Chonde Chonde Mama Zinduna, hata Mimi nina moyo!

Robert Heriel Mtibeli

JF-Expert Member
Mar 24, 2018
21,339
51,884
CHONDE CHONDE MAMA ZINDUNA, HATA MIMI NINAMOYO!

Anaandika, Robert Heriel
VPN.

Manyanyaso yalizidi pale Ukweni, kama mtakumbuka Taikon nilileta Stori zaidi ya tatu humu tangu nimeenda kuchumbia, mpaka nikaishi Kwa Shemeji, kisha nikaitwa nikaishi ukweni na Mke wangu. Baada ya kupigwa ngumi mchomoko na Mama Mkwe wangu nikaamua isiwe shida, nikahama pale Mwanzoni mwa mwezi huu, November. Hii ni kusema mpaka sasa ninawiki Kama tatu ninajitegemea kibachela.

Natamani nifanye Siri, nisiseme kilichotokea. Sipendi Kueleza maisha yangu mbele za watu. Lakini kwa Siri ipi hiyo, wenzangu wanaficha Siri za Utajiri na kufanikiwa Mimi naye ni mtu mwenye Siri; Siri za kutunzwa ukweni nayo ni Siri ya kuficha, Siri ya kulishwa kama Mbuzi ukweni nayo ni Siri, labda ninaposema najidhalilisha, sijali lolote Mimi!
"Mbona kama Taikon umepagawa, embu tulia usimulia Kwa utulivu, Acha Wenge"

Okay! anyway!
Nikazuiwa nisiondoke na Mke wangu kipenzi, mama Taikon, Bebe madaha, Sweetmelody, Hapetaiza wangu, Binti ndembo mrembo aliyeninasa Kwa maringo na uzuri wake.
Sasa niliiishi mwenyewe kama Funza dume niliyevimbiwa matatizo ya Dunia,

Nikapata chumba katika mtaa wa Mtoni mtongani huku Temeke. Ni kizuri lakini Kwa mwenye shida. Nilishazoea Kiyoyozi ukweni, huku ni joto mwanzo mwisho, nyumba zimebanana na kushikamana kama Meno ya Manka wa Uru.
Lakini ilikuwa Akheri kwangu, amani ndio ilikuwa muhimu zaidi. Nilichoshwa na songombingo na usongo wa Mama Mkwe wangu. Pia nilichoshwa na maneno ya washikaji zangu hata ninyi WA humu Mtandaoni mlikuwa mnanisagia kunguni na kunipiga Spana.

Nilipofurumushwa Kule ukweni, mke wangu alinipa kipesa kidogo ambacho ndicho nilikitumia kununulia Kigodoro cha futi 4*6 na shuka mbili, kisha iliyobaki nililipia Kodi ya miezi mitatu. Sasa sikuwa nimebakiwa na kiasi chochote cha Pesa.

Ikanibidi niuze simu moja Kwa maana nilikuwa na simu mbili.
Hapo nikapata kijihela ambacho kingenisogeza nikiwa nasoma Rada ya namna ya kuchomoza katika msitu huu wenye kiza kinene.

Nilikutana na Dalali mla sonyo, nilizungushwa Kama Mstaafu anayefuatilia mafao yake. Hatimaye nikapata hicho chumba, ambacho kulikuwa na wapangaji wenzangu watatu, na mama Mwenye nyumba.

Sitaki kukumbuka siku Ile ninahamia, nilikuwa Kama mkimbizi wa kirundi anayekimbia vita ya kimbari. Kigodoro changu na shuka zangu mbili nilizifunga mgongoni, sikuwa na haja ya kuhamia usiku, nifiche nini sasa! Mambo ya kufuata mkumbo yalinishindaga miaka mingi iliyopita. Nilihamia pale jioni ya saa kumi na moja hivi, hapo niliwakuta Wanawake wamekaa kibarazani na vitoto kadhaa wakiwa wananishangaa ungedhani wameona Kakakuona.

