HADITHI: KIZUIZI
SEHEMU YA KUMI NA MOJA
"Mama naulizia godoro lililokuwa chumbani kwangu...."
"Mguu wako na godoro kipi bora??" mama akauliza swali gumu....Jose B akauma memo kwa ghadhabu, na alikuwa ametaharuki. Ndani ya lile godoro kulisaliwa na takribani milioni moja na laki tano.
Sasa halipo lile godoro.
Kizuizi!!
Mama akatoweka akimwacha Jose B akihangaika kujiuliza na kujipatia majibu. Majibu ambayo si sahihi.
Usiku ule ulipita Jose akibakia kuwa mlinzi wa familia. Hakulala kabisa, alilia machozi kama kuna msiba ulitokea.
Muda wote aliotumia kuzisaka pesa zile, sasa hana hata senti.
Inauma sana.
Harakati za Jose B kurejea jijini Dar kwa ajili ya kufanya biashara zikaanza kupotea.
Atatoa wapi nauli, atatoa wapi pesa ya kuishi jijini Dar wakati akifuatilia biashara yake??
Kizuizi kikubwa sana.........****
Jose B, mlinzi bila silaha alikurupuka na kuanza kufagia uwanja majira ya saa kumi na moja na nusu. Hakuwahi kufagia kwa sababu alikuwa anapenda usafi. La alikuwa amepagawa bado. Hakuamini kama milioni na ushee zilikuwa zimeuzwa sanjali na godoro.
Huenda liliuzwa elfu hamsini. Elfu hamsini pamoja na milioni kadhaa, biashara nzuri kupita zote duniani. Lakini muuzaji ni mmoja kati ya watu washenzi kupata kutokea duniani.
Jose B aliendelea kulalamika hovyo hovyo, mara atupe uchafu ambao ameuzoa tayari.
Kijana alikaribia kuchanganyikiwa.
Alijisachi mifukoni, mara arudishea alivyovitoa awali na kuvihamishia katika mfuko mwingine.
Alisikitisha sana. Pesa asiyoitolea jasho ilimuhuzunisha.
Katika kujipekuapekua mara alifanikiwa kukamata simu kutoka katika mojawapo ya mifuko yake.
Ilikuwa simu yake.
Kuitazama simu ile mara ikarejea na kumbukumbu ya jiji la Dar es salaam. Akazikumbuka namba zilizotajwa katika mojawapo ya chumba katika nyumba za kulala wageni jijini humo.
Namba za mke wa James ambaye alikuwa akiisaliti ndoa yake ambayo hata haikuwa na miezi miwili, Jose B akaanza kuziimba zile namba kama mtoto mdogo anayekariri alfabeti.
Dili!!
Akalipuka kwa furaha Jose B, na kisha kujiaminisha kuwa huenda yeye ni mzuka uliofufuka.
Kwa mara ya kwanza baada ya muda mrefu Jose B akaiwasha simu yake.
****
Nyumba kubwa ya vyumba vitatu pamoja na sebule ilionekana kupwaya sana kwa kukaliwa na watu wawili. Furaha ilikuwa kubwa kutokana na kumngojea mzaliwa mpya.
James na Emmy wote kwa pamoja waliungoja ujio wa mtoto katika nyumba yao.
Kila mara walizungumzia juu ya mtoto, mwingine angesema atazaliwa wa kiume mwingine alisisitiza kuwa lazima awe wa kike.
Simu iliyoita ilikatisha ubishi huu ambao haukuwa na dalili za kumalizika.
Ilikuwa simu ya Emmy.
James akajongea kuifuata akaitazama, ilikuwa namba mpya kabisa.
Akamshirikisha mkewe.
Emmy akamwomba apokee.
"Hapana ...sio utaratibu mzuri mke wangu....je kama ni rafiki zako watajifikiriaje??" Jimmy akapinga.
Emmy akakubaliana naye, lakini kabla simu haijapokelewa ikakatika baada ya kuwa imeita kwa muda mrefu.
Walingoja huenda angepiga tena. Hakupiga.
Wakaendelea kupata chakula huku ubishi wao ukisahaulika.
Baada ya chakula. Emmy akiwa uani akiosha vyombo akasikia tena simu yake ikiita.
Safari hii, James alikuwa amelala hakuisikia.
Emmy akaitwaa. Namba nyingine tena.
Akapokea.
"Mambo shem...."
"Poa vipi.." alijibu kwa mkato sana.
"Huku kwema..mimi ni...hauwezi kunijua jina lakini nilikupokea siku ile ulipokuja kwa Lameck....." alijitambulisha. Emmy akawa amemkumbuka. Mapigo ya moyo yakaenda kasi sana.
"Nimekukumbuka nambie...."
