4
ASUBUHI hiyo, baada ya kuoga na kufungua kinywa, Joram alichukua simu na kupiga namba mbili tatu akitaka kuzungumza na rafiki zake wa zamani. Alipowapata aliwapa maekelezo fulanifulani kwa lugha ambayo wangeielewa wao tu. Baada ya hapo akajitokeza mitaani na kuanza matembezi. Akiwa kavaa vizuri suti yake ya kijivu aina ya three peace, kofia ikiwa imezifunika nywele zake ili kuficha mchubuko uliokuwa upande wa kushoto na miwani myeusi ikilificha jicho lake ambalo lilikuwa halijatii dawa kikamilifu, alionekana kama alivyotaka, mwungwana asiye na tatizo lolote mwilini wala akilini.
Msafara wake wa kwanza uliishia Barabara ya Sokoine katika tawi la Benki ya Taifa ya Biashara City Drive. Aliingia ndani na kuomba kuonana na meneja. Akaelekezwa hadi katika chumba ambamo alikaribishwa vizuri na afisa huyo ambaye uso wake ulimdhihirishia Joram kuwa hakuwa akiwajibika ili kuitikiwa wito bali kuwajibika kulikuwemo katika damu yake tangu alipozaliwa.
"Nikusaidie nini ndugu yangu?"
"Naitwa Joram Kiango. Ninayo akaunti hapa."
"Nakufahamu sana, ingawa ni mara yangu ya kwanza kukuona ukija huku kwetu. Mara nyingi unaishia huko huko kwenye pesa." Baada ya kutabasamu kidogo kwa mzaha huo aliongeza harakaharaka. "Umefuata mkopo?"
"Hapana mzee," Joram alimjibu. "Nikikopa nitashindwa kulipa. Ninachohitaji ni kutazama uwezekano wa kuweka mali yangu fulani ya thamani katika akaunti mnayoita Self-Custody. Ningependa mnifahamishe utaratibu ulivyo."
Meneja alitikisa kichwa huku akisema, "Hilo tu? Kwanini wamekusumbua hadi huku? Utaratibu wake si mrefu sana. Ziko fomu maalumu ambazo utajaza. Baada ya hapo utakabidhiwa ufunguo mmoja, ufunguo wa pili tutakuwa nao. Utakwenda huko chini na kuhifadhi mali yako hadi siku ambayo utapenda kuikagua au kuichukua. Malipo yake ...."
Joram alimsikiliza kwa makini, akitupa swali moja moja. Kisha alimwomba meneja akatazame hali ilivyo huko chini kabla hajajaza fomu zozote. Meneja akainuka na kushuka nae hadi shimoni. Walipita vyumba vya kuhifadhi nyaraka, baadhi vinahifadhiwa pesa na kimoja alielezwa kuwa kiliazimwa na Benki Kuu baada ya jengo lao kuharibika kwa moto. Baada ya kupewa picha kamili ya ulinzi na usalama wa hifadhi hiyo Joram aliaga na kuahidi kuwa angerudi baadaye kukamilisha kazi hiyo.
Toka hapo Joram alipita hapa na pale akifanya hili na lile, sigara baada ya sigara zikiteketea mdomoni, mwendo wake ukiwa wa utulivu kama mtu asiye na tatizo lolote ulimwenguni. Ungemwona kamwe usingefikiria kama mtu ambaye usiku wa jana mpenzi wake alitekwa nyara, bila shaka baada ya kuteswa sana.
Ni hali yake hiyo ya utulivu ambayo ilimshangaza Inspekta Kombora alipokutana nae katika mtaa wa Samora. Kombora alisimamisha gari lake na kumfuata Joram kando ya duka alipokuwa kasimama. "Joram," alisema baada ya kumsalimu. "Nasikia yule msichana wako ametekwa nyara".
"Hata mimi nasikia hivyo," lilikuwa jibu la Joram.
"Mbona hufanyi lolote."
"Nifanye nini? Barua imenionya nisithubutu kufanya lolote. Vinginevyo, msichana wa watu atauawa. Unapenda afe, Inspekta?"
