Hadithi: Kisu chenye mpini mwekundu

Hadithi: Kisu chenye mpini mwekundu

Samahanini wakuu,nimekuwa na mambo mengi kidogo ndio maana nimeshindwa kuendeleza....ila nkitulia hata kesho inshallah itaendelea
 
Kisu Chenye Mpini Mwekundu-5

Sehemu ya tano

"Mh,makubwa.Yunifomu,vifaa vya masomo,ada na nauli juu...."Aliongea peke yake.
"vipi Mama Sanga mbona hivyo?" Aliuliza yule mama mtu mzima.
"Mwenzangu makubwa madogo yana nafuu,eti Beda kafaulu"
"Pole mwaya,majukumu ndo'yanaanza hivyo."Aliongeza yule bibi

"Mwenzangu ndio nimechanganyikiwa hapa hata sijui niingilie wapi."
Maneno ya mama yake yakaanza kumliza tena Beda.Huyu ndiye mtu pekee ambaye angeweza kumsaidia.
"Tangulia nyumbani nakuja" Alisikika mama Beda kwa sauti ya kukata tamaa.

* * *

Mvua kubwa ilikuwa imetulia na kuruhusu watu watoke majumbani mwao.Hali hii ilimuathiri sana mama Beda.Siku hiyo hakwenda kufagia barabara.Siku alizokuwa anapumzika ilikuwa kawaida yake kufanya biashara ndogondogo kama hii ya muhogo.Lakini leo alikuwa ameangukia pua,hakunusa wala hakupumua.Hakuna aliyekuja kununua muhogo zaidi ya watu watatu wa kwanza ambao walikuja kabla mvua haijaanza kunyesha.
Beda Sanga alitoka ndani ya nyumba ile ambayo haikuweza kuwasitiri vizuri kwa mvua kwani ilikuwa inavuja.Akajisogeza karibu na mama yake ili aweze kusikia lolote ambalo lingempa matumaini ya kwenda shule.Alijionea wazi ugumu wa biashara ya mihogo.Aliiona wazi huzuni iliyokuwa kwenye macho ya mama yake.Akukumbuka jinsi mama yake alivyoenda kuomba msaada kwa jirani yao ambaye anauwezo kidogo.
"Mama uliambiwa nini ulipoenda kwa mzee Uwesu?" Ilikuwa kama aliyemtonesha,mama yake hakujibu badala yake akaanza kulia kilikuwa kilio kamili.Huku akiwa katika hali ya kwikwi akaamwomba mwanae amsaidie kunyanyua vyombo warudishe ndani.Hakukuwa na biashara tena.Ilikuwa ni hasara tupu.Beda akaendelea kudadisi mama hakutaka kujibu.Akarudisha fikra jinsi alivyoenda kuomba msaada kwa Mzee Uwesu
"Baba mwanangu amefaulu naomba msaada wa mchango wenu kama inawezekana." Alikumbuka vema maneno hayo mara baada ya salamu
"We mama husinletee uchuro hapa kwani huko mnakofanya uchawi wenu hakuna michango.Kwa taarifa yako nakujua sana kuwa ni mchawi mkubwa hapa mtaani ndio maana huendelei,umemuua mumeo makusudi leo unakuja kutaka msaada kwetu?"
Baada ya maneno hayo Mama Beda akaondoka bila kuaga huku akilia.Hakutaka kabisa kumsimulia Beda mambo yale.
Usiku huo huo pamoja na kilio chake bado hakukata tamaa.Akaenda kwa Diwani wa kata yao.
"Hodi,hodi...." Alibisha hodi nyumbani kwa diwani.
"Karibu.." Sauti ya kike ilijibu kutoka ndani.Akafunguliwa
"Karibu ndani".Akamfuata yule binti ambaye mikono yake ilikuwa imelowa maji,bila shaka alikuwa anaosha vyombo muda huo.
"Karibu ukae." Alikaribisha binti huyo ambae alionekana wazi ni 'house girl'
Akakaa kwenye moja ya sofa za thamani zilizokuwepo pale sebuleni.Akaruhusu macho yake yaisanifu sebule ile.Thamani ya kile kiti alichokalia tu ingetosha kabisa kutatua matatizo yake yote ya ada na vifaa vya shule.Alistaajabu ukubwa na uzuri wa sebule ile.Akastaajabu zaidi kuona samaki ambao walikuwa wanafungwa kwenye kabati maalumu la vioo pale sebuleni.Hakumaliza kuisanifu sebule ile,diwani alifika pale sebuleni.Mzee Athumani Kipande diwani wa kata ya Charambe alikaa kivivuvivu katika moja ya viti vilivyokuwemo mle sebuleni.Alikuwa mzee mfupi mwenye mvi chache,mazingira ya nyumbani alipenda kuvaa sana msuli na kizibao
"Karibu mama" Aliita kwa mazoea tu kwani kiumri alikuwa mkubwa kuliko yule mama aliyekuwa mbele yake
"ahsante,shikamoo."
"Marhaba habari za nyumbani?"
"Nzuri kiasi baba"
"Kwanini kiasi?"
"Ahh." Alijikuta akishindwa kuongea na badala yake akaminyaminya vidole ambavyo vilikuwa vinatoa mlio kama vijiti vidogo ambavyo vilikuwa vinavunjika.Hatimaye akaamua kupasua jipu
"Baba nimekuja unisaidie juu ya swala la mwanangu,amachaguliwa kuijiunga na shule ya sekondari."
"Msaada gani unaihitaji?" Aliuliza diwani.
"Ili aweze kuanza masomo ninahitaji shilingi elfu arobaini kwani tayari mwenyewe ninayo shilingi elfu ishirini.Aliongea mama Beda huku hali ya kujiamini ikiongezeka.
"Aah,samahani mama unajua wiki hii kuna kundi la ngoma za kienyeji linakuja kutoka Botswana kwa hiyo akiba yangu nitaitumia huko mimi na familia yangu maanakiingilio kwa familia yote ni laki nne."Akatulia diwani na kumwangalia mama yule kwa jicho lililokosa huruma.Moyoni mama Beda alilaani sana kauli ile bora hata hasingeambiwa
Akanyanyuka pale kwenye kiti na kumuaga diwani wake.

