nameless girl
JF-Expert Member
- Apr 22, 2012
- 4,195
- 2,675
1
KAMA maji ya bahari ya hindi yangekuwa na hisia, basi yangejisiskia fahari sana kwa kupata fursa nyingine ya kuiburudisha miili ya viumbe hawa wawili ambao walikuwa wakiogelea kandokando ya ufuko huku wakicheza na kucheka. Walifanya picha ya kuvutia sana, hasa sura zao nzuri zilipoibuka na kutoka majini na kumezwa na tabasamu lililosababishwa na mzaha waliokuwa wakifanyiana chini ya maji. Baada ya kuogelea kwa muda walirejea nchi kavu ambako walijibwaga juu ya mchanga ulioruhusu joto likaushe maji miilini mwao.
Ufuko pia ungekuwa na kila sababu ya kusheherekea johari ya kulaliwa na viumbe kama hawa kwani walioana kimaumbile kama pacha, ingawa hawakuwa mtu na dada yake. Walikuwa kama jozi ya kiatu cha kiume kwa cha kike. Mwanamume hakuwa mwingine zaidi ya yule kijana mwenye umbo refu, kakamavu, lililokaa kiriadhariadha na sura nzuri, yenye dalili zote za hekima, ushujaa na ucheshi. Kwa jina anaitwa Joram Kiango.
Naye msichana alibahatika kupewa umbo lenye kila kitu ambacho msichana anahitaji kuwa nacho, wakati huohuo akiwa na kile ambacho mvulana legelege asingekuwa nacho. Ni yule ambaye akutazamapo ungependa aendelee kukutazama, achekapo unafarajika, atembeapo unaburudika, yule ambaye kuna madai kwamba alikuja duniani kwa makosa baada ya kuumbwa ili awe malaika. Kama madai hayo si kweli, basi yako mbali sana na uongo. Hata jina lake halikutofautiana sana na sura yake. Wanamwita Nuru.
Baada ya kuhakikisha kuwa miili yao ilikuwa imekauka, wakajifuta vizuri; kisha wakayachukua mataulo yao na kwenda kwenye gari lao. Macho ya watu wengi, Waswahili kwa watalii ambao walikuwa katika ufuko huo, hayakukoma kuwafuata. Kutazamwatazamwa, hasa wanapokuwa pamoja, halikuwa jambo geni tena kwao. Mara kwa mara macho ya kiume yalimwandama Nuru, hali ya kike yakimfuata Joram, kila mahala walipopita. Walijifunza kuyazoea hata wakaanza kusahau kuwa wanatazamwa. Hivyo, walipolifikia gari waliingia na kulitia moto wakilielekeza mjini kwa mwendo usio wa haraka.
Hawakuwa na sababu yoyote ya kufanya haraka. Ratiba yao ya starehe ilikuwa ikielekea kwisha mapema zaidi ya walivyokusudia. Walikuwa wamekubaliana wakae katika miji yote mashuhuri hapa nchini kwa muda wa wiki nzima kila mji. Lakini hii ilikuwa wiki ya pili tu na tayari walikuwa wameishi Zanzibar, Moshi, Arusha, Dodoma, Mwanza na kujikuta wamerejea Dar es salaam. Kila mji waliuona unakinaisha baada ya siku mbili tu. Maisha ya hotelini waliyaona yanawafaa watu wavivu, nazo mbuga za wanyama ziliwasisimua watalii, ilihali miji iliwaridhisha wenyeji, na safari za hapa na pale zilikinaisha.
Hivyo, ingawa walirejea Dar es Salaam na kuendelea na starehe zao wakiishi katika hoteli ya Kilimanjaro na ingawa waliendelea kucheza na kucheka, na hakuna aliyetamka neno, lakini bado haikuwa siri tena kuwa maisha ya kula, kulala… kula tena, kulala tena yalianza kuwachosha. Maisha hayo yalianza usiku ule ambao Joram Kiango asingeweza kuusahau, usiku ambao hadi leo unamtia maumivu moyoni kila anapokumbuka alivyodhulumiwa haki na wajibu wake wa kuitia risasi katika kichwa cha Proper, yule katili ambaye, pamoja na kuwaangamiza watu wengi wasio na hatia, alimwua Neema Iddi kinyama. Ni siku hiyo ambayo Joram aliitupa bastola yake na kuamua kuishi kivivu kama wanavyoishi watu wengine. Msichana huyu Nuru alihusika sana katika mkasa huo ambao tayari mtu mmoja aliuandikia kitabu na kukiita SALAMU TOKA KUZIMU. Nuru alishindwa kuachana na Joram na hangeweza kustahimili kumwona Joram akiteseka na msiba huo peke yake.
Alimfuata na kumsihi hata palipopambazuka wakajikuta wako pamoja, juu ya kitanda kimoja.