Kombora alitikisa kichwa kwa mshangao. "Joram niliyemfahamu mimi alikuwa hapokei amri kwa watu kama hao, hasa katika suala hili ambalo ni la uhai na kifo cha mtu na taifa zima. Mimi nilidhani wamekuchokoza. Nikategemea kuwa wangejutia uamuzi wao. Nilikosea?"
"Umekosea sana Inspekta. Joram unayezungumza naye si yule wa awali. Usishangae, Inspekta. Usiupoteze bure mshangao wako. Bado kuna mengi utayasikia juu ya Joram huyu ambayo yatakushangaza zaidi," Joram alisema huku akitupa kipande kimoja cha sigara na kuwasha nyingine. Alipomuona Kombora kama mtu ambaye hajui la kufanya au asiyeyaamini masikio yake, akaamua kuondoka polepole. Kombora alimsindikiza kwa macho yake yaliyojaa mshangao na huzuni.
Baada ya pitapita hii ya hapa na pale, Joram alirejea chumbani kwake ambako alijipumzisha kwa muda.Wafanyakazi na baadhi ya wapangaji wenzake, ambao walikuwa wamemzoea Nuru, walimsumbua Joram kwa kutomuona.
"Anaumwa?"
"Hapana. Kapata safari ya ghafla."
"Bila kuaga?"
"Ilikuwa ghafla."
Aliujenga vyema uongo wake huo hadi ukafanana na ukweli. Jioni hiyo, baada ya kula, kuoga na kupiga simu nyingine alijitokeza mitaani na kuanza matembezi yake. Safari hii matembezi hayo yaliishia Ilala, nyumbani kwake. Alielekea chooni ambako alifunua mahala fulani pa siri ukutani na kutoa kijisanduku alichokuwa kakificha hapo. Alishangaa kukuta kikiwa kitupu bila ya bastola na risasi zake ambazo alikuwa ameziweka huko. Hifadhi hii ilikuwa siri yake binafsi. Mtu pekee ambaye aliifahamu siri hiyo ni Neema Idd ambaye sasa ni Marehemu. Mtu mwingine ambaye angeweza kufahamu ni Nuru. Uko usiku mmoja, kati ya zile chache ambazo waliwahi kulala katika nyumba hii, alimtoroka Nuru akidhani yuko usingizini, akaja hapa na kuisafisha bastola hii. Pengine Nuru aliwahi kumchungulia. Lakini Nuru huyo sasa yuko mikononi mwa wateka nyara. Nani mwingine aliyeijua siri hii? alijiuliza kwa hasira, hasira ambazo zilimfanya atupe kasha hilo na kutoka nje baada ya kuifunga milango yote kwa ukamilifu. Msafara huu uliishia katika hoteli ya Embassy. Akaagiza vinywaji na kuanza kunywa. Baada ya bia mbili akaenda kaunta kuzungumza na yule msichana wa mapokezi.
"Shem, za kutwa."
"Nzuri sana, shemeji," msichana huyo alizungumza kwa furaha huku akimtazama Joram kwa mshangao. "Pole sana shemeji," aliongeza.
"Kwa?"
"Ule mchezo wa jana. Unajua mimi mpaka sasa siamini kama mlikuwa mnacheza tu. Nilidhani mlikuwa mnapigana. Yule bwana kashikilia kuwa ni mchezo tu".
"Ulikuwa mchezo. Mazoezi ya viungo. Wazungu huita practice."
"Mpaka mtoane damu?"
Hakujua Joram alivyoisherehekea habari hiyo. Alitupa maneno mengine mawili matatu, kisha akairudia meza yake. Akaendelea kunywa na kuvuta. Japo alionekana katika hali ya utulivu, lakini macho yake yalikuwa makini, yakimtazama kila anayeingia na kutoka. Aliwaona wengi. Na kati yao alikuwemo yule ambaye alihitaji kumwona.
