Serikali yaishukia Bongo Star Search
Wapewa onyo, wakikaidi kufutiwa kibal
na John Joseph
SERIKALI imesikitishwa na kulaani vikali udhalilishwaji unaofanywa na majaji wa programu ya kusaka vipaji vya wasanii, Bongo Star Search (BSS), kwani wamekuwa wakitumia lugha chafu isiyostahili kutumika mbele ya jamii iliyostaarabika.
Akizungumza na Tanzania Daima ofisini kwake jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Ghonche Materego, alisema wakiwa wasimamizi wakuu wa shughuli za sanaa, wanalaani vikali kilichofanywa na Bongo Star Search chini ya Kampuni ya Benchmark Production.
Materego alisema, kadiri siku zinavyosonga mbele, majaji wa programu hiyo ambao ni Rita Paulsen, Master Jay na P. Funk, wamekuwa wakivuka mipaka, kwa kuwadhalilisha washiriki, kitu ambacho ni kinyume cha maudhui ya programu hiyo, kwa mujibu wa maombi ya Benchmark Production.
Alisema, kwa muda mrefu majaji hao wamekuwa wakilalamikiwa, ingawa si kwa kiwango kikubwa kama ilivyo sasa, lakini wameshindwa kubadilika, hivyo wanatoa onyo kali dhidi ya majaji, programu na BSS kwa ujumla.
Tunashukuru Watanzania kuonyesha wanajali vitu vya kwao, hii si mara ya kwanza majaji wa BSS kulalamikiwa, kwani hata mwaka jana yalikuwepo, lakini safari hii hali imekuwa mbaya zaidi, alisema Materego huku akionyesha kukerwa na kitendo hicho, Materego alisema majaji wanapaswa kujua vijana (wasanii) ni binadamu kama wao (majaji) na kuwataka kuwa na moyo wa kibinadamu badala ya kuudhalilisha utu wa vijana hao.
Kama ni njia ya kunogesha kipindi, wahusika wanapaswa kutafuta nyingine, si kuwadhalilisha vijana wenye nia ya kutaka kujikwamua kimaisha kupitia tasnia ya sanaa ya uimbaji, kitu ambacho kinaungwa mkono na Serikali ya Awamu ya Nne chini ya Rais Jakaya Kikwete.
Rais Kikwete aliahidi kutoa ajira milioni moja, kwa jinsi BSS walivyoleta maombi yao, ilikuwa ni lazima mwisho wa siku vijana wanufaike na ajira. Sasa kama ajira zenyewe zinapatikana kwa manyanyaso kiasi hiki, sidhani kama ni sahihi, alisema Materego.
Aliongeza kuwa, anaamini majaji hao ni watu wenye taaluma, ni imani yake kwamba, watajisahihisha, yaani kuwapa heshima washiriki hao ambao ni Watanzania wenzao, badala ya kuwachukulia kama wadudu.
Naelewa majaji wanapata changamoto kubwa ya kukutana na vijana wengi katika muda mfupi, lakini hiyo isiwe sababu ya wao kuwatukana na kuwatolea lugha chafu washiriki, alisema na kuongeza:
Master J na P. Funk ni wafanyabiashara, kwani wanamiliki studio za kurekodia, siamini kama huko kwenye studio zao wanawafanya kama wanavyowafanya kwenye BSS, alisema Materego.
Alisema, itakachofanya BASATA ni kukutana na uongozi wa Benchmark Production haraka iwezekanavyo kujadili suala hilo na kama wahusika wataendelea na udhalilishaji, watasimamisha au kuifuta kabisa programu hiyo. Hii ni mara ya tatu kufanyika kwa shindano hilo ambalo hurushwa na kituo cha ITV. Mshindi wa mwaka 2007, alikuwa ni Jumanne Iddy kabla ya Misoji Nkwabi kushinda mwaka jana. Mei 17, Gazeti la Tanzania Daima Jumapili (gazeti dada na hili), lilikuwa na makala iliyozungumzia namna vijana wenye fikra na nia ya kujikwamua kimaisha kupitia sauti zao (achilia mbali kama wana vipaji au la), wanavyoishia kuvuliwa thamani ya utu wao na majaji wa BSS.