BigTall
JF-Expert Member
- Mar 9, 2022
- 422
- 1,049
Mbowe, jana Machi 6, 2024 kupitia Wakili wake John Mallya aliwasilisha shauri hilo chini ya Hati ya Dharura mbele ya Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Mary Mrio.
Amefungua shauri dhidi ya Maregesi Paul, Fidelis Felix, Christina Mwakangale, Janeth Josiah, Exuperius Kachenje, Hellen Sisya, Kulwa Mzee, Nora Damian, Makuburi Ally, Mkurugenzi wa Gazeti la Tanzania na Kampuni ya Udalali ya JJ Auctioneers& Debt Collectors.
Wakili Mallya alidai wajibu maombi tayari wamepewa madai yao pamoja na hati ya kiapo iliyopwa na Mbowe Februari 26, 2024.
“Mheshimiwa wajibu maombi tumeshawapa nakala hivi karibuni tusikilize kama wamekuja na majibu,” alidai Mallya.
Dudley Mbowe
“Mheshimiwa tumepitia nyaraka wenzetu wametupa siku 15 tujibu, tunaihakikishia Mahakama kwamba tutajibu ndani ya muda tuliopewa,” alidai Kulwa.
Wakili Mallya aliomba kujibu hoja hiyo, alidai shauri lao wameliwasilisha chini ya hati ya dharura, maombi yao ni kuiondoa nyumba hiyo kwani tayari ilishabandikwa matangazo kwa ajili ya kupigwa mnada.
Alidai ikiendelea kuwa kama ilivyo inaweza kupigwa mnada kwa sababu suala hilo lina muda wa utekelezaji.
Akijibu Kulwa alidai ni kweli maombi yako katika hati ya dharura lakini lazima wasome vizuri ili wajibu kwa kuwasilisha hati ya kiapo kinzani kwa sababu katika maombi hayo kuna suala la kumlipa mwombaji gharama .
Aliomba kama siku 15 nyingi watajibu ndani ya siku saba, Mahakama ilikubali majibu yawasilishwe mapema, shauri hilo litasikilizwa Machi 12, 2024.
Mbowe katika madai yake anadai nyumba hiyo iliyokamatwa si mali ya Dudley na kwa kuthibitisha hilo amembatanisha na hati ya nyumba hiyo yenye jina la Freeman Mbowe.
Mahakama hiyo pia imepanga kuendelea na shauri la madai ya waandishi hao kwa Mkurugenzi wa Gazeti la Tanzania Daima, Dudley Machi 12, 2024.
Februari 13, 2024, Mahakama ilikubali maombi ya wadai na kumteua dalali wa Mahakama kukamata nyumba kwa ajili ya kuipiga mnada.
Februari 28, 2024 dalali wa Mahakama, Jesca Massawe alifanikiwa kubandika matangazo ya kukamata nyumba ya Mkurugenzi tayari kupigwa mnada kufidia deni la malimbikizo ya mishahara wafanyakazi.
Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Mary Mrio alitoa amri hiyo baada ya kupitia hoja za washinda tuzo katika Tume ya Usuluhishi na Uamuzi(CMA) Julai 2023.
Shauri hilo namba 28461 la mwaka 2023, wadai Maregesi Paul na wenzake tisa dhidi ya Mkurugenzi wa Gazeti la Tanzania Daima, Dudley Mbowe.
Baada ya mdaiwa kukaidi kulipa, wadai walikubaliana njia sahihi kukamata nyumba yake namba 9 iliyopo Mtaa wa Feza, Mikocheni B barabara ya Chipaka na Mahakama ilikubali.
Walalamikaji hao walipata tuzo Julai 17, 2023 mbele ya Msuluhidhi wa CMA Ilala, Bonasia Mollel.
Madai ya awali yalikuwa jumla ya Sh milioni 114 baada ya kukaa mezani kwenye majadiliano kwa pamoja kiwango hicho cha fedha kilishuka na kufikia Sh milioni 62.7.
Dudley alikubali kulipa fedha hizo kwa awamu tatu, Oktoba 30, Desemba 30, 2023 na awamu ya mwisho ilikuwa mwishoni Februari 2024 lakini hakulipa.
Vilevile anadai yeye si sehemu ya wadaawa katika shauri hilo la maombi ya utekelezaji baina ya wanahabari hao na mkurugenzi wa gazeti la Tanzania Daima.
Hivyo anaiomba mahakama hiyo ifanye uchunguzi kubaini usahihi wa ukamataji wa nyumba hiyo kwa ajili ya utekezaji wa shauri la maombi ya utekezaji (tuzo ya CMA) na ichunguze kama yeye alikuwa ni mdaawa katika shauri hilo.
Kisha anaiomba Mahakama hiyo baada ya uchunguzi huo itamke kuwa kukamatwa kwa nyumba hiyo si halali na ni batili na iwaamuru wajibu maombi walipe gharama halisi alizozitumia mpaka tarehe ya kuachiliwa kwa nyumba hiyo na nafuu nyingine kadri Mahakama itakavyoona inafaa.
Katika shauri la maombi ya utekelezaji lililofunguliwa na wanahabari hao, wakati lilipoitwa leo, mjibu maombi yaani mkurugenzi wa gazeti la Tanzania Daima/ Dudley hakuwepo mahakamani yeye mwenyewe wala mwakilishi wake.
Hivyo, Mahakama hiyo imeahirisha na kupanga kuendelea nalo katika hatua ya usikilizwaji Machi 12, 2024.
Mwanzo wa sakata hilo
Awali, wanahabari hao walifungua shauri hilo la mgogoro wa kikazi namba 28461 la mwaka 2023, CMA Mkurugenzi wa Gazeti la Tanzania Daima, baada mwajiri wao huyo kuvunja mikataba yao ya ajira, wakiomba kulipwa malimbizo ya mishahara yao jumla ya Sh114 milioni.
UPDATES
- Waandishi wambwaga Freeman Mbowe Mahakamani. Nyumba yaachiwa
Chanzo: Bestmedia