CHADEMA: Siasa za TAKUKURU zinalenga ‘kuokoteza’ makosa (fishing expedition), Uchunguzi wao hauna nia njema

CHADEMA

JF-Expert Member
Apr 13, 2013
488
2,468
TAARIFA KWA UMMA KUHUSU KINACHOITWA UCHUNGUZI WA TAKUKURU DHIDI YA CHADEMA

Ndugu waandishi wa habari
Mnamo tarehe 27 Mei, mwaka huu, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) walitoa kauli kupitia mojawapo ya vyombo vya habari nchini kuwa wanachunguza kile kilichoitwa michango ya Wabunge wa Chama inayokatwa kwa mujibu wa Katiba, Kanuni na Miongozo ya Chama chetu na kueleza kuwa wamepokea malalamiko kuhusu ‘uwepo wa matumizi mabaya ya michango husika’.

Hivyo basi, kwa zaidi ya mwezi mmoja sasa tangu wakati huo, Chadema kimekuwa katika mawasiliano ya kikazi na taasisi hiyo kuhusu suala ambalo chama chetu, kwa kuegemea kwenye kanuni ya ‘the benefit of the doubt’, kiliamini kuwa mamlaka hiyo inafanya uchunguzi wa kitaalam na huru, kwa nia njema kwa kadri ya wajibu na majukumu yake ya taratibu za kisheria.

Kutokana na uelewa huo, Chama katika sehemu yake ya kutoa ushirikiano kwa taasisi hiyo, kiliamua kwa makusudi kutolizungumza suala hili kwenye vyombo vya habari, hata pale ambapo kulikuwa na kauli za upotoshaji kutoka kwa mamlaka hiyo na waandishi wa habari walihitaji kusikia kauli ya upande wetu. Tulifanya hivyo ili kuwapatia nafasi Takukuru kufanya uchunguzi wake na kujiridhisha.

Tofauti na msimamo huo tuliokuwa nao awali, sasa Chadema tumeamua kulizungumzia suala hili kwa njia hii, baada ya kubaini kuwa ile imani yenye shaka tuliyowapatia Takukuru imeanza kudhihirika kuwa ilikuwa si sahihi, baada ya kuona viashiria vya wazi kuwa hatua ya taasisi hiyo kuichunguza Chadema haikulenga kutekeleza taratibu na misingi ya kisheria, bali tumeanza kuona viashiria vya malengo ‘fulani’ ya kisiasa hasa kwa muktadha wa Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba, mwaka huu.

Usuli wa mawasiliano ya Chadema na Takukuru

Ndugu waandishi wa habari

Mnamo Mei 21, mwaka huu, Chama kilipokea barua kutoka Takukuru iliyokuwa na mkanganyiko kwa sababu ya kuwa na maudhui yaliyo kinyume na taratibu za kisheria ambazo zinaongoza utendaji kazi wa chombo hicho.

Katika barua hiyo, Takukuru walitutaka Chadema tuwasilishe nyaraka zifuatazo;

Taarifa za hesabu za fedha zilizokaguliwa za miaka ya fedha 2015/2016, 2016/2017, 2017/2018 na 2018/2019.

Mwongozo/Kanuni ya chama inayotoa idhini ya kuwakata fedha kwa kila mwezi waheshimiwa Wabunge wa kuchaguliwa na Wabunge wa viti maalum .

Nyaraka/ stakabadhi za Chadema kukiri kupokea makato ya fedha za Waheshimiwa Wabunge.

Muhtasari wa Chama unaoonesha makubaliano ya Chama cha Chadema ya kuwakata waheshimiwa Wabunge wa kuchaguliwa na viti maalum na makundi mengine.

Katiba na kanuni za Chadema zilizotumika kati ya mwaka 2015 hadi sasa.

Mihutasari ya vikao vya chama iliyoidhinisha kutumika kwa fedha walizokatwa waheshimiwa Wabunge.

Nyaraka za mapato na matumizi ya fedha walizokatwa waheshimiwa Wabunge.

