SEHEMU YA 26
Alikuwa akimsifia Mapoto, alimfanya kujiona yeye alikuwa mtu muhimu, mwenye akili kuliko Watanzania wote, kumfanya kujiona kwamba hakukuwa na mtu mwingine aliyetakiwa kuwa balozi nchini Marekani zaidi yake.
Hilo likaulegeza moyo wa Mapoto na mwisho wa siku kukubaliana naye, hakujua kwamba kwa kufanya hivyo ndiyo ilikuwa njia moja ya kumpoteza kisiasa, hakuangalia mbele, kwake, kuwa balozi nchini Marekani ilionekana kuwa heshima kubwa.
“Una uhakika hili litakusaidia?” aliuliza mke wake.
“Ndiyo! Naamini kwamba litasaidia. Najua jinsi watu wanavyonipenda, haijalishi kama nitakuwa nchini Marekani au wapi, nitakachokifanya ni kuendeleza mapambano hukohuko na ninakuhakikishia mpaka mwaka 2003 nitakuwa na nguvu hiihii,” alisema Mapoto huku akiwa na uhakika kwa kile alichokuwa akikizungumza.
“Sawa.”
Baada ya siku mbili, Mapoto akatangazwa kama balozi nchini Marekani. Hilo likaibua maneno mengi, watu wakakasirika, wengine wakatukana kwani walijua kabisa kwamba Bokasa alitumia njia hiyo kama kumzima Mapoto kisiasa.
Watu wakamuona Mapoto kama msaliti kwani hawakutaka kuona akiwa balozi, kitendo cha kumpeleka Marekani kingemfanya kutokuonekana, kumdhoofisha kisiasa na hivyo kupotea kabisa.
Maneno mengi mitaani, lawama zote hazikuweza kubadilisha kitu chochote kile kwani baada ya wiki mbili, yeye na watoto wake wakaondoka kuelekea nchini Marekani. Mke wake, Rosemary hakwenda naye, aliendelea kukaa nchini Tanzania akiendelea na kazi yake ya ualimu katika Shule ya Wasichana ya Azania alipokuwa akifundisha.
“Nakutakia safari njema! Usisahau kuendelea kuwafundisha watoto wetu kuhusu kumjua Mungu,” alisema Rosemary wakati akiagana na mumewe katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere.
“Usijali katika hilo.”
“Nakupenda sana mume wangu!”
“Nakupenda pia,” alisema Mapoto, wakakumbatiana na kuagana huku muda wote Rosemary akilengwa na machozi. Alitamani kumzuia mume wake lakini alishindwa kabisa.
Je, nini kitaendelea?