Ni mpaka pale Bodi ya mikopo ya elimu ya juu itakapothibitisha kama itaendelea kuwalipia ada wadahiliwa , Hii ni kwa wale wa mwaka wa pili na kuendelea .
Mkurugenzi Mtendaji wa bodi hiyo Abdul - Razaq Badru alisema watu wasijaribu kulinganisha idadi ya waliopata mkopo mwaka jana na wa mwaka huu , kwa kuwa kila serikali ina vipaumbele vyake .
Chanzo - Nipashe .
MyTake:
Unaweza kuwa ulipewa mkopo mwaka wa kwanza lakini mwaka wa pili ukanyimwa , tujiandae .
========
Huku giza likitanda kwa wanaoendelea na masomo baada ya baadhi ya vyuo kusitisha usajili wao kusubiri hatima ya mikopo yao.
Katika mwaka wa masomo uliopita, bodi ilitoa mikopo ya Sh. bilioni 459 kwa wanafunzi 122,486, kati yao 53,618 wakiwa ni wa mwaka wa kwanza na 68,916 waliokuwa wakiendelea na masomo.
Fedha hizo kwa ajili ya wanafunzi wa mwaka wa kwanza zilitolewa kwa awamu zaidi ya nne ambapo ya kwanza ilikuwa na wanafunzi 12,282 huku ya pili ikiwa na wanufaika 28,554.
Juzi Mkurugenzi Mtendaji wa bodi hiyo, Abdul-Razaq Badru, alisema watu wasijaribu kulinganisha idadi ya waliopata mkopo mwaka jana na wale wa mwaka huu kwa kuwa kila serikali ina vipaumbele vyake.
Nipashe ilitembelea Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ambako ilishuhudia baadhi ya wanafunzi wa mwaka wa pili na tatu waliokuwa wakisajiliwa kuanzia juzi kwa ajili ya mwaka huu wa masomo, wakishindwa kusajiliwa kutokana na taarifa za serikali kusitisha mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu kwa ajili ya kupitia upya vigezo vinavyotumika kuwapatia mikopo.
Jumanne Bakari, mwanafunzi wa mwaka wa pili anayesomea Shahada ya Uhandisi wa Viwanda, alieleza kuwa alikataliwa kusajiliwa na kutakiwa kusubiri hadi majina mapya ya wanufaika wa mikopo yatakapotolewa na HESLB.
Makamu Mkuu wa UDSM, Profesa Rwekaza Mukandara, alisema ili mwanafunzi aendelee na masomo chuoni hapo ni lazima alipe ada ama taarifa rasmi kutoka HESLB zitolewe chuoni kuwa bodi hiyo itamlipia mwanafunzi husika.
“Kwenye usajili ni lazima alete vyeti vyake vikaguliwe, alipe ada, apewe kitambulisho, anapewa chumba kisha anaendelea na masomo, ila kwenye udahili tunapokea majina kutoka Tume ya Vyuo Vikuu (TCU), tunayakagua majina hayo na kuyachuja, tunapeleka tume majina ya Wanafunzi ambao wahajakidhi vigezo vya kujiunga na UDSM,” alisema Prof. Mukandara.
Alisema chuo bado hakijapewa majina ya wanafunzi wanaoendelea na masomo (kuanzia mwaka wa pili) kutoka HESLB kama uthibitisho kuwa bodi hiyo itaendelea kuwalipia.
Kwa Upande wake, Mkurugenzi wa Shahada za Awali wa UDSM, Profesa Allen Mushi, alisema hadi juzi, chuo kilikuwa hakijapata majina kutoka HESLB kwa wanafunzi wa mwaka wa pili na tatu ambao watalipiwa.
Alisema mwongozo wa chuo hicho unataka mwanafunzi kuruhusiwa kujisajili kwa kipindi cha wiki mbili, na kwamba kwa sasa wanafunzi wanaruhusiwa kuingia darasani wakati wakisubiri taarifa za HESLB.
“Tumeona tangazo katika mtandao wa bodi na tulimtuma mtu wetu aende kufuatilia majina akaambiwa bado, lakini tunaimani ndani ya wiki mbili kila kitu kitaenda sawa, ila kwa sasa wanafunzi wanaruhusiwa kuingia darasani na hata kulala kwenye vyumba,”alisema Prof. Mushi.
