Dowans sasa yalainika, wafuta deni kwa Tanesco
Na Richard Makore
25th February 2011
Sasa wataka walipwe tu Sh. bilioni 36
January Makamba
Kampuni ya Dowans Tanzania Limited ya kufua umeme wa dharura ambayo ilishinda kesi dhidi ya Tanesco katika Mahakama ya Usuluhishi wa Migogoro ya Kibiashara (ICC) na kupewa tuzo ya Sh. bilioni 94, sasa imelainika na imetangaza kusamehe deni hilo.
Uamuzi huu ambao unatangazwa baada ya kuwapo kwa malumbano makali nchini juu ya hukumu ya ICC na kiasi cha fedha kilichotolewa, sasa Dowans wanataka Tanesco ilipe tu Dola za Marekani milioni 24 (Sh. bilioni 36 tu). Fedha hizo ni gharama halisi ya umeme uliouzwa kwa Tanesco.
Uamuzi wa Dowans ulitangazwa na Stanley Munai ambaye ni Mkurugenzi wake wa Fedha, akiwa pia mwakilishi wa kampuni hiyo nchini.
Mbele ya waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Munai alisema kuwa wamechukua hatua ya kufuta deni hilo kutokana na kusikia kilio cha Watanzania.
Hata hivyo Dowans imesema licha ya kutoa msamaha huo, Tanesco bado imeshindwa kujibu kama imeukubali msamaha huo au la ili mazungumzo yaanze.
Munai alidai fedha wanazolidai shirika hilo kwa sasa zinakaribia Sh. bilioni 99 badala ya Sh. bilioni 94 za mwaka jana.
Alisema ongezeko hilo limetokana na kampuni ya Dowans kuitoza Tanesco kila siku Dola za Marekani 11, 800 (Sh. milioni 15.3) kama gharama za kuweka mtambo hata kama hauzalishi umeme na kwamba nyongeza ya gharama hizo ilianza kutozwa kila siku tangu Juni 15, mwaka 2010 hadi sasa.
Alisema deni la Sh. bilioni 94 liliishia Juni 14, mwaka 2010 na baada ya hapo limekuwa likiongezeka siku hadi siku. Munai aliwaambia waandishi wa habari walioambatana na kamati ya kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuwa kampuni yake haina tatizo kuhusu kusamehe deni hilo, lakini Tanesco muda wote imekuwa haitaki kukubali msamaha huo.
Aliongeza kuwa ikiwa Tanesco na Serikali watakataa kupokea msamaha huo nje ya mahakama na wao wataacha sheria iendelee kuchukua mkondo wake.
Munai alisema mkataba kati ya Dowans na Tanesco unasema kuwa ikiwa pande hizo mbili zitatofautiana na zikaenda kwa msuluhishi maamuzi yatakayotolewa yatatakiwa kuheshimiwa na pande zote na hakuna upande utakaoruhusiwa kukata rufaa.
"Kwa mujibu wa mkataba huu, Tanesco haiwezi kukata rufaa kwa kuwa kipengele hicho kinawazuia na wao wanajua, lakini hajui ni kwanini hawataki kuwaambia wananchi ukweli," alisema.
Alifafanua kuwa endapo serikali na Tanesco wataendelea na msimamo wa kugoma kupokea msamaha huo wataendelea na utaratibu wa kimahakama ili wapate kibali cha kukamata mali za Tanesco za ndani na nje ili ziuzwe ili kufidia fedha za Dowans.
"Tumewandikia barua Tanesco kwamba tukae meza moja kwa maelekezo ya mmiliki wa Dowans ili tuwasamehe deni, lakini hawataki kujibu, sasa tuwafanyeje?" alihoji Munai.
Alisema Dowans inaidai Tanesco Dola milioni 24 (Sh. Bilioni 31.2) kutokana na kuwauzia umeme kabla ya kuvunjwa kwa mkataba.
Alifafanua kuwa deni la umeme lazima lilipwe kwa kuwa waliwauzia Tanesco nishati hiyo na wakawauzia wateja wao hivyo wana uhakika fedha hizo walizichukua na wanazo.
Mtambo huo wa Dowans jana ulikuwa umezimwa lakini, Munai alibainisha kwamba muda wowote wakitakiwa kuwasha watafanya hivyo.
Alisema mtambo huo una uwezo kuzalisha megawati 120 na kwamba endapo watauwasha una uwezo wa kuanza kuzalisha umeme baada ya dakika 12 tangu kuwashwa.
Wakati huo huo, kampuni ya Dowans imekiri kudaiwa na benki ya Baclays Tanzania Dola za Marekani milioni mbili na kusema kuwa wanaendelea kulipa kama ilivyo kwa wateja wengine wanaokopa katika taasisi za fedha.
Jumapili iliyopita mmiliki wa Dowans, Brigedia Jenerali Mstaafu Suleiman Yahya Al Adawi, alikutana na wahariri wa vyombo vya habari na kueleza kuwa alikuwa radhi kukukana na Tanesco kwa mazungumzo. Alisema walikuwa tayari kusamehe sehemu ya deni hili kwa masharti wakubaliwe kuendelea kuzalisha umeme.
Wakati huo huo, Kamati ya Nishati na Madini jana ilitembelea mitambo ya gesi ya Tanesco iliyopo Ubungo, mitambo ya Dowans na ya Songas ambayo pia inatumia gesi.
Akizungumza wakati wa kutembelea mitambo hiyo, Mwenyekiti wa kamati hiyo, January Makamba, alihoji ni kwa nini mitambo hiyo ya Dowans isihamishwe eneo la Tanesco kwa kuwa haifanyi kazi.
"
Sasa hii mitambo inafanya nini hapa wakati haifanyi kazi na mmeizima au mna malengo gani nayo," January alimhoji Munai.
Akijibu swali la January, Munai alisema awali walitaka kuondoa mitambo yao lakini Tanesco wakawazuia.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, William Mhando, akizungumzia maamuzi ya Dowans, hakutaka kutoa ufafanuzi badala yake alisema kinachosababisha matatizo yote hayo ni kauli za kisiasa na wanasiasa.
Naye January alipoulizwa kuhusiana na maamuzi ya Dowans, alijibu kwa kifupi kuwa suala hilo ni la Tanesco.
Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, hakupatikana kuzungumzia msamaha wa Dowans kutokana na simu zake za kiganjani kuzimwa.
CHANZO: NIPASHE