Rais wa Muungano wa Visiwa vya Comoro, Ahmed Sambi, amesema alipokea vitisho, vikiwamo vya kuuawa baada ya kukubali kuanzishwa kwa Benki ya Exim mjini Moroni kisiwani Ngazija.
"Niliambiwa kama nataka kubaki madarakani au kuendelea kutawala, nisilete benki yoyote Comoro… nikasema kama ni kufa acha nife, lakini benki hii lazima ianze kazi hapa,"
alisema Sambi kwenye uzinduzi wa tawi la kwanza la Benki ya Exim.
Akiwa na mgeni wake, Rais Jakaya Kikwete, Sambi alisema umuhimu wa benki kwa nchi yake ulikuwa ni mkubwa na sasa fursa nyingi za biashara zinaweza kufanyika kati ya nchi hizo mbili.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Bodi ya Exim, Yogen Manek, hiyo ni benki ya kwanza kutoka Tanzania kuwekeza nje ya nchi ambapo ina mwaka mmoja sasa Comoro na wateja 5,000 na kabla ya mwishoni wa mwaka huu, itafungua matawi mengine Sudan na Djibouti.
Sambi aliwataka Watanzania wengi zaidi kuja kwa wingi kuwekeza Comoro, ikiwa ni njia mojawapo ya kurejesha fadhila kwa Tanzania kuikomboa Anjouan. "Marafiki zetu njooni mtusaidie kuboresha maisha ya watu wa Comoro, nchi yetu ni kama bikira katika uwekezaji, ina vivutio vya kutosha," alisema.
Kabla ya tawi la benki, Comoro ilikuwa na benki mbili; ya Posta inayomilikiwa na Serikali na ile ya BIC. Rais Sambi alimpongeza Rais Kikwete, kwa kusema alikuwa muungwana kuikomboa Anjouan kwa mtutu wa bunduki, na sasa amekuwa muungwana kuikomboa kifedha (kiuchumi). Rais Kikwete alikuwa na ziara ya siku tatu katika visiwa hivyo na alitarajiwa kurejea nchini jana.