Nahitaji kufikia kiwango gani cha uelewa ili niweze kuelewa jinsi Mungu anayeelezwa kuwa na Upendo usio na kifani, mwenye uwezo wote na mamlaka yote, anaweza kuruhusu mabilioni ya watu kupoteza maisha wakubwa kwa wadogo kutokana na majanga ya asili kama matetemeko ya ardhi, milipuko ya volkano, na magonjwa hatari kama Ebola?
Ikiwa Mungu ni mwenye upendo mkamilifu, kwa nini ulimwengu umejengwa kwa namna ambayo sheria zake za kimaumbile husababisha maafa makubwa yanayogusa hata wasio na hatia? Je, ni aina gani ya mpango au hekima inayoweza kuhalalisha mateso ya mtoto anayekufa kwa ugonjwa au familia inayofutwa na tetemeko la ardhi?
Zaidi ya hapo, leo hii nchini Tanzania na katika nchi nyingi za Afrika, wapo watu wenye albinism wanaoishi katika mateso ya kudumu kutokana na miale ya jua inayochubua ngozi zao kwa sababu ya ukosefu wa melanin. Kama Mungu ni mwenye huruma na uwezo wa kuzuia hali hiyo, kwa nini aliruhusu wazaliwe katika mazingira ambayo miili yao haiwezi kustahimili hali ya kawaida ya mazingira?
Na si watu wenye albinism pekee. Kuna watu wengi huzaliwa na matatizo mazito ya kibaolojia, kasoro za kinasaba, ulemavu wa viungo, au magonjwa sugu hali ambazo, kwa mujibu wa imani ya Mungu mwenye uwezo wote, zingeweza kuzuiwa kabla ya kuzaliwa kwao.
Hoja hii si mpya. Charles Darwin aliwahi kuandika kuhusu nyigu aina ya Ichneumonidae (ichneumon wasp) ambao hutaga mayai ndani ya mwili wa mdudu-hai; watoto wa ichnemonidae hula mwili wa mwenyeji polepole (mdudu-hai) hadi afe. Darwin aliona ugumu wa kuoanisha ukatili huu wa kimaumbile na wazo la Mungu mwenye huruma kamili. Alisema hangeweza kushawishika kwamba Mungu mwenye rehema angeumba mfumo wa namna hiyo kwa makusudi.
Aidha, ni muhimu kufafanua msimamo wa wasioamini Mungu (atheists). Wengi wao hawadai kutokuamini kwa sababu tu “hawamwelewi Mungu anayefanya kazi beyond human comprehension.” Badala yake, wanadai kutumia njia zilezile zinazotumiwa na waumini wanapojaribu kumuelewa Mung, kuuliza maswali, kuchambua maandiko, kutafakari hoja za kifalsafa, na kutafuta ushahidi.
Wanapouliza maswali magumu ambayo kwa karne nyingi hayajapatiwa majibu yanayokubalika kwa wote, kuhusu uovu wa asili, na wanapoomba uthibitisho wa uwepo wa Mungu kama Allah, Mungu wa Utatu (Trinitarian God), au Yahweh, lakini hawapati ushahidi wa kimajaribio au wa kimantiki unaowaridhisha, wao huchagua kutokuamini.
Kwao, tatizo si kukataa kitu wanachokielewa; bali ni kutokushawishika na hoja au ushahidi uliopo. Kwa mantiki yao, kama madai ni makubwa, Mungu mwenye uwezo wote, mwenye kujua yote, na mwenye upendo kamili, basi kiwango cha uthibitisho kinapaswa kuwa kikubwa sawasawa na madai hayo.
Hivyo basi, swali la msingi linabaki:
Je, tatizo liko katika mipaka ya uelewa wa kibinadamu, au kuna mvutano wa kimsingi kati ya dhana ya Mungu mwenye upendo mkamilifu na uhalisia wa mateso makubwa yasiyochaguliwa na binadamu?