Familia yaomba uchunguzi kifo cha aliyechapwa viboko 280

BARD AI

JF-Expert Member
Jul 24, 2018
3,376
8,119
1673638052070.png
Serikali imeombwa kufanya uchunguzi na kuwachukulia hatua waliohusika na kifo cha mkazi wa Sanawari, wilayani Arumeru, Mkoa wa Arusha, Nelson Mollel (32) aliyefariki dunia kwa kudaiwa kupewa adhabu ya kuchapwa viboko 280.

Mollel alifariki Januari 8, 2023 kwa madai ya kuchapwa baada ya kutuhumiwa kumtukana mama yake mzazi.

Wazee wa jamii ya Kimasai na Kimeru wilayani Arumeru Mkoa wa Arusha wamekuwa wakitoa adhabu ya kuwachapa viboko vijana ambao wamekuwa wakibainika kufanya matendo ambayo ni kinyume cha maadili.

Ombi hilo limetolewa leo Ijumaa Januari 13, 2023 na msemaji wa ukoo huo, Richard Mollel katika ibada ya maziko iliyofanyika nyumbani kwa wazazi wa marehemu Sanawari.

Msemaji huyo amesema kifo hicho kina utata na kuwa hadi sasa hawaelewi kilichotokea kwani hawajui nani kafanya tukio hilo na kwa sababu gani.

"Tulikosa jibu mpaka sasa hivi, tunaomba serikali itusaidie tupate majibu stahiki ili aliyehusika asirudie kuyafanya haya, kwani kifo hiki kina utata," amesema.

"Kilichofanyika ni uzembe na hili likemewe ili mwingine asirudie. Niwaombe wana familia tuendelee kuwa na moyo wa mshikamano wa upendo tusilipize kisasi," amesema.

Awali akiongoza ibada ya mazishi, Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Mjini Kati, Daniel Sadera amewataka wazazi na walezi kuhakikisha wanazingatia malezi kwa vijana wao kwani wengine wamekuwa chanzo cha vijana kukosa maadili.

Amesema kila mzazi na mlezi ana wajibu wa kuhakikisha maadili ya vijana yanazingatiwa ili kuwa na kikazi chenye maadili mema kwa kuonya vijana wao.

"Kama mzazi uliwajibika? Kijana akikutana na mzazi anakuambia tabia unayofanya siyo njema ni wajibu wake chukua moyo wa hekima na utulivu kupokea yale mafundisho. Niombe jamii tuone jinsi ya kuwajibika kwa ajili ya vijana na watoto wetu. Pia wazazi zingatieni maadili, angalia vijana wa miaka 30 hadi 18 hata ukimwambia nyanyua tofali hawezi, kwa ajili dawa za kulevya bangi na sigara au pombe," amesema.

"Akina mama wa Kiarusha mnachangia hili kukumbatia watoto, laiti tungechukua wajibu wetu mapema mengi tungeyaepuka kama hili. Tuwafundishe watoto maadili ya imani kwani kuna umri huwezi kumsemesha kama hana maadili ya kijamii au kiimani," amesema kiongozi huyo.

"Misingi tumeiharibu sisi wenyewe hata haya tunatoona ni madogo na yanatuuma. Tujifunze kupitia matukio haya, aliyefanya hivi kafanya ukatili lakini hata wewe ambaye ulikuwa naye umemsaidiaje aliyefanyiwa hivi. Damu inapomwagika inazaa laana na hukumu, tusifarakane isije kuwa mwanzo wa damu kumwagika zaidi na laana kuendelea," ameongeza.

Juzi dada wa marehemu, Jackline Elias Mollel amesema mdogo wake amepigwa viboko 280 badala ya fimbo 70 vinavyopaswa kwa mujibu wa taratibu zao ambapo anadaiwa kumtukana mama yake mzazi Januari 1, 2023 na kufariki baada ya kuchapwa fimbo hizo.

MWANANCHI
 
Back
Top Bottom