Katika uhai wake wote wa kimatibabu Daktari Omari Shaka, hakupata kupokea mgonjwa wa aina hii, mgonjwa ambaye alijileta mwenyewe hospitali, huku akigugumia kwa maumivu, lakini akakatalia vipimo na dawa zote isipokuwa ‘kitanda’ na ‘vidonge vya usingizi tu.’ Mgonjwa huyohuyo alionekana mchovu kiafya na kiuchumi, bila kudaiwa, alitoa shilingi 50,000 kama malipo ya awali ya gharama za matibabu yake.
Daktari alichukulia siku hiyo kama siku mpya, ambayo ilianza na maajabu.
Ilikuwa ndio kwanza anaingia kazini, kushika zamu ya daktari mwenzake ambaye alimaliza saa kumi na mbili asubuhi. Ikiwa hospitali yao binafsi, mpya, iliyojengwa katika eneo la watu wenye kipato cha chini, siku zote kwao wagonjwa waliendelea kuwa bidhaa adimu. Si kwa kuwa magonjwa yalikuwa yamepungua, la; isipokuwa gharama za matibabu ndizo zilizokuwa zikiwakimbiza. Wengi waliugulia majumbani na kupoteza maisha. Wengi walikimbilia kwa waganga wa jadi ambao waliwapokonya hadi senti za mwisho bila uhakika wa tiba. Wengi, kati ya wachache waliokuja hospitalini hapo, waliondoka na madeni makubwa na, hivyo, kutorejea tena.
Hivyo, anapokuja ‘mgonjwa’ mwenye shilingi elfu hamsini mkononi, na madai ya kuujua vizuri ugonjwa wake, kwamba anachohitaji ni kitanda cha mapumziko na vidonge vya usingizi, baada ya hapo ndipo atakubali vipimo, nani amkatalie?
Alilitupa chini gazeti alilokuwa akilisoma na kuvuta jalada jipya ambalo aliliandika tarehe na kisha kumgeukia mgonjwa wake.
“Jina lako?”
“Sharif Mkono wa Birika.”
“Umri?”
“Miaka sitini na tano.”
“Unakoishi?”
“Kinondoni B”
“Mjumbe…” na kadhalika na kadhalika.
“Una hakika kuwa usingependa kupimwa walao presha? Unajua tuna taratibu zetu…”
“Daktari vipimo vyote utachukua. Lakini baada ya mapumziko yasiyopungua masaa ishirini na nne. Najifahamu, Daktari. Niwahishie kitanda, tafadhali.”
Alipatiwa kitanda katika chumba pekee maalumu hospitalini hapo.kilikuwa chumba chenye vitanda vitatu, yeye akiwa mgonjwa pekee, jambo ambalo lilimfurahisha sana. Baadaye nesi alipomletea vidonge viwili vya piritons, alivipokea na kusingizia kuvimeza. Alikunywa maji matupu, akamrejeshea nesi glasi na kisha kujifunika gubigubi. Muda mfupi baadaye alisikika akikoroma kwa mbali.
Joram alikuwa amejisingizia ugonjwa ilia pate nafasi ya kujificha, akiwa ametulia, ili aweze kupata fursa ya kufikiri na kutafakari kwa kina kitu gani kinamtokea, nini kinachofuata na achukue hatua zipi kukabiliana na hali hiyo.
Kutoweka lilikuwa jambo la awali na muhimu sana. Alijua kwa vyovyote usingepita muda kabla ya mauaji hayo kuarifiwa polisi nay eye angekuwa mtuhumiwa wa kwanza. Kwa tabia ya polisi wa Tanzania, nap engine kote duniania, alijua ambacho wangefanya ni kumkamata kwanza na kuanza upelelezi baadaye. Akiwa na pingu mkononi, nyuma ya nondo kubwa, Joram alijua kuwa huo ungekuwa mwisho wa ndoto yake ya kukielewa kiini cha mkasa huo na mwisho wa dhamira yake ya kumwadhibu yeyote ambaye amemuua msichana mpole kama yule, mzuri kama yule, malaika asiye na hatia yoyote.
