Dar Es Salaam Jiji, linalokua haraka kuliko Mipango yake

Dar Es Salaam Jiji, linalokua haraka kuliko Mipango yake

Nicolas J Clinton Gabone

JF-Expert Member
Joined
Mar 13, 2014
Posts
897
Reaction score
559
DAR ES SALAAM, JIJI LINALOKUA HARAKA KULIKO MIPANGO YAKE

Nianze kwa RAI kuhusu upanuzi wa Barabara za Sam Nujoma na New Bagamoyo kwa kutumia njia zile zile za awali. Kwa maoni yangu, huenda tumeelekeza nguvu yetu katika suluhisho la muda mfupi sana badala ya muda mrefu. Kinachonisikitisha ni kwamba, ndani ya kipindi cha miaka mitano ijayo, barabara hizi pamoja na Nyerere Road zinaweza kuwa zimeelemewa tena na ongezeko la magari na shughuli za uchumi, hali ambayo itatulazimu kurudia upanuzi kwa gharama kubwa zaidi. Ni maoni yangu Dar Es Salaam ipangwe kwa maono ya miaka 30 hadi 50 na kuendelea ijayo, badala ya kujenga kwa mahitaji ya leo pekee. Tukikosea sasa, tutalipa gharama kubwa zaidi baadaye.

Sasa tuendelee na hoja yangu. Nimepata fursa ya kutembelea maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam kupitia barabara za Mandela, Kilwa, Nyerere, Ali Hassan Mwinyi, Sam Nujoma, New Bagamoyo, pamoja na barabara za ndani za Charambe, Buza na Mwai Kibaki. Nilichokiona hakikuwa tu msongamano wa magari. Niliona changamoto kubwa zaidi ya hapo. Niliona jiji linalokua kwa kasi kubwa kuliko mipango yake.
Karibu barabara zote muhimu za jiji zimegeuka kuwa maeneo ya foleni kubwa kwa sehemu kubwa ya siku. Safari ambayo inaitaji dakika 10, 20 au 30 sasa inaweza kuchukua saa tatu hadi nne.

Huu siyo usumbufu wa kawaida tena. Ni upotevu wa muda, nishati, nguvu kazi, tija ya uchumi na ubora wa maisha ya wananchi. Lakini swali muhimu zaidi kwa nini, licha ya uwekezaji mkubwa wa serikali katika ujenzi wa barabara, Dar es Salaam bado inaendelea kuzama kwenye foleni na ukuaji holela? Jibu langu liko wazi. Jiji linakua kwa kasi kubwa zaidi kuliko mipango ya serikali. Kwa mujibu wa taarifa za hivi karibuni kutoka ofisi ya Taifa ya takwimu, Tanzania ina zaidi ya watu milioni 70, huku Dar es Salaam ikiwa na zaidi ya wakazi milioni 8 na idadi hiyo ikiendelea kuongezeka kwa kasi kila mwaka. Hata hivyo, sehemu kubwa ya mipango ya maendeleo ya jiji bado inaonekana kujielekeza katika fikra za miongo kadhaa iliyopita. Tunapanua barabara, lakini hatupanui uwezo wa jiji.

Tunajenga miundombinu, lakini hatujengi mfumo wa maisha wa jiji la kisasa.
Tunatatua matatizo ya leo kwa kutumia mipango ya jana. Matokeo yake ni kuendelea kushuhudia makazi yasiyopangwa vizuri, miundombinu inayochoka mapema, usafiri usiyo na ufanisi, gharama kubwa za maisha na kupungua kwa ushindani wa uchumi wa jiji.

BANDARI KAVU KATIKATI YA JIJI, SULUHISHO AU CHANZO CHA TATIZO?

Kwa muda mrefu sasa wananchi wamekuwa wakilalamika na kueleza athari za malori makubwa ya mizigo katika miundombinu ya Dar es Salaam. Lakini bado tunaendelea kushuhudia kuongezeka kwa shughuli za bandari kavu katika maeneo mbalimbali ya jiji na pembezoni mwake.
Swali ambalo mamlaka zinapaswa kulijibu, ikiwa Bandari Kavu ya Kwala imejengwa mahsusi kupokea na kuhudumia mizigo kwa kiwango kikubwa, kwa nini shughuli nyingi za mizigo bado zinaendelea kusongamana katika maeneo ya mjini?

