Rushwa yatanda chaguzi za CCM
2008-09-05 09:23:29
Na Futuna Seleman
Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimesema kimepokea taarifa kwamba, kuna baadhi ya wagombea wake ambao wameanza kujihusisha na mambo yanayoashiria rushwa, ikiwemo kuzunguka mikoani na wilayani kujitangaza wakati majina yao hayajateuliwa na vikao kwa ajili ya kugombea uongozi wa jumuiya za chama hicho.
Chama hicho hivi sasa kipo katika mchakato wa chaguzi za jumuiya zake katika ngazi mbalimbali.
Chaguzi hizo zinazohusisha jumuiya za Vijana, Wanawake na Wazazi zinatarajiwa kukamilika Novemba, mwaka huu katika ngazi ya taifa.
Taarifa ya tamko la CCM kuhusu chaguzi za jumuiya zake lililotolewa kwa vyombo vya habari jana na kusainiwa na Naibu Katibu Mkuu, Kapteni George Mkuchika, lilisema baadhi ya wagombea wanakwenda mikoani na wilayani kuwarubuni wajumbe.
Aidha ilielezwa kwamba wengine wanatuma wapambe na kuwagharimia kwa kila kitu kuzunguka nchini kote kwa niaba yao kwenda kuwanadi, kugawa bahasha au takrima kwa wajumbe.
Kapteni Mkuchika aliongeza kuwa wagombea wengine wanapakana matope, mambo ambayo ni kinyume kabisa cha maadili ya Chama hicho.
``Sisi katika CCM tunaamini kwamba viongozi wazuri na watakaoweza kukisaidia chama ni wale tu watakaochaguliwa bila ya rushwa, kwani viongozi waliochaguliwa kwa njia hiyo hawawezi kukisaidia chama kwa kuwa hawawezi kukemea rushwa na badala yake wenyewe watakuwa sehemu ya tatizo kwa jumuiya zao na chama kwa jumla,`` aliongeza Kapteni Mkuchika.
Kufuatia hali hiyo, alisema chama hicho kimewapiga marufuku wagombea wote wa nafasi za uongozi katika jumuiya zake na wapambe wao kuzunguka mikoani na wilayani kujinadi au kumnadi mgombea yeyote, pamoja na kuacha kujihusisha na vitendo vya rushwa ya aina yoyote.
Pia CCM kimewapiga marufuku wagombea kutoa takrima au bahasha kwa wajumbe, kutumia lugha za kupakana matope katika kipindi chote cha mchakato hadi uchaguzi wenyewe na kuonya kuwa yeyote atakayebainika kujihusisha na vitendo vilivyo kinyume cha maadili ya chama, uteuzi wake utatenguliwa wakati wowote.
Pia CCM imeziagiza kamati za maadili za chama hicho katika ngazi zote kuchukua hatua mara moja na bila ya kuchelewa kwa watakaaobainika kujihusisha na vitendo hivyo.
* SOURCE: Nipashe