Alikuwa rafiki au adui yake, Chonde. Aliingia na kuifuata meza ambayo haikuwa na mtu, akaketi. Mara tu Joram alipomwona akainuka na kwenda kupiga simu ambayo alizungumza maneno machache sana. Kisha alikirudia kiti chake na kumwita mhudumu ambaye aliombwa kuleta bia nne. Mhudumu huyo alipozifikisha chupa hizo Joram alimwelekeza azipeleke kwa Chonde. Kisha alitulia akimtazama Chonde alivyokuwa akibishana na mtumishi huyo kwa zawadi hiyo ambayo hakujua ilikotoka hadi alipoelekezwa na kumwona Joram. Akazipokea na kuanza kunywa.
Lakini baada ya dakika kumi meza ya Joram ilifurika kwa chupa kumi zilizoletwa na mtumishi yuleyule kwa niaba ya Chonde. Walitazamana kwa muda. Baada ya muda Chonde alihamia meza ya Joram.
"Za tangu jana?"
"Siyo mbaya."
Wakaendelea kunywa kwa muda. Kila mmoja akimsoma mwenzake. Kisha Chonde alitokwa na kicheko chembamba. Joram aliungana naye kwa tabasamu dogo.
"Pole sana."
"Kwa?"
"Yale ya jana."
"Lilikuwa zoezi tu. Usijali."
Kikafuata kimya kingine, kimya ambacho Joram alikivunja kwa kuanzisha maongezi ambayo Chonde alizungumza kwa uangalifu akiepuka lolote ambalo Joram alihitaji kufahamu juu yake. Pamoja na Joram kuzungumza kwa ujanja na hila za kila aina, bado Chonde alimfanya ajione mtoto sana katika dunia ya upelelezi na mzembe katika elimu ya saikolojia. Ni hapo alipozidi kuamini kuwa Chonde hakuwa mtu wa kawaida. Na kama alikuwa jasusi bado hakuwa jasusi la kawaida. Alikuwa zaidi. Jambo hilo liliongeza hasira za Joram dhidi ya mtu huyo. Amshinde vipi katika mapambano ya mwili na amshinde tena katika mapambano ya kiakili? Hata hivyo Joram hakujali sana, akijua kuwa dakika hii ambayo anaipoteza na Chonde, mahala fulani, yuko mtu ambaye anaifanya kazi ile ambayo yeye alishindwa kuifanya jana, kazi ya kufungua kile kijaluba cha Chonde na kuona kimehifadhi nini hata kilindwe kwa kiwango kama kile. Hivyo, akaamua kumruhusu Chonde aendelee kumlaghai na kumdhihaki.
"Mwanamapinduzi aliyekata tamaa," Chonde alisema. "Aibu ilioje kukata tamaa hali nchi yako iko mashakani? Si ungejaribu kutoa mchango wako?"
Joram hakumjibu.
Kisha kama aliyekumbuka jambo Chonde alisema ghafla, "Nasikia msichana wako ametekwa nyara!"
“Umesikia wapi?"
"Kwani ulidhani siri?"
Hilo lilimshitua Joram. Alishangaa kuona mtu huyo alivyo mwepesi wa kupata habari. Baada ya kuisoma barua ile Joram hakuipeleka polisi wala kuchukua hatua zozote zaidi ya kutabasamu tu. Lililomfanya asifanye lolote hasa ni kule kuwa kwake na uhakika kuwa barua ile aliielewa zaidi ya mwandishi wake alivyotaka aielewe. Bila shaka mtu huyo alikuwa amezidokoa habari hizo kwa polisi. Jambo hilo lilimfanya azidi kumfanya Joram kuamini kuwa hakuwa mtu mwenye mkono mrefu tu bali alikuwa na masikio mapana.
Yeyote aliyeketi kando akiwatazama watu hawa wawili wakiongea angeamini kuwa ni kikao cha marafiki wa siku nyingi. Asingeamini kuwa yalikuwa kama maongezi baina ya Chatu na Mbwa, au baina ya Malaika Gabriel na Ibilisi.
Yule msichana wa mapokezi alikuwa mmoja kati ya watu walioamini hivyo. Alikuwa amewatazama kwa muda mrefu na kushuhudia wanavyocheka na kutabasamu, akayasahau mashaka yote aliyokuwa nayo juu ya urafiki wao na kuamini kuwa pambano la jana lilikuwa zoezi la viungo. Hivyo, alizama katika shughuli zake na kuwatupia jicho mara moja moja.
