Hadithi: Mtambo wa mauti

Hadithi: Mtambo wa mauti

nameless girl

JF-Expert Member
Joined
Apr 22, 2012
Posts
4,195
Reaction score
2,685
MTAMBO WA MAUTI
BY: BEN R. MTOBWA

KIDOKEZO
Muhimbili, Dar es Salaama, Tanzania.
April 1, 2004
Madaktari bingwa sita, waliokubuhu katika taaluma ya tiba, waliduwaa mbele ya microscope wakishuhudia kitu ambacho hawakupata kukiona maishani mwao. Kwa muda wa dakika moja, kirusi kimoja tu cha UKIMWI kilichowekwa katika damu yenye ujazo wa milimita 3, kilikuwa tayari kimeteketeza chembechembe nyeupe 5,000 kati ya chembechembe zisizopungua 10,000 zilizokuwemo!
Si hilo tu, kirusi hicho, ambacho katika hali ya kawaida hakijihusishi na chembechembe nyekundu, hapa kilionekana kikizishambulia chembechembe hizo moja baada ya nyingine kwa kasi ya ajabu.
Chembechembe nyeupe kwa jina la kitaalamu T-Cells au CD4+, zina kazi maalumu ya kuhakiki kinga ya mwili na kurekebisha uharibifu wowote unaotokea. Chembechembe nyekundu ambazo, kwa kawaida, huishi siku 120 kabla ya kuharibiwa katika ini au wengu na nyingine kuchukua nafasi yake, kazi yake kubwa ni kusafirisha oksijeni mwilini. Inaaminika kuwa kiasi cha chembechembe 200,000,000 hutengenezwa na kuharibiwa kila siku. Kasi ya kirusi hiki katika kuteketeza chembechembe hizo na kuzaliana ilionyesha wazi kuwa binadamu aliyeambukizwa asingeishi zaidi ya siku tatu! Jambo ambalo liliwafanya madaktari hao bingwa watazamane kwa hofu na mshangao.
Uamuzi wa kufanya majaribio haya ulichukuliwa na uongozi wa hospitali hiyo baada ya mgonjwa wa kumi na moja, kati ya kumi na wawili walioletwa hospitalini hapo, kufa saa ishirini nan ne baadaye kama waliomtangulia. Wote walilalamika maumivu ya kichwa na homa kali. Walipopimwa damu zao zilionekana kuathiriwa na virusi vya UKIMWI, jambo ambalo si wao wala ndugu zao walioafikiana nalo. “Jana tu alikuwa mzima wa afya, leo niambiwe kuwa ana UKIMWI!” Mmoja wa ndugu wa wagonjwa hao alimaka.
Kitu kingine kilichowasukuma madaktari hao kufanya uchunguzi huo ni historia ya maradhi yao. Wote walionekana kuugua ghafla baada ya kula chakula cha aina moja katika tafrija ya arusi iliyofanyika mjini hapa. Walikuwa wamekula nyama ya kusaga ambayo baadaye waandaji wa tafrija hiyo walikana kuhusika nayo!
Awali, hospitali ilidhani kuwa wamekula sumu. Lakini vipimo vilionyesha tofauti. Vifo vyao vilitokana na shambulizi kubwa la virusi vya UKIMWI. Virusi vinavyoshambulia kwa kasi kubwa kuliko ile ya maradhi yote mengine ya mlipuko ikiwemo Ebola na hata kipindupindu.
“Mungu wangu!” Dakktari mmoja alilalamika. “Mnajua kwamba kirusi hiki kikiruhusiwa kuendelea kuishi mwaka mmoja tu baadaye nchi hii haitabakia na mtu au mnyama yeyote aliye hai?”
“Hilo liko wazi, hasa baada ya kuona kuwa kinaweza kuishi ndani ya vitu vingine kama maji na chembechembe za chakula badala ya damu pekee kama ilivyo ada!”
“Nakichukia kirusi hiki!” Daktari mwingine alisema kwa kufoka.
“Kwa hiyo, la kufanya ni lipi?”
