Cheka, simulia, lakini usiombe yakukute

Umesoma hadithi hii mwanzo hadi mwisho?

  • Ndio

    Votes: 3 50.0%
  • Hapana

    Votes: 3 50.0%

  • Total voters
    6
Cheka, Simulia, Lakini Usiombe Yakukute - 17

Isingemshangaza Grego kama dada angeacha tu kuingia chumbani, kwa vile mahali alipokuwepo Grego palikuwa pakimzuia dada asiweze kufungua dirisha bila kuchelewa. Lakini siyo tu dada hakuingia chumbani, lakini alirudi nyuma na kufunga mlango.

Angekuwepo mgeni angeweza kudhania kwamba Grego alikuwa amejibanza akimvizia dada yake ili amng’ate. Sawa, Grego mara hiyohiyo alienda kujificha chini ya kochi, lakini ilimlazimu kusubiri hadi muda wa mlo wa mchana kabla dada yake kurejea, na alionekana utulivu wake ulikuwa umepotea kwa kiwango kikubwa kuliko ilivyokuwa kawaida.

Kutokana na hayo, Grego alibaini kwamba muonekano wake ulikuwa bado hauvumiliki kwa dada yake na utabakia kuwa hivyo siku zote, na kwamba ilimchukua dada yake nguvu nyingi kujizuia asimkimbie amuonapo japo sehemu ndogo ya mwili wake iliyokuwa inajitokeza wakati Grego amejificha chini ya kochi.

Na ili kumuepushia dada asimuone hata kiasi hichi kidogo, siku moja Grego aliburuta shuka mgongoni mwake na kulifunika kochi analojichia (jukumu hili lilimchukua masaa manne) na kuliweka kwa namna ambayo sasa alikuwa amefichwa kabisa kiasi kwamba dada yake, hata angeinama, hangeweza kumuona.

Kama shuka hili halikuwa na ulazima mbele ya dada, basi dada angeweza kuliondoa, kwani ilikuwa ni wazi kabisa kwamba Grego hakupata raha yoyote kwa kujificha kabisa namna ile.


Inaendelea Sehemu ya 18
 
Cheka, Simulia, Lakini Usiombe Yakukute - 18

Lakini dada aliliacha shuka kama lilivyokuwa, na Grego aliamini kwamba alimbamba dada yake akionyesha sura ya kushukuru pale Grego alipochungulia kwa uangalifu wa kuinua shuka kidogo kuona dada yake anachukuliaje mpangilio huu mpya.

Majuma mawili ya kwanza wazazi wake hawakuweza kwenda kumtembelea, na mara nyingi aliwasikia jinsi ambavyo walivyokuwa wanatambua kazi kubwa aliyokuwa akiifanya dada yake: kulinganisha, mara nyingi awali walikuwa wakikerwa na dada yake ambaye alionekana kwao ni binti mzembezembe.

Lakini, sasa wote wawili baba yake na mama yake mara nyingi walisubiria nje ya mlango wa Grego wakati dada yake akifanya usafi chumbani, na pindi tu atokapo alilazimika kueleza kwa kina namna mambo yaonekanavyo mle chumbani, nini Grego alikula, tabia yake ilikuwaje mara hii, na iwapo pengine alikuwa na maendeleo mazuri japo kidogo yanayoweza kuonekana.

Kwa vyevyote vile, mama yake kiaina mapema alitaka kwenda kumtembelea Grego, lakini baba Grego na dada yake walimzuia, mwanzoni wakitoa sababu ambazo Grego alizisikiliza kwa makini sana na ambazo alizikubali. Baadaye, lakini, walianza kumzuia kwa kutumia nguvu, na pale ambapo alilia, ‘Niacheni niende kwa Grego. Ni mwanangu aliyekutwa na masaibu mabaya! Hamuelewi ni shurti niende kumuona?’ Grego hapo alidhani pengine ingekuwa ni jambo jema kama mama angeingia chumbani, siyo kila siku, hiyo ilikuwa wazi kabisa, lakini labda mara moja kwa juma.

Mama alielewa vema kila kitu kuliko dada yake, ambaye licha ya ujasiri wake wote, alikuwa bado ni mtoto na, ukiangalia kwa makini, pengine alichukua majukumu haya kutokana tu na ujahili wa kitoto.

Grego alitamani kuona matamanio ya mama yake yakitimizwa mapema.

Ingawa wakati wa mchana Grego, kwa kuheshimu matakwa ya wazazi wake, hakutaka kujionyesha dirishani, hakuweza kutambaa kwenye mita chache za mraba zilizokuwa pale sakafuni.

