HADITHI: KIZUIZI
SEHEMU YA SABA
EMMY JOHN alimuaga mama yake mzazi kuwa anaelekea ufukweni kupunga upepo kwani hawezi kuishi kipweke bila uwepo wa James.
Mama alimsikitikia mwanaye, akamruhusu huku akimtia moyo kuwa muda si mrefu mume wake atarejea.
Aliyoyazungumza mama yalipenya kama upepo wa kawaida tu usiokuwa na maana. Emmy hakuwa akimuwaza James hata kidogo.
Mawazoni mwake Lameck alijikita, kwa kuwa alimuahidi jambo jema. Kumsaidia kuificha aibu.
Emmy akatoweka, safari ya kuelekea nyumbani kwa Lameck.
*************
ENDELEA...........
Chumba cha Lameck kama ilivyo kawaida kilikuwa hakipo katika mpangilio mzuri sana kuonyesha kwamba hakuna mwanamke wa kukipendezesha. Emmy alikikuta katika mpangilio huo huo.
Alikiri katika nafsi yake kuwa hakikuwa chumba cha kuvutia lakini bado hakufanya jitihada za kukiweka katika hali ya usafi, labda kwa sababu sio hicho kilichomleta katika nyumba hiyo.
Lameck alimpokea Emmy kwa bashasha na kimuhemuhe cha namna yake, licha ya Emmy kujaribu kuvaa mavazi ya kawaida sana lakini bado alimteka Lameck ambaye alishindwa kusema neno lolote kwa sekunde kadhaa.
Baada ya kimya kirefu hatimaye aliweza kumkaribisha Emmy, huku akitumia jina mpenzi jambo ambalo lilimkera Emmy lakini hakuwa na budi kukubali kwa shingo upande hasahasa akizingatia kuwa mchezo huo waliuanza zamani sana na hakuna aliyekuwa amemshawishi mwenzake bali ilitokea tu ikawa hivyo.
Ulisema hofu yako ni nini? Lameck alimuuliza Emmy huku akimkazia macho. Emmy akaona aibu kujibu, Lameck akajiongeza.
Njoo huku hebu.
Emmy akasimama na kumfuata, walielekea chumbani. Kitandani palikuwa na kikopo kidogo cheupe pamoja na kitu mfano wa ndimu.
Hii unaikamua katika haya maji, kisha unachukua kitambaa unachovya kidogo unakandakanda, fanya hivi asubuhi kabisa na usiku bila kukosa. Lameck alitoa maelekezo hayo kama daktari bingwa wa magonjwa ya kike.
Emmy alitamani kuuliza maswali zaidi lakini hakuwa akijiamini sana. Akaipokea ile dawa akaitia katika mkoba.
Yale majimaji yalikuwa ni Shabu dawa ya kutakatisha maji na kuua vijidudu, ni mfano wa Waterguard na kile kipande kilichofanana na ndimu kilikuwa ndimu yenyewe. Dawa kamili kutoka kwa mganga mashuhuri.
Bwana Lameck.
Walizungumza mengi, kisha Emmy akaondoka.
****
JOSE B waukweli alifika mapema sana msibani, alijiweka mbali sana. Hakutaka kuonekana kujihusisha sana na ule msiba, ni mengi yalikuwa yamekizonga kichwa chake. Alihitaji sana kuyafahamu kwani yalimuumiza kuliko huo msiba.
Mara ajipitishe dukani mara ajiunge katika vikundi vya vijana wanaobadilishana mawazo, huku napo alichombeza kasha akahama tena na kujiunga na wazee wanaojadili ya kwao kuhusu msiba huo. Alipogundua hakuna kubwa walilofahamu kuhusiana na kifo cha Bibiana aliwafananisha na wanadamu waliopitwa na wakati huku wakijiona wanaenda na wakati.
Katika hangahika ya huku na kule hatimaye alipata kitu kilichomvutia na kumfanya aachane na mengine yote yahusianayo na msiba huo.
Akaanza kumfuatilia kiumbe huyu ambaye bila kujijua alikuwa anahitajika sana kwa kipindi hicho. Jose B hakusema neon lolote na kiumbe yule aliyetawaliwa na huzuni kuu.