Hizo zote zilikuwa kumbukumbu za siku mbaya ambazo zinapita katika maisha yake.Alisononeka sana moyoni.Ngalawa ya mawazo ikamfikisha kwenye mawimbi ya siku zile tamu ambazo alikuwa uhusinao mzuri na diwani yule.akakumbuka jinsi alivyoimba na kucheza ili diwani apate ushindi.Kumbukumbu zikamfikisha siku zile zenye ugwadu ambazo alipewa kitenge kipya cha waksi kutoka kwa mbunge mtarajiwa huku wakiongezewa na maji na soda kutoka kwa diwani wao.Akatikisa kichwa.

* * *

Ni siku nyingine saa 7:30 ilimkuta mama Beda akiwa na beseni lake la mahindi ya kuchemsha maeneo ya Mtongani.Ilikuwa ni katika jitihada zake za kuhakikisha Beda anaenda shule.Kidogo siku hii ilikuwa nzuri kwake kwani alibakiza mahindi mawili tu.Akaendelea kuzunguka maeneo ya pale kituo cha magari,hatimaye akamaliza.
Akaanza kuhesabu alichikipata.Ilikuwa ni shilingi elfu kumi na nne na mia saba.Akatoa elfu kumi aliyonunulia mahindi,elfu nne mia saba akaweka kibindoni.Akatembea taratibu kuelekea nyumbani.Hakutaka kupanda gari kwani faida ilikuwa ni ndogo mno.Hatimaye chakara chakara za miguu zikamfikisha Mbagala rangi tatu.Bado mjeledi wa kashfa iliyotolewa na jirani yake uliendelea kumtesa ndani ya nafsi yake.Inamaana hapa mtaani ndio ninavyotafsirika,etu nimemuua mume wangu!Aliwaza na kusikia fundo likiushika moyo wake kwa uchungu
Akatua beseni lake kisha akaingia ndani.Hakujua alifuata nini ndani akaamua kutoka.
Hakugundua njaa aliyokuwa nayo kutokana na fikra nzito alizokuwa nazo.Akakaa chini ya mpera,bado jinamizi la shutuma za jirani yake liliendelea kumuandama.Fikra zake zikamfikisha kwa marehemu mumewe.Hawakuwa na maisha mazuri lakini hasingeweza kushindwa kumlipia ada mwanae.Kitu kikamshika kooni.Akaanza kulia.
"Heheee,mumewe kamuua mwenyewe leo anamlilia." Kicheko cha Mama Suzi mke wa jirani yake kikamzindua.Akageuka na kumwangalia kwa hasira.Mama Suzi ambaye alikuwa anamwaga takataka kwenye kiwanja wa Mama Beda akaondoka huku akishusha maneno ya majigambo."Hunifanyi lolote nimeaga kwetu,umemuweza huyo huyo mumeo."Aliendelea kumwaga maneno ambayo yalimuumiza Mama Beda.Mama Beda alishindwa kuvumilia akaokota chupa ya konyagi akaanza kumfuata jirani yake huyo.Mama Suzi akaanza kukimbia huku akiangusha ndoo ya takataka ambayo aliibeba mkononi.Kwa nguvu zake zote Mama Beda akairusha ile chupa.

