HADITHI: KIZUIZI
SEHEMU YA KUMI
Wawili wale wakakokotana hadi chumbani. Jose B akachungulia kwa mbali.
Ule uzuri wa gesti bubu ukawa faida kwa Jose B.
Chumba namba 18!!
Jose B akaweza kukisoma kile chumba walichoingia wawili hawa.
Lazima nijue kunani humo ndani haiwezekani yanipite. Jose B akajiapiza huku akikumbwa na hasira kana kwamba yanamuhusu ama ni mkewe ameingizwa humo ndani.
Uswazi ni uswazi tu. Upande wa nyuma wa ile nyumba ya kulala wageni ilikuwa ni chochoro ya kupita watu.
Jose B akashtukia huo mchezo.
Huku akichechemea akaanza kupiga mahesabu ya kupata udaku.
Laiti kama angekuwa mwandishi wa habari hizo. Basi angekuwa maarufu sana.
****
ENDELEA..............
Msichana dhaifu, mwenye macho mekundu, akatokea katika chumba baada ya masaa matatu kupita.
Alikuwa ana kila dalili ya kuchoka sana na ni kama alikuwa aidha katika maumivu ya nafsi ama mwili moja kwa moja.
Jicho la Jose B ambaye tayari alikuwa amedaka mawilimatatu kupitia dirishani liliweza kumuona.
Kilichomfurahisha Jose B na kujiona kijana anayefanikiwa upesi sana katika harakati zake na kuzisikia namba za simu za yule binti wakati akimtajia mwenza wake katika kile chumba. Alizitaja namba zake baada ya kuwa katika uhitaji wa kupata salio katika simu yake na yule bwana bila shaka alikuwa na salio la kutosha, akatajiwa namba kwa utulivu, Jose B naye akazinakiri kwa umakini katika ubongo wake.
Zoezi la kawaida kwa watu wenye tabia kama yake.
Namba hizo zikamsahaulisha Jose B wivu na matamanio aliyoyapata wakati akimsikia yule binti akigumia kimahaba katika chumba kile cha uchochoroni.
Jose B hakutaka kumfungia tela. Alimsindikiza kwa macho huku moyo wake ukiteketea kwa maumivu kadri yule binti alivyozidi kutikisika huku akipotelea mbali.
Jose B waukweli akafanya ishara ya msalaba, katika namna ya kumshukuru Mungu.
Sijui kwa lipi? Labda kumpatia ule umbea. Anajua yeye.
Akiwa hajapoteza kumbukumbu ya kituo alichoambiwa, alipanda taksi tena ikamrejesha hospitali ya taifa ya Muhimbili.
Bahati nzuri hakuna aliyeshtukia kutoweka kwake, kwani hakuwa chini ya uangalizi mkali kama awali.
Jose B akakirejea kitanda chake. Akafumba macho na kuitafakari siku hiyo.
Akamjengea picha yule bibi harusi aliyetoka kumuona katika luninga siku kadhaa nyuma lakini leo hii amemuona tena akiwa katika kuisaliti ndoa yake.
Roho ikamuuma. Akatamani sana kuitua siri hii kwani ilikuwa nzito sana kwake.
Ataitua kwa nani tofauti na muhusika wa mali hii. James.
Mtihani mkubwa.
****
Simu yake iliita majira ya saa nane usiku. Alipotazama aligundua kuwa alikuwa mkuu wake wa kazi. Hakuruhusu uzembe wa usingizi kuitawala sauti yake. Alipokea na kuzungumza kikakamavu.
Baada ya mazungumzo kuisha alianza kujiuliza ni nini kimemfanya mkuu wake wa kazi kumpigia simu usiku kama huo kisha kumweleza kuwa asubuhi na mapema alikuwa anahitajika ofisini.
Sheria ya jeshi ni kwamba ukiitwa huna haja ya kuuliza kwa nini umeitwa, hasahasa akiwa mkuu wako wa kazi. Cha msingi ni kutii amri.
Bwana Lameck naye alitii amri.
Asubuhi na mapema alikuwa katika ofisi ya aliyempigia simu. Cha kushangaza hakumkuta ofisini.
Alisubiri hadi majira ya saa nne asubuhi ndipo bwana mmoja mwenye kitambi alifika, alikuwa katika mwendo wa taratibu.
Lameck akasimama na kumpigia saluti.
Akaruhusiwa kuingia ofisini.
Baada ya salamu za awali. Likafuata kubwa aliloitiwa.
Ilikuwa safari ya kuelekea Sudani kusini, safari ya kijeshi kwenda kulinda amani ambayo ilikuwa imetoweka kabisa kutokana na mapigano ya ana kwa ana huku waasi nao wakiwa wamechachamaa sana.
Mapigo ya moyo ya Lameck yalienda kasi lakini alijitahidi sana kujificha ili mkuu wake asiugundue udhaifu huo.
Ni kosa kwa mwanajeshi kuonyesha uoga mahali popote pale.
Kwa Lameck ilikuwa kawaida kufanya mazoezi ya kulinda amani lakini sio kuilinda kweli.