Chonde alikuwa akifunua mdomo kuongea kitu wakati saa yake ilipotoa mlio ambao haukuwa wa kawaida. Ulikuwa mlio wa sauti nyembamba sana, ulimfikia Joram kwa mbali sana. Chonde aliitazama saa hiyo kwa utulivu, kisha alimtazama Joram kwa makini zaidi. Dakika mbili baadae aliendelea kunywa kwa utulivu. Dakika ya tatu aliinuka na kuaga kuwa anaelekea msalani. Joram alisubiri dakika tano, kisha akamfuata. Hakumkuta. Akafahamu kuwa mlio katika saa ya chonde ulikuwa ishara ambayo ilimkumbusha kitu fulani, jambo lililomfanya Joram kuhofia mtu wake ambaye wakati huu alikuwa katika chumba cha Chonde. Hivyo, akakiendea kibanda cha simu na kuzungusha namba za simu za chumba hicho. Haikupokelewa. Toka kwenye simu, Joram alitoka nje ya hoteli na kukodi gari ambalo lilimpeleka New Afrika. Akajipenyeza kwa hila hadi ghorofani, mbele ya chumba hicho. Akatega sikio na kusikiliza kwa makini. Chumba kilikuwa kimya kabisa. Ukimya huo ulimtisha sana. Aliyaamini sana masikio yake. Na kwa vyovyote alitegemea kuwa na mtu chumbani humo. Akasikiliza kwa makini zaidi. Bado hakusikia chochote. Akaufungua mlango taratibu na kuchungulia.
Macho yake yalivutiwa na mtu aliyelala chali juu ya sakafu utumbo wake ukiwa nje, macho yake yakidhihirisha kuwa roho ya mtu huyu pia ilikuwa nje. Kabla Joram hajajua kuwa ilimpasa kuingia chumbani humo au la, sauti nzito aliyoifahamu sana ilimhimiza ikisema, "Usiogope. Karibu ndani."
Msemaji alikuwa kajificha nyuma ya mlango, bastola kubwa ikiwa mkononi mwake ikimtazama Joram kwa uchu.
"Ingia na ufunge mlango. Nadhani hutapenda kufia hapo mlangoni kama paka. Njoo ndani ufe kistaarabu kidogo."
Joram akaingia. Hakujishughulisha kumtazama Chonde aliyesimama nyuma ya mlango na bastola yake. Badala yake alimtazama marehemu na kushuhudia alivyouawa kinyama. Tumbo lake lilikuwa limebomoka kwa kitu ambacho hakikuwa risasi wala kisu. Bila shaka ulikuwa mlipuko wa bomu. Kifo hicho kilimsikitisha sana Joram. Huzuni ikamshika. Kwa huzuni hiyo alimgeukia Chonde na kufoka kwa hasira akisema, "Shetani mkubwa. Kwa nini umemwua mtu huyu asiye na hatia?"
"Ni wewe uliyemwua," Chonde alimjibu Joram.
"Mimi! Nimemwua vipi?"
"Usijifanye hufahamu. Bila shaka ni wewe uliyemtuma kuifanya kazi ile ambayo mwenyewe ilikushinda. Kazi ya kujua katika kisanduku hicho mna nini. Nami nikifahamu kuwa pamoja na kukuadhibu, kama nilivyokuadhibu usiku wa jana usingekata tamaa ndipo niliamua kutega bomu dogo kando ya kisanduku hicho. Wakati huohuo mtu yeyote anayekigusa saa yangu inaniashiria. Hivyo tulivyokuwa tukinywa hapo hotelini nilishangaa kuona dalili za mtu.
“Nikafahamu kuwa mtu asiye na hatia anakufa. Nimemkuta kisha kata roho.” Akageuka kumtazama marehemu kwa muda. Kisha aliyarejesha macho katika uso wa Joram na kusema, "Ni wewe uliyestahili kuwa chali, utumbo nje, badala ya mtu huyu, Joram.”
