HADITHI: KIZUIZI
SEHEMU YA NANE
Akapapasa kilipo kitufe cha kuwashia akakipata, akawasha taa. Macho mawili yasiyokuwa na kasoro yakakutana na mwili ambao umeshasahau nini chungu na tamu ya ulimwengu.
Maiti!!
Jose B alirudi kinyumenyume, akaangusha bila kutarajia kile kifurushi alichopakata mkononi, akageuka na kutimua mbio.
Jirani na nyumba aliyokuwa akiishi Deo palikuwa na mbwa, Jose B hakujua ni kwa kiasi gani alitoa vishindo vikubwa, mbwa wakavutika na vishindo hivyo, ni kama waliambizana, mbwa wawili wanaojua nini maana ya kulinda wakaanza kumkimbiza Jose B.
Mshikemshike...
ENDELEA...............
Mbwa wale kama walivyo mbwa wengine walibweka kwa sauti za juu wakati wanamkimbiza Jose B, hali hiyo ilizua utata katika akili ya Jose katika kufanya maamuzi. Akaongeza mwendo ili asiweze kudhurika na wale mbwa.
Sauti zilizosikika pekee katika masikio ya Jose zilikuwa za wale mbwa wenye hasira, kiatu kimoja kikiwa kimechoropoka mguuni Jose alibakiwa na kiatu kimoja tu huku mguu mwingine ukiwa peku.
Umakini wa Jose katika kuwakwepa mbwa ukamsababisha asiweze kuisikia honi iliyokuwa inapigwa na pikipiki, Jose akaifikia kona, akajaribu kuwahi kuruka upande mwingine baada ya kukutana ana kwa ana na pikipiki ikiwa katika mwendo wa kasi.
Akili yake ya kuhama upande ikafanana na ya yule dereva nay eye akahamia upande aliorukia Jose.
Mlio mkubwa kisha kimya kikatanda.
Jose kimya, dereva kimya.
Kiza kinene kikatanda.
****
Haikuwa mara yake ya kwanza kumfungia tela mtu ili aweze kufahamu anachokihitaji. Zoezi lake alilotegemea kuwa litakuwa gumu sana lilibadilika na kuwa jepesi.
Hali hii ilikuja baada ya kumuona Jose B.
Akampigia mahesabu kuwa ni huyo ambaye atamuonyesha wapi alipo Deo na kisha wote wawili atawaangamiza aweze kubaki bila hatia inayoleta kizuizi.
Kila hatua aliyokuwa anaenda Jose, jicho la James lilikuwa makini kumfuatilia. Na hata alipomuona akimfuatilia Deo na yeye aliendelea kufuatilia.
Jose B hakujua kabisa kama kuna uwezekano wa kuwa anafuatiliwa na mtu nyuma yake, alijiamini kuwa ni yeye pekee anayemfuatilia kiumbe yule.
James alijiegesha mahali ambapo hawezi kuonekana kirahisi hadi alipomuona Deo anaagana na Jose B. Alisikia maneno yao ya mwisho wakisisitizana juu ya kuwahi kesho wakutane msibani. Maneno haya yakawa na umuhimu sana kwa James.
Akahisi zoezi lake litakuwa na wepesi.
James alitaka kuanza na Jose B kwa wakati ule lakini akaona wa muhimu zaidi ni huyu Deo ambaye wamekuwa naye ujanani na utotoni na anamfahamu fika. Kuhusu Jose, hakumtilia sana maanani kwani alifahamu kuwa hajui lolote kubwa kuhusu yeye. Pia akaamini alikuwa na nafasi kubwa ya kumteka Jose wakiwa msibani siku inayofuata.
Dakika kumi baada ya Jose kutoweka, James akiwa amechemkwa na hasira kichwani aliingia bila kubisha hodi katika chumba kidogo cha Deo. Taa ilikuwa inawaka, ana kwa ana na rafiki wa utotoni na ujanani.
Deo na James.
