na Mwandishi wetu
SIKU moja baada ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), John Chiligati, kueleza mkakati wa kutaka kuwaondoa bungeni wabunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), chama hicho tawala sasa kinajiandaa kuleta hoja binafsi kuwaondoa wabunge wa CHADEMA, Tanzania Daima Jumapili imeelezwa.
Habari za uhakika ambazo Tanzania Daima Jumapili imezipata kutoka ndani ya CCM, zilisema chama hicho kimetoa maagizo kwa wanasheria wake ili waandae hoja binafsi itakayowasilishwa bungeni na mwanasheria, Andrew Chenge, kisha kupiga kura ya kutaka wabunge hao waondolewe bungeni.
Mchezo uliopangwa kufanyika ni kama ule aliofanyiwa Zitto Kabwe alipotoa hoja ya Buzwagi. Licha ya utetezi wake mzuri, aliondoka. Safari hii kazi hii atapewa Chenge, tumepania lazima wabunge wa CHADEMA waondoke bungeni hadi hapo watakaposema wanamtambua rais, alisema mmoja wa makada wa CCM.
Kwa mujibu wa habari hizo, mpango huo unasubiri baraka za Katibu Mkuu, Yusuf Makamba, ambaye alitarajiwa kuwasili jijini Dar es Salaam jana baada ya kuwa nje ya ofisi yake kikazi.
Kada huyo alipohojiwa ni kifungu gani cha Katiba au cha kanuni za Bunge kilichovunjwa, alishindwa kujibu, lakini alisisitiza kuwa chini ya mkakati huo, CCM itahakikisha inamtumia spika wake mtiifu, Anne Makinda, kuhakikisha wabunge wa CHADEMA wanashughulikiwa.
Hakuna kitu kilichomuumiza rais kama kitendo cha wabunge wa CHADEMA kusimama na kuondoka kwa dharau. Bora wasingekuja bungeni na katika hilo chama kimedhamiria, Bunge lijalo moto utawaka, alisema mpashaji habari huyo.
Wakati mkakati huo ukisukwa, CCM Mkoa wa Dar es Salaam, jana iliitisha mkutano na waandishi wa habari kueleza mkakati wake wa kutaka kufanya maandamano ya kulaani kitendo cha wabunge wa CHADEMA kususia hotuba ya Kikwete.
Licha ya kwamba gazeti hili halikualikwa kwenye mkutano huo, taarifa zilizotufikia baadaye zilisema kuwa uongozi wa CCM taifa uliingilia kati na kuamuru maandamano hayo yasifanyike leo hadi watakapopata maelekezo mengine.
CCM juzi ililazimika kutoa taarifa mbili tofauti, moja ikitolewa na Kaimu Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana (UVCCM), Beno Malisa na nyingine ikitolewa na Chiligati, kulaani kitendo hicho na kuahidi kuchukua hatua dhidi ya wabunge wa CHADEMA.
Tamko lililotolewa na Chiligati lilieleza kuwa kitendo hicho cha CHADEMA ni cha uasi na uhaini dhidi ya demokrasia na utawala wa nchi.
Chiligati alisema CHADEMA wanapaswa kutambua kuwa zoezi la uchaguzi lilishuhudiwa na waangalizi wa ndani na nje ya nchi na wameishatoa taarifa kuwa uchaguzi ulikuwa huru na wa haki.
Waangalizi wa uchaguzi walishatoa taarifa kwamba uchaguzi ulikuwa huru na wa haki, sasa iweje CHADEMA peke yao kutotambua matokeo kama si uchochezi unaoweza kusababisha uvunjaji wa amani na kuleta vurugu nchini? alihoji Chiligati katika taarifa hiyo.
Alisema kwa mujibu wa sheria na Katiba ya nchi, matokeo ya rais yakiwa yametangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) hayapaswi kuhojiwa na mahakama wala chombo chochote, hivyo rais yuko madarakani kwa matakwa ya Katiba hiyo.
