Mzee Mwanakijiji
Platinum Member
- Mar 10, 2006
- 33,378
- 39,319

Habari zinazoingia sasa hivi zinasema kuwa Helikopta ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania ikitokea Arusha imeanguka ikiwa njiani kuelekea Dodoma na kuua watu sita papo hapo. Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi Mwandamizi Matei Basilio amethibitisha kutokea ajali hiyo ambayo amesema haikuhusisha wajumbe wa mkutano wa Sullivan kama ilivyoripotiwa awali.
Akizungumza na KLH News muda mfupi uliopita Kamanda Basilio (SACP) amesema kuwa ajali hiyo imetokea eneo la kijiji cha Matevesi-Kisongo umbali wa kama Kilomita 17 kutoka Arusha majira ya saa sita mchana. Bw. Basilio amesema kuwa waliofariki katika ajali hiyo ni watu sita wakiwemo rubani na fundi, mama na mtoto wa kike wa miaka kumi na maafisa wa jeshi hilo ambao walikuwa wamepewa lifti kuelekea Dodoma.
Kamanda Basilio amesema kuwa ndege hiyo ilianguka kwenye eneo hilo na kuwaka kulipuka na ni wanakijiji wa eneo hilo waliotoa taarifa kwa vyombo vya ulinzi na usalama mkoani humo. Hata hivyo Kamanda Basilio amesema kuwa ndege hiyo haikusababisha madhara ardhini kwani iliangukia umbali na makazi ya watu na hilo limechangia kuepusha maafa makubwa.