliongeza kwa kusema kuwa mahakama huwa haiamini imani potofu za kichawi kama mimi nilivyokuwa nikidai.

Hata kuhusu wakili wangu mwendesha mashtaka alidai kuwa wakili huyo alijaribu kufanya usanii mbele ya mahakama kwa kujifanya kashindwa kuongea kutokana na uchawi aliokuwa akisingiziwa Sharifa ili kujenga hoja yetu, lakini ukweli ni kwamba shahidi huyo alikuwa ameishiwa hoja za kisheria kutokana na ukweli uliokuwa umetolewa na mashahidi wa upande wa mashtaka.

Suala la wakili wangu kufariki dunia mwendesha mashtaka alisema kuwa hiyo ni mipango ya Mungu hivyo asisingiziwe Sharifa.
“Hivyo kulingana na mashahidi waliotoa ushahidi mbele ya mahakama hii tukufu, ni juu ya mahakama kumuona mshtakiwa ana hatia ya kuua kwa kukusudia na hivyo tunaitaka imuhukumu kifo kwa mujibu wa sheria.” Alimalizia mwendesha mashtaka na kuketi.

Niliumia sana kumsikia mwendesha mashtaka huyo akaniona mharifu na kuiomba mahakama inihukumu kifo wakati maskini wa Mungu nilikuwa sijatenda hiyo dhambi ya mauaji. Hata hivyo sikuweza kumlaumu sana kwa vile wajibu wa waendesha mashtaka ni kuwaona washtakiwa wana hatia hata kama hawajafanya makosa.

Baada ya mwendesha mashtaka kumaliza kutoa maelezo yake, jaji Aneth Mwalukwa alinitazama na kuniuliza,
“Na upande wako mshtakiwa unajibu nini?”

Nilighutuka na kujikuta mapigo yangu ya moyo yakiongeza kasi. Hata hivyo sikuwa na lolote la kuongea bali nilisema kuwa upande wa mashtaka umeniona na hatia kwa vile mauzauza hayakuwatokea wao. Laiti kama yangewatokea hata mara moja basi wangeamini yote niliyoyasema.

Pia niliongeza kwa kusema kuwa mimi sijabobea sana katika mambo ya sheria hivyo nisingeweza kutoa mapingamizi ya kishera juu ya maelezo ya upande wa mashtaka. Nilimalizia kwa kusema kuwa ni juu ya jaji kuyapima maelezo yangu na ya upande wa mashtaka.
Wakati wote huo jaji alikuwa ‘busy’ kuandika maelezo niliyokuwa nikiyatoa. Baada ya kumaliza aliniambia kuwa ninawajika kujitetea kwa kosa lililokuwa linanikabili kwani ushahidi uliokuwa umetolewa ulikuwa unaonyesha ya kwamba nimetenda kosa.

Nilianza kujitetea palepale. Niliiambia mahakama ya kuwa sikuwa na chuki na Kishoka wala hatukuwa katika mgogoro. Niliendelea kueleza kuwa tukio la kuuawa kwa kifo hicho lilinisikitisha sana kwani siku hiyo asubuhi niliagana naye na nikaenda katika mizunguko yangu.
“Ndipo aliponipigia simu muda wa jioni akiniambia kuwa kuna mgeni wangu hapo nyumbani, mgeni mwenyewe alikuwa ni yule aliyekuwa anatusumbua toka asubuhi akiwa anagonga geti wakati mimi napata kifungua kinywa.”

Nilizidi kueleza jinsi mgeni huyo ambaye kwa pale mahakamani nilikuja nikamjua jina lake kuwa ni Sharifa. Nilieleza jinsi nilivyopokea taarifa kutoka kwa Kishoka ya kuwa mgeni huyo alikuwa amekataa kuingia ndani na kunitaka niende hukohuko getini nikaonane naye.

Niliendelea kuieleza mahakama kuwa baada ya kwenda hapo getini sikukuta mtu. Kwa kirefu kabisa nilieleza mauzauza yote aliyokuwa akinifanyia msichana huyo mpaka ile jioni niliporudi kwangu na kumkuta Kishoka kashauawa chumbani mwangu.

