Zak Malang
JF-Expert Member
- Dec 30, 2008
- 5,404
- 236
CHADEMA, CUF: Mpinzani halisi atajulikana kesho
Na Yusuf Aboud
NIMEMSIKILIZA vema Hamad Rashid Mohammed, Mbunge wa Wawi, akizungumza katika mdahalo wa wazi ulioandaliwa na Vox Media na East Africa Business and Media Training Institute (EABMTI), kwa ufadhili wa ITV, mwishoni mwa wiki.
Katika mdahalo huo, alikuwa akichuana na Kiongozi wa kambi ya Upinzani bungeni, Freeman Mbowe, ambaye pia ni mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Majadala ulihusu mwelekeo wa upinzani, na waliulizwa maswali mengi kwa pamoja, kubwa likihusu azima yao kuungana ili kuwa na upinzani imara.
Lakini Hamd Rashid alipotosha wasikilizaji katika hoja nyingi alizojenga, huku akishangiliwa na kundi la mashabiki wake, kuhusu haja ya wapinzani wote kuungana.
Kwanza, alikosea kusema CUF inakataa kuunda kambi na CHADEMA kwa sababu wao wanaitambua serikali, na CHADEMA haiitambui serikali.
Lakini palepale, Mwenyekiti wa CHADEMA aliposema chama chake kinaitambua serikali, bali kinashinikiza mabadiliko makubwa ya kimfumo, alikuwa ameimaliza nguvu hoja ya Hamad Rashid.
Lakini upotoshaji wa Hamad Rashid unasisitizwa na ukweli kwamba anajipendekeza kwa CCM. Zipo sababu. Kwa miaka 15 mfululizo, CUF hawakuitambua serikali ya Zanzibar. Lakini waliunda upinzani ndani ya Baraza la wawakilishi, chini ya uongozi wa Abubakari Khamis Bakari.
Pili, kwa muda wa miaka 15 CUF hawakuitambua serikali ya Zanzibar inayoundwa na CCM. Lakini, katika Bunge la Muungano, waliweza kushirikiana na CHADEMA na vyama vingine ambavyo havikujiingiza katika mgogoro wa Zanzibar. Sasa huu unafiki wa sasa wa CUF unatoka wapi?
Tatu, Hamad anataka upinzani ushirikishe vyama vyote vya upinzani bungeni. Lakini mwaka 1995, CUF walishirikiana na UDP na kuacha NCCR-Mageuzi nje ya kambi, huku wakijua NCCR-Mageuzi ilikuwa na wabunge 19; na CUF haikuwa na mbunge hata mmoja kutoka Bara.
Fatuma Maghimbi ndiye alikuwa kiongozi wa upinzani na John Cheyo naibu wake. Sasa kama aliweza kuacha vyama vingine nje, kwa nini analazimisha CHADEMA waingize vyama vingine katika kambi yao?
Hamad Rashid anataka gari, nyumba, posho na kuwatumia wabunge wa CCM kushinikiza mabadiliko ya baadhi ya vifungu vya kanuni za Bunge. Analilia posho na marupurupu kutoka serikalini, ambayo ameyafaidi kwa miaka mingi iliyopita.
Hakuwa amefikiria kwamba CHADEMA wangeweza kupata wabunge wengi wa kutosha kukiondoa chama chake katika uongozi wa upinzani. Sasa anataka kufuta kifungu kilekile ambacho alikiasisi mwenyewe wakati CUF kikiwa na wabunge wengi kuliko vingine.
Lakini kinachomuuma zaidi ni kwamba viongozi wenzake wa CUF, huko Visiwani, walijiandaa kuingia serikalini, wakati yeye akijiandaa kuendelea na uongozi wa upinzani bungeni.
Inamuuma kwanza yeye kakosa, wenzake wamepata; na sasa anataka kubadilisha vifungu ili kujipatia fursa nyingine. Kwa nini tusiseme anaonyesha ubinafsi wa hali ya juu?
Kifungu ambacho Hamad anashinikiza kubadilishwa ni kanuni ya 14 (3), 14 (4) na 113 (11) za Kanuni za Bunge za mwaka 2007.
Kanuni ya 14 (3) ambayo CUF na washirika wake wanashinikiza kubadilishwa inataka chama cha upinzani kitakachoruhusiwa kuchagua kiongozi wa upinzani bungeni, kiwe na wabunge wasiopungua asilimia kumi na mbili ya wabunge wote.
