ILIPOISHIA...
Juliana hakujua kilichokuwa ndani ya moyo wa shangazi yake. Alichukulia suala lake kama uzembe tu wa fikra katika uhusiano. Laiti angeingia moyoni mwake na kujua siri aliyokuwa nayo!
Angejua!!!
SASA ENDELEA...
SIRI ilitulia ndani ya moyo wa Lilian. Aliificha ndani ya kifua chake na hakuwa tayari hata kidogo kufungua kinywa chake kueleza ukweli.
Alijua ni kwa namna gani angejizidishia mateso ya kihisia ndani ya moyo wake. Alibaki kuwa mwenye mawazo lakini akijiapiza kufa na siri hiyo moyoni mwake.
Anti, akaita Lilian.
Unasemaje? Una nini kipya cha kuniambia? sasa Juliana alionekana dhahiri kuwa na hasira isiyo na kifani.
Usinifanyie hivyo anti.
Ni kitu gani nisichokijua kuhusu mapenzi? Kipi kigeni kwangu kuhusu uhusiano? Najua kila kitu, ndiyo maana nakushangaa, eti unakuwa tayari kuhairisha mwaka wako wa masomo kwa sababu kuna mpumbavu tu amekuvuruga.
Sikia... wewe una maisha yako, yeye naye ana maisha yake. Si mume wako huyo. Ingekuwa mmeoana, labda ungepaswa kuumia lakini boyfriend tu. Hebu get serious bwana. Sitaki kusikia upuuzi wako hapa, akasema tena anti yake kwa hasira ileile.
Lilian akamwaga machozi!
Ilikuwa ni haki yake kulia. Afanye nini sasa? Amwambie ukweli? Nani kasema?
Siwezi kusema, itakuwa tatizo mara mbili ya hivi, lazima nitumie akili zaidi, akawaza Lilian.
Juliana alijaribu kuzungumza kama mzazi, akichukua nafasi ya kaka yake, kumshauri Lilian akiwa hajui kabisa kuwa nguvu aliyokuwa akiitumia ilikuwa siyo mahali pake. Hilo hakulijua kabisa.
Nina ombi moja kwako anti.
Ndiyo.
Naomba nikae hapa kwa wiki mbili tu nikitafakari, kisha nitakujibu cha kufanya.
Juliana alikaa kimya kwa muda.
Alionekana amezama kwenye tafakuri ya muda akimfikiria shangazi yake. Kidogo ombi lile lilionekana kumwingia.
Na ninataka iwe wiki mbili kweli. Sikia... sina tatizo lolote kwa wewe kuishi hapa kwangu. Nina nyumba kubwa, kuna kila kitu ndani. Utakula, utalala, utavaa na kufanya kila kitu. Kwa hiki Mungu alichonijalia, sina tatizo kabisa ndugu zangu wakikitumia.
Lakini kumbuka, naumizwa na uamuzi wako. Sitaki kuona mapenzi yanaharibu maisha yako. Umeshapita vizingiti vingi Lilian. Kwa nini uje kuharibu mwishoni?
Nakuelewa anti, najua ni kwa kiasi gani unaumia, nisamehe tafadhali.
Yamekwisha.
Ahsante shangazi, akajibu Lilian alijitahidi kuachia tabasamu usoni mwake.
Tabasamu lilikuwa zito lakini kwa sababu ya vijishimo mashavuni mwake, liliweza kuonekana sawasawa.
***
Kutokana na upweke mara nyingi alipenda kwenda kushinda kwenye saluni ya kike iliyokuwa jirani na nyumbani kwa shangazi yake. Alipenda kwenda pale kwa sababu ya ucheshi wa dada aliyekuwa akihudumia katika saluni hiyo.
Aliitwa Maimuna lakini rafiki zake walimkatishia na kumwita Mai. Alikuwa msichana mrembo kwelikweli. Mwenye kila kitu kizuri mwilini mwake. Nyama za mwili wake zilikuwa zimeshikana vyema.
Alikuwa mrefu kiasi, mwenye shepu sawasawa, umbo likionekana kufanana kabisa na tarakimu namba nane. Alikuwa na makalio makubwa. Hipsi pana, miguu minene, mizuri na kiuno chembamba kama cha nyigu!
Kifupi alikuwa mrembo kupitiliza. Pamoja na urembo wake, hakuwahi kuonekana akiwa karibu na wanaume. Wanaume wengi mtaani walimmezea mate. Wenye roho za kupenda haraka, walijaribu kutupa ndoano zao, wakaambulia patupu!