Joram asingeweza kukanusha. Kifo cha kijana huyo kilimsikitisha sana. Alikuwa mmoja kati ya vijana wake smart ambao huwatumia kwa hili na lile, kijana ambaye alikuwa amemsaidia sana katika harakati zake zilizopita. Hakupata kushidwa hata mara moja isipokuwa leo ambapo ameyapoteza maisha yake. Joram akajilaumu kumtuma katika kadhia hiyo. Hamu yake ilikuwa ni kumshinda na kuutawanya ubongo wake sakafuni...
Kama aliyekuwa akiyasoma mawazo yake, vilevile Chonde aliongeza kwa sauti nzito, "Hata mimi sikufahamu kama wewe ni mtu hatari sana Joram. Unastahili kufa mara moja."
Maisha yakiwa ukingoni, Joram alijua kuwa alihitaji kuikusanya akili yake yote ili ajiokoe. Hakujua afanye nini. Walikuwa na bastola moja tu, na ilikuwa katika mikono ya Chonde. Kuipata bastola hilo ilikuwa ndoto ya mchana. Chonde alikuwa macho kama kipepeo. Na bado Joram asingemudu kuitumia mikono yake. Hata hivyo, alitegemea kitu kimoja tu kimsaidie kutafuta muda wa kuokoa maisha yake. Muda. Muda waweza kufanya maajabu. Hata asipookoka, si inapendeza endapo ataufaidi uhai wa dakika chache zaidi.
"Najua ninakufa," alisema. "Nadhani unafahamu vizuri kuwa nakufa kwa ajili ya tamaa ya kutaka kujua siri uliyoificha katika kijisanduki hicho. Nifanyie basi wema wa mwisho. Nifungulie kisanduku hicho nife nikijua mna nini."
Chonde alicheka, "Tatizo lako Joram ni kule kufikiria kuwa unacheza na mtoto mdogo. Unachojaribu kufanya ni kuvuta muda. Wakati huohuo unathubutu kuendelea na upelelezi wako ili endapo lolote litatokea - kitu ambacho siamini - utoroke na kutoa siri hiyo nje. Kwa taarifa yako siri iliyoko katika kisanduku hicho ni nzito kuliko bara zima la Afrika. Kwa maneno mengine, ni siri ambayo dunia nzima inapigania kujua. Kwa bahati mbaya watu tunaoifahamu siri hiyo ni wachache sana. Na tumeshona midomo. Hata maiti siwezi kuisimulia siri hiyo. Nadhani hilo linakutosha. Sasa jiandae kufa. Ungependelea risasi ya kichwa au kifua?"
Joram alimtazama usoni na kuliona tabasamu la kifedhuli katika macho yake, tabasamu ambalo halikuwa na mzaha. Akajaribu kuicheza tena karata yake ya mwisho. "Jana ulinishinda kwa judo. Vipi ukiniua kwa mikono? Nadhani ni aibu na dalili za uoga kutumia risasi pasipo na umuhimu."
Chonde alicheka tena. "Ningependa kukuua kwa mikono mitupu. Hata hivyo, sina muda wa kutosha. Umebakiwa na nusu dakika ya kuishi. Utapenda kufa ukiwa umefumba macho au nikuue ukinitazama?"
Sasa mzaha ulikuwa mbali na sauti ya Chonde. Mauaji yalikuwa wazi katika macho yake. Joram akajua kuwa maisha yake yamefika ukingoni. Akiwa ameshuhudia vifo vingi vya risasi alitabasamu kimoyomoyo na kuamini kuwa hatimaye zamu yake imefika. Hata hivyo, bado aliyapenda maisha. Bado aliipenda dunia. Na alikuwa akiiacha moja kwa moja. Hivyo, badala ya kuyafumba macho yake aliyafumbua kwa nguvu na kuyakaza usoni. Hiyo pia aliifanya kuwa karata yake ya mwisho kwani kuua si mchezo, hasa kumwua kiumbe asiye na uwezo wa kujitetea.