Moyoni nilikereka na kuwatukana matusi ambayo kama wangeyasikia sijui ingekuwaje. Nikafungua mlango na kuzama zangu ndani.

Chumba kilikuwa na dirisha moja, Pazia nitatoa wapi, Sufuria, jiko, ndoo ya kuogea. Hayo yote nilikuwa nayafikiria nikiwa nimelala kwenye kigodoro changu cha futi4*6.

Nakukumbusha tuu, Taikon ninashahada kutoka Chuo kikubwa ndani ya nchi hii. pia nilibahatika kusoma degree ya pili huko Afrika Kusini nikiwa nimedhaminiwa na upande wa Ukweni. Na kote huko NILIFAULU Kwa kiwango cha juu kabisa. Lakini kumbe maisha hayaangalii unadegree ngapi, hayaangalii unaonekanaje, Kwa maana mbali na elimu na akili pia nilijaliwa mvuto Kwa wanawake waliowengi.

Lakini maisha ni Majaliwa kutoka Kwa muumba. Haya sitaki kuwa muhubiri Leo. Acha niendelee na Stori

Nikatoka nikaenda zangu kutafuta sehemu ya Kula Kwa Mama ntilie. Baada ya Kula nilirejea Ghetto. Sikuwa na sehemu ya kwenda, ningeenda wapi Mimi, kufanya nini Mimi, Acha nipumzike huenda shida zangu nazo zitapumzika.
Giza lilianza kuingia kumaanisha siku Ile ilikuwa imeisha, lakini nilihisi kwenda Haja kubwa; Si nilikula Kwa Mama Ntilie.

Sasa chooni nitaendaje wakati sina ndoo, lakini kadiri nilivyobanwa na Haja ndivyo ujasiri ulivyoongezeka, liwalo na liwe, nikatoka hapo nje walikuwa Wanawake wakipika pika, hiyo ni saa moja kwenda saa mbili.

Nikaenda, nikamgongea Mama mwenye nyumba, akafungua, nikamuomba nahitaji msaada wa ndoo kwani nimetingwa.

Akanitathmini Kwa macho yake makubwa yenye utukufu wa utu uzima, kisha bila kusema chochote akageuka na kunipa mgongo akaanza kutembea akiniachia mitetemo ya Makalio yake makubwa yaliyonona, Kwa nukta chache alizokuwa akitembea nilijikuta nimesahau kama nilibanwa na NNYA! Hata hivyo sikufikiria Jambo lolote Ovu dhidi yake. Akanipa ndio yenye maji yaliyojaa. Kisha akaniambia ukaoge kabisa sasa, alafu akatabasamu.

Nilimshukuru Sana. Ni Kama akijua kuwa mwili wangu ulikuwa unanata kama Nta ya Asali ya nyuki. Pilikapilika za mchana ziliufanya mwili wangu kutoa jasho na kuukinaisha mwili wangu.

Nilitoka Uani nikiwa Kama mtu aliyebatizwa ubatizo wa Maji mengi. Nilikuwa mtu mpya kabisa nikiwa na nguvu mpya lakini matatizo ya zamani.

Palikuwa na mbu wengi lakini hawakunizuia kulala, nilikuwa nimechoka Sana.

Asubuhi ilifika, nikasema nikachukue ndoo na Pazia Kwa kale kahela nilikokapata baada ya kuuza simu yangu. Nikachukua na Jiko la njaa, na sufuria mbili na sahani. Sasa hela ilikuwa imebakia ndogo mno. Hata hivyo nilijiona nimepiga hatua Fulani kutoka katika ule msitu wenye kiza kinene.

Maji yalikuwa ya mgao, nilizoea ukweni maji yakitiririka masaa 24, kama hiyo haitoshi umeme nao ulikuwa ni janga, ulikuwa unakatikatika hovyo. Lakini kwangu haukuwa na umuhimu wowote. Sikuwa na kifaa chochote kinachohitaji umeme zaidi ya taa na simu yangu ambayo tangu niondoke ukweni hakuna aliyenipigia. Hata usiku wa Jana kabla sijalala nikijaribu kumpigia mke wangu lakini alikuwa hapatikani.

