Nafikiri umefika wakati wa serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini kupitia kwa Waziri Ngeleja na pia TANESCO kuuelezea umma wa Tanzania ni nini kinachoendelea katika ya ALI HADAIWI (Brigedia AL ADAWI) na TANESCO.
Maana RADIO MARIA, GAZETI LA NIPASHE na hapa chini gazeti la TANZANIA DAIMA vinatoa maelezo ambayo yanazidisha shauku ya Wa-Tanzania ni nini kinachoendelea baina ya DOWANS na TANESCO:
TANZANIA DAIMA JUMAMOSI 26/02/2011:
Makamba atoboa siri ya mgawo• Dowans yawekewa ngumu TANESCO, LHRC
na Betty Kangonga na Bakari Kimwanga
Wakati huo huo, siku moja baada ya kampuni ya Dowans Tanzania Limited, kutangaza kuwa iko tayari kusamehe deni la sh bilioni 94 kadhalika kukiwa na msukumo wa kulitaka Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) kuingia mkataba nao ili kupunguza makali ya mgawo wa umeme, hatua hiyo imeonekana kutiliwa shaka.
Hivyo TANESCO imesema inahitaji kutafakari juu ya hatua hiyo ya Dowans kuwafutia deni kwani jambo hilo ni la kisheria na si la makubaliano ya kawaida.
Uamuzi wa Dowans kuifutia deni TANESCO, ulitangazwa juzi na Mkurugenzi wa Fedha wa Kampuni hiyo, Stanley Munai, ambaye alisema kuwa hatua hiyo imefikiwa baada ya kusikia kilio cha Watanzania, lakini TANESCO imeshindwa kuitikia wito huo wa kusamehewa.
Akizungumza na Tanzania Daima, kuhusu kauli hiyo ya Dowans, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Wiliam Mhando, alisema ni muhimu kwa sasa kuzingatia masuala ya kisheria kuliko kukurupuka na kuonekana wao ndio waliovunja sheria na kusababisha kuibuka kwa mjadala mpya.
"Hili suala linazungumzika lakini kinachosababisha haya ni kauli za kisiasa, jambo la kisheria huenda kisheria ni muhimu kwanza tukae na timu yetu ya wataalamu kuliko kukubali na kukurupuka, ni mchakato kufikia makubaliano nao na tunahitaji ufafanuzi wa kina," alisema Mhando.
Juzi, Munai alisema kuwa licha ya kutoa msamaha huo, TANESCO bado walishindwa kujibu kama imeukubali au la ili mazungumzo yaanze.
Akifafanua zaidi kuhusu ombi la Dowans kutaka kukutana na TANESCO, Mhando aliwataka Watanzania kuvuta subira ili kuona juhudi zinazofanywa na TANESCO katika kukabiliana na hali ya mgao wa umeme nchini na hata kuondokana nao kabisa.
Dowans ilishinda kesi dhidi ya TANESCO katika Mahakama ya Usuluhishi wa Migogoro ya Kibiashara (ICC), na hivyo kuamriwa ilipwe shilingi bilioni 94, uamuzi ambao ulizusha malumbano makubwa nchini na kusababisha Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu Nchini (LHRC)
kuwasilisha pingamizi Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, kupinga usajili wa tuzo iliyotolewa na Mahakama ya ICC.
Hata hivyo, uamuzi wa Dowans kutaka kuifutia deni TANESCO haujaweza kubadilisha mawazo ya LHRC ambao wameapa kuendelea na msimamo wao mahakamani.
Tanzania Daima iliwasiliana na mkurugenzi mkuu wa kituo cha sheria na haki za binaadamu nchini (LHRC), Francis Kiwanga, kuhusu uamuzi wa kuendelea na kesi hiyo au la, alisema ni vizuri mahakama ikaheshimiwa kwani ndicho chombo muhimu katika kusimamia na kutafsiri sheria.
"Kimsingi hebu tuheshimu mahakama suala la kufuta kesi au vinginevyo mahakama ndiyo yenye uwezo wa kuamua lakini sisi bado tutaendelea na kesi yetu ya msingi," alisema Kiwanga.
Januari mwaka huu kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kwa kushirikiana na wanaharakati wa haki za kijinsia nchini waliwasilisha pingamizi Mahakama Kuu kupinga serikali kuilipa kampuni ya Dowans sh bil. 94.
Mahakama hiyo ya kimataifa ilikuwa imesikiliza malalamiko ya Dowans dhidi ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na kuamua iilipe fidia kampuni hiyo baada ya kubaini kuwa ilivunja mkataba kinyume cha taratibu.
Hata hivyo Februari 22, mwaka huu, Mahakama Kuu ya Tanzania ilipokea na kusajili kesi nyingine ya kikatiba kupinga malipo ya kampuni ya umeme ya Dowans.
Kesi hiyo ya kikatiba ilifunguliwa mahakamani hapo na Watanzania saba wakiwemo wabunge watatu na kupewa namba tano ya mwaka 2011 chini ya Kampuni ya Mawakili ya Mpoki na Lukwaro.
Msingi wa kesi hiyo ni kwamba malipo ya Dowans ni kinyume cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 sehemu ya tatu kifungu cha 27 Ibara ya kwanza na ya pili. Hivyo katika kesi hiyo Watanzania hao wanaiomba Mahakama Kuu kutengua uamuzi wa malipo hayo kwa kuwa yanakwenda kinyume na katiba ya nchi.
Hali kadhalika, deni ambalo Dowans wanaidai TANESCO hivi sasa limeongezeka na kufikia sh bilioni 99 badala ya sh bilioni 94 za mwaka jana.
Kwa mujibu wa maelezo ya Dowans wenyewe, ongozeko hilo linatokana na kampuni ya Dowans kuitoza TANESCO kila siku Dola za Marekani 11,800 (ambazo ni sawa na sh milioni 15.3) kama gharama za uzalishaji umeme ambapo nyongeza hiyo ilianza kutozwa kila siku tangu Januari 15, mwaka 2010 hadi sasa.
Source:
Makamba atoboa siri ya mgawo