Akienda kushoto Jose B naye aliketi kushoto. Aliporejea kulia Jose B naye alifuata, hatimaye yule kiumbe alisimama na kujizungusha huku na kule, Jose naye akafanya hivyo lakini kwa tahadhari kubwa sana asiweze kugundulika.
Yule bwana akiwa katika huzuni ileile sasa aliambaa katika umati kisha akaifuata barabara ya lami, akatoweka bila kuaga.
Jose B naye akatoweka bila kuaga vilevile.
Akaendelea kumfuata mtu ambaye mara ya mwisho alionana naye kanisani, alikuwa pamoja na marehemu na alikuwa akizungumzia juu ya kizuizi. Kizuizi ambacho kilipenya katika masikio yake na kisha akakigeuza biashara ambayo sasa ilikuwa imempatia pesa lakini kabla ya kuitumia ile pesa yanatokea yakutokea.
Sasa Jose B anataka kujua kuna siri gani nyuma ya haya mauaji. Anamfuatilia Deo.
Deo hajui kama anafuatiliwa.
Hadi nyumbani kwake, anapotaka kuingia ndipo anasikia akiitwa kwa jina lake fasaha Deogratius.
Akageuka, akakumbana na sura ngeni machoni pake, akakutana na Jose B waukweli.
Mbea, mnafiki, mwongo, msema chochote katika sherehe na kondakta wa daladala. Hawa viumbe hawawezi kuhangaika iwapo wataamua kuwa madalali. Huwa na maneno mengi matamu tena yanayoshawishi, Jose B alikuwa mmoja kati yao alikuwa na virusi vya unafiki, uongo na umbea. Alipovichanganya vikazaa tabia ya ushakunaku.
Ana kwa ana na Deo. Jose b akaanza kurusha karata zake huku akijifanya kumjua sana Deo.
Ujue tangu msibani mi nakutazama nikajisemea huyu ndiye ama siye.
Deo akaiva akaisahau huzuni akatekwa na maneno ya Jose B na sasa walikuwa katika chumba kidogo kilichopunguzwa joto na feni aina ya pangaboi. Deo akizidi kufahamiana na Jose B.
Baada ya kufahamiana Jose B akaleta mada juu ya kifo cha Bibiana.
Hapa Deo akainamisha kichwa na kufanya aina ya kumbukumbu huku akiunganisha meno yake kwa huzuni kuu.
Hakutaka kusema lolote juu ya msiba huu zaidi ya kukiri kuwa hata yeye alishangazwa sana.
Nimesikia sikia wale wazee wanadai ishu iliyomuondoa Bibiana ni Kizuizi Jose aliongea kwa kunongona.
Kizuizi? Kivipi yaani.....
Hata sijui lakini...hivi kwani alikuwa anataka kufunga ndoa huyu Bibiana maana nimesikia sijui kawekewa kizuizi sijui.... Jose B akampiga Deo chenga ya mwili, Deo akalainika.
Mh..Bibi hakuwa hata katika uchumba sema kuna ishu moja hivi lakini sidhani kama James anaweza kufanya jambo kama hilo....
James ndo nani?? Jose aliuliza.
Kuna mshkaji mmoja anataka kuoa....Bibi alitaka kumuwekea kizuizi.......lakini hata kwa paroko hakufika ndo amekufa.....James hawezi kuhusika...sawa jamaa ni katili lakini sio kiasi cha kuua..... Deo alijibu huku akiamini Jose B hakuna anachoambulia.
Unajua nini Jose...ngoja tumzike kwanza Bibiana halafu sisi tutakaa tuzungumze juu ya hili ujue sisi wanaume tutaangalia nini cha kufanya..
Deo alimaliza maongezi ambayo Jose B alitamani yaishe siku hiyo hiyo. Alitamani kumchombeza Deo ili aendelee kuzungumza lakini alihofia kuwa haraka zake zinaweza kumkosesha baraka. Akakubaliana na Deo kisha wakaagana.
Waliimaliza siku huku wakipeana ahadi za kukutana msibani siku inayofuatia. Jose B alimuachia shilingi za kutosha ili kumnunua Deo bila yeye kujua kama ananunuliwa.
Jose B aliondoka huku akijiaminisha kuwa kwa makali aliyoyaonyesha lazima siku inayofuata Deo atamwaga siri yote juu ya kizuizi.