Baada ya wiki ya Kwanza kupita nilishazoea mazingira, tatizo ni pesa ilikuwa imeisha,
Nilijaribu kutafuta vibarua kwenye viwanda Kwa kupaki Mando Asubuhi Asubuhi kwenye malango ya viwanda tukisubiri kuitwa lakini kama kawaida waliitwa walewale waliozoeleka kwenye viwanda hivyo. Nikaenda Kariakoo kuona Kama ningepata kazi walau ya kubeba mizigo lakini hata huko pia kunahitaji connection, kila sehemu inahitaji Nani anakujua. Doooh!

Chakula nilichonunua ndani kikaisha, pesa sina, yaani hata Buku ya Nauli ili nitoke niende kutafuta vibarua. Nikasema huu Msala Kama sio msalaba.

Mama mwenye nyumba alishaanza kuniletea PIGO Sizo, lakini kutokana na kuwa nilikuwa natoka kutafuta vibarua na kurudi jioni haikuwa shida. Sasa sitoki Kwa sababu sina Pesa na ninashinda nyumbani ndipo vioja vyake vilipoongezeka,

Siku moja Majirani wote walikuwa wameondoka wameenda kwenye sherehe ya rafiki Yao mtaa WA tatu huko. Waliondoka wamevaa Sare ya Madera na Vijora. Mama Zinduna ndiye Mama mwenye Nyumba aliniita, nikaenda nikijua anajambo la maana,
Nilimkuta kavaa Kanga yake aipendayo ambayo Kwa chini ilikuwa na maandishi yaliyosomeka "Raha ya Tende Kumung'unya"
Maandishi Yale kwangu hayakuwa na maana yoyote. Lakini nilianza kuyakumbuka nilipoingia sebuleni mwake, Mama Zinduna alikuwa amejiachia Mno. Bila haya aliachia eneo kubwa la mapaja yake makubwa manene huku akinitazama Kwa macho ya mawindo.

Muda huo tumboni mwangu mambo hayakuwa mazuri. Na siku zote Njaa haijifichi usoni. Mtu mwenye njaa hata asiposema Kwa kinywa chake basi USO wake na macho yake yatasema.
Nikashangaa Mama zinduka akiamka na kuniacha pale Sebuleni Mimi nikimsindikiza Kwa macho, nikitazama Double Kibini mbili zilizokuwa zinapimana uzito nyuma yake, lilikuwa Banda kubwa la Uani lenye Tairizi ambalo lilifanya macho yangu kuteleza kila yalipotua katika Banda lake.

Macho yangu yalishuka mpaka kwenye Yale maandishi yaliyosomeka " Raha ya tende kumung'unya" hapo akanigeukia akiwa anakaribia kukatisha, nikahamisha USO wangu Chapu, ni Kama alijua lazima nitakuwa nayatazama mabanda yake mawili, labda aliniona ninamaswali mengi kuhusu mabanda hayo. Akatabasamu kisha akapotelea kwenye Korido.

Kitambo kidogo akarejea akiwa amebeba Hotpot, akaweka mezani kisha akaondoka tena, akarudi akiwa na sahani na bilauri. Kisha akaiweka Ile sahani mezani alafu akaifuata Jokofu(Fridge) iliyokuwa pembezoni ya ukuta, akatoa juisi ya embe na kuja kunimiminia kwenye glass.
Muda wote alikuwa akifanya hayo huku akinitazama kwa macho ya uchu huku mara kadhaa akitabasamu, na wakati mwingine akijichekesha na kuzungumza vitu ambavyo ninauhakika vilikuwa havitoki akilini.

Kwa habari za USO wake ulikuwa hivi;
Alikuwa amepaka wanja Kiswahiliswahili, ambao ulimkaa kisawasawa ingawaje haukumfanya aonekane wakisasa. Kutokana na umri wake alikuwa na mikunjo midogomidogo usoni mwake ambayo ilimfanya awe na Sura ya mamlaka ya utu uzima licha ya kujitahidi kuufanya USO wake kuwa WA mahaba lakini Hilo halikutokea.
Alikuwa na macho makubwa yaliyochoshwa na umri wake mkubwa ingawaje yalifanya uzuri uendelee kuwapo.
Pua yake Pana kiasi na midomo yake ilimfanya awe mama wakibantu hasa.

