Cheka, Simulia, Lakini Usiombe Yakukute - 15
Tena na tena Grego alisikiliza wakati mmoja wao akimkaribisha mwenzie chakula pasi na fanaka na asipokee jibu lolote zaidi ya “Asante. Nimeshiba” au maneno yanayokaribiana na hayo.
Na pengine walishasitisha hata kunywa, pia. Dada yake mara kwa mara alimuuliza baba iwapo angependa kupata bia na akijitolea kwenda kumchukulia yeye mwenyewe, dada alisema, na pale baba alipokuwa kimya, ili kuondoa pingamizi zozote ambazo angekuwa nazo, kwamba dada angeweza kumtuma mke wa kijana wa kazi aende kumchukulia. Lakini kisha baba alihitimisha mjadala kwa kusema “HAPANA” kubwa, na hakuna chochote tena kingeweza kuongelewa kuihusu.
Tayari siku ile ya kwanza baba yake aliweka bayana hali halisi ya kifedha na matarajio kwa mama Grego na kwa dada yake pia. Mara kwa mara aliinuka kutoka mezani na kuchopoa kibubu kidogo alichobakia nacho toka kwenye biashara yake, ambayo ilikufa miaka mitano iliyopita, dokumenti hii au ile au kijidaftari fulani.
Sauti yake ilikuwa ya kusikika kadiri alivyokuwa akifungua kufuli tata, na baada ya kuondosha alichokuwa akikitafuta, kukifunga tena.
Ndicho kitu cha kwanza cha kufurahisha ambacho Grego alipata nafasi ya kukisikia toka masaibu yake yamkute. Alikuwa anadhani kwamba hakuna kilichopona kutoka biashara ya baba yake; walau baba yake hakuwahi kumwambia chochote kinachokinzana na mawazo hayo, na Grego kwa upande wake hakuwahi kumuuliza. Wakati ule jambo moja tu alilolijali Grego lilikuwa ni kujitoa muhanga kwa kila kitu ili kuiwezesha familia kusahau mapema inavyowezekana masaibu ya kwenye biashara ambayo yaliwaletea wote hao kwenye hali ya ufukara.
Na hivyo kuanzia wakati huo alipoanza kufanya kazi kwa bidii na kutokea tarishi alipanda na kufikia afisa mauzo asafiriye, kama vile kwa kutwa moja, afisa mauzo asafiriye, ambaye ni wazi alikuwa na fursa kadhaa za kujiongezea kipato na ambaye mafanikio yake kazini yaligeuzwa kuwa pesa taslimu za kamisheni, ambazo zingeweza kuwekwa mezani nyumbani mbele ya wanafamilia waliostaajabishwa na kufurahishwa.
Hizo zilikuwa siku njema, na hazikujirudia kamwe baadaye, walau si kwa kiwango cha kusisimua kilekile, licha ya ukweli kwamba baadaye Grego alikuwa akipata pesa nyingi sana kiasi cha kuwa kwenye nafasi ya kubeba mzigo wa gharma za matumizi yote ya familia nzima, gharama ambazo, kwa hakika, alizibeba.
Na walifikia mahala pa kuzoea kabisa hali hiyo, pande zote mbili familia na Grego. Walichukua pesa hizo kwa shukrani, naye aliziachilia kwa furaha, lakini lile fukuto maalum halikuendelea tena kuwepo. Ni dada yake tu ndiye bado aliyebakia karibu na Grego, na ulikuwa ni mpango wa siri wa Grego kumpeleka (tofauti na Grego alivyo, dada alipenda sana muziki na alijua namna ya kupiga zumari maridhawa) mwakani chuoni, bila kujali gharama kubwa ambayo ingehitajika na ambayo ingeleta pengo ambalo lingehitaji kujaziwa kwa namna nyingine.
Mara hii au ile wakati wa muda mfupi Grego anakuwepo jijini, chuo cha muziki kilikuwa kinatajwa kwenye mazungumzo na dada yake, lakini mara zote kama vile tu ni njozi njema, ambayo kufikiwa kwake hakufikiriki, na wazazi wao hawakusikiza matarajio haya kwa furaha kamwe.
Lakini Grego aliyatafakari kwa kuyazingatia kwa makini na alikusudia kulielezea kwa mashamsham mkesha wa Krisimasi.
Katika hali yake ya sasa, fikra hizo zisizo na tija zilipita kichwani mwake, wakati akijisukumiza mlangoni na kusikiliza yanayojiri.
Wakati mwingine kutokana na kujichokea hakuweza kuendelea kusikiliza zaidi na aliachia kichwa chake kigonge mlango kizembezembe, lakini mara moja alijiweka sawa, kwani hata kasauti kadogo kalikotokana na kujongea kwake kalisikika huko sebuleni na kumnyamazisha kila mmoja.
ITAENDELEA