“Mambo ya ushirikina yapo na yanatokea sana katika jamii zetu hivyo mahakama isinione kama naongea uongo.” Nilizidi kujitetea.
Mwisho wa utetezi wangu niliitaka mahakama inione sina hatia na iniachie huru kisha nikafunga kinywa changu.

Baada ya kutoa utetezi huo, jaji Aneth Mwalukwa ambaye alikuwa ni mwanamama alipanga siku ya hukumu yangu baada ya mwezi mmoja.


HAYA SASA, TAREHE YA HUKUMU YA BRIGHTON YATAJWA. JE, ITAKUWAJE? USIKOSE SEHEMU IJAYO.......
 
MIRATHI YA KAKA sehemu ya 23



ILIPOISHIA SEHEMU ILIYOPITA....

Baada ya kutoa utetezi huo, jaji Aneth Mwalukwa ambaye alikuwa ni mwanamama alipanga siku ya hukumu yangu baada ya mwezi mmoja.

SASA ENDELEA.......

Kwa namna moja au nyingine nilifurahi kusikia hivyo kwani nilikuwa na shauku kubwa ya kujua hatma ya hiyo kesi yangu. Japokuwa nilikuwa najua fika ya kwamba kuokoka kwangu ilikuwa ni bahati nasibu, kitendo cha kupelekwa mahakamani na kupandishwa kizimbani mara kwa mara kilikuwa kimeshanikifu.

Niliona ni heri hukumu yangu ikitoka, hata kama nitahukumiwa kunyongwa basi nitakaa gerezani bila bughudha siku zote za kungojea kunyongwa kwangu.

Niliteremka kizimbani na kuchukuliwa na askari magereza kwa ulinzi mkali mpaka kwenye karandinga lao kama ilivyo ada. Tulikaa kidogo kuwasubiri baadhi ya mahabusu ambao kesi zao zilikuwa zinaendelea kusikilizwa. Baada ya kukamilika wote, tuliondoka mahakamani na kuelekea magereza.

*****************************

Mwezi mmoja ulitimia tangu siku ambayo kesi yangu ilisikiliza. Hayawi hayawi hatimaye sasa yakawa, siku ya hukumu yangu iliwadia.
Mapigo ya moyo wangu yalikuwa yakinidunda kasi kuliko kawaida. Pamoja na kwamba nilikuwa naiombea siku ya hukumu ifike, siku hiyo nilikuwa nimenyong’onyea na kuwa mpole kama shilingi mia.

Usiombe kuwekwa kizimbani kwa mara ya mwisho ukisubiri hukumu, tena hukumu yenyewe ya kesi ya mauaji! Hakika nilikuwa nipo maji siku hiyo.

Nilipandishwa kizimbani huku nikiwa nimenywea pasipo mfano. Yaani ilikuwa ni tofauti kabisa na siku zingine zote nilizofika mahakamani hapo.

Jaji alianza kusoma hukumu yangu kwa kutaja kosa lililokuwa linanikabili na kutangulia kusema kuwa adhabu ya kosa hilo ni kifo endapo mtuhumia atapatikana na hatia.

Niliposikia hivyo moyo wangu ulilipuka pu kana kwamba ilikuwa ndiyo mara ya kwanza kusikia hiyo adhabu ya mtu mwenye hatia ya kuua.
Jaji huyo aliendelea kwa kusema kuwa hakuna shaka yoyote kwa ushahidi ambao ulitolewa ya kuwa nilimuua Kishoka Mpoto siku ya tukio hilo.

“Hata katika utetezi wake mshtakiwa kashindwa kutoa maelezo sawasawa ambayo yanaweza yakailinda hoja yake kuwa hajaua. Suala la kudai kuwa shahidi aliyetoa taarifa za tukio kituoni ni mchawi au ni jini haliwezi likaaminiwa na mahakama hata siku moja kwani hakuna uchawi juu ya sheria.” Aliendelea kutema maneno jaji Aneth Mwalukwa.