Uamuzi wa kujificha hapa kwa muda aliuchukua mara alipotoka pale hotelini. Alijua fika kuwa pindi taarifa za mauaji zitakapowasilishwa kwenye vyombo husika, na yeye kutajwa kama mtuhumiwa, msako kabambe dhidi yake ungetangazwa. Nchi jirani n azote zilizo katika mkataba wa INTERPOL pia zingeusishwa. Hoteli na majumba yote ya wageni yangepekuliwa, madanguro na magenge yote yangekaguliwa. Hata magari mabovu na magofu yote jijini yangechunguzwa. Joram alikuwa na hakika kuwa mahala pa mwisho ambapo polisi wangepafikiria kumtafuta, ni hapo, wodini.
Kichwani mwake hakuona kama ni jambo jema sana kujisingizia ugonjwa, akichelea kuwa unaweza kumchukiza Mungu ukajikuta umekuwa mgonjwa kwelikweli.
Aliwahi kusoma mahala Fulani, juu ya mtu mmoja kule Harare, wakati ule wa shida kubwa ya mafuta kufuatia vikwazo vya kiuchumi dhidi ya nchi ile, kwamba walisubiri mgao wa mafuta tangu saa mbili usiku na kuja kuyapata saa tisa alfajiri. Magari pekee yaliyotiliwa maanani yakiwa yale yaliyobeba wagonjwa au maiti. Hivyo jamaa Fulani walilazimika kununua jeneza na sanda, mmoja wao akijilaza katika jeneza hilo na kuvishwa sanda. Wakapatiwa mafuta na kuondoka zao. Lakini walipofika mbele ya safari na kusimamisha gari ili wamtoe mwenzao walimkuta tayari amekufa kikweli kweli. Msiba wa kusingizia ukaanza upya.
“Yasije yakanitokea hayo…” Joram aliwaza huku akicheka kimoyomoyo ndani ya shuka zake za hospitali alimojifunika.
Akaituma akili yake kuanza kufikiri kwa makini Zaidi. Jambo la awali ambalo hakuona kuwa lilihitaji kumpotezea muda ni vipi muuaji alivyoweza kuingia chumbani mule na kumuua Mona Lisa kwa risasi, yeye akiwa kwenye usingizi wa pono. Bila shaka muuaji huyo aliwapulizia dawa ya usingizi na, hivyo, kuingia chumbani humo na kufanya mauji yake kwa kutumia bastola yenye kiwambo cha kuzuia sauti bila yeye kuwa na habari.
Alihisi dawa hizo hadi sasa bado ziliufanya ubongo wake ushindwe kufanya kazi yake kwa kiwango chake halisi.
Hata hivyo, akiwa kitandani hapo, taratibu aliona kama utandu katika ubongo wake ukianza kudondoka na mambo kadhaa aliyokuwa akiyaona katika hali ya ukungu yakianza kutoweka na kuonekana katika hali yenye uhalisia Zaidi.
Kilichozindua akili yake ni pale alipokumbuka kumwona Daktari Omari, wakati akimwandikia cheti, aliandika kitu kama jumatatu, tarehe 25 Septemba! Hata gazeti lililolala pale mezani pake lilikuwa la Jumatatu.
Jumatatu! Joram alishangaa. Alikumbuka vizuri sana, kwamba alikutana na Mona Lisa siku ya Jumamosi na aliingia naye chumbani mle usiku mwingi wa Jumamosi ileile. Ilikuwaje aamke, akiwa amemkumbatia Mona Lisa yuleyule, au maiti yake, siku ya Jumatatu? Inawezekana kuwa walilala chumbani mule kwa takribani saa ishirini na nne? Inawezekana!
Joram aliituma akili yake kufikiri. Alizirudisha fikra zake kama mkanda wa picha toka pale Mona aliporejea ghafla na kumwambia “Mpenzi nimerudi…” kinyume cha rai yake ya awali kurudi kesho yake. Aliufikiria uchangamfu wake uliomfanya ajikute yuko naye chumbani. Aliufikiria utundu wake kitandani uliopelekea ajione kuwa yuko peponi anayeburudishwa na malaika halisi. Akaifikiria ile kauli yake ya mwisho, kabla usingizi haujampitia.
