ILIPOISHIA...
Mwanga wa maisha mapya ukafunguka. Alimwamini sana Mai. Alimsogelea na kumvutia kwake. Wakakumbatiana.
Machozi hayakuwa hiyari yake tena, yakamwagika kama maji! Mashavu yake yakawa tepetepe!
SASA ENDELEA...
USILIE mpenzi, tafadhali usilie. Unatakiwa kujipa moyo
angalia, huu ni mwanzo mzuri kwako. Mwanzo mwema wenye matumaini makubwa, akasema Mai akiwa bado yu kifuani mwa Lilian.
Ni kweli usemayo, na ndivyo nifanyavyo sasa. Machozi haya si ya huzuni tena Mai rafiki yangu. Umenifumbua macho. Naona kila kitu kwa upya kabisa mbele yangu. Usijali.
Tulia...tena naona, hebu twende nyumbani sasa hivi, akasema Mai.
Nyumbani?
Ndiyo. Nyumbani kwangu.
Ofisi?
Nitafunga. Kwanza, nani wa kuniuliza? Ni salon yangu mwenyewe.
Najua...lakini wapo wa kukuuliza, wapo mabosi wako.
Bosi wa hapa ni mimi.
Si kweli. Wateja wako ndiyo mabosi wako. Vipi wakija wakukose? Sioni kama ni busara. Huu ni mwanzo mzuri kwetu, lakini kamwe usiharibu kazi.
Lilian alizungumza kwa sauti ya taratibu iliyojaa ushawishi. Kwa hakika alionekana kuzungumza mambo ya msingi ambayo yalimwingia Mai kwa kiasi kikubwa sana.
Ahsante kwa ushauri. Nimekuelewa shoga yangu, akasema Mai.
Poa, ngoja nijirudishe nyumbani, baadaye nitakutafuta ukimaliza kazi.
Sawa.
Lilian akaaga.
Akaondoka zake.
***
Lilian alikuwa na mabadiliko makubwa sana katika maisha yake. Ushauri wa Mai ulikuwa na nguvu kama aliyeshauriwa na mtaalamu wa masuala ya ushauri mwenye uzoefu wa zaidi ya miaka kumi!
Haikuwa hivyo!
Lilian alimwelewa kwa haraka Mai kutokana na mfano halisi na wa wazi kutoka kwake. Kitendo cha kumhakikishia kuwa, hata yeye alikuwa akiishi na virusi hivyo kulimpa faraja kubwa sana moyoni mwake.
Kwake, ukimwi ukawa si tatizo kubwa sana. Kichwani mwake aliwaza jambo moja tu; kuzungumza na shangazi yake Juliana.
Atanielewa kweli? akawaza.
Lakini ndiyo ukweli. Kwa nini nisimwambie wakati huu ambao nina hakika kuwa, sina mashaka tena? Lazima nimshirikishe, akajijibu mwenyewe.
Hata hivyo, akili yake ilikwenda mbali zaidi, akafikiri mambo mengine makubwa zaidi. Aliamini, pengine kwa kumwambia ukweli, angeweza kumnyanyapaa na kumkatisha tamaa.
Aliwaza pengine asingempa ushirikiano na angewatangazia ndugu zake wote kuwa amepata ugonjwa huo. Alikwenda mbali zaidi, akaamini kuwa, pengine wangefikiri kuwa, amepata ugonjwa huo kutokana na tabia zake mbaya.
No! Sina sababu ya kumweleza, na si yeye tu, sitamwambia mtu mwingine yeyote, akawaza mwenyewe kichwani mwake.
Wazo hilo akalipitisha moja kwa moja. Likamwingia kichwani na kulikubali.
Alichokuwa akisubiri kwa hamu ni siku ya kukutana na mshauri aliyemsaidia shoga yake, Mai! Haikuwa mbali sana ni Jumamosi tu! Siku mbili baadaye!
***
Kilikuwa chumba kidogo, kizuri na kilichopangiliwa vitu vizuri. Rangi ya parachichi iliifanya ofisi ile kuwa yenye kuvutia sana. Samani zake pia zilikuwa nadhifu.
Nyuma ya kiti kikubwa cha kuzunguka, alikaa dada mrembo, aliyekuwa amevaa miwani myeupe yenye fremu nyeusi. Vijishimo mashavuni vinaongeza urembo wa michana huyu.
Nyusi zilizojaa juu ya macho yake, zikiwa hazijawekwa kikorombwezo chochote, zinaongeza idadi ya maksi ya uzuri wa mwanamke huyu wa makamo.
