Mtoa mada (kwa kiasi kikubwa tu) na idadi kubwa ya wachangia mada hii wala hawana tofauti kubwa na Wabunge wa CCM!! Wabunge wa CCM wametawaliwa na ushabiki wa kiitikadi na kusahau wajibu wao wa msingi wa kutetea na kulinda maslahi ya taifa! Katika mada hii, ushabiki wa kichama (CDM) ndio umetawala zaidi utafikiri kilichokuwa kinafanyika ni kutafuta nani atakuwa mshindi! Ushindi si wa CCM wala CDM, bali ni wa Watanzania wapenda haki na kuona mustakabali mzuri wa taifa lao. Vyovyote iwavyo, pamoja na ushabiki wao usio na tija bado katika hili sina budi kuwapongeza hata hao wabunge wa CCM ambao walikata shauri la kujirudi na kuangalia maslahi ya taifa pale dhahiri ilipojitenga na upofu kwenye nafsi na utashi wao. Hapa picha ninayopata ni kwamba, kumbe zuri linapoletwa mezani pao hususani likitoka kwa mkuu wa kaya, basi wanalazimika kupigana kiume na kuliafiki hata kama ni kwa ushingo upande!! Suala la katiba, si lelemama, ni la kisheria zaidi kuliko kisiasa na si kama wengi wetu tunavyozani. Niwe na madigrii, kwa matani kadhaa lakini nikakosa japo ka-training ka masiku haba, basi nitalazimika kuufyata ninapokuta wenye weledi wakijadili masuala ya katiba....si jambo la kukurupukia!!! Siwezi walaumu sana wabunge wa CCM kwani kosa kubwa ambalo walifanya ni kukosa tu busara na kuamua kukurupikia jambo wasilo na weledi nalo na kisha wakaingiza itikadi hasi za kisiasa ambazo ima faima ilikuwa ni lazima aonekane nani zaidi "kati yetu; na nyinyi". Sina shaka kwamba, baada ya kupitisha muswada ule mbovu (according to wataalamu), na wabunge wale kutoka nje ya tanuri lenye joto la ushabiki (Bunge) na hatimae kurudi huku uraiani na kusikia maoni ya Watanzania; ndipo hapo wakaanza kuona nuru! Kama ilivyo ada, nuru ukimbiza giza, na kuiacha dhahiri ipate onekana kwa yeyote mwenye utashi wa kufanya hivyo hata kama ukweli bado unabaki pale pale kwamba utashi na uelewa si lazima viwe sawa na mapenzi ya kumbikumbi; kwamba lazima viende pamoja!! Na hili, ndilo lililowakuta akina Anne Kilango Malecela ambao nao si busara hata chembe kuwabeza ama kuwakejeli kwani ni lazima wawepo watu kama hawa ili maandiko yatimie....kwamba, nchi yetu ni ya kidemokrasia na kila mtu ana haki ya kutoa maoni yake ili mradi asivunje sheria za nchi! Hakuna jambo zuri hata moja ambalo litaweza kuwafurahisha Watanzania wote; mwenye kuwa nalo na alitaje! Hata hiyo Qurain tunayoamini imeteremshwa na mungu; nusu ya Watanzania hawaiamini....hali kadhalika Biblia, nayo hivyo hivyo; ije kuwa katiba!!!?!
Si hivyo tu, ukitafakari kwa makini, utabaini uwapo wa jambo ambalo kwangu sina hakika kama ni la kufurahisha ama kuhuzunisha, hata hivyo nazani itategemea unasimamia wapi! Kwamba, kama nilivyoeleza hapo awali huenda jambo liwalo lote, ili mradi linatoka kwa mkuu wa nchi basi CCM squad italiafiki hata kama ni kwa shingo upande!! Hivi ni nani atakayeleta ushabiki wa kiitikadi na kukaidi ukweli kwamba squad ile ilikuwa na uwezo wa kuyakataa mabadiliko yale kutokana na uwingi wao?! Bila shaka, hata kama ni kwa shingo upande, wakakata shauri la kutoonesha kiburi kwa mkubwa wao wa chama!! Ni nini basi ambacho ndicho haswaa kiliwasukuma wabunge wa CCM hivi sasa kuyakubali mabadiliko yale?! Walisukumwa na maslahi ya taifa au hawakutaka kuonesha jeuri kwa kiongozi wao?! Ni bora iwe walisukumwa na kuyaona maslahi ya taifa; so itakuwaje itakapoonekana ni kwamba hawakutaka kuonesha utovu wa nidhamu kwa mkuu wao? Kama hivyo ndivyo; ni nani basi aliye makini kati ya wabunge wa CCM ambao waliamua kujirudi na akina Kilango Malecela ambao waliamua kukisimamia na kukitetea walichokiamini hata kama kilienda kinyume na matakwa ya mkuu wao?! Vyovyote iwavyo, hapo ujumbe mahususi kwa kiongozi wa nchi ni kwamba ni uelekeo wa usukani wake ndio utakaotoa dira ya nchi hii! Kwamba, akileta hoja za mashiko na maslahi kwa taifa basi wabunge wake wataziafiki hata kama ni kwa shingo upande! Kinyume chake, ni maangamizo kwa mustakabali wa nchi hii endapo ataleta mafyongo ambayo pia squad yake itayapigia makofi na kuhitimisha "ndio mzee!"