SoC02 Elimu bure

Stories of Change - 2022 Competition

josephdeo

Member
Nov 23, 2015
95
196
Mara baada ya serikali ya awamu ya tano kuingia madarakani mwaka 2015 chini ya Hayati Dkt. John Pombe Magufuli aliamuru mara moja kuwa elimu itolewe bila malipo ikiwa ni utekelezwaji wa sera zake wakati akiomba ridhaa kwa watanzania kuwa kiongozi mkuu wa nchi. Tamko ili ambalo ni sheria moja kwa moja lilianza kutekelezwa mara moja huku watanzania walio wengi ambao wapo katika wimbi la umasikini hii ilikuwa haueni kwao.

Kwani wakati wa nyuma ili mwanafunzi aweze kuwasili shuleni kulikuwa na michango chungu mzima hivyo kuja kwa tamko hili lilikuwa kama msaada. Kwa mtu aliyezama kwenye maji kisha kufanya juhudi za kujiokoa na baadae kupata msaada.

Haya ni maajabu ndivyo ambavyo yanaweza kuwa na hili ndilo alilolifanya Rais wa awamu ya tano kwani umekuwa ni muujiza ambao umekuja kipindi ambacho atukuutarajia kama utakuja.

Muujiza huu umetendeka na ulikuja wakati mahususi au kipindi ambacho wananchi walihitaji muhujiza huu. Magufuli alituvusha hapa kwani sera hii hata wapinzani waliipigia upatu sana. Kwa pamoja tunasema asante kwa msaada huu mkubwa ambao serikali yako ilitoa ahadi na kuutekeleza moja kwa moja. Mungu airehemu nafsi yako huko ulipo.

Lakini sasa kila kwenye jema kuna baya lake ambapo pengine linaweza lisisemwe kwa sababu ya uzuri wake. Ni sawa kabisa tunapaswa kushukuru kwa mazuri yaliyofanyika lakini hii hatunyimi uhuru wa kuyasema yale ambayo hayapo sawa kwenye mazuri hayo. Ni muhimu kuyasema ili kuondoa hayo makando kando na kufanya mambo hayo yawe mazuri zaidi kwa wanayoyapokea.

kusema binadamu aridhiki hata umfanyie mema ya kiasi gani...lakini anagalau atafurahi kimya kimya kama ikiwa utafanya lile ambalo limekuwa jema machoni pake. Lakini hii aina maana kuwa hatupaswi kukosoa kwenye yale mema kwa kigezo cha kutoridhika. Mpaka kufikia kuyasema haya yote ni katika kuhakikisha tunapata yaliyo mema katika elimu yetu ambayo inatolewa bure.

Siku moja nilipata bahati ya kuhudhuria mkutano ambao ulihusisha wazazi na bodi shule katika maendeleo ya ufaulu wa shule hiyo. Hapo ndipo nilipopata wasaa wa kuyawasilisha haya kama story of change ya humu jukwaani.

Wazazi wengi sana wamekuwa kama vipofu na upofu huu umesababishwa na neno elimu bure. Hivyo kushindwa kufahamu kuwa elimu ni gharama na ikiwa unaona hivyo jaribu ujinga.Watu wengi wamejaribu ujinga kwa sera ya serikali ya elimu bure kwa sababu hawataki kuchangia maendeleo ya elimu kwa sababu wanaamini na serikali imewahakikisha kuwa elimu ni bure.

Matokeo yake ni kuwa wafunzi wanaendelea kuburuza mikia katika mashule hayo ambayo elimu inatolewa bure. Wanafunzi wanamaliza elimu zao huku wakiwa hawana maarifa ya kuweza kuwasaidia kupambana na changamoto za maisha.

Elimu bure imekuwa nguzo muhimu ya kuwaachia majukumu ya malezi waalimu na sio mashirikiano kati ya waalimu na wazazi. Watu wamekuwa wakitaka watoto kwenda shule na kurudi pasipo kuchangia maendeleo ya mtoto anapokuwa shuleni. Lakini ubure wake ni kuondolewa kwa ada na baadhi ya michango. Ila michango ya taaluma inapaswa kuendelea kuwepo ili kutoa nafasi nzuri wa waalimu kufanya vyema.

Wazazi ni muhimu kufahamu kuwa elimu ni gharama na hivyo unapaswa kugharamika haijalishi ni kwa kiasi gani serikali imetoa tamko lake juu ya uhalali wa elimu bure. Wewe kama mzazi unapaswa kushirikiana na waalimu katika upande wa taaluma ili kuona mnamsaidiaje mwanafunzi kwa nafasi zenu kama mzazi na kama mwalimu.