Alijionea taabu kulala kimya wakati wa usiku, na muda si mrefu baadaye kula hakukumpa raha hata kidogo. Hivyo ili kupoteza mawazo, alijipatia mazoea ya kutambaa huku na kule baina ya kuta na singibodi. Alifurahia zaidi kuning’inia darini. Alivyojisikia ilikuwa ni tofauti kabisa na kulala sakafuni. Ilikuwa ni vyepesi kuvuta pumzi, mtikisiko kidogo ulipita mwilini mwake, na katikati ya muda wa furaha aliojipatia Grego juu darini, ilitokea kwamba, kwa mshangao wake, alijiachia na kudondokea sakafuni.

Hata hivyo, sasa aliweza kuuongoza mwili wake kwa namna ya tofauti, na hakuweza kujijeruhi hata kwa kudondoka kimo kirefu vile. Dada yake alibaini mara moja burudani mpya ambayo Grego amejigundulia (kwani kadiri alivyokuwa akitambaa huku na kule aliacha alama ya gundi yake), na dada alipata wazo la kurahisisha kutambaa kwa Grego kadiri inavyowezekana na hivyo kuondosha samani zilizokuwa zikimtinga pa kupita, hasa droo ya kuvalia na dawati la kuandikia.

Lakini hangeweza kufanya hivi yeye peke yake. Hakuthubutu kumuomba baba yake asaidie, na dada wa kazi ndio kabisa asingeweza kusaidia, kwani ingawa binti huyu, umri takriban miaka kumi na sita, kijasiri alibakia baada ya kusitishwa ajira ya mpishi wa zamani, alibembeleza apendelewe ruhusa ya kukaa jikoni tu na kufungua mlango pale tu panapokuwa na mahitaji maalum. Kwa hiyo, dada yake hakuwa na namna ingine zaidi ya kumhusisha mama wakati baba hayuko.


Inaendelea Sehemu ya 19
 
Cheka, Simulia, Lakini Usiombe Yakukute - 19

Mama Grego alikisogelea chumba cha Grego kwa vilio vya furaha iliyozidi, lakini alinyamaa kimya pale mlangoni.

Bila shaka dada kwanza alishakikagua chumba kuona kama kila kitu kiko sawa. Ndipo hapo tu alipomruhusu mama aingie.

Akiwa na papara kubwa, Grego alikuwa ameshusha shuka chini zaidi na kulivurugavuruga. Kwa uhalisia ilionekana ni kama shuka lililotupwa tu kizembe juu ya kochi.

Mara hii, Grego alijizuia asidukue yanayoendelea kwa kule chini ya shuka alikokuwa. Hivyo, alijizuia kumwangalia mama yake mara hii na alikuwa na furaha tu kwamba mama Grego amekuja.

“Ingia; haonekani,” alisema dada, na bila shaka alimwongoza mama kwa kumshika mkono. Sasa Grego alisikiliza wakati wanawake hawa wawili dhaifu walipohamisha droo zito, na kadiri dada yake muda wote alivyofanya sehemu kubwa ya kazi, bila kujali maonyo ya mama yake aliyehofia kwamba dada angejiumiza.

Kazi ilichukua muda mrefu. Baada ya kama robo saa hivi kupita, mama yake alisema kwamba ingelikuwa ni vyema kama wangeliacha droo pale lilipokuwa, kwani, kwanza lilikuwa ni zito mno: hawangeweza kumaliza kabla baba hakurudi, na lile droo lingekuwa katikati ya chumba lingezuia njia nyingi awezazo Grego kupita, lakini, pili, hakuna uhakika kwamba Grego angefurahia kuondolewa kwa samani zile.

Yeye alivyoona, kinyume chake ndio kilikuwa sahihi: muonekano wa kuta tupu ulimrarua mpaka moyoni, na kwa nini Grego asihisi hivyohivyo; kwa vile Grego alishazizoea samani zilizoko chumbani kwa muda mrefu na hivyo kwenye chumba kitupu angeweza kujihisi ametelekezwa.

“Na je si kweli,” mama yake alihitimisha kimyakimya, karibu sawa na anong’onaye kana kwamba alitamani kumzuia Grego, ambaye wapi hasa aliko hakufahamu, asisikie hata sauti ya mama Grego (kwani aliamini kwamba Grego hakuweza kuelewa maneno aliyokuwa akiyasema), “na je si hakika kwamba kwa kuondoa samani tunaonyesha kwamba tumekata tamaa ya tumaini lolote la mabadiliko na tunamtelekeza Grego pasi na kujali? Nadhani ingekuwa vema kama tukikiacha chumba kiwe vilevile kilivyokuwa kabla, ili kwamba, siku Grego akiturejea, akute kila kitu hakikubadilika na aweze kusahau yaliyomsibu kwa urahisi zaidi.”