Waweza kumuita mdada, lakini hata ukimuita mama hutakuwa umekosea sana, maana tayari ni mama wa watoto wawili. Ana umri wa miaka 32 tu, na bado amejitunza vyema na kuendelea kuwababaisha wanaume wakware wa mjini wanaopenda vya mteremko!
Kwa huyu si wa mteremko!
Ni dada mwenye heshima zake. Msomi, aliyeshiba taaluma ya ushauri wa saikolojia ya maisha. Kwa sasa amebobea katika ushauri nasaha, utafiti na upimaji wa magonjwa ya ngono na ukimwi.
Yes! Aliitwa Sista Isabela!
Mbele ya meza yake kubwa, ikiwa na mafaili machache mezani, walikaa wadada wawili wazuri kama yeye! Ni Mai na Lilian.
Baada ya salamu na utambulisho, Mai alimweleza kila Sista Isabela kuhusu hali ya Lilian na hofu aliyokuwa nayo. Sista Isabela akatabasamu.
Nashukuru sana Mai kwa kunisaidia kazi. Ninavyokuamini, najua nina kazi ndogo sana kwa Lilian, akasema akitabasamu zaidi na kuufanya uzuri wake utamalaki maradufu.
Ni kweli kabisa, akasema Lilian.
Utapenda kwenye mazungumzo yetu Mai awepo au akusubiri nje?
Mai ndiye aliyenitoa mimi matongotongo. Sina shida akiwepo, labda kama taaluma yako haikuruhusu, lakini kwa upande wangu. Ni sawa akiwepo.
Sawa...nimekuelewa vizuri kabisa, lakini naomba Mai umsubiri tu nje, acha nizungumze naye kwa uhuru zaidi.
Wote wakacheka.
Mai akasimama na kupiga hatua za kivivu kuelekea nje. Ndani ya ofisi wakabaki wawili tu Sista Isabela na Lilian.
Naamini sasa utakuwa huru zaidi. Nikuambie tu Lilian, umekuja mahali sahihi kabisa. Tuliza kichwa chako, kuwa huru na ondoa wasiwasi wako kabisa. Kila kitu kitakuwa sawa, akasema Sista Isabela.
Najua unafahamu mengi kidogo kwa sasa kuhusu ukimwi. Hatutajifunza wala kuzungumzia sana kuhusu ukimwi. Tayari unao. Nataka kujadili kuhusu maisha. Kuhusu maisha yako mapya baada ya kujua tayari umeambukizwa.
Hebu tuanze na hili. Ni jambo gani linalokupa hofu zaidi baada ya kujua kuwa umeambukizwa? Namaanisha, ni wapi unahisi kuna giza nene mbele yako? Hapo ndipo ninapotaka kuanza napo, alisema Sista Isabela kwa sauti tulivu, akiwa ameyatuliza macho yake usoni mwa Lilian.
Lilian akatulia kwa muda. Akajikohoza kidogo, kisha akavuta pumzi ndefu sana, halafu akazishusha taratibu kabisa.
Kiukweli nina hofu na mengi. Kwanza mimi ni msichana mrembo, naogopa kukonda... kuonekana kama mgonjwa-mgonjwa. Sina mtoto, natamani sana kuwa na wanangu. Nataka kuolewa, ndoto hiyo imefutika, tena tayari nilikuwa na mpenzi wa kweli ambaye alikuwa tayari kunioa, haiwezekani tena.
Ona maisha yangu yalivyoharibika. Nimehairisha mpaka mwaka wangu wa masomo. Naua nitarudi, nitamaliza na nitapata kazi... halafu fedha nitazopata zitakuwa na faida gani? Naona kama nimekwisha! Ni giza tu mbele yangu! akamaliza kusema Lilian akihema kwa kasi.
Tuliza moyo. Yote hayo si matatizo. Labda nikuhakikishie kuwa, huwezi kukonda na kuonekana kama mgonjwa dhaifu. Utaolewa, utazaa watoto tena wasio na uambukizo na utayafurahia maisha yako mpaka siku Mungu atakapoamua vinginevyo na si kwa sababu ya ukimwi, akasema Sista Isabela kwa kujiamini.
Mh! Kuolewa? Kuzaa watoto wasio na uambukizo? Itawezekanaje? Hapo sasa unanidanganya! akasema Lilian akitoa macho.
Hakuna udanganyifu mdogo wangu. Sikia... akasema Sista Isabela, sasa akianza kupekua kitu kwenye kompyuta mpakato iliyokuwa mezani mwake.
Lilian akatulia akisubiri kumsikiliza!
Itaendelea...