Kwa nini malori makubwa yanaendelea kutumia kwa kiwango kikubwa barabara za Mandela, Temeke, Kilwa, Charambe, Buza, Chanika na maeneo mengine ambayo awali hayakujengwa kubeba mzigo mkubwa wa magari ya mizigo kila siku?
Je, barabara hizi zilijengwa kwa matumizi hayo?
Na kama hazikujengwa kwa matumizi hayo, nani anapaswa kuwajibika kwa uharibifu wa haraka wa miundombinu inayojengwa kwa fedha za walipa kodi?

TATIZO KUBWA NI MIPANGO, SIYO BARABARA PEKEE

Changamoto kubwa ya Dar Es Salaam leo siyo ukosefu wa barabara tu.
Changamoto kubwa ni ukosefu wa maono ya muda mrefu yanayolingana na kasi ya ukuaji wa jiji.
Mataifa yaliyojenga miji yenye ushindani mkubwa duniani hayakuwekeza tu katika barabara kuu.
Yaliwekeza katika reli za kisasa za abiria na mizigo, mifumo madhubuti ya usafiri wa umma, miji ya satelaiti, teknolojia za usimamizi wa trafiki, barabara za pete zinazozunguka jiji, na mipango madhubuti ya matumizi ya ardhi. Barabara za pete hapa Dar es Salaam zimeanza kuzungumzwa nikiwa darasa la tatu leo nimemaliza chuo bado hili halijatekelezwa leo wala kesho. Dar es Salaam haiwezi kuendelea kuwa kitovu kikuu cha biashara, viwanda, huduma na makazi huku shughuli zote zikikusanywa katika maeneo yale yale kila mwaka.

DAR ES SALAAM HAIWEZI KUPANGWA PEKEE YAKE

Kwa maoni yangu, ni wakati sasa wa kuanza kuangalia au kufikiria Dar es Salaam kama ukanda mkubwa wa maendeleo badala ya jiji linaloishia katika mipaka yake ya sasa. Ongezekeo la watu, na ukuaji wa biashara, viwanda na makazi tayari umevuka mipaka ya jiji na kuathiri moja kwa moja Bagamoyo, Chalinze, Kibaha, Kisarawe na Mkuranga. Kwa sababu hiyo, kuna haja ya kuanza kufikiria muundo mpana wa maendeleo ya Dar es Salaam Metropolitan Area unaounganisha maeneo haya katika mpango mmoja wa maendeleo, usafiri, makazi na uwekezaji. Lengo si kubadilisha mipaka kwa sababu za kisiasa, bali kuunda mfumo mmoja wa upangaji unaotambua ukweli kwamba maeneo haya tayari yanategemeana kiuchumi na kijamii.

CHUO CHA ARDHI NA DIT VIWE INJINI YA MABADILIKO

Tanzania imebarikiwa kuwa na taasisi bora za elimu ya juu kama Chuo Kikuu cha Ardhi na DIT. Badala ya kuviacha vikibaki kama vituo vya kufundishia pekee, ni wakati wa kuvitumia kama injini ya upangaji wa miji ya karne hii. Serikali inaweza kuanzisha programu maalumu itakayoshirikisha wanafunzi, wahadhiri na wataalamu wa taasisi hizi katika upimaji wa maeneo mapya ya makazi. Uandaaji wa ramani za matumizi ya Ardhi. Upangaji wa maeneo ya biashara na viwanda. Uundaji wa mifumo ya Smart Cities. Ujenzi wa mifumo ya kidijitali ya usimamizi wa Ardhi. Upangaji wa miundombinu ya usafiri na huduma za jamii. Hatua hii itasaidia kujenga uwezo wa ndani wa kitaalamu huku ikipunguza gharama za upangaji wa miji.

TUKOMESHE UJENZI NA UUZAJI WA ARDHI BILA MPANGO

Moja ya makosa makubwa ambayo yamegharimu Dar Es Salaam kwa miongo mingi ni kuruhusu makazi kutangulia miundombinu.

