Kama Jumuia hii ingeendeshwa kwa kufuata madhumuni yake ya awali na pia Katiba yake na kama wanachama wangeifanya Jumuia hii ni yao badala ya kuwabwagia viongozi wake, sina shaka yoyote Jumuia hii ingekuwa ya manufaa kwa wanachama wenyewe na hali kadhalika kwa Watanzania wengine kule nyumbani.
Lakini, wapi! Kama kawaida yetu, wanaoongoza hawajui wanakuongozea wala wanachokiongoza na wanaoongozwa, hawajui wanakotaka kuongozwa. Ili muradi, "bora liende." Jumuia hii, ilianzishwa, kama nakumbuka sawasawa mwaka 1990. Na mpaka leo hii,haina chochote kinachoweza kuorodheshwa, kama mafanikio yake ni majungu juu ya mafiga.
Kinachogombewa ni kutafuna vijisenti kidogo na ile sifa ya kujiita kwa cheo utakachopewa baada ya uchaguzi. Kingine, ni kule kujikomba komba na kimbele mbele, wanapokuja wakubwa kutoka nyumbani.
Hawa viongozi waliopo sio tu wamemaliza muda wao wa uongozi bali wameupitiliza. Bila ya kushinikizwa, hata huo uchaguzi wenyewe usingezungumzwa, sembuse ya kufanyika.
Cha ajabu ni kuwa hawa viongozi waliopo, ndio waliokuwa mstari wa mbele, katika kuwalaumu viongozi waliokuwa kabla yao kwa makosa hayo hayo ambao nao sasa wanaonekana kuyafanya.
Makundi ni lazima katika uchaguzi wowote. Kila mgombea mtarajiwa, anawajibika kuunda na kuwa na kundi lake la kupanga na kutekeleza mikakati yake ya kutafutia ushindi.
Nawatakia wote pamoja na Jumuia yenyewe mafanikio katika kutuletea mabadiliko yenye matumaini.