Daktari aliyekuwa kimya muda mwingi akachangia, “Nadhani hatuna la kufanya kwa sasa, zaidi ya kupeleka sampuli hii Shirika la Afya Duniani, WHO, ili nao wathibitishe juu ya kitu hiki ambacho kimeingia katika soko la maradhi hatari.”
Waliafikiana naye.
Muda mfupi baadaye sampuli hiyo ilikuwa ndani ya kasha maalumu la DHL, ikielekea Jeneva, Uswizi.
Saa ishirini nan ne zilizofuata tayari Shirika la Afya lilirejesha majibu, likionyesha kushitushwa kwake na ‘ugonjwa huo mpya’ ambao haukuwemo katika kumbukumbu zao na ambao, ‘kwa vyovyote vile tiba yake itakuwa ngumu kutokana na kasi yake ya maambukizi.’
Madaktari bingwa waliitana tena kwa faragha na kulitafakari jibu la WHO.
“Kwa hiyo tufanye lipi?” mmoja wao aliuliza tena. “Tuitangazie nchi na dunia hii ili watu wajihadhari?”
Wenzake wawili watatu walimpinga harakaharaka. “Hilo hatuwezi kufanya. Litaleta hofu kubwa miongoni mwa wananchi,” mmoja wao alisema.
“Halafu, maadam hatujajua chanzo, tutakuwa hatujasaidia chochote.”
“Zaidi ya hayo, kazi yetu ni kutunza siri, sio kuzitoa.”
“Una maana hata Waziri wa Afya tusimwambie?” msemaji wa awali alihoji tena.
“Atatusaidia lipi kwa hili?” mwenzake alimhoji “Yeye ni mwanasiasa, si mtaalamu. Ataishia kupiga kelele majukwaani.”
Msemaji wa awali alikuwa hajaridhika, akasema, “Jamani, mnataka kuniambia tumfiche hata Rais wa Jamhuri ya Tanzania taarifa hizi?”
Kila mmoja alimtumbulia macho. Hakuna aliyemjibu.

NB: HII STORY UTAIMALIZIA UTAKAPOJIPATIA NAKALA YAKO. USIJE UKASEMA SIKUKWAMBIA.

 
1
HILI lilianza kama tamthiliya, tena tamthiliya yenyewe nyepesi tu, ya mapenzi. Kama waigizaji katika tamthiliya hiyo, si Joram Kiango kwa upande mmoja; wala msichana huyu, kwa upande wa pili, alipata angalau kuhisi tu kuwa mwanzo wa tamthiliya hiyo ulikuwa sawa na kuanza kwa mkasa mzito kama mkondo wa mto unaopita katika majanga ya nchi yenye kila aina ya ukatili na unyama usiomithilika.
Dar es Salaam ikiwa imefurika wasichana warembo kupindukia, wengi wao wakiwa wameuongeza urembo wao wa asili maradufu kwa vipodozi lukuki vilivyofurika madukani, msichana huyu, machoni mwa Joram alikuwa wa kawaida kabisa. Hata hivyo, baada ya kumtazama kwa makini zaidi alibaini kuwa alikuwa na ziada moja juu ya urembo wake. Si ile ngozi yake ya maji ya kunde, la hasha. Ilikuwa ngozi ya kawaida ingawa weusi wake uliifanya imeremete na kushawishi kuigusa. Si lile tabasamu lake la mara kwa mara. Hilo pia ni jambo la kawaida katika nyuso za wasichana wa kileo na lingeweza kununuliwa kwa fedha tu iwapo mwenyewe angejali kujiunga na chuo kimojawapo cha usanii na kuhitimu. Hali kadhalika, ziada hii haikutokana na macho yake maangavu, pua yake iliyochongoka; wala meno yake meupe yaliyojipanga kikamilifu kinywani mwake kama mistari miwili ya punje za mahindi kwenye kibunzi.
Alikuwa na ziada!

Lakini ziada hii ilikuwa ipi? Joram alijiuliza akimtazama kwa hila mrembo huyo aliyeketi kando. Macho yao yakagongana. Yale ya msichana yalihimili kwa sekunde moja dhidi ya yale ya Joram, sekunde ya pili yakawa yameangukia chini huku lile tabasamu lake likigeuka kuwa katika sura nyingine. Ni hapo Joram alipobaini ile ziada iliyomvuta katika sura na umbile la msichana huyu.