Deo akataharuki zaidi ya kushangaa. James akatoa tabasamu bandia kisha akamsukuma kwa nguvu akatua kitandani, kitanda kikazidiwa nguvu kikaachana na chaga kikatua chini na mwili wa Deo.
Deo aliyezoea utotoni kuwa alikuwa mbabe kwa James, alisimama wima kibabe ili ajaribu kama anaweza kukabiliana na James. Lakini mawazo hayo yalikuwa ‘mawazo mfu', James alikuwa mwingine kabisa wakati huu.
Ngumi moja iliyoshiba haswa ikakutana na mdomo tepetepe wa Deo.
Damu ikaruka.
"Wewe na Bibiana mlitaka kwenda kumwambia nini Paroko??" James aliuliza kibabe.
Deo kimya!!
"Nakuuliza wewe boya, wewe na huyo Bibiana wako mlitaka kumwambia nini paroko?" sauti ya ukali ikamtoka. Deo akawa anatetemeka midomo bila kusema lolote.
"Mnajifanya mnanijua sana eeh..." Aliuliza James huku akilazimisha tabasamu.
"Sio mimi ni Bibiana peke yake ndo alisema.....alisema kuhusu ...Mamu..."
"Mamu kafanyaje??" alihoji kwa ukali.
"Mi sijui, anajua Bibiana...haki ya Mungu tena Jimmy mi sijui kitu kaka.." alijitetea Deo. James akiwa anamsikiliza.
"Okey, kumbe haujui vizuri sana.....sasa naomba nikupe agizo moja." Alizungumza kwa sauti ya chini kama aliyeelewa alichosema Deo.
Amani ya Deo ikarejea kiasi.
"Niagize tu kaka." Deo akanyenyekea.
James alimtazama machoni Deo, Deo akakwepesha macho.
Likafanyika tukio la mara moja lililoambatana na maneno.
"Sasa nakuagiza nenda ukamuulize huyo Bibiana halafu uje unieleze Mamu amefanya nini...." Jose alitoa maagizo haya huku kisu kikiwa kinazama na kutoka katika mwili wa Deo.
Baada ya dakika kadhaa kweli Deo aliyekubali kuagizwa kwa Bibiana akawa ameagizwa.
Agizo la milele lisilokuwa na majibu.
Deo akaiaga dunia bila kumueleza Jose B juu ya kizuizi.
Usiku ulikuwa umeingia, James akarejea kimyakimya hotelini huku mawazo yake yote yakiwa juu ya Jose B, ni huyu pekee alikuwa amesalia katika orodha ili amani ichukue nafasi.
Asubuhi kama ilivyo ada aliwahi sana kuamka, akajiandaa na kupata kifunguia kinywa kisha safari kuelekea msibani.
Kama alivyotarajia alimkuta Jose B akiwa amewasili tayari.
Kama ilivyokuwa siku iliyopita alifanya kumfuatilia nyendo zake ili aweze kupata upenyo wa kupata faragha na kumwondosha duniani mara moja.
Kwa kugundua kuwa amekosa cha kumweleza mkewe mtarajiwa juu ya sababu za kuchelewa kurejea, alitumia sababu ya kuhudhuria mazishi ya Bibiana, sababu ambayo haikupingwa na mkewe huyo, taarifa hiyo akampatia pia mzee Magayane ambaye ni baba yake mzazi. Alifanya hivyo kwa kuhofia mkanganyiko iwapo ataweza kukutana naye msibani.
Mawazo yake yalikuwa sahihi kabisa, akiwa katika kumfuatilia Jose B asiweze kumpoteza hata kwa sekunde moja, alikutana na mzee wake, alitaman i kuongea upesi ili waweze kuachana, lakini mzee yule akamvuta mwanaye pembeni na kumpatia sifa kedekede anazozipata mtaani baada ya kusikia kuwa mwanaye anaoa.
James hakuwa makini kabisa na mazungumzo yale. Na alijitahidi kadri ya uwezo wake kuyafupisha.
Licha ya jitihada zote hizo aliporejea hakumkuta tena Jose B.
Aliangaza huku na huko lakini hata dalili haikuwepo.