"Nilikuwa nakusalimia tu...Lameck amewasiliana na mimi akanipatia namba yako nikusalimie..alifika salama.." Simu ikakatwa wakati huyu bwana anaendelea kutoa hizo salamu.
Emmy hakutaka kusikia chochote juu ya Lameck japo katika nafsi yake alikiri waziwazi kuwa yule bwana anajua kukipendezesha chumba kuliko mumewe.
Lakini hakuwahi kumwonyesha mumewe kuwa anachukizwa na jambo hilo.
Emmy akiwa bado amenuna huku akihema juu juu mara ikaingia simu nyingine.
Namba mpya tena.
Akaitazama na kuwaza kuwa huenda ni yule yule bwana amepiga. Lakini akapingana na hisia zake akaipokea ile simu.
Sauti inayojiamini, ya kiume ikatawala kutoka upande wa pili.
"Mambo shem." Salamu kama ya awali lakini sauti tofauti.
"Poa nani samahani."
"Unaongea na......eeh samahani mumeo yupo hapo jirani?"
"Anahusika vipi katika maongezi haya.." Emmy aliuliza huku akiizuia jazba yake kutokana na swali lile.
"Hausiki hata kidogo ndo maana nimekuuliza kama yupo nisitishe simu hii ili tuzungumze baadaye."
"Ongea tu...umeniita shem halafu unamuhofia mume wangu nini tatizo?"
"Tatizo ni haya maongezi mafupi kati yangu na wewe."
"Kwanza wewe nani kwa jina."
"Sam wa pili."
"Mh!! Ninadhani hatufahamiani."
"Yeah. Lakini maongezi haya yatakuwa mwanzo mzuri wa kukumbushana wapi tulipoonana shem wangu."
"Wapi tumeonana?" sasa alikuwa ameshindwa kuizuia jazba, sauti kali ikamtoka.
"Ubungo....Ubungo dare s salaam." Sauti ya kiume ilijibu pasipo kujiamini sana.
"Ubungo kubwa kakangu ni mwaka gani..ongea ueleweke basi ...."
"ZamZam guest house, unapakumbuka."
"Nadhani umekosea namba...samahani nipo katika ndoa naomba uniheshimu tafadhali."
"Haya nakutakia siku njema, msalimie mumeo mwambie kuna jamaa anaitwa Sam wa pili alikuchungulia wakati unatoka hospitali, kisha ukaenda Ubungo kufanya uzinzi na jamaa....na kama ikibidi mpatie namba yangu ili nimueleze vizuri picha zima lilivyokuwa, bahati nzuri nakumbuka hadi nguo yako ya ndani ilikuwa ya rangi gani, na maongezi yenu nilirekodi......sikia dada sio siri unajitahidi sana. Japo nimefanikiwa kukuona mara moja tu nimeamini kuwa unajua sana haya mambo......amakweli James amelamba dume. Vipi bado unahitaji heshima?" alimaliza mazungumzo kwa mbwembwe huyku akimuachia uwanja mwanadada Emmy wa kujifalagua kama alivyoanza awali kwa kujiita kuwa yupo katika ndoa.
Emmy kimya, pumzi zikipishana kwa kasi, miguu ikiwa imeishiwa nguvu na glasi aliyokuwa ameshika mkononi ikiwa imeanguka chini, ilikuwa bahati kuwa haikuvunjika.
Emmy hakuwahi kutegemea kuwa anaweza kupigiwa simu kama hii na kuelezwa habari nzito kama hizi zisizokuwa na hata chembe ya uongo ndani yake.
Binti wa watu akapagawa. Akataka kusema neno lakini atasema neno lipi.
"Mama James nakusikiliza...." upande wa pili ukauliza kwa sauti tulivu.
"Samahani....naomba kama unaweza tuonane pliiz.....nisaidie kaka yangu nisaidie jamani...'
"Ndo maana nimekuomba umpe James hii namba ili niweze kukusaidia kumsimulia ile filamu ambayo umeicheza halafu ukaishiwa vocha ukamuomba kidume akurushie....." Maneno makali na yenye kuumiza yalizidi kushambulia katika namna ya utani.
Emmy akakimbilia katika choo cha nje akajifungia humo kisha akaendelea kuongea.
"Jamani kakangu pliiiz...ndo kwanza nina mwezi katika ndoa yangu nakuomba tafadhali nakuomba tuonane..nitakupa utakacho tafadhali....nakuomba kaka nipo chini ya miguu yako..nakuomba kaka nisikilize kaka nakuomba...." Emmy alisihi kwa kila namna.
