Just Pray
JF-Expert Member
- Nov 7, 2023
- 2,142
- 4,777
TAARIFA KWA UMMA
KUKOMA KWA AMRI YA ZUIO LA MAHAKAMA KUU LA TAREHE 10 JUNI 2025 KWA CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO (CHADEMA) KUFANYA SHUGHULI ZA SIASA NCHINI
1. Mnamo tarehe 20 Januari 2026 Jeshi la Polisi katika Wilaya ya Kipolisi ya Mbalizi Mbeya Vijijini liliwavamia viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na kushusha bendera ya Chadema katika Ofisi ya Chadema Tawi la Inyala Stendi katika wilaya hiyo wakati wakifanya zoezi la kushusha bendera nusu mlingoti kufuatia kifo cha Mwenyekiti wa kwanza na muasisi wa Chadema, Mzee Edwin Mtei ambapo Chadema imetangaza siku saba za maombolezeo. Aidha, siku hiyo katika wilaya ya Nkasi, uongozi na wanachama wa Chadema wakiwa wanaadhimisha Miaka 33 ya Kusajiliwa rasmi kwa Chadema viongozi wa Jeshi la Polisi waliwatisha na waliwazuia viongozi na wanachama wa Chadema kufanya upandaji miti katika wilaya ya Nkasi, mkoani Rukwa.
2. Kana kwamba hayo hayatoshi, siku hiyo hiyo, Katibu Mwenezi na Mpropaganda Mkuu wa CCM, chama kinachobebwa na mbeleko ya dola, alitoa Taarifa kwa Umma yenye Kichwa "Kuzuiwa kwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kufanya Shughuli zake" akibainisha kuwa Mzee Joseph Butiku alihoji, mnamo tarehe 19/01/2026, uhalali wa CCM kuendelea kufanya kazi zake wakati Chadema imefungiwa. Akaendelea kusema kuwa kufungiwa Chadema ni kutokana na Maombi Madogo (Miscellaneous application) Namba 8960 ya Mwaka 2015, lilifunguliwa na Saidi Mohamed Issa, Ahmed Rashid Khamis, na Maulidah Anna Komu dhidi ya Wadhamini wa Chadema na Katibu Mkuu katika Mahakamu Kuu ya Tanzania. Na kwamba Mahakama Kuu ndiyo iliyotoa amri ya zuio hadi kesi ya msingi Namba 8323 la Mwaka 2025 litakapoamuriwa.
3. Ikumbukwe pia, zuio hilo lilitolewa katika Mwaka ambapo Nchi yetu ilitakiwa kufanya uchaguzi mkuu. Licha ya Chadema kupeleka maombi ya kuondolewa kwa amri hiyo kutokana na ukiukwaji wake mkubwa wa haki za wanachama wa Chadema na wafuasi wake, bado Jaji
Hamidu Mwanga alishikiria msimamo wake juu ya zuio hilo. Hapakuwa na namna nyingine ya kufanya kwa upande wa Chadema labda tu kama Mahakama ya Rufaa ingeamua kuliitisha jalada la kesi hiyo na kuona uhalali wake. Kwa masikitiko makubwa Mahakama ya Rufaa haikuliitisha! Matokeo yake Chadema ililazimika kutii zuio hilo ambalo mpaka leo hii tunasema halikuwa halali na lilikuwa na lengo la kuzuia Chadema kufanya shughuli za kisiasa nchini katika mwaka wa uchaguzi mkuu!
4. Tunapenda kuwaeleza Watanzania wote na wapenda demokrasia kuwa zuio la kufanya shughuli za kisiasa kwa Chadema lilikoma mnamo tarehe 10 Desemba 2025 ambayo ilikuwa ni mwezi wa sita kamili tangu zuio hilo lilipowekwa na Jaji Hamidu Mwanga mnamo tarehe 10 Juni 2025. Kukoma huko ni kutokana na Kanuni ya 3 ya Amri ya 37 ya Sheria ya Mwenendo wa Madai (Civil Procedure Code Act Cap 33 R.E. 2023) ambayo kwa tafsiri isiyo rasmi inasomeka kwa Kiswahili:
Ikiwa ni Pamoja na masharti mengine ya kutunza hesabu na kutoa amana, Mahakama inaweza kutoa amri ya zuio kwa mujibu wa kanuni ya 1 au kanuni ya 2 na amri hiyo itakuwa na maisha kwa kipindi kilichotajwa na Mahakama, lakini kisichozidi miezi sita. (Mkazo umeongezwa.
5. Kifungu hiki cha sheria kilitafsiriwa kwa utuo na Mahakama ya Rufaa ya Tanzania katika kesi ya African Trophy Hunting Ltd vs Attorney General and 4 Others (Civil Appeal 25 of 1997) [1998] TZCA 11 (3 December 1998), ambapo Mahakama hiyo ya juu kabisa nchini ilisema kwa uwazi kabisa kuwa amri ya zuio inaweza kutolewa kwanza kwa miezi sita na inaweza kuongezwa zaidi lakini nyongeza hiyo ikiwa ni Pamoja na zuio la kwanza lisizidi jumla ya mwaka mmoja. Kwa faida ya wote tunaomba kunukuu na kutoa tafsiri ya uamuzi huo muhimu:
Firstly, the order of 13.2.1995 was for an interim injunction, not a perpetual one. Secondly, the law in Tanzania under which the relief was granted, specifically provides for an order of this kind to be in force for a period not exceeding six months. By virtue of Government Notice No. 508 of 22.11.1991, Order XXXVII Rule 4 was amended in order to introduce a maximum period of six months when an interim order of injunction would be in force.
