Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mkoa wa Mara, Chacha Heche , ameibuka kupitia mtandao wa kijamii wa Facebook akijibu wito wa mdahalo wa kisiasa uliotolewa na Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kenani Kihongosi.
Katika ujumbe wake, Chacha Heche amesema mdahalo wa kisiasa unapaswa kuwa na vigezo vinavyoeleweka na kujikita katika masuala muhimu ya kitaifa badala ya kuwa mjadala wa maneno bila hoja zenye tija kwa wananchi.
Amesema iwapo mdahalo huo utaandaliwa kwa kuzingatia misingi hiyo, ni muhimu kujadili masuala yanayogusa maisha ya wananchi ikiwemo utawala bora, usalama wa raia, usimamizi wa rasilimali za nchi, mikataba ya kimkakati kama ile ya bandari pamoja na hali ya uchumi na ugumu wa maisha kwa wananchi.
Aidha, Chacha Heche amegusia pia suala la Tundu Lissu akisema linahitaji kuwekwa wazi kuhusu namna atakavyoshiriki mdahalo huo iwapo utaandaliwa.
Kauli ya Chacha Heche imekuja kufuatia wito wa mdahalo uliotolewa na Kenani Kihongosi wakati akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika wilayani Maswa mkoani Simiyu Machi 7, 2026.
Akizungumza katika mkutano huo, Kihongosi aliwataka viongozi wa upinzani Tundu Lissu na John Heche kujitokeza katika mdahalo wa wazi wa kisiasa ili kujadili hoja zao mbele ya wananchi.
“Nawaambia waje akae mmoja hapa, mwingine hapa kila mmoja aanze kupiga ukweli hapa. Mimi nawatamani wale, kama ni Heche njoo kaa hapa, kama ni Tundu kaa hapa, halafu tujenge hoja tuone watafika wapi, hawatakuwa na hoja watapaniki,” alisema Kihongosi.
Aliongeza kuwa Chama Cha Mapinduzi kinaamini katika kujibu hoja kwa kutumia takwimu na maelezo ya kina badala ya malumbano ya kisiasa.
“Sisi CCM hatufoki, hatugombi tunawapa data, kwa hiyo muwaambie waje tukae kwenye meza tuweke mdahalo halafu tuone hiyo battle ya hoja,” alisema.