HIMARS
JF-Expert Member
- Jan 23, 2012
- 69,373
- 94,566
Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba leo Bungeni Dododma amewasilisha Bungeni taarifa ya Hali ya Uchumi wa Kitaifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa wa Mwaka 2023/2024 ambapo moja ya mambo aliyoyasema ni kwamba hadi kufikia mwezi Aprili 2023, deni la Serikali lilikuwa shilingi bilioni 79,100.19 sawa na ongezeko la 13.9% ikilinganishwa na Shilingi bilioni 69,440.01 kwa kipindi kama hicho mwaka 2022.
“Kati ya kiasi hicho, deni la nje ni shilingi bilioni 51,162.60 na deni la ndani ni Shilingi bilioni 27,937.59, ongezeko la deni limetokana na kupokewa kwa fedha za mikopo kwa ajili ya kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya barabara, reli, viwanja vya ndege, umeme, elimu na afya, aidha tathmini ya uhimilivu wa deni la Serikali iliyofanyika Desemba, 2022 imeonesha kuwa deni ni himilivu na viashiria vya deni viko ndani ya wigo unaokubalika kimataifa katika kipindi cha muda mfupi, wa kati na mrefu”
“Machi 2023, kampuni za Fitch Ratings na Moody’s Investors Service zilianza zoezi la kuifanyia Nchi tathmini ya kukopesheka katika masoko ya fedha ya kimataifa, zoezi hilo lilikamilika ambapo kampuni ya Moody’s Investors Service ilichapisha matokeo ya tathmini hiyo Mei 2023 na kampuni ya Fitch Ratings mwezi Juni 2023, kwa mujibu wa matokeo hayo, Tanzania imewekwa katika daraja la B2 POSITIVE na Kampuni ya Moody’s Investors Service na daraja la B POSITIVE na Kampuni ya Fitch Ratings ambayo yanaashiria taswira chanya kwa Nchi kimataifa”
“Pamoja na mambo mengine, matokeo hayo yamechangiwa na mwenendo mzuri wa ukuaji wa uchumi, usimamizi makini wa deni la Taifa, kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji kwa sekta binafsi, kuimarisha ushirikiano wa kimataifa pamoja na kuleta maridhiano ya kisiasa ndani ya Nchi, kukamilika kwa zoezi hilo, kutaiwezesha Nchi kutambulika katika masoko ya fedha ya kimataifa na hivyo, kuongeza wigo wa upatikanaji wa mikopo kwa Serikali na sekta binafsi”