Ni katika muda huo ambao mzee alimvuta James pembeni ndipo Jose B alikuwa ameamua kumfuata Deo nyumbani kwake baada ya kuwa amechelewa sana kurudi.
Huko anakutana na dhahama ya kukutana na maiti ya Deo, kisha kabla hajakaa sawa anakimbizwa na mbwa wakali, riadha yake haifiki mbali anakutana na ajali mbaya ya pikipiki na sasa kimya kimetanda.
Kimya kinachotia wasiwasi.
****
EMMY JOHN, hakuamini hata kidogo ile dawa aliyopewa na Lameck inaweza kufanya kazi kiasi kile alichokishuhudia, alikuwa anakauka na kurejea kawali.
Furaha ikarejea kwa kasi, akampigia simu Lameck na kumweleza juu ya yale mabadiliko.
Lameck akajipongeza kwa ujuaji huo alioupatia katika kambi ya jeshi. Ujuaji ambao --------- na wasichana matapeli wa mjini kujikausha na kufanana na mabikira. Kisha kuwalaghai wakuja.
"Lameck hivi inaleta kichefuchefu eeeh maana mh!!" Emmy alimuuliza Lameck.
"Kichefuchefu? Yeah..ok..ndio inaleta lakini sio sana.." alijiumauma Lameck. Emmy hakushtukia.
"Ndo maana dah kichefuchefu kama nini dah...." alizidi kulalamika Emmy.
"Usijali lakini...kitaisha cha msingi kutimiza tulichohitaji au vipi?"
"Haya masta"
Lameck akawahi kukata simu baada ya kugundua kuwa alikuwa na dalili za kutetemeka.
Kichefuchefu?? Alijiuliza Lameck.
Hizo hazikuwa dalili za dawa ile kufanya kazi, mjeshi huyu akakaa kitako, kiutu uzima akatafakari kidogo kisha akafanya tabasamu ndogo yenye karaha ndani yake. Akataka kufanya ubashiri lakini akasita maana aliamini atajiumiza kwa ubashiri.
Siku ikapita.
Lameck na shughuli zake na Emmy akiendelea kwa juhudi zote kutumia dozi ya shabu na ndimu kuimarisha bikra feki. Kichefuchefu kikiwa rafiki yake wa karibu sana.
****
Maandalizi ya harusi yalikuwa yakifanyika kwa bidii kubwa. Emmy alikuwa ana furaha sana kwani kizuizi chake aliamini amefanikiwa kukikwepa, James yeye alikuwa hamsini hamsini, jitihada zake za kumsaka Jose B zilivyogonga mwamba jijini Mwanza alikuwa katika taharuki ya kuaibika siku moja baada ya tangazo la tatu, aliamini kuwa lazima Jose B atamuharibia. Alifanya maombi katika miungu yote anayoifahamu ili imwepushe na aibu inayokaribia kumpata.
Alipungua uzito na hakuwa na amani kabisa, hatimaye jumapili ya tangazo la tatu na la mwisho ikafika.
Maajabu!!
Tangazo la tatu lilipita bila kizuizi chochote kile. Hakuna kipingamizi kutoka jijini Mwanza wala Dar es salaam.
Furaha kamilifu.
Yule Jose B aliyekuwa anahofiwa kuleta matatizo hakuonekana kuwa na hatari yoyote tena na wala hakujulikana ni wapi alipo.
Ile harusi babu kubwa iliyokuwa inangojewa hatimaye ikashika hatamu.
James mwenye siri kubwa moyoni akamvisha pete Emmy mwenye siri kubwa zaidi mwilini. Kila mmoja alitoa tabasamu kwa mwenzake, tabasamu la kinafiki, kila mmoja alijiona ni mkosefu kwa mwenzake.
Emmy akajutia kwa kufanya mapenzi na Lameck huku James naye akijutia mengi mazito.
Nani ajuaye siri ya moyo? Hayupo!!
Na ilikuwa hivyo, hatimaye kiongozi wa kiroho akawabariki James na Emmy kuwa mume na mke.