Muda mfupi baadaye.
“Ni kweli hujui… Hujui kama unabaka. Na unambaka afisa wa ngazi ya juu wa Jeshi la Polisi…”
Kicheko.
“Sikujua… nilidhani mimi pia nimebakwa.”
Kicheko.
“Ni wazi kuwa hujaipitia vizuri sheria ya ubakaji. Mwanaume habakwi, anabaka. Unaijua adhabu yake?”
“Sijui.”
“Miaka ishirini na minane jela. Lakini kwako wewe adhabu hiyo haitoshi. Utafungwa kifungo cha maisha, pingu mkononi.”
Kicheko.
“Naanza lini kuitumikia adhabu hiyo?”
“Toka sasa uko chini ya ulinzi. Huruhusiwi kukutana na mwanamke mwingine. Huruhusiwi kuoa wala kuolewa…”
Kicheko. Usingizi…
Kwa mujibu wa kumbukumbu iliyomjia Joram hayo yalikuwa maongezi yake ya mwisho na Mona Lisa kabla hajaamka na kujikuta akiwa amekumbatia maiti yake, tundu kubwa la risasi kifuani pake likiendelea kuvuja damu.
Huo ulikuwa usiku wa Jumamosi au alfajiri ya Jumapili. Kilichomshangaza ni hii hadithi mpya ya kuwa leo ni Jumatatu. Ukweli ni upi, Jumapili au Jumatatu?
Joram hakuona kama alikuwa na haja ya kuupoteza muda wake kufikiria kama leo ilikuwa Jumapili au Jumatatu. Kama daktari ameandika tarehe ya Jumatatu na kama hata gazeti lilikuwa la Jumatatu, kwa vyovyote siku ya leo ni Jumatatu. Alichohitaji kufanya ilikuwa ni kukusanya akili yake ili imwambie kitu gani kilimtokea hata akalala kwa saa ishirini nan ne bila kujua kinachoendelea.
Ilikuwaje? Alijiuliza.
Taratibu, ule utandu uliokuwa ukiudumaza ubongo wake ukaanza kumtoka na picha mpya kuingia akilini. Ilikuwa kama mkanda wa video ambao unarudishwa nyuma na kuchezeshwa upya.
Sasa alikumbuka vizuri kabisa kuwa mara baada ya Mona kumwambia, “Huruhusiwi kuoa wala kuolewa…” na usingizi kuwachukua, Mona Lisa alitoweka.
Joram alibaini kutoweka huko pale alipoamka na kushituka mida Fulani baina ya saa tatu au nne na kujikuta peke yake. Ubavuni mwake, pale alipolala Mona Lisa, sasa palikuwa na mto ambao yeye, Joram, aliukumbatia. Hakujali, akijua kuwa msichana huyo alikuwa ameondoka kimyakimya kwa kuchelea kumsumbua. Akaurudia usingizi wake ambao aliuchapa hadi saa saba za mchana huo. Baada ya kuoga, kunywa supu na chupa mbili za club soda alirejea chumbani kwake ambako alijilaza chali na kuendelea na mswada wa Mona, UBONGO WA MWALIMU NYERERE.
Ilikuwa riwaya tamu. Ilimvutia na kumsisimua kiasi kwamba alijikuta amezama moja kwa moja katika msitu huo wa maneno yaliyopangiliwa kisanii. Ilimwia vigumu Zaidi kuamini kuwa mbunifu mwenyewe alikuwa msichana mpole na mrembo kama yule. Ufundi wa matumizi ya lugha, hila katika mpangilio wa matukio na Zaidi ya yote uhalisia wa matukio ya mambo katika hadithi hiyo ni miongoni mwa mambo yaliyomfanya Joram amezwe moja kwa moja, bila kujua kuwa muda umekwenda, hadi aliposikia mlango wake ukigongwa.
Kabla ya kuinuka kuufungua aliitazama saa yake ya mkononi. Tatu kasoro! Hakuamini. Alipoufungua mlango umbile zuri la Mona Lisa lilikuwa limesimama pale, tabasamu lenye hayahaya na kutojiamini likiwa limechanua usoni pake.