Wakati akisikia maneno ya mama yake, Grego alibaini kwamba kukosa kwake mawasiliano ya moja kwa moja na binadamu, pamoja na maisha yanayoboa akizungukwa na wanafamilia kwa muda wa miezi hii miwili lazima itakuwa imeshamvuruga uelewa wake, kwani vinginevyo hakuweza kujiambia mwenyewe imekuwaje hadi yeye mwenyewe amekuwa makini kutamani chumba kiwe kitupu. Yaani alikuwa tayari kuachilia chumba chenye joto, chenye fanicha za maana alizozirithi, kigeuzwe kuwa pango ambalo, ni wazi angeweza kutambaa pande zote bila shida , lakini wakati huohuo kwa hakika na upesi kusahau pia historia yake kama binadamu?

Ina maana, tayari alishakuwa mahali karibu na kusahau na ni sauti ya mama tu, ambayo hakuwa ameisikia muda mrefu sasa, ndio iliyomzindua?

Hakuna kitakachoondoshwa; lazima kila kitu kibakie. Kwa hali aliyokuwa nayo maisha hayangeenda bila manufaa ya uwepo wa fanicha zake. Na kama fanicha hizo zilimkinza asiendelee na kutambaa kwake kusiko na akili huku na kule chumbani, haidhuru, lakini itakuwa ni manufaa makubwa.

Lakini dada yake kwa bahati mbaya alifikiri tofauti. Alikuwa keshaanza kuzoea, bila shaka pasipo mashiko, kwamba ilimradi mazungumzo yoyote yalikuwa kuhusu Grego, dada alijidai ni mtaalam maalum kwa wazazi wao, na hivyo basi ushauri wa sasa wa mama ulikuwa, machoni pa dada yake, sababu tosha ya kusisitiza kuondoshwa, siyo tu droo lile na dawati la kuandikia, ambavyo ndivyo pekee alivyovifikiria awali, bali pia samani zote, isipokuwa tu lile kochi muhimu sana.

Bila shaka, haikuwa tu ni ubishi wa kitoto na kujiamini kwake kwa hivi karibuni alikokupata kusivyotegemewa baada ya kazi ngumu. Alikuwa tayari pia keshabaini kwamba Grego alihitaji nafasi kubwa chumbani aweze kutambalia; fenicha, kwa upande mwingine, kwa kadiri alivyoona, hazikuwa na manufaa hata kidogo.

Lakini pengine ilikuwa ni ile hamasa ya hisia za mabinti wadogo wa umri wake pia ulichangia. Hisia hizi zilitafuta namna ya kujitutumua kila fursa ilipojitokeza, na kwa hisia hiyo Grete sasa alijihisi kutamani kuifanya hali aliyokuwa nayo Grego kuwa ya kutisha zaidi, ili hapo aweze kumsaidia sana zaidi ya sasa. Kwani ni hakika hakuna mwingine isipokuwa Grete ambaye angethubutu kujiamini kuingia kwenye chumba ambacho Grego alitawala kuta zake tupu akiwa mwenyewe peke yake. Na hivyo hakukubali aondoshwe kwenye maamuzi yake na mama yake, ambaye chumbani humu alionekana mwenye kujishuku kwenye jakamoyo lake, akimsaidia dada yake Grego kwa nguvu zake zote kuliondoa droo litoke chumbani.

Sasa, Grego angeweza tu kuwepo bila lile droo kama hali ingehitaji hivyo, lakini lile dawati la kuandikia lazima kwa kweli libakie. Na punde tu wale wanawake walipokuwa wametoka chumbani pamoja na lile droo, wakigumia wakati wanalisukuma, ndipo Grego alipochomoza kichwa chake kutoka chini ya lile kochi aweze kutathmini ni vipi angeweza kuingilia yanayoendelea kwa umakini mkubwa na kwa uangalifu mwingi inavyowezekana.

Lakini kwa bahati mbaya ilikuwa ni mama yake aliyerudi chumbani kwanza, wakati Grete akiwa ameizungusha mikono yake kwenye droo kwenye chumba kinachofuata akiliinua huku na kule bila kulisogeza. Mama yake hakuwa amezoea kumuona Grego; Grego angeweza kumfanya mama awe mgonjwa, na hivyo, akiwa ameogofywa, Grego aliharakia kinyumenyume mpaka mwisho mwingine wa kochi, lakini sasa hakuweza kulizuia shuka lisisogee mbele kidogo. Hilo lilitosha kumfanya mama abaini kinachoendelea. Mama aliacha kujongea, akasimama tuli pale alipo, na kisha akarejea kule aliko Grete.