Haya!
Alikuwa msichana mwenye haya! Mmoja kati ya wasichana wachache kabisa duniani waliobakia na haya. Wengi wao, toka walipoanza kuvaa suruali kama wanaume, huku wakienda kazini na kurudi jioni kama wanaume, kile kirusi kinachoitwa ‘haya’ kilitoroka zama za kale katika maumbile yao na, hivyo, kuwaacha wakavu kama wanaume.
Akiwa amevutwa na hilo, kwa mara ya kwanza Joram Kiango alijikuta akimtilia maanani na kuamua kumsikiliza, badala ya kuishia kumsikia tu.
“Umesema unaitwa nani vile bibie?” alimuuliza.
“Mona.”
“Mona?”
“Mona Lisa.”
Joram alipata kuziona mara nyingi nakala za ule mchoro maarufu duniani wa Mona Lisa. Aidha, aliwahi kuiona nakala halisi ya mchoro huo katika jumba moja la kumbukumbu za Sanaa nchini Ufaransa. Mchoro huo ulichorwa na msanii maarufu aliyeishi mwaka 1452 hadi 1519 huko Italia, Leonardo da Vinci, akimwigiza mrembo huyo Mona, aliyezaliwa kati ya mwaka 1503 na 1506; mchoro ambao mtu mmoja, Vincenzo Peruggia aliwahi kuuiba toka katika jumba hilo na kuuficha kwa kuamini kuwa ulikuwa umeibiwa na Napoleon wakati wa vita vilivyoifanya Ufaransa iitawale Italia kwa muda mrefu. Lakini mchoro huo ukakamatwa na kurejeshwa tena Ufaransa mwaka 1913, baada ya kibaka huyo kujaribu kuuza.
Aliyempatia msichana huyo jina hilo hakubahatisha. Isipokuwa kwa tofauti ya rangi, Mona huyo akiwa maji ya kunde, yule wa historia akiwa mweupe, vinginevyo walikuwa mtu na dada yake. “Jina lako halisi hilo!” alimuuliza kwa mshangao.
“Nadhani,” alijibu kwa sauti yake ileile, laini inayobembeleza, sauti iliyofuatiwa na tabasamu lilelile la pekee; Tabasamu la Mona Lisa.
“Unadhani? Huna hakika? Kwa nini?”
“Nadhani! Kwa kuwa toka nimepata akili nimejikuta naitwa Mona Lisa. Hata cheti changu cha kuzaliwa kimeandikwa hivyo.
Joram alimtazama kwa makini zaidi. Mara akaanza kubaini mengine katika umbile la msichana huyu ambayo pia yalikuwa ya ziada. Kwa mfano, alibaini kuwa nywele zake fupi zilikuwa asilia, hazikupata kuwekewa aina yoyote ya dawa ili kuzipa mvuto uliokuwa nazo. Hali kadhalika, ngozi yake pia haikupata kuathiriwa na yale madawa ya kileo, yanayowababaisha wasichana wengi kwa faraja ya muda mfupi na athari za maisha. Huyu alikuwa kama alivyozaliwa. Sifa zake hizo zikiwa zimepambwa kwa mavazi yenye heshima, sketi ndefu iliyovuka magoti na blauzi nyepesi iliyokifanya kifua chake kitoe picha ya uhai wa matiti yake.
“Utanisaidia?” msichana huyo alimzindua Joram baada ya kumwona kamtumbulia macho, kimya, kama anayetafakari jambo ambalo binti huyo hakulielewa.
“Hivi ulisema unachohitaji kwangu ni nini vile?” Joram alimwuliza.
Msichana akaangua kicheko. “Acha mzaha, Joram. Unajua, kukupata leo peke yake ni bahati ya pekee? Nimekutafuta wiki mbili katika mahoteli yote na baa zote za jiji hili. Leo imetokea kama ndoto!”
Hilo lilikuwa jingine ambalo Joram aliishangaa akili yake kwa kutolitafakari mapema. Msichana huyu amewezaje kumpata katika hoteli hii ambayo si kila mtu anafahamu kuwa hupenda kuitumia?