“Darling! Karibu sana,” Joram alisema akimshika mkono na kumvuta ndani ambako alimkaribisha tena kwa busu jingine.
Kiasi fulani Mona Lisa alionyesha kushangazwa na mapokezi hayo. Alimtazama Joram kwa muda, kisha akayakwepa macho yake na kujiinamia. Joram pia alishangazwa na hali hiyo. Muda mfupi tu uliopita ulikuwa mchangamfu kuliko mie, mara hii umebadilika tena! Achana na tabia hizo za kinyonga! Alitamani kumweleza. Lakini hakufanya hivyo. Badala yake alimwambia taratibu, “Chumba hiki chako, chagua kukaa ama kitandani, ama kwenye kochi.”
Mona aliliendea kochi na kuketi.
“Kitabu chako kimenishika kwelikweli,” Joram alimwambia. “Sikujua kama muda umeisha kiasi hiki. Nikuagizie chakula na kinywaji gani?”
Mona alitabasamu, “Kizuri?”
“Kitu gani?”
“Kitabu. Ni kizuri kweli?”
Joram akatabasamu. “Kizuri kama alivyo mtu aliyekiandika. Kikitoka utapata washabiki kila pembe ya dunia. Utakula nini?”
“Unaamini kitakubaliwa?” Mona alihoji tena kwa shahuku.
“Ni mchapishaji kipofu wa taaluma peke yake anayeweza kukataa kitabu kama hiki. Ingawa kuna mambo mawili matatu atakayoyatoa na kuyaongeza. Hata hivyo, sijafika mwisho,” Joram akasita, “Hujaniambia utakula nini na utakunywa nini.”
Ilikuwa dhahiri kuwa akili za Mona hazikuwa kwenye chakula wala kinywaji, bali kwenye maandishi yake, hali ambayo ilimshangaza Joram. Jana hakukitaja kabisa kitabu hicho, leo hataki kusikia jambo lolote Zaidi ya kitabu.
Kinyonga!
“Siwezi kukaa hapa na msichana mrembo kama wewe, bila kumkirimu walao maji ya uhai. Nawapigia jikoni watuletee kuku mzima, chupa mbili za wiski na tonic. Sawa?”
Joram alisubiri jibu la Mona Lisa.
“Samahani sijisikii kula wala kunywa chochote.”
“Kwa nini? Za jana bado zipo kichwani?”
“Jana!” ilikuwa zamu ya Mona Lisa kushangaa. “Jana nimekunywa wapi! Sijawahi kunywa pombe toka nizaliwe.”
Joram hakuyaamini masikio yake.
“Wacha mzaha Mona,” akamwambia akicheka. “Jana umerudi hapa ukanipa company ya nguvu, ukanywa kiasi cha kunifariji hapo kitandani hadi ulipotoweka bila kuniaga!”
Kilichofuata baada ya hapo Joram hakukitegemea. Joram alimwona Mona Lisa akisimama na kumtumbulia macho ya mshangao, akiwa ameusahau mdomo wake wazi, huku akitetemeka mwili mzima. Taratibu mshangao ulianza kutoweka katika macho yake na nafasi yake kuchukuliwa na hasira, hasira za mwanamke, hasira ambazo Joram, pamoja na ujabali wake wote hakupata kuziona kwa mwanamke yeyote yule. Lakini hali hiyo pia ilitoweka taratibu katika macho yake na nafasi yake kuchukuliwa na kitu kama msiba au maombolezo, jambo lililofuatiwa na kilio cha kwikwi, kwa sauti ndogo, huku machozi mengi yakimtoka.
Kwa Jpram Kiango ile picha ya kusisimua ilikuwa imerudi, picha ya msichana mpole, mrembo, mwenye maumivu Fulani rohoni mwake, picha ya malaika anayeteseka! Ambayo mwanaume yeyote asingeivumilia. Hivyo, bila ya kujipa wasaa wa kutafakari Zaidi alimwendea na kumkumbatia. Akamvuta taratibu hadi kitandani ambako alimketisha na baadaye kumlaza huku akiwa amemkumbatia, mkono wake wa pili ukijipa kazi ya kumfuta machozi.