Inaendelea Sehemu ya 20
 
Cheka, Simulia, Lakini Usiombe Yakukute - 20

Ingawa Grego aliendelea kujiambia tena na tena kwamba hakuna la ajabu linaloendelea, kwamba ni vipande vichache vya samani vilikuwa vinapangiliwa upya, hakukawia kujikubalia mwenyewe kwamba mienendo ya wanawake wale wakienda na kurudi, mazungumzo yao ya kunong’ona, miburuto ya fenicha sakafuni ilimuathiri mithili ya trafrani la zogo kubwa kila upande, na alikuwa akitumia nguvu nyingi kuvuta kichwa chake na miguu na kuukandamiza mwili wake sakafuni, ikabidi ajiambie bila kuremba kwamba hangeweza kustahimili haya yote kwa muda mrefu.

Walikuwa wanasafisha chumba chake, wakimuondolea kila kitu chake alichokithamini; tayari walikuwa washaliondoa droo ambamo ndani yake msumeno wa chuma na zana nyingine ziliwekwa, na walikuwa sasa wakifungua dawati la kuandikia ambalo lilikuwa limefungwa barabara sakafuni, dawati ambalo yeye, akiwa mwanafunzi skuli ya biashara, mwanafunzi wa shule ya msingi, na kwa hakika hata kama mwanafunzi wa chekechea, aliandikia kazi zake za shule.

Kwa wakati huu hakuweza kwa kweli kuwa na muda wowote wa kuangalia nia njema za wanawake hawa wawili, ambao uwepo wao kwa vyevyote vile ni karibu na alishausahau, kwa vile kutokana na uchovu waliokuwa nao walifanya kazi kimyakimya, vishindo vya miguu yao wakati wakitembea ndio ilikuwa sauti pekee iliyoweza kusikika.

Hivyo Grego akajitokea nje (wale wanawake walikuwa ndio kwanza wamejiegesha kwenye dawati la kuandikia lililoko chumba jirani ili wapumzike kidogo) akibadili uelekeo aliouchukua mara nne.
Hakujua haswa akomboe nini kwanza. Ndipo alipoona kikining’inia bayana ukutani, ukuta ambao vinginevyo ulikuwa mtupu, ile picha ya mwanamke ambaye hakuvaa chochote isipokuwa ngozi yenye manyoya mengi. Grego aliharakia kuifikia na kuukandamiza mwili wake kwenye kioo kilichoishilikia ile picha na ambacho kilifanya tumbo lake lenye joto kujihisi vizuri.

Walau kwa picha hii, ambayo kwa wakati huu Grego alikuwa ameifunika kabisa, hakika sasa hakuna mtu ambaye angeweza kuichukua. Akageuza kichwa chake uelekeo wa mlango unaofungukia sebuleni ili aweze kuwaona wale wanawake wakati wakirejea chumbani.

Hawakuwa wamejipa mapumziko marefu sana na walikuwa wakirudi chumbani mara hiyohiyo.

Grete alikuwa ameweka mkono wake kumzunguka mama yake na kumshikilia kwa karibu.

“Kwa hiyo tuchukue nini sasa?” alisema Grete akiangalia huku na kule. Kisha macho yake yakagongana na ya Grego aliyekuwa ukutani.

Grete alibaki mtulivu kwa vile tu mama yake alikuwa pale. Aliinamisha uso wake kumuelekea mama yake ili kumkinga asiangalie huku na kule, na akasema, ingawa kwa sauti ya kutetemeka na kwa haraka sana, “Twende, haitakuwa ni vema tukirudi sebuleni kupumzika tena kidogo?”


ITAENDELEA
 
Cheka, Simulia, Lakini Usiombe Yakukute - 21

Lengo la Grete lilikuwa wazi kwa Grego: alitaka kumpeleka mama sehemu salama na kisha aje kumtimua na kumshusha pale ukutani. Wee! Athubutu aruone!

Grego alichutama kwenye picha yake na hakuiachilia. Na punde tu atamrukia Grete usoni.

