SEHEMU YA 06
Mapigo ya moyo wa Winfrida yalikuwa yakidunda kwa nguvu, hakuamini kama siku hiyo ndiyo ilikuwa maalum kwake kuzungumza na Godwin, mpiga debe ambaye kila siku aliuendesha moyo wake puta.
Hapo kwa mama ntilie alipokuwa, Winfrida hakuzungumza kitu, mapigo yake ya moyo yalikuwa yakidunda kwa nguvu, alitetemeka huku akiwa na hofu, alimpenda mwanaume huyo na alikuwa mahali hapo kwa ajili ya kuzungumza naye lakini kitu cha ajabu kabisa, maneno yote aliyokuwa ameyapanga yalipotea na hivyo kubaki kama bubu.
“Dah! Wewe dada mzuri kinoma,” alisema mwanaume mmoja, hakutaka kunyamaza, uzuri wa Winfrida ulimchanganya kila mtu aliyekuwa mahali hapo.
Winfrida hakusema kitu, akaachia tabasamu tu na kumwangalia mwanaume huo aliyemsifia. Tabasamu lake lilimchanganya kila mtu aliyekuwa mahali hapo, si wanaume hao tu bali hata mama ntilie aliyekuwa akiwauzia chakula alichanganywa na uzuri wa Winfrida.
“Halafu msichana bomba kama huyu, anakuja kuchukuliwa na boya fulani hivi! Mapenzi yanakera sana, wewe unafikiri atachukuliwa na mshikaji fulani wa kishua, anachukuliwa na mtu asiyejielewa,” aliingilia mwanaume mwingine huku naye akimwangalia Winfrida.
Mpaka dakika hiyo Godwin hakuzungumza kitu, aliyatuliza macho yake usoni mwa msichana huyo. Aliudadisi uzuri wake, alikuwa msichana mwenye uzuri wa ajabu kiasi kwamba hakukumbuka kama aliwahi kumuona msichana wa namna hiyo maishani mwake.
Wenzake waliendelea kumsifia lakini macho yake hatakutoka usoni mwa Winfrida, msichana huyo kila alipokuwa akimwangalia Godwin, aligonganisha macho naye kitu kilichomfanya kuangalia chini huku aibu ya kikekike ikimuingia.
“Kuna siku nitampata msichana kama huyu,” alisema Godwin maneno yaliyomfanya Winfrida kushtuka.
“Hahah! Mzee wa Tandale umpate mtoto kama huyo! Utarogwa! Demu mkali kama huyu unafikiri ataweza kukanyaga Tandale, kwanza kwa ardhi gani? Labda mmuwekee kapeti la kukanyagia,” alisema jamaa mwingine kwa utani na wote kuanza kucheka.
Walizidi kuongea mambo mengi huku yote ikiwa ni kumsifia Winfrida kwa uzuri aliokuwa nao. Msichana huyo hakuzungumza kitu, alibaki kimya huku muda mwingi akiangalia chini.