* * *

Alitembea taratibu kuelekea kituo cha polisi cha Mbagala Charambe.Hakujua ni nini kimemsibu mama yake hadi akajikuta yupo kituoni.Moyoni alikuwa na mswali mengi sana.Hakujua kwanini furaha kwake kilikuwa kitu hadimu.Hata jambo la kufurahisha yeye lilimtia uchungu.Mfano ulikuwa ni yale matokeo ya mtihani ambayo badala ya kumfurahisha yalimuhuzunisha.Angefurahivipi wakati hakuwa na uhakika
wa kusoma, halafu iweje leo akamatwe yule ambaye kidogo alimpa matumaini.
Alipofika pale mapokezi akamkuta yule bibi mfagia barabara akiongea na askari wa
zamu. Ingawa aliwakuta wakiwa katikati ya maongezi aliweza kuelewa wazi kile walichokuwa wanazungumza.
“Kutokana na uzito wa kesi yake ndiyo maana tukaamua kumuhamishia polisi
Chang’ombe.”
“huyu ndiye mwanae niliyekuwa nakueleza.” Aliongea yule mama huku akimkazia
macho yule askari kama anayehitaji msaada zaidi.
‘‘Sawa mama lakini sina namna ya kukusaidia kwani suala lake limeshikwa na wazito.”
Yule bibi mfagia barabara akamgeukia Beda na kumwangalia kwa sura iliyokosa
matumaini. Yule bibi akatoka mle kituoni lakini Beda hakutoka akaganda palepale
kabla ya kuanza kuongea na askari.
“Shikamoo.” Alimwamkia askari aliyemkuta pale.
“Marhaba unasemaje?” Aliuliza yule askari kwa sauti nzito yenye ukali kidogo.
“Nimesikia mama yangu yuko hapa nimekuja kumuona.”
“Umesikia, umemsikia nani?” aliongea yule askari kwa sauti iliyojaa dharau na ujivuni.
“Nimesikia kutoka kwa majirani.” Alijibu
“Anaitwa nani mama yako?” Aliuliza yule askari
“Mrs Sanga.” Alijibu Beda.
“Ahaa, Yule mama aliyetaka kuua mtu?” Swali hilo likamshitua Beda hakuweza
kulijibu.
“yule mama kesi yake ni nzito kahamishwa hapa yuko polisi Chang’ombe” Aliendelea
kuongea yule askari. Beda akaondoka pale kaunta huku machozi yakimtoka.
Alipofika nje akaangua kilio kikubwa. Kilio chake kikakatishwa na mtu aliyemshika
bega. Alipogeuka akamuona yule bibi ambaye mara nyingi alikuwa anafagia barabara
na mama yake.
“Usilie Beda mimi naenda kumuona mama yako huko Chan’gombe,
yatakwisha tu.” Yule mama alimbembeleza Beda aache kulia.
“Kwani ilikuwaje?” Aliuliza Beda huku akifuta machozi yake.
“Kulikuwa na ugomvi na yule jirani yenu Mama Suzi, kamrushia chupa kwa bahati
ikamkosa lakini hawakukubali wakaja kumshitaki huku kuwa amedhamiria kuua.”
Beda akashusha pumzi kwa nguvu. Ulikuwa ni muendelezo wa machungu katika maisha yake.

