Leo nimeona "live" katika bunge wakati wa majumuisho ya bajeti ya Wizara ya fedha, kuna mbunge (sikumbuki jina) alisimama kumtetea mtu wa jimboni kwake kuwa alidhulumiwa wakati wa "uhujumu uchumi" na amekuwa anahangaishwa kulipwa madai yake na mwisho akaambiwa amechelewa. Mbunge huyo alisema kama kuchelewa alikuwa hajachelewa kwani anadai siku zote na ushahidi upo. Ndipo aliposimama Naibu Waziri wa Fedha na kumtaka huyo mbunge kuwa awasilishe madai yake yote kwake na karatasi zake zote na anaahidi kushughulikia hilo na kuhakikisha haki inapatikana kwani ni kweli wengi walidhulumiwa wakati wa (operesheni) ya Uhujumu Uchumi.
Ikumbukwe kuwa hii operesheni ilifanyika wakati marehemu Nyerere akiwa Rais na marehemu Sokoine akiwa Waziri Mkuu.
Huyo mbunge alisema kuwa wapo pia waliolipwa kwa kuonekana kweli walidhulumiwa.
Sasa nnajiuliza, na tusichangie hili kwa jazba, Ikiwa serikali inakiri tena bungeni, watu walidhulumiwa, jee ni hatua gani wale waliodhulumiwa wazee ambao wameshakufa ili kudai haki zao, si kurudishiwa tu mali zao na hukumu ipi "posthumous" inayoweza kutolewa kwa waliodhulumu?
Tukumbuke watu walidhulumiwa si katika uhujumu uchumi tu, kama Serikali ilivyokiri leo bungeni bali pia kuna watu waliodhulumiwa wakati wa Azimio la Arusha. Nao wakati wa Mwinyi waliambiwa wakadai lakini kwa kuwa haikutangazwa sana wengine walipoenda wakaambiwa wamechelewa, hivi haki ya mtu kweli ina kuchelewa katika kuidai?
Kwanza nnaisifu sana Serikali ya awamu hii kwa kukiri hilo bungeni "live" kuwa kweli kuna dhuluma ilitendeka. Kwa hakika Serikali kukiri hilo kosa ni ujasiri mkubwa sana na ni njia nzuri sana ya wananchi waliodhulumiwa kuweza kurudisha imani kwa Serikali yao na sasa wapokelewe na kurudishiwa mali zao na kusiwe na hili suala la kuchelewa.
Naipongeza Serikali kwa hilo, na lisiishie hapo watutangazie tuanzie wapi? Kwani nnaamini si wengi waliosikia hilo bungeni kwani si wengi wanaotazama bunge.
Nawaomba na waandishi wa habari walitangaze hili, kwani ni jambo la kheri kubwa sana, hakuna dua inayopokelewa haraka kama ya mwenye kudhulumiwa, pengine haya majanga yote yanayotupata Tanzania ni kwa hizo dhuluma zilizofanywa na viongozi wetu huko nyuma, ni wakati muafaka Serikali kukiri hilo na kuanza kufanya toba na kurudisha imani ya wananchi kwa Serikali yao.
Hansard zitakuwa zipo kwa wanaotaka kuelewa zaidi.
Ahsante Serikali kwa kuliweka wazi hilo.