Kulingana na muktadha wa barua hiyo na kwa kuzingatia matakwa ya kisheria, Chadema kiliwajibu Takukuru kupitia barua ya Katibu Mkuu wa Chama ya Mei 26, mwaka huu, ambayo sehemu yake ilisema;

“Hata hivyo hakuna mahala popote katika barua yako panapoeleza kuwa ofisi yako inachunguza kosa au makosa au kwamba nyaraka unazozihitaji zinahitajika kusaidia uchunguzi wa kosa kama kifungu kinavyojieleza bali ofisi “…inafanya uchunguzi kuhusiana na mambo ambayo inaaminika ofisi yako ina ufahamu nayo…” kwa mujibu wa barua yako.

“Ikiwa kuna kosa au makosa au kesi ambayo ofisi yako inafanyia uchunguzi unaweza kuwasilisha hati nyingine inayokidhi vigezo na matakwa ya kisheria na Ofisi ya Katibu Mkuu itawasiisha kwa kadri ya mahitaji. Mambo ambayo ofisi ya Katibu Mkuu ina ufahamu nayo si kosa au makosa hivyo hayaangukii chini ya kifungu au vifungu ulivyotumia kuniandikia barua yako.”


Pamoja na kuweka ‘reservations’ kupitia barua hiyo, kwa msingi ule ule wa kuipatia taasisi hiyo imani yenye shaka, Chadema ilitoa ushirikiano wote uliohitajika, ikiwemo kuwasilisha nyaraka zote hizo zilizotajwa hapo juu kama ilivyotakiwa na Takukuru na wametupatia hati ya kukiri kuzipokea. Pia viongozi wetu wa chama pamoja na wabunge wameitikia wito wa mahojiano. Hadi tunapozungumza, taasisi hiyo imehoji zaidi ya watu 60 wakiwemo wanachama wa CCM katika suala walilotuandikia wakitaka ushirikiano wetu.

Siku 6 baada ya kupokea barua hiyo ya Mei 21, Chadema ilipata mshangao baada ya kuwepo kwa taarifa za uongo na upotoshaji kwenye vyombo vya habari, zilizomnukuu Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Brigedia Jenerali John Mbungo akisema kuwa taasisi hiyo imewaita na kuwahoji viongozi wa Chadema na imepokea nyaraka kutoka kwetu.

Tunasikitika kuwaambia kuwa kauli ile haikuwa ya kweli. Tulipata wakati mgumu kuelewa nia ya kauli ile ambayo ilitolewa na msemaji mkuu wa taasisi hiyo akitambua kuwa barua iliyoandikwa kwa niaba yake ilikuwa imetutaka kuwasilisha nyaraka ifikapo Mei 28, mwaka huu na hivyo hadi wakati huo (aliponukuliwa na chombo cha habari) Chadema na Takukuru walikuwa hawajapeana wala kukabidhiana nyaraka yoyote. Kwetu hiyo ilikuwa ishara ya mapema kuanza kuelewa kuwa hakukuwa na nia njema katika hicho kilichoitwa ni uchunguzi.

Hakuna nia njema, Takukuru inafanya ‘siasa’ badala ya kufanya kazi ya uchunguzi
Kinyume na taratibu za kisheria, huku ikitambua kuwa haijawahi kututaarifu rasmi iwapo inatuchunguza wala haijajibu barua ya Chadema iliyohoji maudhui ya barua ya Takukuru ya Mei 21, mwaka huu, taasisi hiyo kupitia kwa Msemaji wao aitwae Dorice Kapwani, ilitoa kauli nyingine kupitia vyombo vya habari kuwa imewaita kwa ajili ya kuwahoji Wabunge (na waliokuwa Wabunge) wa Chadema kwa kile alichosema ni uchunguzi ambao Takukuru Makao Makuu walikuwa wanaufanya dhidi ya Chadema kuhusu alichodai ni matumizi mabaya ya fedha za michango ya wabunge.

Mbali ya kwamba hiyo ilikuwa ni kauli nyingine ya upotoshaji na uongo kutoka mamlaka hiyo, kupitia kauli rasmi kwa vyombo vya habari, kwetu sisi ilikuwa ishara nyingine pia kuwa hakukuwa na nia njema na dalili ya wazi kuwa Takukuru haikuwa inafanya uchunguzi wa kitaalam na huru, bali kulikuwa na hilo lengo la kisiasa.