* * *

Mbu na harufu za mikojo vilikuwa kero ya aina yake kwa mama Beda ambaye
hakutarajia kupatwa na mkasa kama huo katika maisha yake. Ilikuwa kama ndoto pale
Mama Suzi alipokuja na kuanza kumrushia maneno ya kashfa. Bila kutarajia alijikuta
akiokota chupa na kumrushia. Ilikuwa ni bahati kwa Mama Suzi kwani chupa ilimkosa
na badala yake ikapiga ukutani na kupasuka vipande vipande. Mama Beda alijua
yamekwisha.
Siku ya pili akiwa kwenye maandalizi ya kuchemsha mahindi ndipo aliposhuhudia kile
ambacho hakukitarajia. Askari wawili wakiongozana na mzee Uwesu walifika
nyumbani kwake na kumkamata. Alielezwa wazi kuwa kosa lake ni kujaribu kuua.
Alilia, akalia… Kilio chake kikapotelea hewani, hakuna aliyemjali alionekana punguani.
Amlilie nani. Kwa namna ya kudhalilishwa akafungwa mikono yake kwa nyuma.
Watoto wakamzomea, majirani wakamcheka. Mpeleke akaroge gerezani.
Walichombeza safari yake hiyo. Hakuujua uchawi, hakumjua hata mganga wa kienyeji.
Labda umaskini wake na yale macho yake yaliyobadilika na kuwa mekundu kutokana
na kushinda kwenye jiko la kuni huku akibugia na kulizwa na moshi ule mkali.
Alishakubali matokeo sasa alikuwa anasubiri kudra za mola wake.
Akapokelewa na kiza cha mchana kwenye chumba kidogo ambacho hakina hata
dirisha. Baadae akatolewa bila maelezo yoyote na kupandishwa kwenye gari ambalo
lilimfikisha polisi Chang’ombe. Akawekwa mahabusu. Makazi duni kabisa ambayo
hakustahili kukaa hata mbwa. Hakutamani kuendelea kuishi, dunia aliiona chungu.
Hakujua kama kulikuwa na tofauti kati ya dunia na jahannamu ule moto mkali ambao
unaelezwa kwenye vitabu vitukufu.
Akiwa kwenye lindi la mawazo mlango ukafunguliwa. Akatolewa kwa muda.
Akashangaa baada ya kugundua kuwa ni mchana kweupe. Beda mwanae wa pekee
alikuwa kaunta akihitaji kuongea na mama yake. Alitaka kuongea nini? Ilikuwa ni
vigumu kufahamu kwani mtu na mwanae wakaangua vilio ambavyo vilidhihirisha jinsi
askari wale walivyokosa huruma.
“Afande Marwa mrudishe ndani huyo asitupigie makelele hapa.”
“Sawa afande.” Amri ya mkuu ilipokelewa mama Beda akarudishwa tena kwenye
chumba kile kibaya kuliko vyumba vyote alivyowahi kuingia. Akalia, akaliaa….. Sauti
ikakauka lakini bado kilio kiliendelea. Kama alivyolia kwa sauti akashindwa kusikika
sasa ilikuwa zaidi kwani alilia bila kutoa sauti. Alijua fika siri ya kifo cha mumewe,
kumbukumbu hiyo ikazidisha kilio kisicho na machozi.

* * *
JIFUNZE!
“Mwenye pesa si mwenzako na kamwe masikini hathaminiwi katikati ya pesa. Pesa
hubadili mioyo ya wema kuwa miovu, pesa hubadili ndio na kuwa hapana, pesa
hununua utu na mbaya zaidi pesa hiyohiyo hurejesha utu! Isake kwa njia halali, jitume
uwezavyo kuisaka. Ukiipata usiitumie kama fimbo maana utaitumia kuwachapa
wenzako duniani lakini ipo hukumu inakungoja. Nawe utachapwa mara elfu ya
ulivyochapa Duniani!!”…©George Iron, 2010

**MAMA Beda matatani, sauti yake inayolia unyonge haisikiki, wenye pesa wamemnyamazisha…..
Nini kitajiri!!! Beda hajui kama ataendelea kusoma ama la!!

ITAENDELEA!!
 