Ilimsaidia. Nusu ya dakika ilipita Chonde kaielekeza bastola katika kifua cha Joram, kidole chake kikigusa kiwambo cha kufyatulia risasi, lakini alisita kuifyatua. Mara mlipuko wa bastola ukasikika. Joram alijirusha kando na kutua chini ambapo aliruka tena hadi upande wa pili wa kitanda. Risasi mbili tatu zaidi zikasikika, kama zinazopigwa bila shabaha yoyote. Kisha kimya kikafuata. Kimya hicho kilitoweka kwa mkoromo wa mtu aliyekuwa akikata roho. Ndipo Joram alipojiinua na kuchungulia. Ikamshangaza kumuoa Chonde kalala chini, kifudifudi, damu zikimvuja katika tundu kubwa la risasi katika uso wake. Joram alichupa na kuirukia bastola iliyokuwa mikononi mwa Chonde. Akajicheka kwa kuona akipokonya bastola kutoka katika mikono ya marehemu aliyekata roho kitambo. Akaikimbilia suit case ya chonde pamoja na kile kisanduku. Akavichukua na kuanza kutoka.
Mara mlango ulifunguka ukifuatwa na bastola ambayo ilichungulia kwa uangalifu. Bastola ikaingia ikifuatiwa na binadamu ambaye aliufunika uso wake kwa kofia kubwa na miwani. Alikuwa kavaa suruali na koti la kiume katika hali ambayo ingemfanya mtu yeyote amfikirie kuwa pande la mwanamume. Lakini Joram alimfahamu mara moja. Akaitelemsha bastola yake ambayo aliishika na kumkimbilia huku akisema kwa furaha, "Nuru nawezaje kukushukuru Nuru?"
Walikumbatiana na kubusiana kwa furaha.
Kisha walitengana mara moja na kutazamana. "Umewezaje kunifahamu mara moja kwa urahisi kiasi hiki? Tangu nimetoweka watu wanashindwa kunifahamu".
"Nadhani nakufahamu zaidi ya wanawake wote. Zaidi ya hayo nani mwingine ambaye anaweza kuhatarisha maisha yake kuipenyeza risasi katika tundu la ufunguo ili kumwua mtu ambaye alikuwa tayari kuniangamiza? Kwa kweli sijui namna ya kukushukuru Nuru!"
Wakakumbatiana tena.
"Nuru! Niliwahi kukwambia kuwa u mzuri? Niliwahi kukuambia kuwa hawakukosea waliposema kuwa wewe ni binadamu aliyekuja duniani kwa makosa badala ya kuwa malaika kama ulivyokusudiwa? Nadhani walikosea Nuru. Wewe ni malaika. Tazama ulivyo mzuri! Tazama ulivyotokea na kuipokonya roho yangu kutoka katika kinywa cha mauti. Nuru, nawezaje kukushukuru Nuru?"
Hayo yalipita katika kichwa cha Joram wakiwa wamekumbatiana. Joram alitamani kuyatamka kwa sauti, lakini hakufanya hivyo. Badala yake alisema, "Nakupenda."
Ilikuwa mara ya kwanza kwa Nuru kumsikia Joram akilitamka neno hilo. Mara kwa mara alimtesa kwa kutojua kama kweli alimpenda au la. Ingawa walifanya mapenzi, mara nyingi, lakini bado Joram hakuwahi kulitamka neno hilo kwa sauti ambayo ililipa uzito kama huo. Kadhalika, macho yake hayakufichua mapenzi yake kwa hali yoyote. Hivyo, kwake ilikuwa zaidi ya habari njema. Hata hivyo, bado alikuwa na la kusema. "Sikuamini Joram," alimnong'oneza. "Pamoja na kutoweka kwangu nikiwa nimetekwa nyara hukujishughulisha kunitafuta. Walao kutoa taarifa polisi."