Barabara zinajengwa baada ya nyumba. Mifereji inajengwa baada ya mafuriko.
Huduma zinapelekwa baada ya watu kuhamia.
Huu siyo mfumo sahihi wa kujenga jiji la kisasa.

Kila eneo jipya linalofunguliwa kwa maendeleo linapaswa kupimwa, kupangwa na kuwekewa miundombinu kabla ya makazi kuanza.
Hatupaswi kuendelea kuruhusu viwanja kuuzwa na kujengwa kiholela kisha serikali kutumia mabilioni ya fedha kurekebisha makosa ambayo yangezuilika tangu mwanzo.

DAR ES SALAAM YA MIAKA 30 HADI 50 IJAYO IANZE KUPANGWA LEO

Mji wa watu milioni 8 wa leo unaweza kuwa mji wa watu milioni 20 au zaidi katika miongo michache ijayo. Hivyo, miundombinu inayojengwa leo lazima izingatie mahitaji ya miaka 30 hadi 50 ijayo. Hii inahitaji Reli za kisasa zinazounganisha Dar es Salaam, Bagamoyo, Chalinze, Kibaha, Kisarawe na Mkuranga. Barabara za viwango vya juu zinazounganisha ukanda wote wa maendeleo. Miji mipya ya makazi, biashara na viwanda. Bandari kavu na vituo vya mizigo vilivyopangwa nje ya maeneo yenye makazi.Teknolojia za Smart City na usimamizi wa trafiki kwa wakati halisi. Mipango madhubuti ya mazingira na matumizi sahihi ya Ardhi.

Maeneo yote ya Dar es Salaam yaliyokua kiholela au kupangwa kwa viwango visivyokidhi mahitaji ya jiji la kisasa yanapaswa kuingizwa katika mpango maalumu wa maboresho ya miji, kwa kuzingatia mpango wa miaka 20 unaonekana katika eneo la Sinza. Aidha, maeneo kama Posta, Kariakoo, Masaki, Orstabey, Mikocheni, Upanga, Ilala CBD na Kinondoni CBD.
Wakati jiji linaendelea kuboresha barabara, majengo na huduma nyingine za msingi, bado tunakabiliwa na changamoto kubwa ya miundombinu ya nyaya za umeme, simu na intaneti ambazo zimetapakaa juu ya nguzo na kuathiri mwonekano wa jiji. Ni wakati sasa wa kuweka mkakati wa muda mrefu wa kuhamishia miundombinu hii chini ya Ardhi, kuanzia maeneo ya biashara, huduma na yenye msongamano mkubwa. Jiji la kisasa halijengwi kwa barabara nzuri pekee, bali pia kwa miundombinu iliyo salama, nadhifu, yenye ubora na inayotazama mahitaji ya vizazi vijavyo.

KWA NINI BAGAMOYO, KIBAHA, CHALINZE, KISARAWE NA MKURANGA ZINAPASWA KUWA SEHEMU YA MPANGO MMOJA WA DAR ES SALAAM?

Kuna watu wanaweza kujiuliza kwa nini napendekeza Dar es Salaam iyanyakue au iangalie kwa karibu zaidi maeneo ya Bagamoyo, Kibaha, Chalinze, Kisarawe na Mkuranga. Jibu ni rahisi tu. Kwa sababu ukuaji wa Dar Es Salaam tayari umefika katika maeneo hayo na yanakua kwa kasi, lakini ongezeko hili la ukuaji ni holela kiasi kwamba tutatumia mabilioni ya fedha kurekebisha makosa ya leo. Kila siku maelfu ya watu wanaishi Kibaha lakini wanafanya kazi Dar es Salaam. Wengine wanaishi Mkuranga lakini biashara zao zipo Dar es Salaam. Wengine wanaishi Bagamoyo lakini wanategemea huduma, masoko, bandari, viwanda na uchumi wa Dar es Salaam. Kwa maneno mengine, mipaka ya utawala ipo tu bado kwenye ramani, lakini mipaka ya uchumi na jamii tayari imefutika. Ndiyo maana haiwezekani tena kupanga Dar es Salaam bila kupanga Bagamoyo. Haiwezekani kupanga Kibaha bila kupanga Dar es Salaam.
Haiwezekani kupanga Mkuranga bila kupanga mtandao mzima wa maendeleo unaolizunguka maeneo hayo. Inawezekana ni kuamua tu, kuacha siasa dhida ya maendeleo ya watu na kutekeleza mpango huu kwa ajili ya maendeleo ya Jiji la Dar Es Salaam na uchumi wetu.