Kesho Inshallah tutaendelea wakuu
 
RIWAYA: KISU CHENYE MPINI MWEKUNDU
MTUNZI: Ahmad Mussa Mniachi
SEHEMU YA SITA

"Sawa afande." Amri ya mkuu ilipokelewa mama Beda akarudishwa tena kwenye
chumba kile kibaya kuliko vyumba vyote alivyowahi kuingia. Akalia, akaliaa….. Sauti
ikakauka lakini bado kilio kiliendelea. Kama alivyolia kwa sauti akashindwa kusikika
sasa ilikuwa zaidi kwani alilia bila kutoa sauti. Alijua fika siri ya kifo cha mumewe,
kumbukumbu hiyo ikazidisha kilio kisicho na machozi.
* * *
Ilikuwa ni wiki ya machungu kwa Beda, aliwaza mambo mengi. Umri wake mdogo
haukuweza kuhimili mikikimikiki mizito, akaanza kusikia maumivu makali ya kichwa.
Akapiga hatua kuelekea nyumbani kwa bibi mfagia barabara. Akafika maeneo yale ya
Kimbangulile. Bibi mfagia barabara alikuwa amekaa nje kwenye nyumba yake ambayo
ukiiangalia sana jinsi ilivyojengwa ilirandana na sura na umbo la mbwa mwenye lishe
duni. Ilikuwa ni nyumba ya miti ambayo ilijengwa kwa namna ambayo ingekushawishi
kuifananisha na mbavu za mbwa jinsi fito zilivyoizunguka na kujitokeza kama mbavu
za mbwa aliyekonda.
"Bibi shikamoo." Alisalimia Beda.
"Marhaba Beda, karibu sana." Alikaribisha. Beda alikaa chini akajilaza kwenye mkeka
ambao ulikuwa unasubiri amri ya mmiliki wake kuwa utupwe jalalani. Kichwa kilikuwa
kinamgonga hivyo hakuhitaji maongezi zaidi ya kulala na kugaragara. Bibi mfagia
barabara akashikwa na huruma akaenda duka ambalo lilikuwa jirani na pale nyumbani
kwake.
"Unazo panado." Alimuuliza muuza duka
"Zipo za Kenya na Tanzania" aliongea yule kijana huku akiyaweka mezani mapakiti
yote mawili.
"Kwani bei zinatofautiana?" Aliuliza bibi mfagia barabara.
"Hizi za Kenya Bei yake ni kubwa kuliko hizi za Tanzania."
"Haya, naomba hizo za Tanzania" Aliongea bibi mfagia barabara huku akitoa hela
kwenye pembe ya kanga yake. Dawa alizohitaji zikafungwa kwenye gazeti bila kufuata
utaratibu. Hakukuwa na maelezo zitumike vipi kana kwamba wote walikuwa
madaktari.
Alitembea haraka kumwendea Beda ambaye hali yake haikuwa nzuri.
Alipofika akasimama kando yake akiwa ameshika kiuno"Amka umeze dawa." Beda
akajiinua pale kwenye mkeka mbovu na kuanza kujikung'uta mchanga uliokuwa
kwenye shati lake.
"Usifikirie sana Beda mjukuu wangu mama atatoka tu." Aliongea bibi mfagia barabara.
Alimeza zile dawa akalala tena pale kwenye mkeka.
*****
Mwezi mmoja ulikuwa umepita toka mama Beda awekwe ndani. Nenda rudi za kila
siku zilimkatisha tamaa Beda. Kila walipokuwa wanatoka mara nyingi walikutana na
mzee Uwesu yule jirani yao akiingia. Mzee Uwesu alikuwa ni mtu mwenye nafasi ya juu
katika shiria la umeme Tanesco. Hili liliwatia mashaka kwani walihisi kuwa mzee
uwesu aliamua kumkandamiza makusudi mama Beda kwa kutumia umaarufu na fedha
alizokuwa nazo.
Siku ya pili Beda na bibi mfagia barabara walikuwa kituo cha polisi pale temeke
Chang'ombe. Wakamwona yule askari anayeshikilia kesi yao.
"Habari baba." Alisalimia yule Mama mfagia barabara kwa unyenyekevu ingawa
aliyekuwa anamsalimia alikuwa sawa na mwanae wa kumzaa.
"Salama mama , niwasaidie nini?"
"Baba si unaju siku zote tuna kuja kwa ajili ya yule mtu wetu?"
"Enhe sasa, ngoja tuongee kiutu uzima. Munayo elfu arobaini? Kama ipo njooni kesho
nitawasaidia sawa?"
"Sawa" Akajibu yule bibi bila kuwa na uhakika kama kweli ataipata hiyo elfu arobaini.
"Mwanangu Beda hii ndiyo dunia; Hakuna mwema aliyebaki, dunia imevaa joho la
dhuluma na ukatili. Tulipe pesa mama yako atoke unafikiri utasoma?"
Yalikuwa ni maneno makali kama kisu kilichowekwa kwenye moto hata kikawa na
rangi ya moto.
"Itakuwaje bibi?' Aliuliza Beda kwa sauti yenye majonzi ndani yake.
"hivi nyumbani hakuwa na akiba yoyote?"
"Ninapafahamu alipokuwa anahifadhi hela zake lakini sijui kuna kiasi gani maana
sijawahi kukagua."
"Basi nenda ukaangalie kama kuna chochote utaniletea sawa?"
"Sawa bibi." Alimjibu huku wakiingia kwenye daladala lililokuwa linaelekea Mbagala
rangi tatu. Wote walikuwa kimya hakuna aliyeongea chochote mpaka Rangi tatu.
Walipofika Beda hakukumbuka hata kumuaga bibi mfagia barabara, akili yake ilikuwa
pale alipokuwa anamuona mama yake akihifadhi fedha. Akatembea kwa haraka,
uvumilivu ukamshinda akaanza kukimbia. Akakimbia, akakimbia…………