Aliendelea kusema kuwa ushahidi wa picha, alama za vidole kwenye mwili wa marehemu na kwenye kisu kilichokuwa kimetumika kumuulia Kishoka vilikuwa ni vielelezo tosha kabisa kunitia hatiani.

“Japokuwa sababu au chanzo cha mtuhumiwa kumuua marehemu hakijafahamika mpaka sasa kutokana na mshtakiwa kuendelea kushikilia msimamo wa kwamba hajaua, bado haiondoi dhana ya mtuhumia kupatikana na hatia ya kuua kwa kukusudia.” Alizidi kusema jaji huyo.
“Kazi yangu ilikuwa ni kuchambua madai ya pande zote mbili, lakini upande wa utetezi umeonekana kuwa na hoja ambazo hazina mantiki kabisa, hoja za kusingizia ushirikia. Katika kusoma madai ya upande wa mshtakiwa sikuona shahidi yeyote ama ushahidi wowote ulioonyesha kuwa ni kweli mtuhumiwa hajaua zaidi ya maneno matupu ya kudai kuwa tukio liliambatana na ushirikina.” Aliunguruma mwanamama huyo.

Mpaka hapo matumaini yalikuwa yameshaniishia kabisa. Nilijua fika kuwa mwisho wa hukumu yangu ni adhabu ya kifo. Huku maelezo ya hakimu hayajafika mwisho nilianza kuhisi machozi yakinilengalenga huku pua zangu zikionekana kuloa.

Jaji aliendelea kusema kuwa jambo la shahidi aliyetoa taarifa polisi kutotokea kituoni haliwezi likaleta shaka yoyote juu yake kwani jambo muhimu ambalo ni kutoa taarifa alikuwa kashalifanya. Tena kwa kuongeza ushahidi aliamua kujitokeza mahakamani na kutoa ushahidi wa picha ambao ulionyesha hali halisi ya tukio lilivyokuwa.

“Kutofika kituoni huenda kulichangiwa na woga pamoja na kuchanganyikiwa kutokana na uzito wa tukio jenyewe ulivyokuwa.” Aliendelea kufafanua jaji huyo.

Ulikuwa ni uchambuzi ambao ulichukua karibu saa moja. Jaji Aneth Mwalukwa alihitimisha hukumu yake iliyokuwa na kurasa kadhaa kwa kueleza kuwa anakubaliana na upande wa mashtaka kuwa nilikuwa nimetenda kosa la mauaji ya kukusudia dhidi ya marehemu Kishoka Mpoto.

“Kwa mujibu wa sheria za nchi yetu mtu anayepatikana na kosa hilo, adhabu yake ni kifo. Kwa hiyo natamka kwamba mahakama hii imemtia hatiani mshtakiwa Brighton David kwa kosa la kumuua Kishoka Mpoto kwa kukusudi.

Jaji alinyamaza kidogo kisha akanitazama na akuniambia,

“Mshtakiwa Brighton David nakuhukumu adhabu ya kifo, utanyongwa kwa kitanzi mpaka ufe.”

Jaji alipomaliza kusoma hukumu yangu aligonga nyundo mezani kisha akainuka na kuondoka.

Kwa kweli sikuweza kujizuia. Nilijikuta nikiangua kilio cha haja huku simanzi na huzuni zikitawala kwa watu wengi waliokuwa wamefika mahakamani hapo, wale waliokuwa wananijua na hata wale ambao walikuwa hawanijui.

Wakati jaji anaondoka mahakamani askari magereza walinishusha kizimbani na kuanza kunipeleka kwenye karandinga la magereza bila hata kunipa nafasi ya kuagana na baadhi ya watu niliokuwa najuana nao.

Kijana niliyekuwa nimemuachia kuisimamia miradi yangu alikuja mbio akitaka kuongea nami kwa mara ya mwisho, lakini bila huruma askari alinisukuma na kunitaka niingie kwenye karandinga haraka.

Gari lililokuwa limenichukua liliondoka kwa kasi ya ajabu kuelekea gerezani
**************************


HAYA SASA, HUKUMU IMESHATLEWA! BRIGHTON ATANYONGWA KWELI AU ITAKUWAJE? ENDELEA KUFUATILIA!
 
Back
Top Bottom