Naamsha vidole vyangu kuandika haya nikiwa na masikitiko makubwa na moyo mzito wenye majonzi yasiyotamkika. Majonzi ya kupotelewa na rafiki wa karibu, kiongozi mnyoofu na kipenzi cha watanzania wanyonge.
Taarifa za ajali iliyopoteza maisha ya Regia niliipata kupitia kwa afisa wa polisi ambaye sitamtaja, majira ya saa sita ikiwa ni nusu saa tuu tangu kutokea kwa ajali hiyo . Ghafla masikio yangu yakawa mazito kuendelea kusikiliza na macho yangu kupoteza nuru, kwa hakika nilipatwa na ganzi ya simanzi na moyo wangu ulizimia kwa kitambo.
Akiwa kama rafiki niliyefahamiana naye tangu chuoni SUA miaka ya 2003-2006, Regia alikuwa mtu asiye na makuu, mcheshi na mwenye moyo wa unyenyekevu. Japokuwa hakuwa akishiriki kwa kasi siasa za vyuoni bali alionekana kuwa kiongozi katika kundi lolote la watu aliloshiriki.
Kuanzia miaka ya 2008 nilianza kuliona jina la Rejia katika medani za siasa, wakati huu nikiwa mfanyakazi wa serikali mjini Ifakara ambako ndipo nilipo hata sasa. Kwa hivyo, Rejia akawa mbunge wangu akiwakilisha jimbo ninaloishi bungeni. Kwa bahati mbaya nilikuwa nje ya nchi wakati Rejia akifanya kampeni za ubunge jimbo la Kilombero 2010, na wakati huo tulikuwa tukiwasiliana kwa facebook na emails juu ya rundo la kero na changamoto za maendeleo jimboni hapa pamoja na mbio za uchaguzi, Tulipeana moyo kwamba ushindi utapatikana......Hata baada ya kuwa mbunge wa viti maalum tuliendelea kuwasiliana na mara zote aliwakilisha vema kero za wananchi wake. binafsi amenisaidia sana katika masuala fulani ya kikazi.
Mara ya mwisho kuwasiliana na Rejia ilikuwa ni tar 19 Dec. 2011, tulichat kwa muda na akaniahidi tungeweza kuonana nyakati za Chris-mass hapa Ifakara. Kwa bahati mbaya hatukuweza kuonana mpaka mauti ilipomfika mpendwa wetu. Inabaki kuwa kumbukumbu nzuri kwamba tulikuwa tunaishi na mtu wa kipekee na mwenye kila sifa za ubinadamu wema. Kwangu inakuwa kama ndoto, yote niliyoyaona na kuyasikia katika mazishi ya Rejia hujirudia mara kwa mara akilini mwangu. Hakika tulikupenda sana kwa kadri ulivyotupenda pia....lakini yupo aliyekupenda na anayekupenda zaidi hata sasa, huyo alikuleta duniani, na huyo amekuchukua mbinguni, JINA LAKE MUNGU AISHIYE NA KUMILIKI LIHIMIDIWE DAIMA. Mungu anabaki kuwa Mungu hata kama hakujibu kama tuombavyo na kutamani.
Binafsi nitakuenzi Rejia na kushiriki kuendeleza yote uliyoamini na kupigania. Mungu aipe nguvu familia ya Mtema na hasa pacha wake Remija katika wakati huu mgumu mno kwao. Poleni ndugu na marafiki wa Rejia, poleni wananchi wote wa Ifakara, poleni wanachama na wapenzi wa CHADEMA, Poleni watanzania wote.
Mungu aiweke roho ya mpendwa wetu Rejia Mtema Mahali pema peponi, Amen!