‘Comfort Hotel’moja kati ya hoteli mpya zinazojengwa kwa fujo katika ufuko wa bahari ya Hindi, ilimvuta Joram Kiango kwa upya wake. Toka alipoamua kukaa kimya, baada ya kutoridhika na tamati ya mambo katika mkasa ulioandikiwa kitabu na kuitwa Nyuma ya Mapazia Joram alijikuta hana raha. Ndiyo, King Halfan alifanikiwa kuponyoka toka katika mikono ya yule muuaji hatari, Marlone, na kufanikisha taarifa za mauaji ya kutisha yaliyoandaliwa kufanyika kwenye ule mdahalo wa kihistoria wa kumtafuta Rais anayefaa zaidi kuiongoza Tanzania; bado mwisho ule haukumridhisha kabisa Joram. Kutoweka kwa Marlone kabla ya yeye kumtia risasi ya kichwa kulimsononesha sana na ukimya wake hadi sasa ulimkosesha kabisa usingizi.
Wapambe wake jijini London walikuwa wamedokeza juu ya ‘ajali ya kamera’ katika uwanja wa Heathrow, ajali ambayo baadaye hisia zilielekeza kuwa iliandaliwa itokee katika hoteli ya Kilimanjaro, kwenye mdahalo. Lakini Mungu akaingilia kati na kuiepusha. Hata hivyo, mshenzi aliyeyaandaa mauaji hayo alitoweka kama tone la maji baharini, pasi ya kuacha alama yoyote ya kuwepo kwake. Kwa Joram Kiango hilo lilikuwa sawa na bomu lililo hai, ambalo wakati wowote lingeweza kulipuka na kusababisha maafa ya kutisha.
Kutokana na hisia kuwa kwa namna moja au nyingine alikuwa ameshindwa kutimiza wajibu wake, ndipo Joram alipoamua kuingia gizani kwa kujiepusha na vikao vyake vya kawaida, ikiwa pamoja na kumwepuka msaidizi wake mkuu, Nuru, na badala yake kuamua kujichimbia hapa na pale; mara kwa mara katika hoteli hii, ambayo kama wapo watu waliomfahamu kwa jina lake halisi ni wachache sana.
“Utanisaidia?” Mona Lisa alimzindua tena Joram.
Joram akamtazama kisha akamuuliza, “Hebu niambie Mona, umejuaje kama napatikana hapa?”
“Ni hadithi ndefu. La msingi ni wewe uelewe tu kuwa nimekuja hapa Dar toka Arusha kwa ajili yako. Na kwamba nimekutafuta kwa wiki mbili kamili kabla ya bahati kunitokea leo.” Mona alisita na kumtazama Joram. “Tafadhali niambie kama utanisaidia,” akasema kwa msisitizo.
Joram alimtazama. Macho yake yakagongana tena na yale laini, yanayobembeleza, ya Mona Lisa, macho ambayo si kwamba yanabembeleza tu, bali pia yanashawishi na kushurutisha.
“Tutaangalia uwezekano,” alimjibu.
Mona akatoa tabasamu la shukrani. “Lini? Leo?”
“Hata sasa hivi. Kuna ubaya gani?” lilikuwa jibu la Joram.
“Hapana. Labda jioni, nina disketi tu. Hatuna kompyuta. Lakini hoteli niliyofikia ina chumba cha kompyuta za kukodi. Naweza kwenda kuiprint na kuja nayo jioni. Utakuwepo?”
Ndio kwanza Joram akakumbuka msichana huyo alihitaji msaada gani toka kwake. Alikuwa ameandika riwaya ya upelelezi. Tayari ilipitiwa na wahariri kadhaa ambao walimhakikishia kuwa ilikuwa riwaya nzuri sana. Hata hivyo, alisita kuipeleka kwa wachapishaji hadi hapo itakapopitiwa na mpelelezi mashuhuri, kama Joram Kiango, ambaye ana uwezo wa kudodosa kasoro zinazoweza kukifanya kisifikie kiwango kinachohitajika.