Sasa alitakiwa kwenda kuilinda katika nchi yenye hatari kali, raia wanaomiliki bunduki hovyohovyo na pia waasi wasiokuwa na huruma na wanaowachukia sana askari wa umoja wa mataifa wanaoletwa kulinda amani.
"Wewe na wenzako arobaini na nne mtaiwakilisha Tanzania vyema katika nchi hiyo inayokaliwa na waafrika wenzetu....mtakuwa na maandalizi ya siku saba tu. Siku mbili za kuaga wanafamilia, siku nne kwa ajili ya semina fupi ikiwemo makabidhiano kisheria katika serikali ya Sudani na siku iliyosalia ni siku ya safari" alielezea bwana yule huku akiukuna upara wake kwa kutumia kalamu.
"Ni jambo la kifahari sana na la kujivunia kwenda kuiwakilisha nchi yako katika nchi nyingine, nakupongeza sana bwana Lameck....." alimaliza kwa kutabasamu.
Lameck hakuelewa kabisa hizo pongezi ni za nini hasa. Maana kilichokuwa mbele yake ni hatari tupu. Na bado anaambiwa hongera.
Kidogo aulize swali lakini akakatishwa.
"Wenzako nimezungumza nao tangu usiku wa jana na leo jioni mtakutana kwa pamoja kupongezana."
Maongezi yakaishia pale na Lameck akaruhusiwa kuondoka. Akasimama akapiga saluti ambayo haikujibiwa.
Safari yake ya kurejea katika makazi yake haelewi kama iliongezeka masaa kadhaa ama ilikuwa imepungua.
Hakuelewa kama aliwahi kufika nyumbani ama alichelewa.
Hakika alikuwa amechanganyikiwa. Na hakuelewa kabisa ni nini kinapita katika kichwa chake.
Alijaribu kulala lakini usingizi ukagoma kuja.
Akiwa hana hili wala lile simu yake ya kiganjani iliita.
Alikuwa Tino, rafiki yake ambaye walijiunga jeshi pamoja.
"Sema kaka.....vipi nawewe umo kwenye hilo zali.." Tino aliuliza huku akiwa na kimuhemuhe cha kujua kama rafiki yake naye yumo katika orodha.
"Nimo kaka na wewe je?" alijaribu kuchangamka Lameck.
"Daah kaka nina furaha hapa asikwambie mtu...nimo kaka....yaani siamini ujue....kaka manyota hayo manyota yanatuangukia." Tino alizidisha furaha yake.
Lameck akakata simu kisha akazimisha kisha kimyakimya akamtusi Tino.
"-------- nini huyu anachekelea kufa au...manyota manyota mshenzi kabisa...." akasonya kisha akaendelea na mawazo yake yasiyoeleweka.
Lameck alikuwa anaogopa kufa!!
Muda nao ukazidi kuyoyoma lameck akiwa hajui la kufanya. Kuna wakati alifikiria kutoroka lakini mwisho akagundua ni ujinga na aibu sana kwake.
Kama rafiki zake wanafurahia kwa nini na yeye asiwe na furaha.
Lameck akajivika ujasiri akaiwasha simu yake.
Akampa baba yake taarifa hiyo, mzee wake ambaye zamani alikuwa jeshini akampongeza. Jambo ambalo lilimpa nguvu zaidi.
Akiwa amechangamka kabisa alianza kupanga ratiba za kuaga watu wa muhimu ndani ya siku mbili walizokuwa wamepewa.
Katika orodha jina la kwanza kabisa likawa Emmy wa James. Aliamini kuwa alikuwa na kila haja ya kuagana na binti huyu ambaye ni yeye aliutoa usichana wake.
Akampigia simu ya dharula wakazungumza kwa kifupi.
"Kesho nikitoka hospitali tukutane, lakini isiwe kwako tafadhali." Emmy akakubaliana na Lameck.
Siku iliyofuata wawili hawa wakakutana huku Lameck kwa kuangalia asiitie ndoa ya emmy katika utata alimtumia rafiki yake mwingine ambaye pia ni mwanajeshi kumpokea Emmy.
Ilikuwa ni heri agundulike Emmy anamsaliti James kwa bwana mwingine lakini sio kwa baba yake mdogo.
Zoezi likakamilika, wawili hawa wakaonana, Lameck akaagana na Emmy katika namna ya kuchukuza. Kufanya uzinzi!!
Baba na mwana!!
Walidhani kuwa ile ilikuwa siri kubwa lakini kuna kijana wa kileo ambaye amejiajiri katika kufuatilia mambo ya watu bila kujua nini faida yake.
Jose B waukweli alikuwa shuhuda. Bahati mbaya kwao hawakuweza kugundua janja ya bwana huyu kutoka kanda ya ziwa jiji la Mwanza.
Emmy alilia sana, kwanza kwa furaha kisha baada ya tendo akalia kwa uchungu kwa mambo ambayo alikuwa akimfanyia James.
"Lameck...naomba hii iwe mara ya mwisho tafadhali nakuomba...James ananipenda sitakiwi kumlipa hivi ninavyofanya"
"Usijali hata mimi nilitaka kusema hivyo hivyo..." Lameck alijibu kinafiki.