Mona alinyamaza kidogo na kumuuliza Joram kwa sauti ya mnong’ono, “Unaniambia kweli, Joram?”
“Kwamba?”
“Kwamba jana nimerudi hapa na kuwa nawe hadi asubuhi ya leo?”
“Kwa nini nikudanganye?” Joram alimjibu kwa swali vilevile. “Kwani kulikoni, Mona, mbona sikuelewi!”
Mona akaanza kulia tena. Baadaye alinong’ona tena kama anayezungumza peke yake. “Hata wewe! Hata Joram Kiango! Nifanye nini jamani?”
“Kuna nini?” Joram alihoji tena. “Kuna jambo gani la muujiza wewe kurudi hapa na kuwa name?”
“Hujui Joram, hujui; huelewi. Na uwezi kuelewa,” Mona alisema na kuongeza, “Hujui kuwa tayari nimeyaweka maisha yako hatarini. Sijui kitu gani kinachonitokea. Lakini naamini nimekuweka katika hatari kubwa sana katika maisha yako.”
“Hatari gani?”
“Ya kifo.”
Joram akaangua kicheko. “Yaani kufurahi na wewe usiku mmoja kwangu ni hukumu ya kifo! Acha mzaha Mona. Mie sio mshirikina kiasi hicho!”
“Joram, hufahamu,” Mona aliongeza. “Kwanza, hukulala na mimi. Halafu, suala la ushirikina halipo.”
Joram akacheka tena. Akasema, “Kwa hiyo tuachane na ushirikina. Twende kwenye elimu ya akhera. Ni kwamba nimelala na jini linalotumia sura yako, jini ambalo baadaye linatiua, sio? Usinichekeshe Mona”
“Huwezi kuelewa,” Mona alinong’ona tena. Ingawa sasa kile kilio cha kwikwi kilikoma, machozi yaliendelea kutiririka juu ya mashavu yake laini, Joram akiendelea na kazi ya kuyafuta na kumfariji.
Kuna ugonjwa Fulani. Ugonjwa adimu, ambao ni madaktari wachache hadi sasa wanaoufahamu. Ni aina fulani ya matatizo ya akili ambapo mhusika hujikuta amesahau yeye ni nani na kujihisi kama mtu mwingine kabisa mwenye jina na tabia tofauti. Akiwa katika hali hiyo anaweza kufanya chochote, hata kuua bila kujua analolifanya.
Maradhi hayo yanaweza kumfanya mtu kuwa na nafsi mbili au tatu zenye majina na tabia tofauti. Anaweza kuwa Amina, Asha au Aisha kivitendo na kitabia kwa nyakati tofauti. Wakati mwingine Amina au Asha huyo anaweza kuchukiana au hata kuoneana wivu na Aisha, kwa kutegemea wakati huo mgonjwa yuko katika taswira ipi.
Zipo kesi kadhaa za aina hiyo, baadhi zikihusisha hata mauaji, lakini watuhumiwa wakaachiwa huru na mahakama baada ya kuthibitisha kuwa wanaugua ugonjwa huo.
Joram aliamini kuwa Mona Lisa alikuwa na tatizo hilo. Aliamini kuwa alipomfuata jana na kunywa, ambako anaapa kuwa hajawahi kunywa maishani, alikuwa katika taswira yake mpya amabayo yeye binafsi haifahamu, taswira ya msichana wa kileo, sister doo, asiye na haya na mwingi wa mbwembwe.
Ni hilo lililomfanya aamue kumfariji na hata pale Mona Lisa alipoomba kuondoka Joram alikataa katakata kwa maelezo kuwa asingemruhusu kuondoka katika hali hiyo.
“Joram, mara hii naona unafanya jambo ambalo hujui hatma yake. Laity ungenisikiliza…” Mona alimtahadharisha.
“Najua… Usijali…”
Wakiwa katika hali hiyohiyo ndipo usingizi ulipowapitia. Na ndipo Joram Kiango alipozinduka alfajiri na kujikuta akiwa amekumbatia maiti ya aliyekuwa Mona Lisa huku tundu la risasi katika kifua chake likiendelea kuvuja damu.
Ndivyo ilivyokuwa.