Lakini maneno ya Grete mara moja yalimfanya mama awe na wasiwasi sana. Mama alisogea pembeni, akaona dubwasha kubwa la hudhurungi pale kwenye ukuta uliofunikwa na karatasi yenye mapicha ya maua, na, kabla hajabaini vyema kwamba akiangaliacho kilikuwa ndiye Grego, alipiga kelele kwa sauti yake kali, “Mungu wangu, Mungu wangu” na kuanguka mikono ameiinua, kana kwamba alikuwa amejisalimisha kila kitu, kwenye lile kochi na kulala pale bila kutikisika.

“We Grego, ..,” dada alipiga kelele huku akiwa ameinua ngumi na akimtazama Grego kwa jicho la ubaya.

ITAENDELEA
 
Cheka, Simulia, Lakini Usiombe Yakukute - 22

Tokea yamkute, hayo ndiyo yaliyokuwa maneno ya kwanza ambayo dada yake alimwambia Grego moja kwa moja.

Dada alikimbilia chumba jirani ili kuleta spiriti au chochote ambacho kingesaidia kumzindua mama yake kutoka kwenye kuzirai kwake.

Grego alitaka kusaidia pia (pangebaki bado muda wa kutosha kuilinda picha ile) , lakini alikuwa ameganda kwenye kioo na ilibidi ajikwamue kwa kutumia nguvu.

Kisha naye akakimbilia chumba jirani, kama ambaye angeweza kumpa dada yake ushauri hivi, kama ilivyokuwa kwenye maisha yake ya awali, lakini ikamlazimu kusimama vivi hivi tu nyuma yake, wakati dada akipekua huku na kule miongoni mwa vyupa vingi vidogodinyo.

Hata hivyo, dada alistushwa sana alipogeuka. Chupa moja ikadondoka chini na kupasuka vipandevipande. Kipande cha chupa kikamjeruhi Grego usoni, huku dawa au nini sijui ilikuwa iumizayo ikitiririka juu yake.

Ndipo, bila kusita zaidi, Grete alichukua vyupa vingi kadiri alivyoweza kuvibeba na kukimbia navyo kwa mama yake. Akafunga mlango kwa mguu wake. Grego sasa alikuwa amefungiwa nje mbali na mama yake, ambaye pengine alikuwa karibu ya kufa, yote hayo shauri ya Grego.

Hakuweza kuufungua mlango, na hakutaka kumfukuza dada yake ambaye ilimbidi abaki na mama yake.

Kwa wakati huu hakuwa na lolote la kufanya zaidi ya kusubiri, na akiwa amezidiwa na majuto na wasiwasi, alianza kujongea na kutambaa juu ya kila kitu: kuta, fenicha, na dari. Hatimaye, katika sintofahamu yake, kadiri alivyokuwa akiona chumba chote kinaanza kumzunguka, alidondoka katikati ya meza kuu.

Muda mfupi ulipita. Grego alilala pale kilegelege. Kila kitu kumzunguka kilikuwa kimetulia. Pengine hiyo ilikuwa ni ishara njema.

Kisha kengele ya mlangoni ikalia.

Yule dada wa kazi alikuwa amejifungia jikoni kama ilivyo desturi, na ilimlazimu Grete kwenda kufungua mlango.

Baba alikuwa amerudi.

“Nini kimetukia,” yalikuwa ndio maneno yake ya kwanza. Muonekano wa Grete ulimwambia kila kitu.

Grete alimjibu kwa sauti chovu; wazi kabisa kichwa chake kilikuwa kifuani mwa baba:

“Mama alizimia, lakini sasa anaanza kuendelea vizuri. Grego ametoroka chumbani.”

“Ndio, niliyategemea hayo,” alisema baba, “Siku zote nawaambieni, lakini ninyi wanawake hamtaki kusikiliza.”

Ilikuwa ni wazi kwa Grego kwamba baba yake ameelewa vibaya ujumbe mfupi wa Grete na sasa alikuwa anadhani kwamba Grego amefanya jinai hii au ile ya kutumia nguvu. Hivyo Grego sasa ilimbidi atafute namna ya kumpoza baba yake, kwani hakuwa na muda wala fursa ya kumfafanulia baba yake hali halisi ilivyo.

Na hivyo alikimbilia mlango wa chumba chake na kuuegemea, ili kwamba baba yake aweze kuona moja kwa moja pale aingiapo kwamba Grego ana makusudi mazima ya kurudi chumbani mwake mara moja, kwamba haikuhitaji kumswaga ili arejee chumbani, bali ilichohitajika ni kumfungulia tu
mlango naye atatokomea ndani papo hapo.

Lakini baba yake hakuwa kwenye hali ya kuweza kubaini wema wote huo.