ADA YOTE
Aliongeza kuwa mwanafunzi anaweza kulipa ada yote ama sehemu ya ada anayopaswa kulipa wakati chuo kikisubiri majina kutoka bodi, na endapo mwanafunzi husika jina lake likipitishwa na bodi, chuo kitamrudishia fedha zake alizokuwa amelipia.
Alisisitiza kuwa ikiwa wiki mbili za usajili zikipita bila bodi kuwapatia majina ya wanafunzi itakapowalipia ada na mahitaji muhimu chuoni, uongozi wa chuo utakaa na kutoa mwongozo kwa wanafunzi wote.
Kwa mujibu wa bodi hiyo, kwa mwaka huu wa masomo wanafunzi wanaotarajiwa kupata mikopo ni 24,000.
Mkurugenzi Mtendaji wa bodi hiyo, Badru, alisema: "Baadhi ya watu wanajaribu kulinganisha idadi ya watu waliopata mikopo mwaka wa uliopita, wanasahau kwamba ni vitu viwili tofauti na kila serikali ina vipaumbele vyake na kwa sasa suala la viwanda ndiyo kila kitu.”
TCU imepitisha wanafunzi 58,000 ambao wanatarajiwa kujiunga na masomo ya elimu ya juu kwenye vyuo mbalimbali nchini kwa mwaka huu wa masomo.
Kutokana na tangazo hilo la serikali, Jumuiya ya Wanafunzi wa Taasisi za Elimu ya Juu (Tahliso) imeingilia kati kwa kufanya majadiliano na uongozi wa HESLB na Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Prof. Joyce Ndalichako.
Mwenyekiti wa Tahliso, Stanslaus Kadugalize alisema majadiliano hayo yaliongozwa na hoja mbili zinazohusu wadahiliwa wapya na wanaoendelea na masomo na kukubaliana mambo mawili.
Kadugalize alisema kwanza walikubaliana mwongozo mpya wa utoaji mikopo uliotolewa kwa mwaka wa masomo 2016/17, utawahusu mwaka wa kwanza.
Alisema pili walikubaliana wanafunzi wanaonufaika na mikopo wanaoendelea na masomo, wataendelea na utaratibu kama ulivyokuwa tangu awali walivyoingia makubaliano na utaratibu mpya hautawaathiri.
“Kufuatia tangazo la wizara lililotolewa Oktoba 17, mwaka huu linalohusu uhakiki wa wanafunzi wanaoendela na masomo ya shahada, TAHLISO inaomba kila mwanafunzi anayesoma shahada kuangalia majina yaliyotolewa kwenye tovuti ya TCU ili kuhakikisha jina lake lipo, na kwa yule ambaye hataona jina lake awasiliane na uongozi wa TCU ndani ya wiki mbili ili kuepuka usumbufu utakaojitokeza,” alisema Kadugalize.
VIGEZO VIPYA
Katika taarifa ya serikali ililotolewa Ijumaa na Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, vigezo vya kupatiwa mikopo vitapitiwa upya na wanafunzi watakopeshwa kulingana na uwezo wao.
Sehemu ya tangazo hilo lililotolewa na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Mhandisi Stella Manyanya, inasomeka:
“Kwa hivi sasa Bodi (ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu) imekamilisha uchambuzi wa majina ya waombaji ambao wana sifa zilizoainishwa hapo juu na majina ya wanufaika wapya yatatangazwa Oktoba 14, 2016 (Ijumaa).
"Aidha, kuanzia mwaka huu wa masomo, wanufaika wote wa mikopo, wapya na wanaoendelea na masomo, watakopeshwa kulingana na uwezo wao katika vipengele vyote vya mikopo."
Katika tangazo la serikali, pia kulitajwa fani ambazo wanafunzi wanaozisomea watapewa kipaumbele ambazo ni Sayansi za Tiba na Afya, Ualimu wa Sayansi na Hisabati.
Nyingine ni Uhandisi wa Viwanda, Kilimo, Mifugo, Mafuta na Gesi Asilia, Sayansi Asilia na Mabadiliko ya Tabianchi, Sayansi za Ardhi, Usanifu Majengo na Miundombinu.
Serikali katika tangazo hilo pia imebainisha kuwa itawapa kipaumbele kwenye mkopo wanafunzi wenye ulemavu na yatima.
Chanzo: Nipashe