Dalili ya wazi na kubwa kabisa kuwa Takukuru hii ya Brigedia Jenerali John Mbungo inafanya kazi ya siasa kwa malengo ya kisiasa, na inajipotezea fursa ya kuaminiwa kufanya uchunguzi huru na kitaalam, ilidhihirika zaidi mnamo Juni 17, mwaka huu, siku moja baada tu ya Rais John Magufuli na Mwenyekiti wa CCM, kufunga Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Siku hiyo, Takukuru kupitia kwa Mkurugenzi Mkuu wake, ilitoa kauli ya kushabikia Chama cha siasa na alienda mbali zaidi na kuwahamasisha wapiga kura kuwa wanapoenda kupiga kura mwaka huu basi wakumbuke miradi mikubwa ambayo imefanywa na Serikali ya awamu ya tano. Haya yalikuwa maelekezo kwa wananchi juu ya ni nani wakampigie kura huku akiendelea kuikandamiza Chadema kwa kuonyesha kuwa kuna matumizi mabaya ya fedha za michango ya Wabunge ili kukikosesha Chadema imani na kuharibu taswira yake kwa wananchi ambao ni wapiga kura.

Si hivyo tu, hata msingi wa hiki kinachoitwa ni uchunguzi, ni kauli zilizotolewa kisiasa, kwa malengo ya kisiasa na waliokuwa Wabunge wa Chadema, ambao baada ya kufukuzwa au kujiondoa wenyewe na kujiunga na mahasimu wetu wa kisiasa. Kuanzia hapo Takukuru ikazidandia na kuita kuwa ni malalamiko.

Ikiwa hiyo haitoshi, katika wakati wote wa mahojiano ambayo Takukuru wamekuwa wakifanya dhidi ya Viongozi wa Chadema na Wabunge wetu, taasisi hiyo imekuwa ikifanya ‘media shows’ kwenye suala hili. Hatujawahi kuona chombo cha dola, kinafanya uchunguzi wa siri, kitaalam na huru, kwa namna hii. Ukiangalia kwa undani, jambo hilo lilikuwa na hilo ‘lengo’ la kisiasa kama tulivyosema hapo awali.

Siasa za Takukuru zinalenga ‘kuokoteza’ makosa (fishing expedition)

Ndugu wanahabari

Hivi karibuni, Juni 27, mwaka huu, Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, alitoa taarifa kwa Vyombo vya Habari kuwa taasisi hiyo wamemaliza uchunguzi waliokuwa wanafanya dhidi ya Chadema juu ya matumizi mabaya ya fedha za michango ya Wabunge na walikuwa wamebakiza uchambuzi wa nyaraka kuhusiana na michango hiyo.

Huku kukiwa na kauli ya msemaji mkuu wa taasisi hiyo kuwa wameshahitimisha uchunguzi, ghafla, katika hali ya kuendeleza na kudhihirisha kuwepo kwa lengo la kisiasa, Takukuru wametuandikia barua nyingine Juni 29 na 30, mwaka huu, ambayo ukiisoma inajibainisha wazi kabisa kuwa inalengo la kufanya kile kinachoitwa katika taaluma ya kisheria, ‘fishing expedition’, kwa tafsiri ya haraka ni ile hali ya kuokota okota au kuokoteza makosa, pengine baada ya kukosa kosa/makosa kwenye uchunguzi waliotangaza kuwa walikuwa wanaufanya kwa malengo wanayoyajua wao.

Jambo la kushangaza zaidi, hata baada ya kauli hiyo kuwa wamekamilisha uchunguzi, wametuletea barua tatu mfululizo na miongoni mwa vitu wanavyovitaka ni pamoja na nyaraka mbalimbali za Chama za kuanzia mwaka 2014 hadi mwaka 2020.

Kitendo cha Takukuru kuomba nyaraka za mipango na vikao vya chama vikiwemo vikao vya kimkakati na vyenye mbinu na mipango yetu ya kuiondoa CCM madarakani, imetuongezea shaka kuwa sasa Takukuru nayo imeingia kwenye kutekeleza kauli iliyotolewa na Katibu Mkuu wa CCM kuwa watatumia vyombo vya dola kuendelea kubakia madarakani.

Kwa mwenendo huu wa Takukuru ambapo wamekuwa wakitueleza kuwa uchunguzi huu ni wa siri, wanaleta hati zikiwa na mihuri ya siri na wanatutaka sisi kutunza siri lakini wao Takukuru wanatoa taarifa kwa umma, inazidisha shaka kuwa tukiwapatia nyaraka za mipango na mikakati yetu tangu mwaka 2014, Chama hakitakuwa salama kwenye mipango yake kwani inaweza kuangukia mikononi mwa mahasimu wetu wa kisiasa .