“Ah,” alipiga kelele mara tu alipoingia, kwa sauti inayoashiria kwamba alikuwa kwa wakati mmoja amekasirika na kufurahi.

Grego alikiondoa kichwa chake kutoka mlangoni na kukiinua uelekeo alikokuwa baba yake. Hakuwahi kwa kweli kumfikiria alivyo baba yake kama alivyokuwa amesimama pale.

Ndio, kwa mbinu yake mpya ya kutambaa huku na kule, alikuwa ameacha kuzingatia yanayoendelea mle nyumbani, kama ambavyo alikuwa anafanya awali, na kwa kweli impasa kutarajia ukweli kwamba atakuana na hali tofauti.

Hata hivyo, pamoja na hayo, yule kweli alikuwa ndiye baba yake yuleyule? Alikuwa mtu yuleyule ambaye alilala hoi amejitupa kitandani siku za mwanzo wakati Grego akifunga safari za kibiashara, ambaye alimpokea mida ya jioni siku arudipo akiwa amevaa nguo za kulalia na amekaa kwenye kiti cha uvivu, asiyeweza kabisa kuinuka, ambaye aliweza tu kuinua mkono kama alama ya kufurahi, na ambaye alienda kutembea Jumapili chache katika mwaka na kwenye sikukuu muhimu alijongea polepole baina ya Grego na mama yake (ambao nao walijongea poleple), mara zote akiwa polepole zaidi yao, akiwa amejifunika koti lake la zamani, muda wote akitumia mkongojo wake kwa makini, na ambaye, pale ambapo alitaka kusema kitu, karibu mara zote alisimama tuli na kuwakusanya wanafamilia waliomzunguka?

Lakini sasa alikuwa amesimama wima hasa, amevaa ovaroli la bluu lililomkaa vizuri, lenye vifungo vya rangi ya dhahabu, kama vile watumishi wa benki wavivaavyo.

Juu ya kola ngumu ya jaketi lake videvu vyake dabali vilijitokeza vikiwa imara kabisa, chini ya nyusi zake nyingi macho yake yalijaa nuru yakiwa imara kabisa, na nywele zake nyeupe ambazo alizoea kuziona zikiwa zimevurugika zilikuwa zimetanwa vema kuwa zing’arazo.

Baba alitupa kule kofia yake, ambayo ilikuwa na maandishi ya dhahabu (huenda yakiwa ni alama za benki), mpaka ilipotua kwenye kochi lililokuwa upande wa mwisho wa chumba, akajongea, huku pindo za koti lake refu la sare ya ofisi zikisukwasukwa huku na kule, mikono yake ikiwa kwenye mifuko ya suruali, uso wake ukiwa na sura ya kazi, mpaka alipomfikia Grego.

ITAENDELEA

 
Cheka, Simulia, Lakini Usiombe Yakukute - 23

Hakufahamu nini hasa alichokuwa anakiwaza kichwani mwake, lakini hivyohivyo aliinua mguu wake juu kuliko ilivyo kawaida, na Grego alistushwa na ilivyo kubwa sana soli ya kiatu chake.

Hata hivyo, hakukaa sana kwenye suala hilo. Kwani alifahamu tokea siku ya kwanza ya maisha yake mapya kwamba kwa kila linalomhusu Grego, baba yake alichukulia matumizi ya nguvu kubwa kama suluhisho pekee.

Hivyo Grego aliharakia kumkimbia baba yake, na alisimama pale tu baba yake aliposimama, na kuanza kumkimbia tena pale baba yake hata alipojitikisa. Kwa namna hii walizunguka ndani ya sebule mara kadhaa, bila kitu chochote cha kuhitimisha kutokea; hii ilikuwa hivi haswa kwa vile mwendo wa pole ulifanya isionekane ni kukimbizana.



Grego alibakia sakafuni muda wote huu, hasa kwa vile alihofia kwamba baba yake angechukulia mbio zozote juu ukutani au darini kama ni kitendo kinachothibitisha nia ovu.

Kwa vyevyote vile, Grego ilimbidi kujiambia kwamba hangeweza kuendelea kukimbizana huku kwa muda mrefu, kwani pale ambapo baba alipiga hatua moja, yeye ilimbidi kujongea idadi kubwa ya nyendo.

Tayari alishaanza kupata taabu ya kuvuta pumzi, kama ambavyo ilivyokuwa kwenye siku zake za zamani mapafu yake hayakuwa ya kuyategemea kabisa.