Vigelegele, mbinja na makofi vikasikika.
Harusi ya kifahari kabisa.
Ya ukumbini yalikuwa ni kufuru kubwa, pesa ilitumika sana, hayasimuliki kwa ambaye hakuwepo. Ni kama maigizo.
Lameck akamkumbatia Emmy wakati akimpatia zawadi yake kama babamdogo. Msema chochote (MC) naye akawapamba sana wawili hawa kuwa walisoma pamoja na kukua pamoja.
Laiti angejua siri waliyohifadhi wawili hawa ni heri angekaa kimya bila kusema neno.
Siku ikamalizika, bwana na bibi harusi wakisafirishwa hadi Kampala Uganda kwa ajili ya fungate la majuma mawili na siku tatu.
Ni huku Kampala Uganda ambapo mambo mapya kabisa yanazaliwa. Mambo yanayoleta furaha ya muda mfupi kisha linazuka la kuzuka.
****
Harusi hii ya kifahari isingeweza kukosa waandishi wa habari wa kununuliwa. Na kipindi kikarekodiwa na kurushwa katika kituo kimojawapo cha luninga hapa nchini.
Kipindi kilirushwa siku mbili baada ya harusi ile ya kifahari.
Huenda ni maelfu walikitazama kipindi kile b ila ya kuwatambua maharusi wale, lakini kijana mmoja alivutika zaidi na kupagawa sana kwa kile alichokiona, alitambua tukio lile na alijiona kama lilikuwa linamuhusu, alitazama tabasamu la bibi harusi na kisha akachukizwa na cheko la bwana harusi.
Alisikiliza kila kilichokuwa kinasemwa. Alitamani sana kusimama wima aweze kuangalia kwa makini lakini hakuweza, alitaman i kusema neno lakini hakuweza kutokana na kufungwa vifaa maalumu katika taya zake kwa ajili ya kuzilinda, alikuwa amevaa bukta mguu wake wa kuume ukining'inia juu huku ukiwa na bandeji gumu.
Macho na masikio pekee ndio viungo vilivyokuwa huru kufuatilia tukio hili kikamilifu. Kichwani alipitisha maswali mengi lakini akakosa majibu, aliamini kuwa laiti kama angekuwa mzima wa afya hakika angepata cha kusema juu ya ndoa ile ya kifahari. Alipokumbuka juu ya uzima wake akawalaani wale mbwa waliomkimbiza, akataka kumlaani na dereva aliyemgonga na pikipiki lakini akakumbuka kuwa dereva yule alikufa hata kabla ya kufikishwa hospitali.
Laana zake akazihamishia kwa muuaji wa Deo.
Nani amemuua Deo? Alijiuliza tena.
Macho yake yakaitazama luninga akakutana na James akimlisha mkewe keki kwa kutumia midomo. Hasira ikamkamata akataka kutukana, taya lililovunjika likamsaliti akauma meno kwa uchungu, chozi likamtoka kutokana na maumivu ya taya.
"Jose B waukweli hapa sina ujanja aisee. Ila ngoja nipone.." Alikiri kimya kimya wakati kile kipindi kikielekea ukingoni.
Wagonjwa walivutiwa na kipindi kile, Jose B akafurahishwa na huduma bora kutoka hospitali binafsi. Laiti kama angekuwa hospitali ya serikali hata hiyo luninga asingeweza kuiona. Na hiyo ndoa ya James na mkewe asingepata fursa ya kuitazama pia.
***NDOA imefungwa hatimaye...lakini UGANDA linazuka jambo.......ni jambo gani??
***JOSE B bado yu hai lakini kitandani....anaapa akipona ataendelea na harakati zake.....
***EMMY ana siri na JAMES naye ana siri......hazitadumu siku zote.....nini kitatokea SIRI zikivuja.......
***LAMECK ana wasiwasi juu ya kichefuchefu....je kuna tatizo kubwa zaidi ya hapo??
***KIZUIZI hakijavunjwa bado......je ni kipi???
ITAENDELEA.....