There is, however, a proviso to this order which, in appropriate circumstances, upon an application by the party concerned, the court may grant an extension for a further period not exceeding an aggregate of one year. In this case, there being no application made for the extension of the order before the expiry of six months, the order of 13. 2.1995 as correctly held by the learned judge, expired on 13.8.1995 when the six months period ended.
That is, by operation of the law, at the expiry of six months, the order of 13. 2.1995 ceased to have any legal force, it lapsed. Consequently, it follows therefore, that on 23. 9.1996, when the learned judge dealt with the application for varying or rescission of the order for temporary injunction, the order the subject matter of the application, was no longer of any legal force. (Emphasis added)
6. Tafsiri yake isiyo rasmi ni:
Kwanza, amri hiyo ya tarehe 13. 2. 1995 ilikuwa ni zuio la muda, na si la kudumu. Pili, sheria ya Tanzania ambao nafuu (afaa) ilitolewa, inasema kwa kulenga kabisa kuwa amri kama hiyo ina nguvu ya kisheria kwa kipindi kisichozidi miezi sita. Hii ni kutokana na Tangazo la Serikali Namba 508 la tarehe 22. 11. 1991 ambapo Kanuni ya 4 ya Amri ya 37 ilibadilishwa na kuweka ukomo wa miezi sita ambapo amri ya zuio itakuwa na nguvu ya kisheria.
Hata hivyo, kuna uwezekano, wa amri hii, katika mazingira stahiki, kupitia maombi yaliyowasilishwa na mwombaji husika, ambapo mahakama inaweza kuongeza muda wa amri hiyo kwa kipindi kisichozidi jumla ya mwaka mmoja. Katika kesi hii kwa kuwa hapakuwepo maombi ya kuongezwa muda wa amri hiyo kabla haijafikia ukomo wake, amri ya tarehe 13. 2.1995, kama ilivyotamkwa kwa usahihi na jaji msomi, ilikoma tarehe 13.8.1995 pale kipindi cha miezi sita kilipokwisha. Hivyo kwa utekelezaji wa sheria, mara tu baada ya miezi sita kuisha, amri ya tarehe 13. 2.1995 haikuwa na nguvu yoyote ile ya kisheria, ilikwisha. (Mkazo umeongezwa)
7. leleweke kuwa kufikia tarehe 10 Desemba 2025 si Saidi Issa Mohamed, au Ahmed Rashid Khamis, ama Maulidah Anna Komu waliokwenda Mahakama Kuu kuomba muda wa zuio hilo kuongezwa. Kwa kutofanya hvyo inaamanisha kisheria kuwa, amri ya zuio dhidi ya shughuli za kisiasa za Chadema ilifutwa kwa utekelezaji wa sheria (operation of the law).
8. Kwa msingi huo, vitendo vya Jeshi la Polisi kuwazuia viongozi na wanachama wa Chadema katika Wilaya ya Mbeya Vijijini na Wilaya ya Nkasi ni ukiukwaji mkubwa kabisa wa haki za wana Chadema kama ambavyo zimetajwa na Kulindwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania. Ibara ya 13(1); 13(2)-(3) Ibara ya 20(1); 21(1); 26(1); 29(1)-(2) & (5) zinalinda usawa mbele ya sheria; kutobaguliwa; haki ya kujumuika, haki ya kushiriki katika shughuli za kisiasa na maamuzi katika nchi yetu; jukumu la kulinda Katiba na sheria za nchi; haki ya kufaidi haki na uhuru uliotajwa katika katiba; haki ya usawa wa kisheria; na wajibu wa kutozuia watu kufaidi haki zao za kikatiba kwa kufuatana.
9. Aidha, kifungu cha 26(1) sheria ya Vyama vya Siasa (Political Parties Act) inasema wazi kabisa kuwa kila chama cha siasa kina haki ya kupandisha bendera yake. Kifungu hicho kinasema:
26.- (1) A registered political party shall be entitled to own, use and hoist a flag of its party in areas or places as may be prescribed in the regulations to be made under the provisions of this Act. (Emphasis added)
Tafsiri yake ni:
26. --(1) Chama cha siasa kilichosajiliwa kina haki kuwa, kutumia na kupandisha bendera ya chama hicho katka maeneo na Sehemu ambazo zilizotajwa katika kanuni zilizotungwa chini ya vifungu vya sheria hii. (Emphasis added).