"Nitakupigia......msalimie mumeo." Aliyamaliza mazungumzo haya katika namna ya kipekee, alikuwa kijana yuleyule ambaye anafanya mambo ambayo ukisimuliwa huwezi kuamini. Lakini nani atakusimulia iwapo anayafanya bila kumshirikisha mtu?? Akili yake aliijua yeye mwenyewe. Jose B waukweli. Kijana wa Mwanza.
Jose B baada ya kumsikia mwanadada yule akitetemeka alianza kuzisahau shida zake, kauli ya yule dada kuwa atampa chochote kwa kumuokolea ndoa yake ambayo haijakomaa bado ilimpa nguvu sana na kuamini kuwa hana haja ya kujutia zile milioni zilizouzwa pamoja na godoro.
Jose B akajiweka katika kundi la washindi, kundi lisilojua lolote juu ya kushindwa.
Jose B akawa kinara.
Sasa alikuwa katika nafasi ya kumuongoza mwanadada emmy kwa namna aliyotaka yeye.
Jioni ya siku hiyo akampigia tena simu, wakafanya mazungumzo marefu katika hali ya utulivu. Mazungumzo haya kwa maneno yalitawaliwa na Jose B. Emmy akawa msikilizaji tu.
Wakafikia maelewano.
****
Hali ya amani ilikuwa hafifu kiasi fulani. Raia hawakuwa na amani na serikali yao kabila la Dunka lilikuwa linaongoza kwa kupoteza mamia ya watu katika machafuko hayo.
Nyumba za tope zilikuwa zimesambaratishwa kwa wingi na mamia ya watu kukosa makazi.
Hali ilikuwa tatanishi.
Ni familia chache sana zilisalimika bila kuwa na misiba.
Ilikuwa afadhali kwa upande mwingine wa Sudan kuliko upande wa Sudani ya kusini. Hali ilikuwa tete zaidi.
Maisha yalikuwa duni sana. Na asilimia kubwa hawakuijua kesho yao.
Mindombinu haikutiliwa maanani na serikali, macho ya wanajeshi yalikuwa yakitazama hali hii.
Lameck akiwa mmoja wao, gari la kijeshi lilikuwa linayumbayumba katika barabara mbovu kabisa katikati ya mji.
Lameck alijiuliza kulikuwa na umuhimu gani wa kugunduliwa kwa uvunaji wa mafuta katika ardhi ya Sudani mwaka miaka ya 1978. Mafuta hayo hayakuleta mabadiliko yoyote katika ardhi ile zaidi ya raia kuendelea kugandamizwa na kuteseka.
Lameck alifumba macho na kukumbuka maeneo mbalimbali kama mkoa wa Mara nchini Tanzania, akauweka katika rada mgodi wa Nyamongo.
Kisha akafumbua mamcho na kusema ‘yaleyale'.
Hakika yalikuwa yaleyale.
Gari lilisimama, kiongozi wa msafara akawagawanya wajeshi hao waliokuja kwa lengo la kulinda amani katika vikosi mbalimbali. Kisha wakatawanyika, silaha mkononi.
Hapo ndipo uoga ulipomuanza Lameck.
Katika giza nene, hali tulivu inavurugwa na waasi. Milio inaanza kusikika, kila mwanajeshi anajiweka tayari huku akipokea ishara kutoka kwa mkuu wa msafara.
Siku ya kwanza ikapita, ya pili na ya tatu....hatimaye hali ile ya waasi kutokea na kutoweka ikaanza kuonekana ya kawaida tu kwa wanajeshi wageni.
Mazoea hujenga tabia. Lameck naye akazoea na kujiona jasiri sana huku akishangaa ilikuwaje akaijutia nafasi kama ile ya kuliwakilisha taifa kisha akirejea anakuwa na nyota ya ziada na heshima kubwa kama shujaa.
Ikafikia siku isiyosahaulika kirahisi, siku inayotia huzuni na kuihamisha simulizi mahala pasipotarajiwa.
Lameck alivutiwa kuitazama jamii ya watu kadhaa waliomzunguka, maisha yao yakiwa kulala nje ama katika mahema. Hawakuwa na makazi.
Suala hili lilimgusa sana, alijisikia kama yu mmoja wao.
Mwanamke mmoja ambaye anazeeka kutokana na shida lakini akiwa ni kijana anamtazama Lameck kwa macho makavu lakini sura inayolia.
Lameck anamsogelea na kumuuliza anaitwa nani, anajaribu kutumia kiingereza yule binti hamjibu kitu.
Anamkazia macho tu.
"She's from Nuer tribe" (Ni wa kabila la nua). Mhanga mmoja wa vita hii, kijana wa umri usiozidi miaka kumi na tisa anamweleza yule mwanajeshi kamili.
"So you may speak English." Lameck anamuuliza yule kijana naye anakubali.