Tatizo kubwa ninaloliona leo ni kwamba kila Halmashauri ya mji au manispaa hizo zinapanga maendeleo yake kivyake wakati ukweli ni kwamba maeneo haya yote yanategemeana. Matokeo yake ni kuongezeka kwa makazi holela, msongamano wa magari, matumizi yasiyo sahihi ya Ardhi, huduma duni za usafiri na gharama kubwa za kurekebisha makosa ya upangaji baadaye.

DAR ES SALAAM YA KESHO HAITATOSHEA NDANI YA MIPAKA YA LEO

Niwashawishi kukubaliana na maoni yangu kuwa Dar Es Salaam ya miaka 10 ijayo haitakuwa ndani ya mipaka ya sasa. Jiji litaendelea kusambaa kuelekea Kibaha. Litaendelea kuelekea Bagamoyo. Na Bagamoyo tayari ipo kwenye mpango wa uendelezaji. Jiji litaendelea kukua kuelekea Kisarawe. Litaendelea kuelekea Mkuranga.
Litaendelea kuelekea Chalinze. Swali si kama jambo hili litatokea. Swali ni kama tunajiandaa kwa mabadiliko hayo au tunayasubiri yatokee ndipo tuanze kuyakimbilia. Mataifa yaliyofanikiwa kupanga miji mikubwa duniani yalifanya jambo moja muhimu sana.
Yalipanga maeneo ya ukuaji kabla hayajajaa watu.
Yalijenga miundombinu kabla ya msongamano.
Yalitenga maeneo ya viwanda kabla ya makazi.
Yalitengea maeneo ya biashara kabla ya foleni.
Sisi hatuna sababu ya kusubiri matatizo yatokee kwanza.

FAIDA ZA KUUNGANISHA UKANDA HUU KATIKA MPANGO MMOJA WA MAENDELEO

Kama maeneo ya Bagamoyo, Chalinze, Kibaha, Kisarawe na Mkuranga yatawekwa katika muundo mmoja wa upangaji wa maendeleo ya Dar es Salaam, Tanzania itapata manufaa makubwa.
Kwanza, tutapata Ardhi ya kutosha kwa ajili ya makazi mapya yaliyopangwa kisasa. Yenye miundombinu ya usafiri na usafirishaji, biashara na huduma kwa wananchi.

Pili, tutapata maeneo mapya ya viwanda bila kulazimisha viwanda kuingia katikati ya makazi ya watu. Hili tayari linaendelea Ukanda wote wa Bagamoyo, Mkuranga na Kibaha.

Tatu, tutapata nafasi ya kujenga reli za kisasa, barabara za kisasa na mifumo ya usafiri wa umma kabla ya maeneo hayo kujengwa kiholela. Lazima tuyaunganishe maeneo haya kwa Barabara za pete, Reli na Barabara za ndani.

Nne, tutapunguza gharama za maisha kwa kupunguza shinikizo la Ardhi ndani ya Dar es Salaam. Makazi hapa Dar Es Salaam yaendelee kuboreshwa kwa mpango maalumu, mazingira ya jiji yaendelee kutunzwa na kuhakikisha usafiri wa bodaboda na bajaji unatambuliwa na kuwekewa utaratibu wa kusafirisha watu.

Tano, tutaunda kitovu kikubwa zaidi cha biashara, viwanda, huduma na uwekezaji katika Afrika Mashariki, kati na kusini mwa Afrika kutokana na jiografia ya Dar Es Salaam kupakana na Bahari ya Hindi ambayo ni kitovu cha biashara ya kikanda na kimataifa. Dar Es Salaam kiwe kituo au Jiji la kukimbilia kutoka kusini, mashariki na kati mwa Afrika kwa ajili ya mapumziko na utalii.

