Bishop nakubaliana na yote uliyosema. Sasa kuna jitahada zozote ninyi kama wadau wa filamu (umepata kuwa katibu wa Tanzania Film Federatiion (TAFF)) kupambana na hali hii? Wengine tunaowaza kuingia katika medani ya Filamu tunatishwa sana na mazingaombwe haya.
Dah, unajua kuna matatizo mengi sana katika tasnia hii, kwanza watayalishaji wa filamu nchini
wamekosa mafunzo ya msingi (nitty-gritty) ya namna ya kutengeneza kazi zao katika kiwango
kinachokubalika, wengi ni wabinafsi na wanaowekeza kidogo na kutarajia wavune mara dufu
kwa mara moja. Ubinafsi huo umesababisha filamu zetu kuwa ni kitu kisichozingatia au kuhitaji
taaluma yoyote. Watu wanalipua kazi na wanafanya mambo bila kuzingatia utaalam. Wanafanya
mambo ili mradi wanajua watauza na kupata pesa, basi. Ubinafsi huu umekuwa ni sababu kuu ya
kuufanya uwanja wa filamu wa Tanzania kuwa sehemu inayoongoza kwa kutokuwa na mgawanyo
wa majukumu. Si ajabu kuona mkurugenzi wa kampuni ya kutengeneza filamu, ndiye aliyeandika
skripti, ndiye muongozaji mkuu, ndiye muigizaji mkuu na kadhalika.
Lakini hata hivyo kipindi chote nimekuwa nikipigania tasnia hii iwe rasmi, nimeshawahi kumuandikia
Waziri Nchimbi mara kadhaa na nimewahi kuwasilisha ripoti yangu ya utafiti kwa Rais Kikwete ili waone
umuhimu wa tasnia hii na kuirasimisha. Unajua sekta ya filamu hapa nchini licha ya ubovu wa filamu zake
ambazo huwa naziangalia kwa ku-
Fast Forward, lakini imesheheni utajiri mkubwa sana, tatizo ni kwamba
hadi sasa bado si rasmi kiasi cha kuwafanya wadau wake waendelee kuwa masikini wa kutupwa pamoja
na kuingiza mamilioni ya pesa ambayo hata hivyo yanawafaidisha wafanyabiashara wachache huku
serikali ikiwa haiambulii chochote.
Huu mpango wa Serikali wa Kurasimisha Biashara na Rasilimali za wanyonge nchini (Mkurabita)
hauonekani kuwasaidia wajasiriamali katika tasnia hii ili waweze kufanya kazi kwenye mazingira
yaliyo rasmi kwa kuwa hali ilivyo sasa inawafanya wakose fursa nyingi za kukuza kazi zao ikiwa ni
pamoja na kutoa kazi bora. Pia inawakatisha tamaa wanaotaka kuwekeza katika tasnia hii kama
wewe kwa kuwa hawana uhakika na soko. Mimi mwenyewe ingawa nipo kwenye tasnia hii kwa
miaka mingi na nimebahatika kuisomea lakini sijawahi kutoa filamu kwa kuwa kuna mambo mengi
yanayokwaza. Na hata ukitengeneza filamu nzuri hali hii inazifanya filamu zionekane hazina thamani kutokana
na tasnia kutokuwa rasmi. Kwa sasa kidogo serikali imeanza kuitambua tasnia hii, labda tusubiri kuona
watu makini wakijitosa katika ulingo, kwani katika kukabiliana na wimbi la watendaji wasio na uwezo wala
taaluma, Serikali kupitia Bodi ya Ukaguzi wa Filamu na Michezo ya Kuigiza ilizindua kanuni mpya za Sheria
ya Filamu na Michezo ya Kuigiza mjini Musoma mkoani Mara, zilizozinduliwa na Makamu wa Rais,
Dk. Mohamed Gharib Bilal. Kanuni hizo zimeainisha adhabu mbalimbali ikiwemo kulipa faini ya papo kwa
hapo isiyopungua Shilingi milioni mbili kwa watengenezaji, waoneshaji na wasambazaji wa filamu watakaozikiuka.
Kuzinduliwa kwa kanuni kuliambatana na kauli ya Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo,
Dk Emmanuel Nchimbi, kuwataka wote kufuata sheria na kusajiri kazi zao kabla hatua za kisheria
hazijachukuliwa dhidi yao. Waziri Nchimbi alisema Serikali imechoshwa na uwepo wa filamu zisizo na maadili.
Kanuni hizi zinaelekeza kuwa anayetaka kutengeneza filamu lazima aombe kwanza kibali. Miongoni mwa
mambo yanayohitaji kibali ni pamoja na kutumia vifaa na mavazi rasmi yanayotumiwa na majeshi ya
ulinzi na usalama, madaktari, viongozi wa dini, manesi na sare za wanafunzi. Kibali hakitatolewa kwa
picha ambazo uchezaji, miondoko ya mwili wa mshiriki au msanii unalenga ama lengo pekee ni kushawishi,
kuwashawishi watazamaji kupata, kujenga taswira na hisia za ngono au kujamiiana.
Naamini kama serikali watazingatia haya, tutashuhudia watu makini wakiwekeza kwenye tasnia na
kuzika zama za utitiri wa hizi Bongo movie zisizo na kichwa wala miguu zinazokopi tamaduni za nje...