Joram akaangua kicheko. "Usinichekeshe Nuru. Waweza kuwa ulifanikiwa kuwalaghai watu wote pamoja na polisi, lakini mimi hukunidanganya. Nilijua kuwa ilikuwa hila uliyoiandaa tu ili unishawishi kuingia katika vita. Mwandiko wa barua ile pamoja na kuuvurugavuruga, kwa mtu aliyesomea miandiko kama mimi, nilifahamu kuwa ni wako. Vilevile ile damu iliyodondoka pale haikuwa na uzito wowote. Nilijua umejikata kidole makusudi. Na ile vurugu iliyofanyika chumbani haikuwa na umuhimu. Kwa vyovyote, majasusi khatari kama hawa wasingefanya mchezo usio na umuhimu kama ule. Hivyo, nilikuwa nikikusubiri nikitegemea utokee na tuendelee na starehe zetu."
"Starehe?" Nuru aliuliza kwa mshangao. Alishangaa kuona Joram alivyoigundua hila yake kwa urahisi. Ilimshangaza zaidi alipodai starehe wakati wamesimama kando ya maiti mbili ambazo zilikuwa hata hazijapoa kwa ajili yao. "Starehe Joram? Nilidhani tumeingia kazini."
Joram akatabasamu. "Sikia Nuru, siyo tabia nzuri kuzungumza kando ya maiti za binadamu. Pamoja na kwamba bastola zilizotumika zilikuwa na viwambo vya kupoteza sauti bado mtu yeyote anaweza kutokea na kutukuta katika hali hii. Nasi hatuna muda wa kuyajibu maswali ya polisi. Twende zetu mara moja," alimaliza akiichukua mizigo yake na kuanza kutoka. "Nifuate. Twende kwa utulivu kama tutokao chumbani kwetu."
"Kumbuka tu wanaume wawili," Nuru alisema akitabasamu.
Waliteremka na kuiacha hoteli bila ya tatizo lolote. Watu wawili watatu waliokutana nao waliwatazama kikawaida.
Baada ya kuingia mitaani Nuru aliifichua bastola na kumpatia Joram akisema. "Chukua bastola yako. Samahani kwa kuichukua bila idhini yako. Nadhani uliihitaji sana. Ningeweza kukupotezea maisha."
Tabasamu likamtoka Joram. "Hata hivyo umeniokoa. Kama ningeingia nayo pengine Chonde angeniua kwanza na kunisimanga baadaye," Joram alijibu. "Nimepata nyingine. Hii umeipataje?"
"Nilienda kwako kuichukua".
"Na umewezaje kunusa kuwa niko katika chumba kile nikisubiri kufa hata ukaja kuniokoa?"
"Ni rafiki yako aliyekuokoa. Hayati Edward ambaye, kwa bahati mbaya, mshenzi yule amemwua. Unajua nilipotoka hotelini kwa kisingizio cha kutekwa nyara, nilienda kujificha kwake? Tulijadiliana nae namna ya kurudisha moyo wako katika msimamo unaotakiwa. Mara ukampigia simu na kumpa maelekezo ya kwenda kufungua kisanduku hicho. Aliponieleza maelezo yako na jinsi ulivyoponea chupuchupu mara ya kwanza ndipo nilijua kuwa umerudi kazini. Nilitaka nije kwako mara moja. Lakini yeye aliniomba nisifanye pupa. Akaniomba nifuatane nae katika hoteli na kujificha kando nikimlinda. Nilifanya hivyo. Mara nikaona mtu mwenye dalili za kikafiri akiingia chumbani humo, bastola mkononi; ingawa ilifichwa sana. Kabla sijafahamu la kufanya nilikuona wewe pia ukinyatia na kuingia. Ndipo nilipojivuta mlangoni na kuchungulia katika tundu la ufunguo. Nikamwona Chonde akiwa tayari kukuua. Sikuwa na la kufanya zaidi ya kumlenga na... na ..."
Mara Nuru aliangua kilio. Akamgeukia Joram na kumkumbatia kwa nguvu akisema, "Nimeua mtu... Nimeua mtu, Joram..."
"Watu huuawa," Joram alimnong’oneza. "Hebu jitahidi kuwa msichana shujaa kama ulivyo, Nuru. Usingemwua angeniua. Watu watakusikia. Twende zetu chumbani."
"Lakini nimeua, Joram... nimeua..."