Mara nyingi tunazungumza kuhusu Dar es Salaam ya leo. Lakini watunga sera au taasisi za mipango kama TUME YA MIPANGO na mamlaka zingine hawakujenga kwa ajili ya watu wa leo pekee. Walijenga kwa ajili ya watu ambao hata hawajazaliwa. Miundombinu tunayojenga leo inapaswa kuangalia Tanzania ya mwaka 2050 au hata 2100. Tujifunze kwa wengine kama China, Malaysia, Dubai na Qatar mipango katika miji yao ya miaka 40 iliyopita matokeo yake tunayashuhudia leo na miaka kadhaa mbele. Dar Es Salaam ina nafasi kubwa kuwa moja ya majiji ya kisasa yanayopatikana katika ukanda wa Bahari ya Hindi, uwezo huo tunao leo, kesho. Ndiyo maana mjadala wa kuunganisha Bagamoyo, Kibaha, Chalinze, Kisarawe na Mkuranga katika muundo mmoja wa maendeleo ya Dar Es Salaam si suala la mipaka ya kisiasa.
Ni suala la maono.
Ni suala la uchumi.
Ni suala la mipango.
Ni suala la kuhakikisha kuwa kizazi kijacho hakirithi foleni, makazi holela na miundombinu iliyozidiwa uwezo, bali kinarithi Jiji lililopangwa kwa akili, maarifa na maono ya muda mrefu.

Dar es Salaam haitakuwa kubwa kwa sababu ya majengo marefu. Itakuwa kubwa kwa sababu ya uwezo wake wa kupanga kesho kabla haijafika. Aidha, Dar es Salaam siyo jiji la kawaida tena. Ni moyo wa uchumi wa Tanzania.
Kila dakika inayopotea kwenye foleni ni hasara kwa mfanyakazi, mfanyabiashara, mwekezaji, serikali na Taifa kwa ujumla. Swali si kama tunahitaji miundombinu mipya. Swali ni kama tunaijenga miundombinu hiyo kwa kuzingatia Dar Es Salaam ya kesho au tunaendelea kutumia fedha nyingi kutatua matatizo yale yale kila baada ya miaka kumi, tena kwenye kampeni za uchaguzi.

Wakati wa kampeni za uchaguzi wa 2025, wananchi tuliambiwa kuwa mwezi Januari 2026 ujenzi wa Reli ya Mjini Commuter Rail ungeanza. Ahadi hii ilitolewa hadharani na kurudiwa mara nyingi na viongozi na wasaidizi wao katika mikutano mbalimbali ya kampeni. Hata hivyo, hadi sasa hatujaona utekelezaji wa ahadi hiyo, na jambo linalozua maswali zaidi ni kwamba mradi huo haujaonekana kupewa kipaumbele katika bajeti ya mwaka 2026/2027. Wananchi tuna haki ya kupata maelezo ya wazi Je, mradi umeahirishwa, umebadilishwa ratiba au umefutwa kabisa? Ahadi za kampeni zinapaswa kuambatana na uwajibikaji, kwa sababu maendeleo ya jiji letu hayawezi kujengwa kwa maneno pekee bali kwa utekelezaji wa yale yaliyoahidiwa.

Historia ya maendeleo ya miji duniani inaonesha jambo moja muhimu, Miji mikubwa haikwami kwa sababu ya kukosa fedha pekee, bali kwa sababu ya kukosa maono ya muda mrefu. Dar es Salaam inahitaji maono hayo sasa kuliko wakati mwingine wowote katika historia yake.
 
Hongera sana Kwa uchambuzi makini, lakini kama Taifa tuna shida au mkwamo mkubwa la viongozi wasio na maono.

Mwaka 2016 walijenga barabara ya Victoria Kwa njia nne za lami lakini Cha kushangaza Mwaka 2021/2022 wakabomoa kuweka mwendokasi na hapo ni miaka 5/6 tu ndio waje na mipango ya miaka 20 !! Hizo AKILI ni above their levels.

Narudia hongera Kwa uchambuzi mzuri hata wezi wa uchaguzi kamwe hawawezi kukuelewa.
 
Back
Top Bottom