“Lakini mimi sio mwandishi wala mhariri. Bado sioni naweza kukusaidia kwa namna gani,” Joram alionya.
“Sihitaji msaada wa ajabu, Joram. Ukikitazama tu utaona kama kinafaa au la. Kama hakifai…”
“Sitasita kukueleza,” Joram alimalizia.
“Usisite, tafadhali. Naomba uniruhusu nikaprint ili niulete jioni,” Mona aliomba huku akiinuka.
“Kuna ubaya gani?” Joram alimjibu na kuongeza, “Nitatoka na kurudi hapa saa moja na robo usiku. Saa tatu kamili nina mihadi mahala. Nadhani muda wa saa moja unatosha kuutazama mswada wako na kutoa maoni yangu ambayo naamini hayatakusaidia sana.”
“Mie naamini yatanisaidia sana,” Mona Lisa alisema hali akiinuka na kuondoka.

***
Ndiyo, kwa kila hali alikuwa msichana wa kawaida. Macho yake yenye haya yasingekuwa na uwezo wa kuficha chochote ambacho angependa kuficha bila ya Joram Kiango kumshuku. Hata hivyo, hilo halikuondoa ule ‘u-Joram Kiango’ katika fikra za Joram Kiango. Si wahenga walisema kuwa tabia haina dawa? Ni tabia hiyo, au ‘u-Joram Kiango’ huo uliomfanya Joram kupitia katika kioo cha moja ya madirisha ya hoteli hiyo amchunguze msichana huyo toka alipotoka hotelini, alivyotembea kwa mwendo wake wa kusisimua, hadi alipoifikia teksi iliyomleta hotelini hapo. Mara tu gari hilo lilipoondoka Joram naye alitoka nje ya hoteli na kuliendea gari lake la kukodi, akaliwasha na kulielekeza mjini, akilifuata gari la Mona Lisa.
Aliiacha njia ya kutokea hotelini na kuingia barabara ya Bagamoyo. Gari moja, Toyota Hilux lililokuwa likiendeshwa kasi bila sababu za msingi lilimpita kwa kasi na kumtenganisha na lile la Mona Lisa jambo hilo lilimfurahisha Joram. Hakutaka Mona amwone au kuhisi kuwa anafuatwa au kuchungwa.
Waliiacha tegeta, wakaingia Kunduchi, Mbezi na, hatimaye Tangi Bovu. Hadi wanaingia Mwenge tayari yalikuwepo magari matano baina yake na lile la Mona Lisa. Mawili kati ya hayo yakiwa daladala, moja likiwa gari la abiria na mawili yaliyosalia magari madogo.
Umbali huo baina yake na gari la Mona haukumsumbua hata kidogo. Alikwishazisoma namba za gari hilo. Hali kadhalika, aliweza kuona vizuri hatua zote ambazo dereva wa gari hilo alikuwa akichukua, kama kusimamia, kulipita gari lingine au kupinda kona kabla ya dereva huyo kufanya hivyo.
Pengine kilichokuwa kikimsumbua Joram Kiango wakati huo ni hatua yake hii ya kumfuatilia msichana mpole kama huyo. Mona Lisa hakuonekana kuwa na madhara ya aina yoyote. Zaidi, alikuwa ameahidi kurejea hotelini hapo jioni hiyohiyo akiwa na mswada wa riwaya yake ya upelelezi aliyoiandika. Ya nini kumfuatilia hadi huku? Joram alijiuliza. Kisha, alijicheka kimoyomoyo alipokumbuka usemi wa mwanamke wa kiingereza; Never marry a Cop. Usilogwe kuolewa na polisi kwani akikosa mtu wa kumshuku kwa uharifu ataanza kukushuku hata wewe mwenyewe.
Wakati huo walikuwa wakimalizia barabara ya Ally Hassan Mwinyi. Gari ya Mona Lisa lilipoonyesha ishara ya kuingia kushoto kuifuata barabara ya Maktaba. Joram naye alihamia kushoto na kuifuata barabara hiyo. Waliifuata moja kwa moja kuelekea baharini. Gari ya Mona Lisa ilipoonyesha ishara ya kuingia hoteli ya New Afrika Joram, ambaye alikuwa magari manne nyuma, alipinda kushoto kuifuata barabara ya Samora hadi mbele ya ukumbi wa MAELEZO ambapo alisimama na kupaki.