Kutokana na hali hiyo, Chadema kimeiandikia barua Takukuru, kupitia Katibu Mkuu wa Chama ya Julai 1, ikijibu barua hiyo ya Juni 29, ambapo Chadema pamoja na kufanya rejea ya barua zingine zote za Takukuru tangu Mei 21, mwaka huu na yote ambayo yamejiri tangu wakati huo ambayo moja baada ya jingine, yamekuwa yakidhidhirisha kuwepo kwa lengo la kuokoteza makosa kwa lengo la kisiasa, imeeleza yafuatayo;

Hadi sasa Takukuru haijaeleza kosa au makosa ambayo inayachunguza kwa mujibu wa kifungu cha 10(1) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na. 11/2007 jambo ambalo Chadema ililieleza mapema kwenye barua ya Mei 26/5/2020.

Hadi sasa Chadema imeshatoa nyaraka nyingi pamoja na mahojiano mbalimbali yanayohusu fedha za michango ya wabunge, lakini kwa lengo ambalo halijaelezwa, ghafla tunaona wameanza kutaka nyaraka ambazo hazihusiani kabisa na suala walilodai kupitia vyombo vya habari kuwa wanafanyia uchunguzi.

Wigo wa hicho kinachodaiwa uchunguzi hakioneshi kikomo wala kosa/makosa ambayo taasisi hiyo inachunguza hadi sasa kama Chadema ilivyohoji katika barua ya tarehe 26/05/2020.

Kutokana na mazingira ya kisiasa ya sasa nchini, hususan kwa kuzingatia kuwa Chadema kiko kwenye maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa Nchi, 2020, kinapata wakati mgumu kuendelea kutoa ushirikiano kwa Ofisi ya Takukuru Makao Makuu bila kufahamu ukomo wa uchunguzi au jambo mahsusi au kosa/makosa wanayoyachunguza.

Chama kinatatizwa zaidi kwa namna ambavyo Takukuru inaliendesha suala hili kisiasa kwa kauli za kisiasa, zinazotolewa na wakuu wa chombo hicho, badala ya kuongozwa na utaratibu wa kisheria na taaluma ya uchunguzi.

Chama kimeitaka Takukuru kufuata taratibu za kisheria katika kuendelea na huo uchunguzi wao ambao haujulikani mawanda yake na wala utaisha lini, huku tukiwataka waache kutoa kauli za ushabiki wa kisiasa na ambazo zinaifanya taasisi hiyo kupoteza imani kwa wananchi.

Tumewataka Takukuru watujulishe rasmi na kwa mujibu wa sheria kuhusu wanachokichunguza kama kipo, ili tuweze kuendelea kuwapa ushirikiano.


Imetolewa leo Alhamis, Julai 2, 2020

Chadema, Makao Makuu.
PIa soma;

TAKUKURU yaanza kuichunguza CHADEMA kwa tuhuma za matumizi mabaya ya fedha

TAKUKURU kuwahoji Wabunge 69 kuhusu matumizi ya pesa za CHADEMA
 
Takukuru wanachezea kodi za wananchi. Hii taasisi ibomolewe yote.


Imeshindwa kuchunguza mabilion ya vitambulisho vya wajasiriamali zinazokusanywa kila mwaka kutoka jasho la wanyonge, wao wanachunguza michango ya wabunge ambayo walitoa kwa ihali yao.
 
Mnacho kiogopa ninini!!
Kama mpo wasafi shida nini
tatizo ni kuwa mmejificha kwenye Siasa Wakati wote ni wahuni na wachumia tumbo tu
na hampendi kukosolewa kwa lolote
Viongozi Wenu ni Miungu mtu
no kuhoji maamuzi au jambo lolote
 
Mnacho kiogopa ninini!!
Kama mpo wasafi shida nini
tatizo ni kuwa mmejificha kwenye Siasa Wakati wote ni wahuni na wachumia tumbo tu
na hampendi kukosolewa kwa lolote
Viongozi Wenu ni Miungu mtu
no kuhoji maamuzi au jambo lolote
Yes. Ni vita. Wanapigwa kila kona. CHADEMA be vigilant. You will emerge out triumphantly. Kinachosumbua ni Uchaguzi Mkuu ujao.
 
Back
Top Bottom