Sasa madai ya CHADEMA kwamba iundwe tume huru ya uchaguzi ichunguze nini?...Nia yao wanataka tuache kazi ya kushughulikia maendeleo ya wananchi ili tuingie katika mgogoro wa kikatiba utakaodumu kwa muda mrefu na kuiingiza nchi katika misuguano na mzozo wa kisiasa? aliuliza.
Alieleza kuwa chama hicho kimeshangazwa na kitendo cha chama hicho kukubali matokeo ya ubunge na madiwani na kuacha kutambua ya urais, wakati uchaguzi ulifanyika kwa siku moja na kusimamiwa chini ya chombo kimoja kinachodaiwa kuendesha uchakachuaji.
Tunawasihi CHADEMA waache unafiki, wasiisingizie NEC. Wanalalamikia kura za urais pekee na si za wabunge wala madiwani... kama NEC ilichakachua matokeo ya urais kwa manufaa ya CCM, ilishindwaje kufanya hivyo kwenye kura za wabunge na madiwani? ilihoji taarifa hiyo.
Chiligati alieleza kuwa walichofanya wabunge wa CHADEMA kususia hotuba ya Rais Kikwete ni kumridhisha Dk. Willbrod Slaa ambaye hana shughuli za kufanya kutokana na kukosa urais na kushindwa kugombea ubunge.
Alisema wabunge hao wamevunja katiba kutokana na kitendo chao cha kutomtambua rais aliyewaweka madarakani kwa mujibu wa kiapo walichokula, hivyo hawastahili kuwepo ndani ya Bunge.
Tunawashauri wajiondoe bungeni haraka, vinginevyo wajiandae kuondolewa kwa Azimio la Bunge hadi hapo watakapogundua kwamba rais yupo, na serikali ipo, alisema.
Alieleza kushangaa kuona chama hicho kinapingana na madai yao ya kwamba ni wavumilivu wa kisiasa na wanalinda amani, hali kitendo cha kukacha hotuba ya rais ni wazi kuwa wanaandaa wafuasi wao kuweza kuleta vurugu na uvunjifu wa amani nchini.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Benno Malisa, amelaami kitendo hicho na kusema ni ishara ya utovu wa nidhamu kwa wapiga kura waliowachagua.
Lakini CHADEMA kwa nyakati tofauti, wamesema kuwa CHADEMA haisemi haimtambui Kikwete kama Rais wa Tanzania, bali haiyatambui matokeo ya uchaguzi yaliyompa Kikwete mamlaka ya kuwa rais, wakimfananisha na marais wa nchi nyingine wanaotumia mbinu mbalimbali kuupata urais bila ridhaa ya wananchi wanaowaongoza.
Wanasisitiza kuwa Rais Kikwete amewekwa madarakani na Tume ya Uchaguzi, si wapiga kura; na kwamba hawaongelei matokeo ya kura za ubunge kwa sababu sheria inaruhusu kuhoji matokeo ya ubunge kwenye vyombo vya kisheria.
Katika majimbo ambayo CHADEMA haikuridhika na matokeo, inatarajiwa kuyapinga mahakamani. Lakini kwa kuwa sheria haziruhusu kuhoji matokeo ya urais mara Tume ya Uchaguzi ikishayatangaza, jitihada pekee zinazoweza kutumika ni za kisiasa.
Na licha ya CCM kusisitiza kwamba CHADEMA imevunja Katiba, wameshindwa kuonyesha kifungu cha Katiba kilichovunjwa, huku Mnadhimu Mkuu wa Upinzani Bungeni, Tundu Lissu, akisema hawajavunja Katiba.
Hata hivyo, uamuzi huu wa CHADEMA kususa matukio yanayomhusisha rais umemfadhaisha na kumsumbua rais mwenyewe na CCM mbele ya umma na macho ya kimataifa.
Tanzania Daima 21/11/2010
CCMinachofanya ni kutafuta huruma ya wananchi mbumbumbu wasiojua sheria ili waisapoti itakapofanya uhaini wowote, hakuna kipengele kwenye katiba au kwenye kanuni za bunge kinachoweza kuwawezesha kuwatimua chadema, otherwise wajue kuwa wananchi wameamka si kama ilivyokuwa hapo awali.