"Isitoshe nina mimba yake tayari, sitaki kumtenda vibaya huyu mtoto..." Emmy alikazia akidhani jambo hilo litamuua nguvu Lameck. Lakini badala yake likamshtua.....
Lameck hakutaka kuhoji sana....kuna mjadala ukazuka kichwani mwake. Mjadala ambao aliuanza tangu siku Emmy alipomwambia kuwa alikuwa na kichefuchefu baada ya kutumia dawa za kurejesha bikra iliyopotea.
Lameck akaguna . hakusema neno zaidi.
Baadaye waliagana huku Emmy akimtakia mema huko anapoenda.
Jicho la Jose B lilimsindikiza binti huyu hadi alipotokomea kuelekea ambapo Jose b hakuhitaji sana kupatambua kwa wakati ule.
Tayari alikuwa ana namba za simu.
Baada ya juma moja Lameck na wanajeshi wengine walikwea ‘pipa' wakaipasua anga kuielekea nchi ya Sudani.
Lameck akijiahidi kuwa baada ya kurejea nchini atafuatilia juu ya hiyo mimba ya Emmy.
Hakutaka kuweka hisia kuwa huenda anahusika nayo. Aliamua kujipa muda zaidi, pia hata kama angekuwa anahusika naye bado asingeweza kumuhitaji kwani ni skendo ya baba kuzaa na mwanaye.
Aibu kubwa.
****
Wakati Lameck anakwea pipa. Jose B yeye alikuwa katika siti ya basi akiwa ameketi na baba yake mzazi wakirejea katika jiji la Mwanza, Jose B alikuwa amepona kabisa.
Mzee Boniphace hakujua lolote ambalo lilipita katika kichwa cha mwanaye.
Jose B alikuwa akiliwaza jiji la Dar es salaam na kuliona kuwa jiji zuri sana kibiashara.
Si biashara ya nguo wala vyakula.
Biashara ya umbea. Aliona kuna kila dalili jiji hilo likatoa neema kwake.
Hakumweleza mtu yeyote juu ya pesa alizokuwa amebakisha katika chumba chake katika godoro jijini Mwanza. Hakutaka kuulizwa maswali mengi. Akiwa katika kuwaza alizipigia mahesabu kuwa akifika anazichukua kisha anasafiri peke yake kurejea jijini Dar es salaam kwa ajili ya kufanya biashara ya umbea. Hasahasa kwa wateja wake wakuu, James na mkewe ambaye hadi wakati ule alikuwa hajalifahamu jina lake.
Waliwasili Mwanza majira ya saa tatu usiku. Moja kwa moja wakaelekea nyumbani.
Mama Jose aliwapokea kwa mashamushamu huku akimkumbatia Jose b ambaye aliondoka jijini Mwanza akiwa katika machela.
Sasa alikuwa amepona.
Jose B alipofika katika nyumba yao ndipo alipata jawabu la ni wapi ilitoka pesa ya kumsafirisha hadi jijini Dar kwa ajili ya matibabu.
Kabati la vyombo, luninga, jozi ya sofa, kompyuta na vitanda viwili. Vyote havikuwa pale ndani.
Viliuzwa Jose B aweze kutibiwa na kupona kabisa.
Roho ikamuuma Jose. Alipoingia chumbani kwake moja kwa moja alitazama kitanda.
Hapakuwa na lile godoro lake alilolitambua, bali palikuwa na mfano wa godoro, ambalo limechakaa na halifai tena kulaliwa.
"Mama....godoro langu...." aliuliza huku akiwa amehamaki Jose B.
"Godoro lako? Lipi tena na ulinunua lini?" alijibu huku dhahiri akionyesha kukereka.
"Mama naulizia godoro lililokuwa chumbani kwangu...."
"Mguu wako na godoro kipi bora??" mama akauliza swali gumu....Jose B akauma memo kwa ghadhabu, na alikuwa ametaharuki. Ndani ya lile godoro kulisaliwa na takribani milioni moja na laki tano.
Sasa halipo lile godoro.
Kizuizi!!
Mama akatoweka akimwacha Jose B akihangaika kujiuliza na kujipatia majibu. Majibu ambayo si sahihi.
Usiku ule ulipita Jose akibakia kuwa mlinzi wa familia. Hakulala kabisa, alilia machozi kama kuna msiba ulitokea.
Muda wote aliotumia kuzisaka pesa zile, sasa hana hata senti.
Inauma sana.
Harakati za Jose B kurejea jijini Dar kwa ajili ya kufanya biashara zikaanza kupotea.
Atatoa wapi nauli, atatoa wapi pesa ya kuishi jijini Dar wakati akifuatilia biashara yake??
Kizuizi kikubwa sana.........
******************
***LAMECK anaelekea Sudani kuwakilisha taifa...anamuacha EMMY huku nyuma......Mimba ya Emmy bado ina utata......
***JOSE B...amechanganyikiwa mipango yake inaingiliwa na kizuizi...pesa zimeuzwa pamoja na godoro....
****EMMY...alionwa na Jose B..mshakunaku wa kimataifa.....je nini hatma ya siri hii???
ITAENDELEA......