Kabla hajashuka alifunua kiti cha abiria na kutoa miwani yake mieusi, kofia pana ya Cowboy na ndevu zake za bandia ambazo alizivaa mara moja huku akizidi kujishangaa kwa hatua zote. Alijipapasa katika sehemu yake ya siri ambapo huficha bastola yake, na baadaye kuanza safari yake fupi ya mguu kuiendea hoteli ya New Afrika.
Mbele ya lango kuu la hoteli, Joram alimpita Mona Lisa amabaye alikuwa akibishana jambo na dereva wake. Baadaye alimsikia akimwambia ‘nisubiri’, na kuingia ndani. Kama ambavyo Joram alitegemea, msichana huyo hakuonyesha dalili yoyote ya kumjua. Badala yake alimpita baada ya kumtupia ‘shikamoo’ ambayo Joram aliitikia kwa kutikisa kichwa. Alitembea mwendo wa haraka hadi kaunta ambako aliomba kadi ya kufunguliwa mlango wa chumba chake na kisha kuiendea lifti.
Hotelini humo Joram alielekea ukumbi wa baa. Aliagiza toti mbili za John Walker ambazo alizinywa kavukavu kwa mikupuo mitatu na kuisindikiza kwa sigara moja ambayo aliivuta nusu, akaizima na kuisindika katika kasha la taka.
Huku akiwa na hakika kuwa hakuna mtu yeyote anayemtazama zaidi ya mtazamo wa kawaida, alitoka katika ukumbi huo na kuiendea lifti. Ilikuwa chini kama inayomsubiri. Aliingia na kubonyeza tufe la ghorofa ya tano. Aliutumia upweke katika lifti hiyo kubandua ndevu zake za bandia na kuvua miwani yake mieusi na kufutika vitu hivyo katika moja ya mifuko yake ya koti. Aliyesimama hapo mbele ya chumba namba 512, alikuwa Joram Kiango yuleyule ambaye Mona Lisa alimwacha kule Comfort Hotel dakika arobaini zilizopita. Mkono wake wa kulia ulikuwa ukigonga mlango taratibu hadi ulipofunguka na uso mzuri wa msichana huyo kuchungulia.

***
“Joram!” Mona Lisa alitamka kwa mshangao. “Siamini macho yangu!”
“Shauri yako. Ni macho yako mwenyewe. Ukiyaamini sawa, usipoyaamini sawa,” Joram alimtania akitabasamu. “Nakaribishwa nyumba hii au sitakiwi?”
“Lakini si nimekuacha ufukweni muda mfupi uliopita?” Mona Lisa alizidi kusaili.
“Si tulikuwa wote?” Joram alimhoji.
“Mimi nilikuja kwa gari.”
“Mimi nimekuja kwa helkopta,” Joram alizidi kumtania. “Nakaribishwa humu ndani?”
Mona Lisa alimpisha kuingia. “Karibu sana. Keti tafadhali,” alimhimiza. Hata hivyo bado ilikuwa dhahiri kuwa ujio huo wa Joram ulikuwa umemshangaza sana. “Sikujua kuwa siku hizi Dar mnazo helkopta za kukodi,” alichokoza mara baada ya Joram kuketi kwenye kochi.
“Zipo ingawa hazionekani kwa macho ya kawaida,” Joram aliongeza mzaha. “Bibi yangu alinifundisha namna ya kuruka kwa ungo.” Alipoona msichana huyo akizidi kuduwaa Joram aliamua kumtoa wasiwasi kwa kumweleza, “Usijali mpenzi. Mimi ni mtu wa utani kila wakati. Unajua sikuwahi kupata mapenzi ya bibi wala babu? Unajua sina binamu? Hivyo, napenda kulazimisha utani kwa kila mtu. Kwa kweli, nimekuja hapa kwa gari kama wewe. Kilichonileta hapa ni hiki!” alitia mkono wake katika mfuko wa koti na kuutoa ukiwa umeshikilia pochi. “Uliisahau pochi yako. Nikaona nikodi gari kukufuata kwa kuhofia kuwa ungepata shida ya kumlipa dereva wako na mahitaji mengine. Ndipo nikakodi gari kukufuata. Kwa bahati mbaya dereva wangu aliendesha gari kwa mwendo wa kinyonga. Wakati nafika hapa niliambulia kukuona ukiingia katika lifti. Nikauliza namba ya chumba chako mapokezi na kukufuata.
