Dodoma: Askari Polisi aliyemnywesha sumu mtoto wa dada yake, apandishwa Kizimbani

figganigga

JF-Expert Member
Oct 17, 2010
25,492
54,895
Mjomba wa Mtoto Aliyenyweshwa Sumu, Kizimbani. Ashitakiwa Kwa Jaribio la Kuua, RCO Aomba Asidhaminiwe.

Christopher Charles (23) ambaye alikuwa askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) cha Mkoa wa Dodoma, jana Oktoba 24, 2019 amefikishwa mbele ya Hakimu wa Mahakama ya Mkoa huo, Lucas Jang’andu akishitakiwa kwa kosa la kujaribu kuua.

Kesi hiyo namba 21 ya Mwaka 2019, imeitwa Mahakamani ili kupokea kiapo kinzani cha Charles, kufuatia maombi ya Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa Mkoa huo (RCO), yanayotaka asidhaminiwe.

Mazungumzo ndani ya mahakama yalikuwa kama ifuatavyo;

Mh. Jang’andu: Mshtakiwa umeleta majibu ya hoja hizi?

Charles: Mheshimiwa sikuona sababu ya kufanya hivyo, ikiwa mahakama yako ina mtu wa kuweza kuzuia dhamana ambayo ni haki yangu ya kikatiba.

Mh. Jang’andu: Nani amezuia dhamana yako?

Charles: Nilivyosoma na maelezo niliyopewa inaonesha ni RCO.

Mh. Jang’andu: Hajazuia bali ameiomba mahakama kuona umuhimu wa kutokupa dhamana.

Ndiyo kiapo kilicho mbele yangu na hivyo unatakiwa kuleta majibu ya hoja zake, ili mahakama ifanye uamuzi kwa kuzingatia hoja za pande zote mbili. Huo ndiyo utaratibu.

Charles: Lakini mheshimiwa hakimu, mahakama nayo si ina maamzi yake?

Mh. Jang’andu: Ndiyo maana unatakiwa kujibu hoja za zuio hili, ili mahakama izipitie na kufanya uamuzi ikiwa imesikiliza pande zote mbili.

Charles: Mheshimiwa kwani huyu RCO anahusikaje na mashtaka yangu?

Mh. Jang’andu: Anahusika kwa mujibu wa sheria maana ndiye anahusika na matukio yote ya jinai yanayotokea ndani ya mkoa.

Ametumia kifungu kinachoeleza kuwa lengo la ombi hilo ni kwa manufaa ya usalama wako.

Hatahivyo, una hiyari ya kuleta pingamizi au kutoleta na kuiruhusu mahakama iendelee na hatua ya kutoa uamuzi kwa kuzingatia hoja zilizowasilishwa mahakamani.

Charles: Mahakama iendelee tu kutoa uamuzi maana hata kama nitaleta kiapo kinzani changu, sidhani kwamba kitachukuliwa kwa uzito kama kinavyochukuliwa hicho.

Mheshimiwa Hakimu Jang’andu ameahirisha kesi hiyo mpaka itakapotajwa tena mahakamani, Novemba 7 Mwaka huu, kwa ajili ya kusikiliza pingamizi lililopelekwa na RCO. Mshtakiwa amerudishwa rumande.

Na Editha Majura,
Dodoma.

Zaidi soma;
 
Back
Top Bottom