* * *
Mwanamke aliyekonda mwenye nywele chafu huku akiwa na ukurutu mikononi na
sehemu zote ambazo ukurutu hupenda kujihifadhi alifunguliwa kutoka mahabusu ya
polisi Chang'ombe. Alishachoshwa na dunia, alikuwa anasubiri siku ifike ajiondokee.
Huenda nyumba ile ya mchanga ikamsitiri vema. Alijihisi kuichukia dunia. Alitamani
angekuwa mti mchungu wenye matunda yasiyoliwa ili tu aepukane na adha ya
binadamu. Hata hivyo alipingana na wazo hilo kwani miti michungu ndiyo ambayo
hutumiwa kwa ajili ya dawa za maradhi mbalimbali hivyo angeendelea kumnufaisha
binadamu. Akatamani bora angekuwa moto lakini akakumbuka umuhimu na matumizi
ya moto. Basi bora ningekuwa ukoma au matende…… Akaridhika na wazo hilo la
hatari.
Huyu hapa Sakina Msomba au Mrs Sanga ingawa mtaani anajulikana zaidi kwa jina la
mama Beda. Alitoka mle ndani huku akitoa harufu ambayo ilimfanya mwanae Beda
aangue kilio upya. Furaha ya kuachiwa huru mama yake ikamezwa na hali mbaya
aliyomuona nayo. Hakuweza kumtazama mara mbili mama yake. Alikuwa mama
mchafu aliyechakaa, anayejikuna na bila shaka mwenye chawa mwilini. Ilihuzunisha,
ilitia uchungu pia ilisikitisha. Mama Beda akamtazama mwanawe jinsi alivyokuwa
analia akatikisa kichwa, akamtazama bibi mfagia barabara akashindwa kuvumilia
akaanza kuangua kilio. Kilio hiki kilisababisha baadhi ya watu wenye roho nyepesi
ambao walikuja kwa matatizo madogomadogo kutokwa na machozi. Jinsi alivyokuwa
huyu mama ingekuwa sababu tosha ya kumliza binadamu yeyote mwenye huruma.
Alitembea kwa kuchechemea. Hatimaye alikuwa huru, uhuru mchungu ambao hauna
maana yeyote, katika fikra zake alijua kuwa uhuru wa kweli ni kifo. Angelala,
angelala…… Asingeamka tena ingekuwa ni usingizi wa milele usio na kero.
Kutokana na harufu mbaya aliyokuwa nayo hata wenye daladala walikataa kumchukua.
Ikalazimika kidogo kilichobaki wakodi teksi. Kweli wakakodi. Mwendesha teksi alikuwa
anasonya na kujiona aliyekosa bahati kwa kumchukua abiria yule wa aina yake. Kweli
alichukiza bado alitakiwa mtu aliyeshiba imani ya dini inayomjua Mungu muumba
kuweza kuvumilia na kujua kuwa ule ni mtihani katika mitihani ya Mungu.
Wakafika pale nyumbani kwao. Nyumba ilikuwa imepooza. Majirani wakawa
wanachungulia kwenye madirisha. Mama Juma tu ndiye aliyetoka kwenda kuwalaki.
Naye huyu alikuwa na sehemu ya ubinadamu hakuweza kuvumilia kwa hali aliyomuona
nayo jirani yake. Akaanza kulia huku akiweka sawa mtandio wake kichwani. Mama
Salome alikuwa anawasili nyumbani kutoka kanisani akasikia kilio hicho, akaacha
biblia mezani akakimbilia kule alikosikia kilio. Majirani hawa wawili ndio walioungana
na mama Beda kwenye kilio kile.
"wallahi, mie n'lishasema mtaa huu hawamuogopi Mungu." Aliongea Mama Juma kwa
lafudi ya kipemba huku akionyesha wazi kusikitishwa na kitendo cha majirani kutokuja
kumlaki mwenzao katika wakati ule mgumu. Mama Salome naye akaangua kilio.
"Jamani tumpeleke hospitali huyu." Alipendekeza Mama salome huku akijifuta
machozi yaliyotokana na kumhurumia jirani yake. Akatoa noti tatu za shilingi elfu
kumi. Mama Juma akaondoka kwenda kuomba hela kwa mumewe. Aliporudi alikuwa
ameongozana na mzee yule wa kipemba. Mzee Sudi Nassoro Bilali alipomuona mama
Beda akajishika kichwa kwa dakika kadhaa. "Wallahi, hawa polisi hawana ubinadamu."
Akakunjua msuli wake. Ndani alikuwa amevaa kaptura ambayo ilivuka kidogo magoti.
Akaingiza kwenye mfuko wa ile kaptura akatoa noti za shilingi elfu tano tano takribani
nane akakabidhi kwa bibi mfagia barabara.