Na kadiri sasa alivyokuwa akijongea huku na kule namna hii, ili aweze kukusanya nguvu zake zote kumwezesha kukimbia, macho yake kwa nadra ameyafumbua, katika mashaka yake hakukumbuka kabisa njia yoyote ya kujiponyea zaidi ya kukimbia na ni karibu na kwamba alishasahau kwamba kuta ni mbadala mwingine aliokuwa nao, ingawa zilikuwa zimekingwa kwa fenicha zilizochongwa kwa uangalifu zilizojaa ncha kali na vijiti vilivyojitokeza vyenye ncha kali – kwa wakati huu kitu hiki au kile kilichorushwa kizembe kilimpitia karibu na kuvingirika mbele yake.

Lilikuwa ni tunda la tufaa; pasi na kuchelewa la pili likaruka kulifuatia. Grego akasimama tuli kwa hofu. Mbio zaidi zisingekuwa na tija, kwa baba yake alishaamua kumshambulia.

Kutoka kwenye bakuli lenye matunda kabatini, baba yake alijaza mifuko yake, na sasa, bila kupumzika kwa muda ili kulenga vizuri, alikuwa akitupa tufaa baada ya tufaa.
Matufaa haya madogo mekundu yalivingirika kwenye sakafu mithili ya yanayoendeshwa na umeme na kugongana yenyewe kwa yenyewe.

Tufaa moja lililorusha kizembe liligusa mgongo wa Grego lakini likateleza na kuanguka bila madhara. Lakini lingine lililorushwa mara tu baada ya hilo lilimpiga Grego mgongoni kwa nguvu hasa. Grego akataka kujikongoja, kana kwamba maumivu makali asivyotegemea yangemuacha iwapo angeondoka alipokuwa. Lakini alijihisi ni kama aliyepigiliwa misumari pale alipokuwa na akajilaza amejinyoosha akiwa amechanganyikiwa kabisa.

Ni pale tu hatimaye alipotupa jicho alipobaini ya kwamba mlango wa chumbani kwake ulikuwa umefunguliwa na namna, mbele ya dada yake (aliyekuwa akipiga kelele), mama yake alikimbia akiwa amevaa nguo zake za ndani, kwani dada yake alikuwa amemvua nguo ili kumpa huduma ya kwanza wakati alipokuwa amezirai, na jinsi mama yake alivyomkimbilia baba yake, njiani akijifunga sketi yake moja baada ya nyingine kudondoka sakafuni, na namna, sketi zikimkwaa, alivyojirusha kwa baba yake akirusha mikono kumshikilia, kwa ushirika kamili na baba yake – lakini ni wakati huu ndipo uwezo wa Grego kuona ulipomkimbia – wakati mikono ya mama ilipofika usogoni mwa kichwa cha baba na akimbembeleza asimuue Grego.

ITAENDELEA
 
Cheka, Simulia, Lakini Usiombe Yakukute - 24

Jeraha la kutisha la Grego, ambalo lilimuuguza kwa zaidi ya mwezi mmoja (kwa vile hakuwepo hata mmoja aliyethubutu kwenda kuliondoa tufaa, kwani lilibakia mwilini mwake kama kumbushio lionekanalo), ilionekana lenyewe lilimkumbusha baba kwamba, licha ya hali yake ya sasa ya kuhuzunisha na kuchukiza, Grego bado alikuwa ni mwanafamilia, kitu ambacho huwezi kukishughulikia kama adui, na kwamba ilikuwa, kinyume cha hayo, ni wajibu wa familia kujizuia na kustahamili – na siyo kitu chochote kingine, kustahimili tu.


Na kama vile kupitia jeraha lile, Grego sasa alikuwa ni kama amepoteza moja kwa moja uwezo wake wa kujongea na kwa muda huu alihitaji dakika nyingi nyingi kutambaa kutoka upande mmoja wa chumba hadi mwingine, kama mgonjwa mzee (kwa sasa kutambaa kwenda juu kuhusikavyo, hilo halikufikirika), hata hivyo pamoja na hali yake izidiyo kuwa mbaya, kwa maoni yake, alipata fidia ya kuridhika kabisa, kwani kila siku inapokaribia magharibi mlango unaeleka sebuleni, ambao alikuwa na tabia ya kuuangalia kwa makini hata kwa saa moja au mbili kabla, ulifunguliwa, ili Grego, aliyelala kizani chumbani mwake, asiyeonekana kwa waliokuwa sebuleni, aweze kuiona familia nzima iliyokuwa kwenye mwangaza mezani na kusikiliza mazungumzo yao, kwa kiasi fulani kwa ruhusa yao ya pamoja, hali ambayo ilikuwa ni tofauti sana na yaliyotukia kabla.