Tangu hapo hawakuachana, Joram hakuwa mtu anayeweza kuachwa kirahisi. Naye Nuru kadhalika, alitofautiana sana na wale wanawake wazuri ambao uzuri wao ni pale wanapokuwa wamevaa nguo tu. Alikuwa na mengi ambayo aliyatenda kwa nia moja tu; kumfariji Joram naye Joram alijikuta akianza kujisamehe. Lakini asingeweza kusahau…
***
Walipowasili chumbani mwao walijipumzisha vitandani mwao kwa muda huku wakilainisha koo zao kwa vinywaji vitamu. Kisha wakafuatana bafuni na kuyaondoa maji ya chumvi miilini mwao kwa kuoga vizuri kwa sabuni. Baada ya hapo walikwenda katika chumba cha maakuli ambapo walikula na kujiburudisha kwa vinywaji vikali na maongezi laini.
Akiwa katika vazi lililomkaa vema, suti ya kijivu iliyooana na viatu vyeusi kama kawaida, alikuwa tishio kubwa kwa wanaume waliokuja na wasichana wao. Hata hivyo, walijifariji kwa kujua kuwa asingekuwa “mwendawazimu” wa kuvutwa na yeyote kwani aliyeketi nae hakuwa msichana wa kawaida. "Kwanini watu kama wale wanaishi hapa bongo?" mtu mmoja alimnong'oneza jirani yake. "Tazama wanavyopendeza! Wangeweza kwenda zao nje na kutajirika sana endapo wangecheza mchezo mmoja tu wa sinema"
"Kweli kabisa," aliungwa mkono. "Hata maumbile yao yanafikiana. Yule dada anatosha kabisa kumtia mwanaume yeyote wazimu kiasi cha kumfanya auze nyumba.”
Maongezi hayo hayakumfikia Joram wala Nuru. Lakini alikwishazoea kuyasoma katika macho ya watazamaji wake. Hivyo, alitabasamu kidogo na kuagiza kinywaji kingine. Nuru alikuwa akiongea neno. Joram aliitika bila kumsikia. Waliendelea kunywa kwa muda hadi walipoamua kuwa wametosheka. Ndipo walipofuatana katika ukumbi wa muziki ambapo walisikiliza muziki na kucheza kwa saa kadhaa. Walipokinai walikiendea chumba chao ambacho kiliwalaki na kuwapa usiri. Katika usiri huo, kwa mara nyingine, miili yao iliburudika na kusherehekea afya zao.
Kesho yake, baada ya kifungua kinywa walitazamana katika hali ya kuulizana siku hiyo waitumie vipi. Nuru aliweza kuzisoma dalili za kuzikinai ratiba zao ambazo zilikuwemo katika macho ya Joram. Ingawa walikuwa wakistarehe na kujiburudisha furaha, ilikuwa dhahiri kuwa burudani hizo, kama zilikuwa zikiuburudisha mwili wa Joram, kamwe hazikuwa zikiburudisha akili yake. Ingawa uso wake ulitabasamu mara kwa mara, lakini roho yake iliwaka kwa hasira kali dhidi ya adui zake, adui wa taifa na maendeleo ya jamii, adui ambao walifanya maovu mengi yasiyokadirika na kumtia lile donda la rohoni kwa kumuua kikatili msiri wake mkuu, Neema. Kwa dhamira ya kumsahaulisha Joram uchungu huo ndipo Nuru akajitoa kwake mwili na roho. Lakini ilikuwa dhahiri kuwa jeraha hilo lilikuwa bichi katika roho ya Joram, na lisingepona kabisa isipokuwa kwa dawa moja tu:kulipiza kisasi. Hayo aliyaona wazi katika macho ya Joram ingawa alijisingizia kufurahia starehe zao.
Iko siku Nuru aliwahi kumwambia, "Sikia Joram. Huonekani kufurahia lolote tunalofanya. Kwa nini usiirudie ofisi yako na kuendeleza harakati zako? Nitakuwa kama alivyokuwa Neema. Nitakusaidia kwa hali na mali.”
Joram alicheka na kumjibu, "Mara ngapi nikwambie kuwa nimeacha shughuli hizo. Nitaendelea kustarehe hadi nitakapoishiwa na senti yangu ya mwisho.Ndipo nitakapotafuta kazi na kuifanya kwa Amani na utulivu kama vijana wenzangu."
"Kwanini lakini? Kifo cha msichana mmoja tu kinakufanya usahau wajibu wako!"
"Sivyo Nuru. Isieleweke kuwa nimechukia kwa ajili ya kufiwa na Neema. Yeye ni mmoja tu kati ya mamia ya wasichana wanaouawa kwa dhuluma na ukatili ainaaina ulioko duniani. Ni mmoja tu kati ya maelfu ya vijana wanaoteseka kwa shida ambazo wanazipata kwa makosa ya watu wengine. Ni mmoja tu kati ya mamilioni ya binadamu wanaoumia kwa umasikini ambao hawakuuomba na dhiki ambazo hazina umuhimu wowote."
