Mzee Mwanakijiji
Platinum Member
- Mar 10, 2006
- 33,476
- 39,995
Na. M. M. Mwanakijiji
Mojawapo ya mambo ya kwanza kabisa tunayojifunza kama wazazi ni kubembeleza watoto. Mtoto anapozaliwa anakuwa ni mtegemezi mkubwa wa mzazi kwa kila kitu na pole pole anavyozidi kukua ndivyo anavyozidi kupunguza utegemezi huo. Lakini kama kuna kitu ambacho mzazi anaendelea kuwa nacho kwa mtoto ni nguvu yake ya kuweza kumuumiza mtoto kwa maneno au kumbembeleza. Ni nguvu kubwa sana kwa mzazi kuweza kumuita mtoto wake (hata kama ameshakua mtu mzima) na kumtuliza anapokuwa katika matatizo. Hili ni jukumu la kama mzazi na tunalipitisha jukumu hili kwa watoto wetu ili na wao wawe wazazi bora kwa watoto wao.
Hivyo, mzazi mara nyingi haumizwi sana na mtoto wake na anajifunza kumvumulia mtoto wake sana. Uvumilivu wa mzazi kwa mtoto wake nao ni mkubwa sana. Kama mzazi amemkuza mtoto toka anavyojimwagia kinyesi hadi makamasi basi mzazi anaweza kuvumilia mengi tena hata kwa mtoto mkubwa. Mtoto ambaye amekua na maisha yakamharibikia bado anaweza kupata uvumulivu kwa mzazi wake. Inapofika mahali mtoto anamuumiza mzazi hadi mzazi anaona ameshindwa kabisa kuvumilia jambo lile ndio hugeuka kile kinachoitwa "laana".
Ndugu zangu serikali na watumishi wa serikali si wazazi wa Watanzania. Uvumulivu au upendo wao kwa wananchi haulingani na wazazi na hawapaswi kututendea kama watoto wao au sisi kuwachukulia kama wazazi wa taifa. Wanasiasa na viongozi wa kuchaguliwa wote ni watumishi tu wa wananchi. Hawapaswi kuumizwa sana na maneno ya watu au matendo ya watu kiasi cha kukwazika sana.
Mojawapo ya mambo yananikera - na hili nimeshawahi kulisema mara kadhaa huko nyuma - ni kuwa viongozi wetu wasijione kama wao ni wazazi na hivyo wanataka watu wawabembeleze kwa maneno matamu. Sipendi kuona viongozi wako huru kusema lolote kwa yeyote lakini wao wakisemewa yale yale wanayoyasema wao wanajisikia kuumia. Hili la Spika na CAG ni mfano mdogo tu wa jinsi gani chombo kikubwa kama Bunge kinaumizwa na maneno! Hii ni fedheha! Yaani, kuna watu wameumia sana hadi kufanya kikao na kupitisha azimio kabisa kuwa wameumizwa! Huu ni udhaifu wa namna gani?
Wadudu kama nzi ni wasumbufu sana na wana madhara wakati mwingine; lakini hakuna mtu ambaye ana akili timamu ambaye anaamua kutumia gobole kuua nzi! Kuna mtu aliwahi kuishia kuchoma nyumba yake kwa sababu alitaka kujaribu kuua mende kwa kuwachoma na mshumaa! Kauli ya CAG hata kama angekuwa amemaanisha kabisa kuwa Bunge ni dhaifu (kwa utendaji na kwa namna ilivyo) bado haikuwa sababu ya msingi ya kumuita kujieleza wala kutumia muda wa Bunge kujadili! Huku ni kutumia nguvu kubwa kushughulikia jambo dogo; kujaribu kuonesha nguvu katika udhaifu!
Ni lazima tujifunze kuvumulia maoni hata kama yanaudhi sana. Viongozi au kiongozi ambaye hawezi kuvumulia maoni ni muhimu sana asitafute uongozi! Kutofautiana maoni au mawazo ni sehemu ya uhuru wa maoni na mawazo. Mwaka 2008 niliandika hapa kuwa haki ya maoni na uhuru wa mawazo vilivyomo katika Katiba haulindi maoni na mawazo mazuri! Haki hizi ziko kwenye Katiba kulinda maoni mabovu, ya kuudhi, ya kijinga na wakati mwingine ya kukera kweli kweli. Haya ndio maoni yanayolindwa kwa sababu maoni mazuri, ya kufurahisha na ya kutuliza mioyo hayahitaji kulindwa!
Nafahamu pia kuwa kuna watu kwa asili yao hawana uvumulivu; wanaumizwa sana moyoni wakipingwa, wanakwazika sana kuwajibiwa, na wanajisikia kutukanwa wakipingwa. Hili ni kweli hasa kama watu wana madaraka makubwa. Mwalimu akijibishiwa na mwanafunzi anajisikia amedharauliwa hata kama mwanafunzi yuko sahihi; polisi akikataliwa na raia kwenye jambo fulani anaona basi ngoja ampige kirungu! Ndio maana mojawapo ya misemo ya awali niliyoiasisi ni kuwa "hoja ijibiwe kwa hoja na si kwa vihoja". Mtu anapojibu hoja kwa vihoja anake ameshindwa hoja!
Hili la Spika na wabunge wenzake kutumia nguvu kubwa hata - naamini wakiwa timamu - kuamua ati kutoshirikiana na CAG ni ushahidi kabisa kuwa Bunge ni dhaifu, linajifedhehesha na limelewa ule ugimbi uleweshao wa madaraka! Wanaamini kabisa kwa kuwa wao ni wabunge na wako wengi basi wanaweza kufanya lolote, popote na kwa lolote kwa kusema kwa kauli moja tu "ndiyo".
Nani atawaambia ukweli huu bila kuonekana naye anawaumiza? Inawezekana basi kama taifa tuendelee kuwabeba kwenye mbeleko na kuwabembeleza wasiumie sana moyoni wakikosolewa, wasinung'unike wakikataliwa, na wasijisikie unyonge wakinyimwa! Tutakuwa na taifa la viongozi wa namna gani.
Sitaki hata kufikiria.