Laiti kijana huyu angepewa nafasi ya upendeleo kujua yatakayotokea baada ya masaa machache huenda angemlazimisha Deo aseme yote juu ya kizuizi, lakini Jose naye ni mwanadamu kama wanadamu wengine hakuyajua yanayotokea baada ya dakika moja.
Kama ilivyo kawaida alifika msibani mapema, siku hii alikuwa amebeba pesa nyingi zaidi na zawadi ndogondogo kwa ajili ya kumnunua Deo reja reja.
Alitegemea kuwa Deo atawahi kutokea kama alivyomuahidi lakini haikuwa hivyo. Alitamani kumpigia simu lakini akakumbuka vitu viwili, kwanza hakuchukua namba yake ya simu na kubwa zaidi bado hakuwa tayari kuwasha simu yake ambayo aliamua kuizima tangu kifo cha kushtukiza cha Bibiana kitokee.
Jose akaendelea kuivuta subira isiyokuwa na dalili ya heri.
Saa sita mchana hatimaye. Bado Deo hakuonekana.
Jose akiwa bado anaduwaa mara aliguswa began a mzee wa makamo kiasi kikubwa.
Kijana....poleni sana. Nawe upo hapa kumbe. Alizungumza kwa sauti murua ya kizee.
Jose b akamtazama kwa dakika chache huku akiilazimisha sura ile kujichora katika ubongo ambao kazi yake ni kukumbuka. Hatimaye akamkumbuka.
Shkamoo mzee.... alimsalimia mzee yule.
Marahaba....poleni..ulianza kunisahau. Aliuliza.
Si unajua tena mambo ya msiba. Alijaribu kujitetea.
Yule mzee akatabasamu kisha akampiga begani ishara yak umpooza.
Ngoja nizungumze na kijana wangu mara moja hapa. Aliaga yule mzee. Jose b akakiri kimoyomoyo kuwa yule mzee alifanana sana na mtoto wake wa kiume.
Duuh yaani hadi kutembe wanafanana aisee. Alijisemea huku akiunda picha ya James nay a huyu mzee.
Mtu na baba yake.
Yule mzee alipotoweka, Jose b naye akatoweka baada ya subira kuwa shubiri kwake. Akaamua kuelekea nyumbani kwa Deo ili kutazama kulikoni.
Kwa mwendo wa miguu akaona anachelewa akaamua kukodi pikipiki impeleke.
Dakika tano akawa amefika, akamlipa mwenye pikipiki akaondoka zake ndipo akaanza kuiendea ile nyumba.
Mlango ulikuwa umeegeshwa, haukuwa umefungwa. Jose B akamlaani Deo kimoyomoyo kwa kuchelewa kuamka kiasi hicho, akamuweka katika kundi la wazembe maradufu.
Akaizuia hasira yake ili asiweze kumsemea mbovu kijana mwenzake. Akaunda tabasamu la bandia kabla ya kubisha hodi.
Kimya!!
Akajaribu tena. Kimya!!
Hili ----- linalala kama limekufa. Akashindwa kujizuia akatukana.
Hakubisha hodi tena akausukuma mlango, ukafunguka akaingia, akakumbana na giza, feni ikiwa inazunguka.
Oyaa.... Aliita kishari.
Kimya!!
Akapapasa kilipo kitufe cha kuwashia akakipata, akawasha taa. Macho mawili yasiyokuwa na kasoro yakakutana na mwili ambao umeshasahau nini chungu na tamu ya ulimwengu.
Maiti!!
Jose B alirudi kinyumenyume, akaangusha bila kutarajia kile kifurushi alichopakata mkononi, akageuka na kutimua mbio.
Jirani na nyumba aliyokuwa akiishi Deo palikuwa na mbwa, Jose B hakujua ni kwa kiasi gani alitoa vishindo vikubwa, mbwa wakavutika na vishindo hivyo, ni kama waliambizana, mbwa wawili wanaojua nini maana ya kulinda wakaanza kumkimbiza Jose B.
Mshikemshike...
**EMMY amepatiwa dawa ambayo itarejesha bikira yake...je itafanya kazi????
***DEO ameuwawa katika mazingira tatanishi...IMEKUWAJE??
****James ana kizuizi gani kinachompelekea kuua.......
**JOSE B na mbwa.........kazi ipo......
ITAENDELEA..