Mai alikuwa na msimamo sana!
Urafiki wake na Mai ulishamiri kwa wiki moja tu. Lakini Mai hakufurahishwa na ukimya kupitiliza wa shoga yake. Kwa alivyomuona, haraka sana aligundua alikuwa kwenye tatizo kubwa ambalo hakutaka kumshirikisha mtu.
Leo hii hayupo tayari kumuona shoga yake akiendelea kuwa mwenye mawazo wakati yeye yupo. Wakiwa wawili tu saluni, mchana huu. Mai ameamua kuvunja ukimya.
Lilian... akaita Mai.
Abee...
Mimi ni rafiki yako siyo?
Ndiyo.
Tunaaminiana siyo?
Hakika.
Kwa ninavyokuona, naona una mzigo wa mawazo. Kuna kitu kinakusumbua na kinakutesa, lakini kwa bahati mbaya, inaonekana huna mpango wa kumweleza mtu yeyote jambo hilo.
Sidhani kama uamuzi huo ni sahihi. Acha kujikondesha mtoto wa kike. Mimi ni shogako kama ulivyosema na umesema unaniamini, nakuamini pia. So please, tell me, whats wrong with you my dear? akasema Mai kwa sauti tulivu, yenye kusihi na ushawishi wa hali ya juu.
Kama Mai angesomea masomo ya saikolojia, bila ya shaka angeifanya kazi hiyo kwa ubora wa hali ya juu sana. Aliweza kuwa mshauri mzuri.
Mbona hakuna tatizo? Nipo sawa kabisa Mai, Im absolutely okay, nothing wrong with me... please be happy my sister, akasema Lilian akitengeneza tabasamu ambalo Mai aliligundua haraka kuwa halikuwa halisi.
Your smile is not real Lilian. Tafadhali niambie, unasumbuliwa na nini? Nipo hapa kwa ajili yako, akasema Mai kwa sauti tulivu.
Let me tell you the truth... its true that a have a big problem. Angalia.... akasema Lilian machozi yakimlenga, huku akijionyesha mwili wake kwa Mai.
Im HIV Positive.... you think what is next to me? Im finished Mai. Im nothing.... (Nina virusi vya ukimwi... unafikiri nini kinafuata? Nimekwisha Mai. Mimi si lolote...).
Hapana... pole sana kwa kusumbuliwa na tatizo kubwa kihisia lakini lisilo kubwa kinadharia. Tuliza moyo. Ishu yako ni ndogo sana... akasema Mai.
Unamaanisha nini? Kuwa na ukimwi ni tatizo dogo?
Matatizo ni matatizo tu Lilian, ila ukimwi umepewa sifa ya kuwa tatizo kubwa, lakini si kweli. Ngoja... nitakuambia ukweli leo na nitakusaidia uishi maisha safi. Subiri kidogo, akasema Mai akifuata pochi yake.
Aliporejea, alikuwa na simu. Akaonekana akitafuta kitu katika simu yake, kisha akamkabidhi Lilian. Juu ya kioo cha simu hiyo, kulikuwa na mwanaume mtu mzima, amesimama kando ya gari la kifahari.
Ni nani huyu? Na kwa nini umenionyesha hii picha? akauliza Lilian.
Huyu ni Sadick Kisummi. Ni marehemu kwa sasa. Amefariki miaka nane iliyopita. Mwaka mmoja baadaye, alifuata mkewe. Alikuwa mpenzi wangu. Huyu ndiye chanzo cha matatizo yangu. Ndiyo sababu mpaka sasa sihitaji kuolewa.
Mzee Kisummi alinipa ukimwi. Hivi ninavyozungumza na wewe, ninaishi na virusi vya ukimwi takribani miaka kumi sasa. Awali niliogopa kama wewe, niliishi kwa mawazo na mashaka kama wewe, lakini kumbe nilikuwa najiumiza tu. Yupo sista anaweza kukusaidia.
Utaishi kwa amani na utarudi kwenye masomo yako kama kawaida. Kifupi utakuwa Lilian mpya, pengine mwenye furaha zaidi kuliko Lilian ninayezungumza naye sasa hivi hapa.
Kweli?
Kabisa.
Lilian akatabasamu!
Mwanga wa maisha mapya ukafunguka. Alimwamini sana Mai. Alimsogelea na kumvutia kwake. Wakakumbatiana.
Machozi hayakuwa hiyari yake tena, yakamwagika kama maji! Mashavu yake yakawa tepetepe!
Je, nini kitatokea? Usikose kufuatilia.