RIWAYA: KISU CHENYE MPINI MWEKUNDU
MTUNZI: Ahmad Mussa Mniachi
SEHEMU YA TISA
Ubwabwa mtamu, amepika nani?
Mimi. Alijibu Beda.
Mmmm, acha kujisifia amepika mama yako. Aliongea Vick huku akijilamba vidole
vyake.
Ahsante kwa chakula kilikuwa kitamu sana. Aliendelea kumwaga sifa Vick. Beda
hakuongea chochote akatabasamu. Naona muda umeenda wacha nirudi nyumbani.
Hautaki kusubiri umsalimie mama mkwe? Hapo Vick akacheka mpaka jino la
mwisho likaonekana.
Nitamwona siku nyingine, wazazi wangu wamerudi leo baba alikasirika alikuwa
anashangaa mbona hela zake zimepungua?
Hakukuuliza?
Hakumuuliza yeyote ana wasiwasi eti amepoteza kazini. Yaani, mama anatamani
sana kuonana na wewe.
Usijali ataniona tu kama tutaendelea kuwa hai. Akajibu huku akimvutia Beda upande
wake. Akamkumbatia. Zilikuwa dakika mbili za hisia kali kwa kila mmoja.
Kwaheri
Akaaga na kuondoka mle ndani huku akikimbia. Huyo, huyoo
.. Akatokomea gizani.
Beda akaanza kuingiwa na hofu baada ya kuona mama yake anachelewa
kurudi.Hakuweza kulala. Mama yake alikuwa mtu wa matukio mabaya, hakuweza
kusahau lile tukio la kuwekwa ndani mwezi mmoja na nusu. Aliogopa sana kwani
hakuamini kama jinamizi la matukio mabaya limeacha kuiandama familia yao.
Alikuwa anaingia na kutoka ndani. Asingeweza kutulia usiku kama ule. Kuna nini tena?
Alijiuliza bila kupata jibu. Aliangalia saa yake ya mkono ambayo mikanda yake
ilishaharibika, ilisomeka saa 4.23 Mama yake alikuwa hajarudi. Akaamua kulala bila
kufunga mlango wa kuingilia pale sebuleni.
* * *
Mama Beda alirudi nyumbani saa 6.30 usiku. Alikuta mlango ukiwa wazi. Akaingia
ndani akiwa amechoka sana. Akachukua ndoo ya bafuni akajaza maji kisha akaenda
kuoga. Alipooga akarudi na kukaaa kitandani. Machozi yakaanza kumtoka. Safari hii
hakulia kwa ajili ya udhalilishaji aliojifanyia, kilichomsikitisha ni adhabu kubwa
aliyompa yule afisa elimu. Yule alikuwa amejitakia mwenyewe mkewe Je. Hilo ndilo
lililomtesa alimuhurumia sana mke wa Gervas ambaye kaenda kujifungua huko kwao.
Fikra zake zikampeleka miaka kumi nyuma. Akakumbuka jinsi mumewe alivyoiaga
dunia. Akakumbuka jinsi alivyomuuguza muda mrefu. Akaanza kulia, alimhurumia
mtu ambaye hamjui, mke wa Gervas Msangi ambaye amemchukulia mumewe.
Akapapasa pale kwenye meza ndogo alikuwa anatafuta kiberiti. Hatimaye akakipata.
Akawasha kibatari, akatembea kuelekea kule lilikokuwa begi la marehemu mumewe.
Ndugu walimsusia kila kitu kwa madai kuwa yeye ndiye alimroga mumewe. Hakuwahi
kutembelewa na ndugu upande wa mume hata siku moja baada ya kifo kile.
Ndugu zake walikuwa Kigoma adha ya usafiri iliwafanya washindwe kuhudhuria hata
mazishi ya mumewe.
Alipekua lile begi akatoa karatasi mbili ngumu za rangi ya kaki. Akasoma karatasi ya
kwanza kisha akaiweka mezani. Akachukua ile ya pili, haikuwa na maelezo tofauti na ile
ya kwanza, tofauti ilikuwa ni majina yaliyotumika. Ile ya kwanza ilikuwa ni ya
marehemu mumewe na ile ya pili ilikuwa ya kwake. Jina Sakina Msomba, Result HIV
Positive. Alikuwa ni muathirika, alikumbuka vema jinsi alivyomuuguza mpaka
mumewe anakufa mikononi mwake. Mumewe hakuwahi kutumia dawa za kupunguza
makali hivyo alikufa mapaema. Alipoenda kuomba ajiunge akaambiwa CD4 zake
zilikuwa zinatosheleza kwa wakati huo hakuhitaji kujiunga. Akaishi hivyo kwa muda wa
miaka yote kumi. Baada ya kupata ile kashikasi ya kukamatwa na polisi hali yake
ilibadilika ikawa mbaya.
Ndipo alipoanza dozi rasmi pale hospitali ya Temeke. Ni siri aliyoijua mwenyewe na
madaktari tu. Leo amemuambukiza Gervas yule afisa elimu aliyekataa kutumia kinga.
Hakuona sababu ya kumueleza ukweli amembembeleza mara nyingi atumie kinga
hakutaka pia alijihisi kama aliyebakwa kutokana na hila aliyotumia afisa yule.
Angefanya nini?
Wazo moja lilimtesa, mke wa Gervas hakustahili adhabu ile. Afanye nini kumuokoa?
Lazima nimuokoe, siwezi kuacha mtu asiyehusika anapata adhabu asiyostahili, yule
mumewe amestahili kwani ilikuwa vigumu kumpeleka PCCB, ningethibitisha vipi kuwa
alihitaji rushwa ya ngono. Aliwaza mama Beda.
Nafsi yake yenye huruma haikutaka kusikia mwanamke mwenzake akipata mateso kwa
sababu ya ufuska wa mumewe. Akalala akiwa na azma ya kumuokoa Mke wa Gervas.
Nitamuokoaje? Ni swali lililopita kichwani mwake kabla hajapitiwa na usingizi.
* * *
Saa 1.30 Beda alienda kwenye mlango wa chumba cha mama yake. Akamsikia akiwa
kwenye mkoromo wa usingizi . Akashusha pumzi kisha akakusanya vyombo
alivyovitumia na Vick akakaa nje akaanza kuosha. Alikuwa na hamu kubwa ya kutaka
kujua nini kimejiri kuhusu mpango wake wa kujiunga na masomo ya sekondari.
Aliendelea kuosha vyombo huku akiimba kwa mluzi. Alipomaliza alivianika kwenye
uchanja kisha akarudi tena ndani. Wakati anaingia ndani akakutana na mama yake
mlangoni. Alikuwa anapiga miayo ya uchovu.
shikamoo mama .
Marahaba ngoja nioge mwanangu tutaongea vizuri nikirudi bafuni.
Beda aliingia ndani na kusubiri kwa shauku kubwa.
Dakika za kuoga zilikuwa chache lakini Beda aliona kama siku nzima. Siku zilikuwa
zinaenda wenzake walishaanza masomo. Akasubiri mpaka mama yake aliporudi. Mama
yake akaingia chumbani akabadili nguo kisha akaja pale ambapo wenyewe walipatumia
kama sebule. Kulikuwa na mkeka, kiti kimoja na kigoda tu. Beda aliona aibu pale
alipokumbuka sebule alizotembelea kwa rafiki zake. Kidogo ilimshangaza kuona Vick
mtoto aliyetoka kwenye familia yenye uwezo akiyakubali mazingira yale.
Mama unabadili nguo mwaka nzima. Alilalamika Beda
Nakuja Beda mbona una haraka hivi? Alisikika mama yake akiongea kutoka
chumbani.
Enhe, imekuwaje huko mama ? Aliuliza Beda kwa kiherehere baada ya mama yake
kutoka mle chumbani.
Afisa elimu kanijazia hizi fomu tumebahatika kupata shule ya hapo jirani
Lini natakiwa kuanza? Aliuliza Beda.
Nikishapeleka hizi fomu nitapata jibu hukohuko.
Aliondoka pale nyumbani huku akikabiliwa na mtihani mgumu kwa mke wa Gervas.
Atampata vipi ili amweleze ukweli wa mambo. Iwapo atamueleza kweli haitamletea
matatizo. Aliona wazi kuwa kuna hatari ya kushtakiwa kwa kueneza maradhi wakati
anajua wazi kuwa yeye ni muathirika. Lakini kama angeweka wazi kweli angepata ule
msaada? Angeupata vipi wakati Gervas alikataahata fedha. Kwanini Gervas ambaye
kafunga ndoa kanisani atake liwazo lingine nje ya ndoa? Labda haya ni malipo mazuri
ya usaliti. Hapana lazima nimuokoe mkewe, nitajibu nini mbele ya Mungu kama yule
mwanamke atakufa kwa ajili yangu? Alijiuliza maswali mengi bila kupata njia sahihi ya
kumnusuru mwanamke mwenzake.....
ITAENDELEA...