"Sidhani kama nimekuelewa Joram, unazungumza kama mshairi."
"Labda. Ninachotaka kusema ni kwamba bastola yangu haitoshi kukomesha maovu yote yanayotendeka hapa duniani. Kote Afrika, na duniani kwa ujumla, binadamu hawako sawa kiuchumi. Wako wanaoshinda njaa na kuna wanaomwaga chakula. Kama kweli nakusudia kuondoa dhuluma na ukatili kwa nchi dhidi ya nchi nyingine, basi sina budi kuukomesha pia ukatili dhidi ya mwingine. Maadamu hayo yako nje ya uwezo wangu, naona sina budi kusahau yaliyopita na kuanza kula na kunywa kama vijana wenzangu."
"Hasira hizo Joram. Upende usipende ukweli ni huo huo: bastola yako haiwezi kuwaelekea viongozi wazembe na wenye choyo ambao wanasababisha hali ngumu kwa mwananchi. Lakini inawajibika kuwakomoa maadui ambao dhamira yao ni kuhakikisha hatulifikii lengo letu la kujenga taifa ambalo raia wake wanafaidi matunda ya uhuru wao. Unafahamu fika kuwa wanatunyima nafasi ya kufanya hayo"...
Maongezi hayo yalifanyika siku chache zilizopita. Nuru aliyakumbuka tena leo baada ya kuziona dalili za kukinai katika macho ya Joram. Alijua na kuamini, kama wanavyoamini watu wote wanaomfahamu Joram, kuwa starehe yake kuu ni pale anapopambana na adui na burudani yake ni hapo anapowashinda. Vinginevyo Joram alikuwa akijisingizia starehe.
"Leo wapi mpenzi", Nuru aliona amchokoze.
"Leo najisikia kulala tu".
"Kulala mchana! Tangu lini umeanza tabia hiyo?"
"Tangu nilipoacha kuwa Joram Kiango na kuamua kuwa kijana mtumiaji anayeitwa Joram Kiango."
"Nilijua utachoka, Joram. Kwanini usirudi ofisini na kuanzia leo?"
"Sikia Nuru. Usianzishe tena ule ubishi ambao siupendi. Wakati wote nitakuwa hapa nikiendelea kutumia."
"Sidhani kama unasema ukweli. Huonekani mtu wa kustarehe maishani."
Joram hakumjibu. Alijilaza kitandani na kujisomea gazeti.
Kisha jirani yao wa chumba cha pili aliingia akiwa katokwa na macho. Hakujali kupiga hodi. Wala macho yake hayakuvutwa kuuhusudu uzuri wa Nuru kama ilivyokuwa kawaida yake. Badala yake alimwendea Joram kitandani akisema, "Hujasikia? Samora amekufa!Ndege yake imeanguka huko Afrika Kusini."
"Amekufa!" Nuru alishangaa.
"Amekufa. Sio bure. Iko namna. Haiwezi kuwa ajali ya kawaida."
"Afrika Kusini? Alienda fanya nini huko?" Joram aliuliza kwa utulivu. Hata hivyo macho yake yaliwaka kwa hasira, ingawa hakupenda kuidhihirisha kwa Nuru.
"Siku hizi hata taarifa za habari husikilizi Joram?" Nuru alisema.
"Samora hakwenda Afrika Kusini. Alikuwa akitoka Zambia ambako alikutana na rais Mobutu na Waziri Mkuu Mugabe kutafuta mbinu za kuiwekea Afrika Kusini vikwazo zaidi vya kiuchumi".
"Wanasema chanzo cha ajali hakijapatikana. Bila shaka watakuwa wameisababishia ajali hiyo kwa njia moja au nyingie," alisema kwa masikitiko.
"Nadhani wamezoea kutuangamiza wapendavyo. Kwao sisi ni sawa na vifaranga waliofugwa. Yeyote ambaye hawampendi wanamponda kwa urahisi. Jambo la kusikitisha ni kwamba sisi hatuwezi kuwafanya lolote. Baya zaidi ni kwamba hatujui tutaendelea kuuawa mpaka lini.Kwanza, walimuua Mondlane: Sasa wamemuua mrithi wake, Samora. Na siyo hao tu. Viongozi wengi wa Afrika wameondokea kuwa kama mifugo yao. Tunaorodha ndefu ya viongozi wetu wanaouawa au kupinduliwa kwa matakwa yao. Tutaendelea kuvumilia mpaka lini?" Nuru alikuwa kama mtu anayezungumza peke yake.
Lakini macho yake yalikuwa yakimtazama Joram. Alitamani aone kitu katika macho yake. Hakukiona. Jambo hilo lilimfanya ainame chini na kuruhusu matone kadhaa ya machozi yamdondoke.
Yalikuwa machozi ya hasira zaidi ya huzuni.