* * *
Wiki moja ya matibabu katika hospitali ya wilaya ya Temeke ilimrejeshea mama Beda
Sura na hali ya kawaida ya kibinadamu. Angalau sasa aliweza kutazamwa bila kuwatoa
watu machozi. Akiwa mwenye faraja kidogo baada ya idadi chache ya majirani kuja
kumuona pale alipolazwa hospitali angalau sasa aliweza kuwaza juu ya mwanae Beda.
Bado alikuwa na mtihani mwingine atasoma vipi mwanae.
Siku zikakatika mama Beda akawa mwenye afya nzuri. Akarudi tena mtaani kutembeza
beseni la matunda na mahindi ya kuchemshwa. Biashara ilikuwa nzuri kias lakini
haikuweza kukidhi mahitaji yote.
Alimaliza mitaa na kona zote za wilaya ya Temeke kusaka noti. Moyoni aliwaza akaona
bora mwanae asingefaulu wangesaidiana biashara zile ngumu. Kwa kiasi fulani
matokeo ya mwanae ilikuwa chanzo cha matatizo yote. Siku za nyuma hakuwa na
mazoea kabisa na yule jirani yao mzee Uwesu, hata pale alipopita na gari yake alifunga
vioo ili wasisalimiane. Matokeo ya mtihani yalimlazimisha kwenda kuomba msaada
katika kasri ile ya shetani. Ndipo alipopokea mvua ya kashfa na matusi, haikutosha
ukaanza uchokozi mkubwa uliomvurugia mambo yake yote.