Basi nikawa ninakula huku akinipigisha Stori na kuniuliza maswali kuhusu mambo yangu binafsi Kama mahusiano n.k.
Baada ya kumaliza Kula akatoa vyombo, kisha akaanza vibweka vyake,
Natamani ingekuwa zamani ili nisikumbuke ilivyotokea lakini ni wiki moja tuu iliyopita tukio hilo ndipo lilifanyika.
Yule mama asiye na Haya akanisogelea kisha akanikumbatia Kwa nguvu nyingi Sana ungedhani ni mzimu wa Mwanamalundi. Nikayasikia mapigo yake yakipiga Kwa nguvu bila kufuata kanuni ya udundaji. Yalikuwa yakipiga harakaharaka Kama mtu mwenye Presha ya kupanda.
Joto lake lilikuwa nyuzi joto kama 40°C hivi.

Alikuwa kapagawa,
nikamuambia asubiri Kwanza, muda huo nami nilihisi mwili na Akili vikipoteza Muhimili wake. Kama sitojichunga hapa nitafanya upuuzi. Nikawaza.
punde Kwa sekunde simu ikaita, ilikuwa siku yangu. Jambo Hilo likamfanya aniachie huku kanga yake ikiwa tayari ilikuwa imefunguka na baadhi ya maeneo ya Mwili wake nikiwa nimeyaona,
Nikatoa simu mfukoni, aliyekuwa akipiga ni Mke wangu. Nilishtuka Sana. Niikamuambia Mama zinduna nitarudi ngoja nikaongee na Ile simu.

Nikatoka nikiwa nimeponea chuplichupli! Na mitego ya mama zinduna.

Sikurudi siku Ile, niliondoka moja Kwa moja. Nikaenda kutembea nikiwaza yaliyotokea. Mambo hayo nilikuwa nayasikia tuu na pengine kuyaona katika filamu au kuyasoma katika Riwaya na simulizi tuu. Leo yananitokea.

Mke wangu aliniuliza nimehamia wapi, na alitaka kujua ninaendeleaje, aliniambia pia mama yake alimzuia asiwasiliane na Mimi ndio maana simu yake ilikuwa haipatikani.
Nikaongea na mwanangu nikafurahi. Sasa mke wangu amebakisha mwezi mmoja ajifungue. Ili nipate mtoto wa pili.

Mama Zinduna chonde Chonde hata Mimi nina Moyo. Mambo yako uliyonifanyia wiki nzima hii niyaaibu, hata siwezi kuyasema yote humu.

Ni kweli ninashida, nimegeuka Swala mwenye Kiu ya maji katika Bwawa lenye maji lililojaa Mamba mkubwa mwenye uchu wa kunila.
Mama zinduna jiheshimu,
Mimi ninamke mzuri na mtamu,
Mitego yako haitoiamsha yangu hamu,
Umasikini wangu usiutumie kama kete ya kunizamisha kuzimu,

Acha nipumzike Sasa.

Robert Heriel
Taikon wa Fasihi
Kwa sasa Dar es salaam
 
Njaa ijayo itakufanya utii masharti ya mama Zinduna.... Ndio, kwani mwenzio alifanya makusudi kuuza urithi wa mzaliwa wakwanza kwa tende?
No, ilikua sababu ya njaa.
 
Njaa ijayo itakufanya utii masharti ya mama Zinduna.... Ndio, kwani mwenzio alifanya makusudi kuuza urithi wa mzaliwa wakwanza kwa tende?
No, ilikua sababu ya njaa.
 
Njaa Haina baunsa, ndo maana wakale walisema adui yako muombee njaa!! Kongole bingwa wa fasihi.
 
Back
Top Bottom