Katika msaada huo hapo ndipo kunaingia swala la kuchangia. Lakini wazazi wa leo kwa kuwa wamehakikishiwa kuwa elimu inapaswa kutolewa bure ivyo wanakuwa wagumu kushirikiana na waalimu katika michango hii.

Hivyo ushauri wangu kwa serikali ni wajaribu kubadilisha approach zao kwa wananchi na kuwaambia ukweli wa mambo ulivyo kwani katika shule hizi hakuna walimu wa kutosha, vifaa na mazingira ya kumuwezesha mtoto kupata ufaulu. Ni vyema ukweli huu ukiriwe hadharani bila kificho chochote kama tunahitaji kuinua elimu yetu katika shule za serikali.

Kuliko kumwambia kuwa serikali inatoa ruzuku ya shule kujiendesha...waelezeni ukweli kuwa ruzuku hizo bado hazitoshi kwani zinatumika kwenye mambo mengine na sio ya taaluma. Ni muhimu serikali kuwaweka wazi kuwa haiwezi kuajili waalimu wa kutosha hivyo wazazi na waalimu wakubaliane kuchangia ili wapate waalimu ambao watalipwa na hizo pesa za ziada ambazo zitatokana na michango yao.

Haya yote nimeyafahamu baada ya kufanya uchunguzi wangu mdogo sana juu ya maswahibu yanayo zikuta shule hizi kwa ajili ya neno hili elimu bure. Waalimu wanashindwa kuwa na muunguniko mzuri na wazazi ili kuleta maendeleo ya shule. Wazazi mara zote wanakuwa na uhakika kuwa elimu inapaswa kutolewa bure bila malipo yoyote wakati mahitaji ya shule hizi ni makubwa kuliko ruzuku za serikali.

Kama jamii ambayo tunahitaji kuona maendeleo ya taifa letu ni muhimu kujumuika katika kuchangia mabadiliko hayo. Mahatma Gandhi aliwahi kusema "unapaswa kuwa sehemu ya mabadiliko ambayo unataka kuyaona ". Kwa hali hii ni kuwa ikiwa tunahitaji kuona ufaulu unaongezeka kwenye shule hizi ni vyema sasa tuwe tayari kuwa sehemu ya mabadiliko hayo na sehemu hiyo ni kutimiza wajibu wetu kama wazazi.

Wacha tuiweke kwa urahisi iko hivi ili matokeo mazuri yapatikane ni muhimu mzazi awe karibu na mwalimu awe karibu na mwanafunzi. Muunganiko huu ndio utatoa mabadiliko hayo kwani mwalimu atakuwa tayari kuyaeleza yote ambayo yatahitajika kwa mazazi na kisha mwalimu huyu atayapeleka mahitaji hayo kwa wanafunzi.

Hapo tutayaona maajabu mengi katika shule hizi lakini kama wazazi wataendelea kuwa na hasira kama za mbogo aliyejeruhiwa pale ambapo wanaambiwa kuchangia michango ili shule hizi zijiendeshe basi mabadiliko hayo hawatakuja kuyaona na matokeo yake tutatengeneza zero nyingi sana mtaani ambazo wakati mwingine ni kero kwa wazazi pia.

Bora kupata elimu iliyobora na kisha kukosa ajira lakini kutokuwa na elimu na kukosa ajira pia hili ni tatizo ambalo hatuwezi kulifungia macho. Serikali na wadau wake wakae chini kuona ni namna gani watafanya juu ya janga hili. Tunaipenda na tunaithamini elimu bure lakini kuwafanya wazazi na walezi wasiwe washirika kwenye maendeleo ya shule hizi kwa kigezo cha elimu bure ndilo jambo ambalo hatutaki litokee.

Fanyeni juhudi ili akili za wazazi na walezi zibadilike kutoka kwenye kutokuchangia chochote kuja mpaka kwenye kuchangia mambo yanayohusu taaluma na mazingira mazuri ya mtoto kuwa shuleni. Mfano wazazi na walezi wanapaswa kukaa chini na waalimu kuangalia ni walimu gani hawapo ili waweze kuchanga fedha na kuwaajili walimu hao na kuwapatia wanafunzi chakula wakati wa masomo ili kuwapunguzia mdororo unaotokana na njaa.

Haya yote yanatakiwa kufanywa na wazazi au walezi wakishirikiana na waalimu na sio wazazi kuelekeza majukumu haya kwa serikali kwani serikali yetu ina mambo mengi sana japo elimu ni muhimu lakini kwa hapo walipofikia na sisi tunapaswa kuendelea ili kuhakikisha wote tunakuwa sehemu ya mabadiliko haya ambayo tunataka kuyaona yakitokea. Asante

Imeandikwa na Joseph.D. Migini
 
Back
Top Bottom