* * *
Alitembea taratibu akitokea dukani ambako alienda kununua majani ya chai.
Alipishana na wanafunzi ambao walikuwa kwenye sare za shule tofauti tofauti
wakigombea magari. Alijisikia uchungu sana alipobahatika kukutana na wanafunzi
ambao alisoma nao shule moja. Walipendeza sana ndani ya sare zao mpya. Alijitahidi
kutembea katika namna ambayo isingemkutanisha na wanafunzi wale. Kwanini huendi
shule? Hilo ndilo swali aliloliogopa zaidi kwani lingeleta mlolongo wa kumbukumbu
mbaya ambazo zingeweza hata kumliza. Hakutaka kulia, kama kulia alilia sana sasa
alikuwa anasubiri matokeo tu. Aliamini kuwa kile kitakachotokea pengine ndicho
alichokadiriwa na Mola jalali. Hakutaka kuwaza lolote juu ya mambo ya shule hakutaka
kumuuliza tena mama yake kwani angemtonesha vidonda vya mahabusu ambako
amekaa mwezi mmoja na siku kadhaa bila kusomewa mashtaka kisha kwa shilingi elfu
arobaini tu akatolewa. Lilikuwa ni pigo baya katika maisha yake. Aliwaza mengi juu ya
tukio lile, pengine yule mzee ana wivu kwani mtoto wake hakuchaguliwa kujiunga na
sekondari. Akayapuuza mawazo hayo na kuendelea kupita njia alizoziona kuwa salama
kwake kwani zisingemkutanisha na wanafunzi wenzake. Alikosea, tena alikosea sana.
Alibadili mwelekeo akapita kichochoro ambacho alidhani kitakuwa salama zaidi.
"Paaa." Moyo wake ulishituka baada ya kukutana na Vick msichana aliyekuwa anakaa
naye dawati moja. Alikuwa amevaa sketi ya kijani na shati jeupe. Chini alikuwa amevaa
viatu vyeusi vya ngozi na soksi nyeupe. Alipendeza.
"Oooh, Beda huyo mambo."
"Poa Vick" alimjibu msichana yule mpole. "Vipi shule badobado?" Kama alivyotarajia
lilikuja lile swali aliloliogopa. Hakupenda kujibu swali lile lakini alikumbuka jinsi Vick
alivyokuwa akimsaidia mambo mbalimbali pale walipokuwa darasani. Ni mara ngapi
Vick amediriki kumnunulia peni na daftari. Hakuona sababu ya kuto mweleza ukweli.
"Vick mwenzi sijui kama nitaendelea na masomo, we mwenyewe si unaifahamu hali
yetu?" "Kwani Ada ni shilingi ngapi huko shuleni kwenu?" "Joining Instruction
zinaonyesha kuwa ni shilingi elfu arobaini ukichanganya na mahitaji mengine
madogomaadogo inafika elfu sitini." "Siku zote hizo mama ameshindwa kupata hicho
kiasi.' "Alikuwa anakaribia kutimiza, angekuwa ashatimiza lakini akakamatwa na polisi
mpaka kuja kutoka kiasi chote kilikuwa kimeishia kwenye matumbo ya polisi na
amekaa huko mwezi mmoja na nusu." "Mh. ilikuwaje mpaka akakamatwa?"
"walirushiana maneno na mama mmoja jirani ndipo kwa hasira yule mama akaenda
kuripoti polisi kuwa Mama anamtishia kifo wakati si kweli na yeye ndiye aliyeanzisha
ugomvi kwa kumwita mama mchawi." Vick alimtazama kwa macho yaliyojaa simanzi.
Ni wazi hakutaka kabisa kusikia Beda akikosa fursa hiyo adhimu ya kuendelea na
masomo. Akainamisha kichwa chini. "Beda, pole sana kwa yote naomba niende shule
lakini nitakutafuta." alimaliza na kumpungia mkono Beda. Beda aliendelea kumkazia
macho binti yule ambaye baba yake alikuwa na cheo kikubwa jeshini. Akaondoka huku
akijilaumu kwa kuruka jivu na kukanyaga moto. Atanitafuta kwa lipi. Aliwaza jinsi binti
huyu anayetoka katika familia inayojiweza kimaisha alivyoweza kumtembelea mara
kwa mara wakati ule wanasoma. Akakumbuka hata pale aliponunuliwa vitabu.
Akaachana na mawazo hayo, akaamua kuongeza hatua ili asije kukutana na mtu
mwingine. Aliogopa sana kama angekutana na Mrisho. Huyu alikuwa anamchukia sana
Beda eti kwa sababu alikuwa anamzidi kwenye matokeo ya mitihani Darasani. Alijua
wazi kuwa kama angesiki kuwa amechaguliwa na ameshindwa kuuendelea angecheka
sana. Alimchukia sana Mrisho kwani ndiye aliyemuanzishia majina mengi mabaya
darasani lakini hata hivyo majina hayo hayakuenea.
"We Beda unaenda wapi?" Akashituka baada ya kusikia sauti ya mama yake.
"He." Akashangaa baada ya kugundua kuwa alikuwa ameipita nyumba yao hatua
kadhaa. Alikuwa na mawazo mengi kiasi cha kukosa umakini na kutaka kupita nyumba
yao. Alijishangaa hata yeye mwenyewe kwa tukio lile.

* * *


NUKUU!!
"HAO nd'o wanadamu, wanayatumia madhaifu yao wanajilinganisha na nyadhifa zao
kisha wanakugandamiza! Mwanadamu kamwe si wa kumuamini kwa asilimia mia
moja, maana anaweza kubadilika sekunde yoyote ile na kukufanya ufumbe macho na
kufumbua ukidhani unaota mabadiliko yale… ishi na viumbe hawa kwa tahadhari,
mwanadamu pekee wa kumuamini kwa asilimia zote ni WEWE MWENYEWE!!"
……George Iron, 2012


Like za kutosha wakuu ili niangushe mzigo mwingine kesho,kazi kwenu wadau
 
jaribu kufupisha mkuu, kuna vitu visivyo vya muhimimu umeviandika kwenye hii sehemu ya tano na sita ............

Grand PA
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom