Mkuu heshima kwako,
Nafikiri alilolisema Dr. Slaa ni kushuka kwa kiasi kikubwa kwa kiwango cha elimu inayotolewa hapo UDSM. Binafsi nilihitimu Chuoni hapo shahada ya kwanza miaka ya mwanzo ya 80, na nimekuwa nikifuatilia sana watu wanaohitimu miaka hii ya sasa. Kwa kiwango kikubwa sana ninashangazwa kila mara ninaposikia watu wanaojiita wahitimu wa UDSM wa miaka hii ya karibuni uwezo wao wa kuchanganua mambo na kufanya tathmini ya masuala mbalimbali. Huwa ninabaki kufikiri sasa kama hawa ndio wahitimu wa UDSM, hao wengine ambao hawakufika hatua hiyo kimasomo wakoje? Wakati tulipokuwa chuoni kuandika 'seminar paper' na kuwasilisha mada kwenye semina ilikuwa ni kitu cha lazima. Na sheria namba moja ilikuwa ni marufuku kusoma, hoja ulizoziandika kwenye karatasi unamkabidhi mwalimu/mhadhiri/mkufunzi halafu wewe unaiwasilisha mada yako bila karatasi na kujibu maswali kuitetea mada yako, unakubali kupewa upinzani na hoja mbadala 'constructive criticism' na unakwenda kuzifanyia kazi. Hakika kimataifa UDSM ilikuwa tishio. Ndipo waliposoma wakina Prof. Shivji, wakina Wadada Nabudere, walikuwepo wakina Walter Rodney, wakina prof. Chachage na wengine wengi, hakuna haja ya kuwataja wote. UDSM palikuwa kitovu cha taaluma, mahali ambapo hata serikali na chama wakati huo kilikuwa kimoja tu CCM, walijua ya kuwa kila changamoto inayotoka pale ilibidi waichukulie kwa makini kwa kuwa walikuwa wanaweza kuwekwa kitimoto na wataalamu na wasomi kutoka Chu Kikuu kuhusu sera mbalimbali zilizokuwa zinaonekana kuwa na mwelekeo usiokubalika kuhusu mustakabali wa maendeleo ya jamii yetu.
Niambie leo hii UDSM imekuwa mahali pa kuipigia kampeni serikali, siyo kitovu cha taaluma huru chenye kutoa changamoto kwa serikali na kujaribu kuipa mwongozo wa kitaaluma kuhusu mustakabali mzima wa maendeleo ya Tanzania. Unakuta mtu anayejisifia na kujiita 'msomi' wengine wanatamba mpaka na kujipa madaraja ya usomi huo, ukimwambia hebu nieleze jambo dogo tu hawezi. 'Msomi' wa UDSM leo hii ukimuuliza kwa nini nchi yetu ni maskini anasema hadharani 'hajui kwa nini nchi yetu ni maskini'. 'Msomi' ambaye hajui maana ya demokrasia hata anadiriki kusema 'ccm itatawala milele' na 'mkichagua upinzani mtakufa'. 'Msomi' ambaye akiambiwa wasilishe mada kwenye kikao anaanza kusoma kuanzia sentensi ya kwanza mpaka ya mwisho, na pengine hata hiyo mada anayoiwasilisha kaandikiwa yote, ukitaka kujua kama kaiandika mwenyewe mtupie swali rahisi tu kuhusu hilo analoliongea uone jinsi atakavyotoka jasho, ama atakavyokenua meno utadhani yuko kwenye mashindano ya urembo. Hiki ndicho kielelezo cha wasomi tulio nao hivi sasa.
UDSM kuwa chuo cha nne haibadilishi ukweli huu. Fahamu ya kwamba hata ukiwapa vichaa mtihani, kutakuwa na atakayeshika namba moja. Haina maana ya kuwa mtu huyo ana akili, ila katika kundi la hao vichaa angalau kwa huyo mmoja dawa zinaelekea kufanya kazi. Ila haina maana ya kuwa amepona!