Vyama vya CUF, NCCR- Mageuzi na TLP vina wabunge 42 ambao hawakidhi matakwa hayo ya sheria, huku CUF ikiongoza kundi la vyama hivyo kwa kuwa na wabunge 36.
Kanuni za Bunge kwanza zinatoa fursa ya chama chenye wabunge wengi, kabla ya kuzungumzia muungano wa vyama. Anataka kuondoa maneno Kambi rasmi ya upinzani bungeni ili kuipora CHADEMA haki yake ya kushikilia nyadhifa za uongozi ndani ya Bunge.
Kwa mujibu wa kumbukumbu za Bunge, Hamadi mwenyewe ndiye alipendekeza maneno kambi rasmi ya upinzani bungeni.
Kumbukumbu za Bunge zinaonyesha kuwa Kamati ya Kanuni ilikuwa chini ya uongozi wa Job Ndugai ambaye sasa ni naibu spika wa Bunge.
Wakati ule, Bunge lilikuwa linafanyia marekebisho kanuni za mwaka 2002, na kwamba kuwekwa kwa neno kambi rasmi kulitokana na Hamad kushindwa katika uchaguzi wa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC).
Alishindwa na John Cheyo ambaye wakatio huo hakuwa katika kambi ya upinzani iliyokuwa inaundwa na CUF pekee.
Nne, Hamad amewasaidia Watanzania kutambua kirahisi kwamba hivi sasa, chama cha upinzani kilichobaki Tanzania, ni CHADEMA.
CCM inashambulia CHADEMA. CUF wanashambulia CHADEMA. NCCR-Mageuzi wanashambulia CHADEMA. TLP wanashambulia CHADEMA. UDP wanashambulia CHADEMA.
Na katika mazingira ambamo CUF ina ushirikiano wa kikatiba na CCM, huko visiwani, chama hicho kinapoteza sifa na nguvu ya kuwa chama cha upinzani kinachopaswa kuaminiwa na wapinzani wa kweli.
Wala hakina haki ya kweli ya kushinikiza kushirikishwa katika masuala ya upinzani, kwa maana kitawahujumu. Hakitaweza kutunza siri za wapinzani.
Na hata kama Hamad Rashid angependa kuzitunza, kwa maelezo kuwa Zanzibar wana katiba yao, serikali yao, mahakama yao; na kwamba masuala ya Muungano yazingatie msingi tofauti, ukweli unabaki kuwa Katibu Mkuu wa CUF ni mmoja, na ndiye anaandaa mikutano ya vikao vyote vikuu vya chama; na ndiye kiongozi mkuu mwenye sauti kuu kuliko wote; na huyuhuyu ndiye Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.
CUF kinamuamini Seif kwa sababu ni kiongozi wake. Kwanini kinalazimisha CHADEMA nao wamuamini Seif?
Na ingawa alitaka kutushawishi Watanzania tuwalazimishe CHADEMA iwashirikishe wabunge wa vyama vingine, Hamad Rashid hajui kwamba hawezi kusemea vyama vingine?
Lakini kikubwa zaidi, hajui kwamba wanasiasa hawa wanaoshirikiana na CCM kukichukia CHADEMA, wanapata wapi ujasiri wa kutaka CHADEMA kiwaamini? Na kama hawaaminiani, kwa nini wanafikiri kwamba wanaweza kuunda ushirikiano ukadumu, bila kuhujumiana?
Je, CUF rafiki wa CCM kiutawala, anaweza kukaa meza moja na CHADEMA wakakipinga CCM kwa dhati? Haiwezekani. Na CHADEMA kama wanajua, ni vema waendeelee na msimamo wao, waongoze upinzani, wahamasishe umma.
Na wala CHADEMA wasitumie mfano wa ushirikiano wa CHADEMA na CCM Kigoma (2005-2010) kama kisingizio. Huu wa CUF na CCM ni wa kikatiba; na wote wako madarakani. Wamegawana vyeo, wakaridhika.
Kule Kigoma, CHADEMA na CCM walitofautiana, walipingana; na hawakuongoza serikali moja kwa wakati mmoja, bali walipeana miaka miwili na nusu kila chama.
Tusidanganyane. Vyama hivi havina nia moja. Haviaminiani. Kinachounganishwa ni nia, si idadi ya wabunge. Hawa hawana nia moja. Wanahujumiana. Na wengine wanatumiwa na CCM kumaliza nguvu za upinzani.
Ushauri wangu ni huu: Kila chama kiende vyake. Mpinzani wa kweli atajulikana baadaye.
Chanzo; MwanaHALISI.