Mazungumzo yanaanzia hapo. Yule binti anamfanya Lameck ajisahau kuwa yupo katika kulinda amani na kujikuta kama muhanga pia.
Simulizi ya binti yule inamfanya Lameck kuliacha lindo lake na kuongozana na yule binti mpaka eneo la nje kidogo ya mji.
Waliongozana na yule mtafsiri wao.
Huku walimkuta yule mwarabu ambaye anamyanyasa yule dada kijinsia, anawanyayasa na wadogo zake ili tu aweze kuwapatia chakula.
"Huwa ananiingilia na wenzake kadri wanavyotaka. Huwa ananipiga sana na wakati mwingine huniita sokwe. Alimuua mama yangu alivyojaribu kunitetea na alimnyonga baba...." hapa sasa hakuweza kusema lolote zaidi ya kulia.
Yule mwarabu hakutegemea ujio wa yule dada akiwa pamoja na mwanajeshi wa umoja wa mataifa lakini ana kwa ana na Lameck.
Lameck, hakuwa mzoefu wa vita. Na pale lindoni aliambatana na wakongwe ambao alitakiwa kujifunza kwao.
Huku kuwa peke yake na kuweka ubinadamu mbele kulimgharimu.
Jicho la Lameck lilishuhudia kifua cha yule dada kikisambaratishwa mara moja.
Wakati anajiweka sawa kukabiliana na shambulizi linalofuata. Ghafla likatokea tukio asiloritarajia.
Alichokiona mara ya mwisho kabla ya kiza kinene ni uso wa yule mwarabu ukitabasamu.
Kisha akausikia mlio wa bunduki.
Kiza kinene kikatanda, harufu ya damu ikatawala.
Kimyaa!!
****
Shughuli anayoifanya akaichukulia kuwa ni moja kati ya kazi bora kabisa kuwahi kutokea duniani.
Hakuamini kama alikuwa ni yeye ama la.
"Na hapa hata mkiaka thelathini bado." Aliwaza wakati wakipokea maelekezo ya jinsi ya kufunga mikanda.
Alijiona mshamba sana kwa kudhani kuwa mikanda ndani ya ndege ni rahisi kufunga kama kwenye gari.
Huku palikuwa na maelekezo tofauti kiasi.
Jose B wa ukweli akiwa anakwea usafiri huu wa anga kwa mara ya kwanza alikuwa mwenye furaha ya kipekee.
Hakuwa amemuaga mtu yeyote na alitegemea kufika jijini Dar na kurejea siku chache baada ya kumaliza biashara iliyompeleka.
Jose B akiwa katika kuitafakari safari hii. Kama iliyo kawaida alianza kujipangia ni kiasi gani ambacho atamtoza mwanadada Emmy kwa kumfichia siri ambayo anaimiliki.
Kwanza alitaka kufanyia bei chee lakini alipokumbuka kuwa alikuwa ametoka kupata hasara baada ya pesa aliyoitumia kuuza kizuizi kupotea kirahisi aliamua kumpangia bei ya juu.
"Milioni saba...na wala sifanyi aina yoyote ya mazungumzo ya kupunguza....kama hataki aache nitaiuza pengine..." Jose B aliwaza kwa tuo, kana kwamba ilikuwa biashara halali.
Akiwa hata hajapata wazo jingine, ndege ilitua katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa mwalimu nyerere jijini Dar es salaam.
Jose B akafuatisha ambayo wenzake walikuwa wanafanya.
Hatimaye akatoka nje.
Akiwa anashangaa shangaa akijiandaa kuiwasha simu yake ambayo aliizima akiwa anakwea ndege. Mara alisita baada ya kuona kama yu katika ndoto.
Binti mrefu wa wastani mwenye umbo lililojikata vyema na kuunda mfano wa namba nane alimkaribia huku akitabasamu.
"Karibu Sam wa pili." Alisema yule binti kisha akamuongoza Jose B katika gari iliyokuwa inawasubiri.
Wakajibweteka katika siti ya nyuma.
Dereva ambaye hapo kabla alikuwa amepewa maelezo ya wapi wanaelekea alifanya kama alivyoagizwa.
Moja kwa moja hadi Kijitonyama katika hoteli ya Grand Villa.
Chumbani.
Jose B akiwa hana hili wala lile, emmy akiwa na mambo mengi yanayopita katika kichwa chake.
Mshikemshike!!
*********************
**JOSE B katika biashara...safari hii amesema hapunguzi bei....ana kwa na na EMMY nini kitajiri??
**LAMECK matatani...risasi imelia damu imetawanyika na sasa yupo kimya...je ndo mwisho wake katika KIZUIZI.
***JAMES hajui juu yas usaliti wa mkewe na mke hakui siri kuu ya mumewe.......ITAFAHAMIKA ........
ITAENDELEA......