10. Hivyo kitendo cha Polisi kushusha bendera ya Chadema wilayani Mbeya Vijjini ulikuwa ni uvunjifu mkubwa wa sheria kama vile ilivyo kwa kitendo cha Jeshi la Polisi kuzuia wanachama kufanya kazi zao za kisiasa ikijumuisha maadhimisho ya miaka 33 ya kusajiliwa rasmi kuwa chama cha siasa nchini.
11. Aidha, kesi iliyofunguliwa na hao wanachama mamluki dhidi ya Chadema ni ya madai na hivyo Polisi hawana mamlaka ya kudai kuitekeleza isipokuwa tu pale kunapokuwa na amri nyingine ya Mahakama inayowaamuru kutekelezwa kwayo kutokana na maombi ya kuwakuta wale wanaodaiwa kuikiuka kuwa wametiwa hatiani na Mahakama kwa kosa la kudharau amri ya mahakama.
12. Tunapenda ieleweka kwamba, licha ya kuwa Chadema haikuridhishwa na zuio la Mahakama Kuu, lililowekwa na Jaji Hamidu Mwanga kwa kuwa tayari kuna uamuzi-banifu wa Mahakama ya Rufaa unaokataza kuwekwa zuio juu ya shughuli za kisiasa nchini bado iliheshimu amri hiyo. Mahakama ya Rufaa ya Tanzania ilitamka msimamo huo kwa uwazi kabisa zaidi ya miaka 27 iliyopita katika kesi ya Augustine Lyatonga Mrema and Others vs Abdallah Majengo and Others (Civil Appeal No. 41 of 1999) [1999] TZCA 44 (11 October 1999) ambapo ilisema:
The result of this unfortunate error was that the appellants have been denied their constitutional and civil right to engage in the political life of their country, this is because in this country political activity is not possible outside registered political parties. We also wish to observe that the High Court, even if it were minded to grant the order for injunction, should not have granted the order as prayed because it was unduly wide, bringing under its umbrella even innocent parties apart from its vagueness.
As no political activity is allowed in this country outside registered political parties, the judge's order amounted virtually to a suspension of the appellants' constitutional and civil rights. The judge should have limited her order to the main complaint against the appellants, namely usurpation of leadership positions in Tanzania Labour Party.
Tafsiri yetu ya Sehemu ya uamuzi huo tulionukuu hapo juu ni:
Matokeo ya kosa hili la kusikitisha ni kuwa warufani wamenyimwa haki zao za kikatiba na kiraia za kushiriki katika shughuli za kisiasa za nchi yao, hii ni kwa kuwa katika nchi hii shughuli za kisiasa haziwezi kufanywa nje ya vyama vya kisiasa vilivyosajiliwa. Tunapenda kusema kuwa Mahakama Kuu, hata kama ingekuwa imeshawishika kutoa amri ya zuio isingeitoa kama ilivyoombwa kwa sababu ilikuwa pana sana, na kuwaingiza ndani yake hata watu wasio na hatia yoyote kutokana na uholela wake.
Na kwa kuwa hakuna shughuli ya kisiasa inayoruhusiwa katika nchi hii nje ya vyama vilivyosajiliwa vya siasa, amri ya jaji ilifikia kiwango cha kusimamisha haki za kikatiba na za kiraia za warufani. Jaji angeikita amri yake kwa lalamiko kuu dhidi ya warufani, ambalo lilikuwa ni juu ya utwaaji wa nafasi za uongozi katika Tanzania Labour Party. (Mkazo umeongezwa)
13. Hitimisho letu ni kuwa Chadema ni chama kilichosajiliwa kihalali nchini chenye haki ya kufanya shughuli zake za kisiasa nchini kote, Jeshi la Polisi lazima lifahamu haliko juu ya sheria na halina mamlaka ya kusimamisha au kupoka haki za vyama vya siasa, wanachama wake na wananchi kwa ujumla nchini kufanya shughuli za siasa. Hakuna zuio lolote lile la Mahakama Kuu juu ya kutenda shughuli za kisiasa kwani amri yake ya tarehe 10 Juni 2025 ilikoma tarehe 10 Desemba 2025. Viongozi, wanachama, na wapenzi wa Chadema ambacho ndicho chama kikuu cha siasa nchini wana haki ya kukusanyika na kufanya shughuli za siasa na hawatakiwi kuzuiwa kufanya hivyo.
Aidha, wanachama na viongozi wa Chadema watakaokwamishwa au kuzuiwa na mtu yeyote yule kwa kisingizio chochote kile ikiwemo amri ya zuio la tarehe 10 Juni 2025 atoe taarifa mara moja kwa Kurugenzi ya Sheria na Katiba ya Chadema Makao Makuu, kwa hatua stahiki za kisheria binafsi dhidi ya mtu huyo. Tunasisitiza kuwa, Chadema itamshitaki mtu au ofisa huyo katika nafsi yake na kudai fidia ikiwa ni pamoja: na kukutwa hana sifa ya kuendelea kuwa mtumishi wa umma na fidia ya kifedha.
PEOPLES' POWER
Imetolewa leo tarehe 23 Januari 2025 Jijini Dar es Salaam.
Dr. Rugemeleza A.K. Nshala MWANASHERIA MKUU-CHADEMA