Ni wazi, hayakuwa tena mazungumzo yaliyonoga kama zama za zamani, ambayo Grego awapo safarini kwenye kichumba cha hoteli aliyafikiria muda wote akiyamisi, pale, achokapo, na kulazimu kujitupa kitandani kwenye mashuka yenye unyevu.

Kwa muda mwingi kilichoendelea kilikuwa ni kimya kirefu. Baada ya mlo wa jioni baba alipitiwa haraka na usingizi kwenye kiti chake cha uvivu; mama na dada waliongea kwa kunong’ona humohumo kwenye ukimya.

Akiwa amejiinamia mbali aliko, mama alifuma nguo nzuri za ndani kwa ajili ya duka fulani la urembo. Dada, ambaye sasa alishapata ajira kama mchuuzi, jioni alichukua mafunzo ya hatimkato na ya Kifaransa, ili pengine baadaye awe na ajira nzuri zaidi.

Wakati mwingine baba aliamka na, kama vile asiyetambua kwamba ametoka kuutulumua usingizi, alimwambia mama “Leo umekuwa ukishona kwa muda gani!” na mara hiyohiyo kurejea usingizini, huku mama na dada wakiangaliana na kutabasamu kichovu.


ITAENDELEA

 
Cheka, Simulia, Lakini Usiombe Yakukute - 25


Kwa namna fulani ya ubishi, baba alikataa kuvua sare zake za kazini hata awapo nyumbani, na wakati nguo yake ya kulalia ikining’inia ya kutundikia makoti bila kutumika, baba aliutulumua usingizi akiwa amevalia, kana kwamba yuko tayari muda wowote kwenda kazini na hata hapa alikuwa anasubiri maelekezo ya bosi wake.

Matokeo yake, licha ya juhudi nyingi za mama na dada, sare yake, ambayo hata pale mwanzoni haikuwa mpya, ilizidi kuwa chafu, na Grego aliiangalia, aghalabu kwa jioni yote, nguo hii, ikiwa na madoa kila mahali na vifungo vyake vya rangi ya dhahabu muda wote vimenakshiwa, ambamo mzee huyu, ingawa ilimsumbua, lakini alilala usingizi wa pono.

Pindi saa ikifika saa nne kamili, mama alijaribu kumwamsha baba taratibu na kisha kumshawishi aende kitandani, kwa msingi kwamba hapo alipo hangeweza kupata usingizi mzuri na baba, ambaye hulazimika kuripoti kazini saa kumi na mbili kamili asubuhi, hakika alihitaji usingizi wa kutosha.

Lakini kutokana na ubishi wake, ambao ulimzidi tangu apate ajira, mara zote alisisitiza kuendelea kubaki pale mezani, ingawa mara kwa mara alipitiwa na usingizi na hapo ndipo angeweza kukubali kuacha kiti chake na kuelekea kitandani.

Japo mama na dada wafanye jitihada za namna gani kumuonya, kwa robo saa hubakia akitikisa kichwa chake polepole, macho yake yamefungwa, bila kuinuka kitini.

Mama humvuta upindo wa shati lake na kumwambia maneno ya kuvutia masikioni mwake; dada huacha kazi yake kwenda kumsaidia mama, lakini hayo hayangeweza kuleta matokeo kwa baba. Baba huzidisha kulala kwenye kiti chake cha uvivu.

Ni pale tu wamama wawili hao walipomuinua kwa kupitisha mikono makwapani, hufungua macho yake, na akihamisha macho yake kumwangalia mama na kumwangalia dada, na aghalabu alisema “Maisha ndio haya. Hii ndio amani na utulivu katika uzee wangu”.

Na kwa kusaidiwa na wanawake hawa wawili, hujitutumua kuinuka, kama asiyetaka, kana kwamba kwa yeye ilikuwa ni kazi kubwa, kujiachia aongozwe kwenda mlangoni na wanawake wawili hao, kuwaambia waondoke, na kisha kuenda mwenyewe kuanzia hapo, wakati mama yake kwa haraka akitupa nyuzi zake za kufumia, na dada akitupa kalamu yake ili aweze kumkimbilia baba yake ili amsaidie zaidi.



ITAENDELEA
 
namuonea huruma grego mtu pekee anayemuelewa ni dada yake tu hivi hii ni hadithi au imebase kwa true story?? Mana najiuliza vipi namie nalala mwanadam naamka bonge la mdudu loh Allah aniepushie mbali

Cheka, simulia, lakini usiombe yakukute.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom