KWELI Cleopa Msuya ameshawahi kushikilia cheo cha Uwaziri Mkuu na Umakamu wa Rais kwa wakati mmoja

Taarifa hii imethibitika kuwa ya kweli baada ya kufanya tathmini ya kina
Salaam Wakuu,

Leo mtandaoni nimeona dokezo likidai Cleopa Msuya katika historia ya Utawala wa Nchi yetu amewahi kushikilia vyeo vya Waziri Mkuu na Makamu wa Rais kwa wakati mmoja.

Kuna ukweli hapa?

cleopa Msuya.jpg

Picha: Cleopa Msuya
 
Tunachokijua
Cleopa David Msuya ni mwanasiasa wa Tanzania. Amezaliwa 4 Novemba 1931 Wilaya ya Mwanga Mkoa wa Kilimanjaro,Tarafa ya Usangi. Cleopa David amewahi kushika wadhifa wa Uwaziri Mkuu mara mbili, 7 Novemba 1980 hadi 24 Februari 1983, na tena 7 Desemba 1994 hadi 28 Novemba 1995. Pia Cleopa Msuya amewahi kushika nyadhifa kwenye Wizara mbalimbali Wizara ya Ardhi, Maji na Makazi; Wizara ya Uchumi na Mipango; Wizara ya Viwanda; Wizara ya Fedha na Wizara ya Viwanda.

Kwa sasa ameshastaafu siasa ingawa anajitokeza kwenye mahojiano mbalimbali na vyombo vya habari.

Je, Cleopa Msuya ameshawahi kushika vyeo Uwaziri Mkuu na Makamu wa Rais kwa wakati mmoja?
Baada ya kuwapo kwa hoja hiyo JamiiForums imepitia vyanzo mbalimbali Ili kupata uhalisia wa hoja hii Kama ifuatavyo:

Kurasa maalumu za Ofisi za Serikali
JamiiForums imepitia katika ukurasa maalumu wa Ofisi ya Waziri Mkuu kutafuta taarifa za Mstaafu Cleopa Msuya. Kwanza, ukurasa huu unamtambua Cleopa Msuya kama Waziri Mstaafu wa 4 baada ya Moringe Sokoine kufariki.

Pia, ukurasa huu unaweka bayana kwamba Cleopa Msuya amewahi kushika Wadhifa wa Uwaziri Mkuu mara mbili mara ya kwanza ni kuanzia tarehe 7 Novemba, 1980 hadi tarehe 24 Februari, 1983. Mara ya pili ilikuwa ni tarehe 5 Desemba, 1994 hadi tarehe 28 Novemba, 1995.

Aidha, Ukurusa huu pia unaweka bayana kwamba Cleopa Msuya alipokuwa waziri Mkuu 1994 - 1995 alishika pia wadhifa wa Umakamu wa Rais. Andiko hili likimuelezea Cleopa Msuya linaeleza:

Aliwahi kushika wadhifa wa Waziri Mkuu mara mbili. Mara ya kwanza ni kuanzia tarehe 7 Novemba, 1980 hadi tarehe 24 Februari, 1983. Mara ya pili ilikuwa ni tarehe 5 Desemba, 1994 hadi tarehe 28 Novemba, 1995 huku akishika pia wadhifa wa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kauli hii kutoka katika ukurasa maalumu wa Waziri Mkuu unaweka msingi muhimu wa kuthibitisha kuwa ni kweli Cleopa Msuya amewahi kuwa na vyeo viwili kwa wakati mmoja (Uwaziri Mkuu na Umakamu wa Rais). Sehemu ya sentensi iliyokolezwa wino hapo juu inaweka bayana kwamba mnamo mwaka 1994 mpaka 1995 Cleopa Msuya alikuwa Waziri Mkuu wa Tanzania kwa mara ya pili lakini pia wakati huohuo alikuwa ndiye Makamu wa Rais ws Tanzania.

Pia Ukurasa maalumu wa Utumishi ukieezea tukio la Jenista Mhagama kumtembelea Cleopa Msuya unaonekana kumtambua Cleopa Msuya kama Waziri Mkuu na Makamu wa Rais Mstaafu. Sehemu ya andiko hilo inaeleza:

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Jenista Mhagama akifafanua jambo kwa Makamu wa Kwanza wa Rais na Waziri Mkuu Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Cleopa D. Msuya alipomtembelea nyumbani kwake jijini Dar es Salaam.

Japokuwa andiko hilo halijaeleza moja kwa moja kwamba Cleopa Msuya alishika vyeo hivi kwa wakati mmoja lakini linatupa picha kuwa Cleopa Msuya amewahi kuwa Waziri Mkuu na pia Makamu wa Rais kwa wakati fulani.

Taarifa kutoka mtandao wa Twitter
Mnamo Julai 5, 2023 Mtumiaji wa Twitter @HistoriaYetu ambaye huandika masuala mbalimbali ya kihistoria alichapisha andiko akidokeza kuhusu Cleopa Msuya kuwahi kushika vyeo viwili kwa wakati mmoja serikalini kwa wakati mmoja. Sehemu ya chapisho hilo lilidokeza:

Cleopa Msuya, Nairobi, Dec 20, 1968 Je, unafahamu kwamba kati ya mwaka na 1994 - 1995 Cleopa Msuya aliwahi kuwa Waziri Mkuu na Makamu wa Rais kwa muda mmoja.
Hata hivyo, wachangiji wengi katika andiko hili lililochapshwa katika ukurasa huu walionekana kukubali hoja hii na kutoa ufafanuzi kuwa Katiba ya wakati huo iliruhusu Makamu wa Rais kuwa waziri pia.​
Mfano: Mchangiaji @Cmafie alieleza

"Kikatiba wakati huo Waziri Mkuu alikuwa pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais, Makamu wa pili akiwa ni Rais wa Zanzibar. Cleopa David Msuya aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu kuchukua nafasi iliyobaki wazi baada ya kujiuzulu kwa aliyekuwa Waziri Mkuu John Samwel Malecela."
Andiko hilo katika ukurasa huu wa mtandao wa Twitter na michango yake inasaidia kutupa picha namna Cleopa Msuya alivyowahi kushika nyazifa mbili kwa pamoja yaani Uwaziri Mkuu na Umakamu wa Rais kuanzia mwaka 1994 - 1995.​
Upi Ukweli wa hoja hii?
Kutokana na suala la Cleopa Msuya kushika vyeo viwili kwa wakati mmoja kuthibitika kuwa na ukweli kutoka katika kurasa rasmi za ofisi za Serikali ikiwamo Ofisi ya Waziri Mkuu na Utumishi. JamiiForums inathibitisha kuwa hoja hii ni ya kweli.​
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom