CCM Simiyu Yaridhishwa na Utkelezaji wa Miradi ya RUWASA Inayotekelezwa Ndani ya Mkoa wa Simiyu

Stephano Mgendanyi

JF-Expert Member
May 16, 2020
1,900
944
KAMATI ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Simiyu imeridhishwa na utekelezaji wa miradi ya Maji inayofanywa na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Mkoani humo ikiwa ni Utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2020-2025 ya kuhakikisha ifikapo mwaka 2025 huduma ya upatikanaji wa maji vijijini unafikia asilimia 85.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Simiyu, Shemsa Mohamed kwa nyakati tofauti baada ya kutembelea Mradi wa Uchimbaji Bwawa na kisima Kijiji cha Lukale Wilaya ya Meatu, Mradi wa Utafiti wa Maji chini ya ardhi katika Kijiji cha Mwaswale wilaya ya Itilima, Mradi wa Maji Byuna na Matongo wilaya ya Bariadi na Kadoto wilayani Maswa.

Alisema RUWASA mkoa wa Simiyu imekuwa ikifanya kazi kubwa sana ya kusambaza maji kwa wananchi katika maeneo ya vijijini na miradi hiyo waliyoitembelea inatafsiri dhamira ya dhati ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ya kumtua mama ndoo kichwani.

Alisema kuwa miradi ya maji ni muhimu sana kwa wananchi hivyo inapaswa kukamilika kwa wakati ili iwanufaishe wananchi kwa kuzingatia ya kuwa maji hayana mbadala lakini changamoto tulizoziona zinatokana na wakandarasi wanaopewa kazi ya kutekeleza miradi hiyo.

“RUWASA mkoa wa Simiyu mnafanya vizuri sana katika miradi yenu na katika miradi hii tuliyoitembelea sisi wajumbe wa kamati ya siasa ya CCM mkoa wa Simiyu tumerishwa nayo, Rais Dk. Samia Suluhu analeta fedha nyingi katika miradi ya miradi ya maji tunachotaka maji yafike kwa wananchi katika baadhi ya miradi tumeona Ruwasa mnaangushwa na hawa Wakandarasi,” alisema na kuongeza.

“Wasimamieni hawa Wakandarasi wafanya kazi vizuri na kwa wakati…nikuagize Mkuu wa mkoa wa Simiyu Kaka yangu Dkt Yahaya Nawanda wale wakandarasi wanaotusumbua katika miradi yetu tunayowapa ndani ya mkoa ni kutowapatia kazi nyingine tena kwenye mkoa wetu maana wamekuwa wanatukwamisha kutokana na kutokamilika kwa miradi kwa wakati,” alisema.

Pia alitumia fursa hiyo kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu kwa kuendelea kuleta fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maeneo katika mkoa huo ikiwemo miradi ya maji.

Aidha aliwaomba wananchi ambapo kwenye maeneo yao kuna miradi ya maji iliyojengwa na serikali au wadau wengine wa maendeleo waitunze na wasiihujumu miundombinu yake kwani ni kwa ajili ya manufaa yao na wakumbuke maji hayana mbadala na pia miradi hiyo imekuwa ikitumia fedha nyingi katika kuijenga.

Awali wajumbe wa kamati ya Siasa walipata taarifa za utekelezaji wa miradi hiyo kwa nyakati tofauti tofauti kutoka kwa wasimamizi wa miradi hiyo ya maji ambao ni Mameneja wa RUWASA wa wilaya.

Meneja wa RUWASA wilaya ya Meatu, Mhandisi David Kaijage amesema kuwa utekelezaji wa Mradi wa Uchimbaji wa Bwawa na Kisima katika kijiji cha Lukale kilichoko Kata ya Bukundi umekamilika na utawanufaisha wakazi 2125 wa kijiji hicho.

“Bwawa tulilochimba lina ujazo wa lita mil. 4.2 ambalo litawezesha eneo la kisima kuwa na maji yasiyo na chumvi nay a kutosha na kisima kilichochimbwa kina urefu wa mita 20 za kufungwa pampu ya mkono,”alisema.

Alisema kuwa kwa wilaya hiyo hali ya upatikanaji wa maji maeneo ya vijijini ni asilimia 60.1 hadi kufikia mwezi Machi mwaka huu na kwa sasa wanafanya kazi ya uboreshaji wa vyanzo vya maji katika maeneo ya Mwangwila, Mwabuzo, Mwabalebi, Mwamanimba na Isengwa na miradi mipya ya visima vimechimbwa katika kijiji cha Bulyashi na Mwamangongu na jumla ya Shilingi mil. 500 zinatarajia kutumika kazi miradi yote hiyo.

Naye Meneja wa RUWASA wilaya ya Itlima, Mhandisi Hussein Yahaya amesema kuwa Mradi wa utafiti maji chini ya ardhi na uchimbaji wa kisima kirefu katika kijiji cha Mwaswale chenye urefu wa mita 100 umekamilika.

Alisema lengo la mradi huo ni mpango wa muda mfupi ni kujenga mradi mdogo utakaotumia nishati ya jua na utakuwa na kituo kimoja cha kuchotea maji chenye jumla ya koki 10 na katika mwaka ujao wa fedha 2024/2025 watajenga mradi mkubwa wa maji ambao utahudumia vijiji vinne vya Mwaswale, Nkuyu, Ndolelezi na Gambasingu kwa gharama ya Shilingi Mil. 100.

Mhandisi Hussein alisema mradi huo utakapokamilika utawasaidia wananchi kupata maji safi na salama na kupunguza magonjwa yatokanayo na kutumia maji yasiyo salama na kupunguza adha ya wananchi kutembea umbali mrefu kutafuta maji badala yake kupata muda wa shughuli zingine za uzalishaji mali.

Meneja wa RUWASA wilaya ya Bariadi, Mhandisi Emmanuel Luswetula alisema kuwa mradi wa maji wa kijiji cha Matongo utagharimu kiasi cha Shilingi Mil. 528 na utawanufaisha wakazi 3200 wa kijiji hicho na ulipaswa kukamilika tangu Okotoba 30 mwaka huu lakini mkandarasi amechelewa hivyo utakamilika Mwishoni mwa mwezi Desemba.

Pia alisema kuwa Mradi wa maji wa Mwadobana katika kijiji cha Byuna utagharimu kiasi cha Sh Milioni 586 na tayari umeshaanza kutumika na wananchi wa eneo hilo wanapata maji safi na salama.

Mkuu wa mkoa wa Simiyu, Dkt. Yahaya Nawanda alimhakikishia Mwenyekiti wa CCM mkoa huo kuwa atasimamia fedha zote zinazoletwa na serikali kwenye mkoa huo kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwemo miradi ya maji ili ziweze kufanya kazi iliyokusudiwa kwa manufaa ya wananchi.

“Nikuhakikishie Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Simiyu, mimi Mkuu wa mkoa wa Simiyu Dkt. Yahaya Nawanda ndiye msimamizi mkuu wa miradi yote ya serikali ya mkoa huu najitolea kwa nguvu zangu zote kuhakikisha fedha yote inayoletwa na serikali kwa ajili ya miradi ya maendeleo inafanya kazi iliyokusudiwa,” alisema.

MWISHO.

IMG-20231127-WA0018.jpg
IMG-20231127-WA0019.jpg
IMG_3863.JPG
IMG_3223.JPG
IMG_3478.JPG
IMG-20231127-WA0017.jpg
IMG-20231127-WA0020.jpg
 
Back
Top Bottom