Mona Lisa alipokea pochi hiyo kwa furaha. “Loo, masikini! Pole sana. Kumbe niliisahau kwako!”
Laiti angejua Joram alikuwa ameisogeza ili apate chochote ambacho angehitaji kupata juu ya msichana huyo! Kwa bahati mbaya hakuambulia chochote zaidi ya kukuta noti za elfu kumi kumi zisizopungua ishirini. Hakukuta kielelezo wala kitambulisho chochote, jambo lililopelekea kujiri kwa safari yake hadi chumbani humu.
“Karibu sana… Jisikie nyumbani,” Mona alimkaribisha tena Joram Kiango, “Sijui nikupe kinywaji gani? Aliuliza.
Joram alichagua John Walker, kavu. Mona alimsogezea chupa nzima na glasi na kuviweka juu ya kijimeza cha kioo kilichokuwa mbele ya kochi alilolikalia Joram. “Tafadhali, jihudumie. Natoka mara moja kumtoa dereva wangu. Nadhani kwa sasa atakuwa na wasiwasi kuwa nimemwingiza mjini,” alisema akiichukua pochi yake na kuelekea mlangoni.
Take your time… Mie niko nyumbani hapa,” Joram alisema akijiweka katika mkao wa kunywa. Aliifungua chupa hiyo iliyojaa pomoni na kumimina nusu glasi ambayo aliitia mdomoni. Mara tu Mona alipotoka nje ya chumba hicho na kufunga mlango nyuma yake, macho ya Joram yaliingia kazini. Alichunguza uvunguni, nyuma ya kabati, paa na kila uchochoro wa chumba hicho. Alitupa macho paani na sakafuni.
Macho hayo yenye uzoefu hayakumfanya ashuku chochote. Kwa kila hali kilionekana chumba cha kawaida, chenye kila hadhi ya chumba cha hoteli ya kisasa. Mlango wa maliwatoni uliokuwa wazi nusu ulimwonyesha marumaru ya kung’ara iliyofunika sakafu na ukuta mzima, huku masinki ya choo, ya kunawia na kuogea, yaking’ara kwa usafi. Kitanda futi sita kwa sita kilifunikwa vizuri kwa shuka nzito ya mauamaua. Kando ya kitanda hicho ilikuwepo televisheni ndogo, friji na shefu ya vitabu. Juu ya kitanda kulikuwa na mashine ya hewa ambayo iliendelea kusambaza hewa safi chumbani humo. Meza ya pili chumbani humo ilibeba kompyuta, printer na begi la nguo.
Kwa kila hali, kilikuwa chumba cha kawaida, kama ambavyo msichana aliyekikodi alivyokuwa wa kawaida. Tulia Joram! Akili yake ilimwambia. Si kila wakati ni wakati wa hatari. Sio kweli kuwa kila chui huvaa ngozi ya kondoo! Mona Lisa ni msichana wa kawaida kabisa. Anahitaji ushauri tu katika riwaya yake ya upelelezi.
Hata hivyo, zile hisia za u-Joram Kiango ziliendelea kumpigia kengele za kuwa makini na msichana huyu; yote yang’aayo si dhahabu, nafsi yake nyingine ilimnong’oneza.
“Mbona hunywi?” Mona ambaye aliingia chumbani humo kimyakimya alimzindua Joram.
Joram alitabasamu, “Kinywaji cha upweke kamwe hakipandi, mpenzi. Ungekuwa chumbani humu, macho hayo mazuri yakiendelea kuniloga, chupa hili lingekuwa limekauka kitambo,” alisema kwa utani.
Kauli hiyo ilimfanya Mona Lisa aangue kicheko. “Kweli hukupata mapenzi ya bibi,” baadaye alisema. Akaketi na kujimiminia toti mbili za pombe hiyo kali na nusu glasi ya soda ya maji. “Unalazimisha utani hata pale ambapo haupo! Nina nini mie hata kuwepo kwangu kukufanye unywe mzinga mzima kama huo!”
“Hujui una nini!” Joram alimjibu, kauli ambayo ilimfanya Mona Lisa azidi kucheka huku haya zake zikianza kumrudia. Shingo yake ndefu aliilaza upande kidogo, macho yake kiasi yakilainika huku vidole vikiitua glasi ya kinywaji chake na kuanza kutekenyana.
Ilikuwa picha ya kusisimua, picha ya kuvutia, picha ambayo, kwa muda ilifanya fikra za Joram zichukue likizo na nafasi yake kuchukuliwa na hisia za ajabu, hisia za kimaumbile zilizomfanya Joram Kiango awaze; faraja iliyoje kumkumbatia msichana huyo akiwa kama alivyozaliwa! Fahari iliyoje kukumbatiwa na mikono hiyo laini! Hadhi iliyoje kumbusu mrembo kama huyu!
Mara Joram akainuka.
Mona Lisa akazinduka, “Vipi, mbona umeinuka?” alimuuliza kwa mshangao.
“Nadhani ni wakati muafaka wa kuondoka.”
“Kwa nini? Nilidhani kwa kuwa huko hapa ningefungua kompyuta na kuchapa sura mbili tatu za kitabu changu ili uziangalie,” Mona aliongeza.
“Hata mimi ningependa iwe hivyo,” Joram alimjibu. “Kwa bahati mbaya haiwezekani.”
“Kwa nini?”
“Unamfahamu mtu anayeitwa Mike Tyson?”
“Kama ni yule bondia, Mmarekani mweusi, nadhani namfahamu.” Mona Lisa alimjibu, kiasi akionyesha mshangao.
“Unafahamu kuwa aliwahi kufungwa?”
“Nafahamu. Alibaka,” Mona alijibu kwa haya kidogo.
“Nani anafahamu kuwa alibaka?” Joram alihoji. “Kinachofahamika ni kuwa alimkaribisha msichana mrembo chumbani kwake hadi kesho yake. Siku mbili baadaye msichana huyo alidai kuwa amebakwa. Tyson akaenda jela.”
Mona Lisa alimkazia Joram macho. Kiasi fulani hasira na mshangao vilijitokeza katika macho hayo, ingawa sauti yake ilikuwa ileile ya upole, “Sijakuelewa, Joram. Una maana kuwa mimi pia naweza kukugeuka kuwa ume… umenibaka!”
Joram akatabasamu kumtoa wasiwasi. “Ninachojaribu kusema hapa,” alimwambia. “Ni kile ambacho watu wengi hapa nchini hawajakitia akilini. Kuwa bunge letu limeshapitisha sharia kama ileile iliyomfanya mbabe Mike Tyson asote gerezani kwa muda mrefu. Mimi ni mtu mwenye maadui wengi katika nchi hii. Na nimejikaribisha mwenyewe chumbani humu. Chochote kinaweza kutokea.
Joram alipomwona Mona Lisa bado kaduwaa, aliongeza harakaharaka, “Isitoshe, nina miadi na msichana mrembo sana jioni hii hotelini kwangu.”
“Msichana gani tena huyo?” Mona Lisa aliuliza.
“Anaitwa Mona Lisa. Kwani hutakuja?”
Mona Lisa aliangua kicheko. Bila kutegemea alijikuta akimkumbatia Joram, ambaye, yeye pia bila hiari yake, alijikuta akimbusu.
Mona aliupokea ulimi wa Joram. “Ni-ta-ku-ja!” alinong’ona kwa taabu.


NB: HII STORY UTAIMALIZIA UKIPATA NAKALA YAKO USIJE UKASEMA SIKUKWAMBIA.
 
Ntakutafuta kwa hard copy. Hizo namba zako kwenye uzi mwingine ziko 'active' muda wote?
 
Back
Top Bottom