BOMU: Riwaya ya kipelelezi (1)

BOMU: Riwaya ya kipelelezi (1)

Six Man ukuje huku au Bomu limekulipukia mwenyewe? Alosto itatuua wahi kutuletea Dozi
 
RIWAYA; BOMU
Imeandikwa na Halfani Sudy
Simu 0652 212391

Sehemu ya Ishirini na Mbili

Gari ya kina Daniel Mwaseba ilikuwa Mbagala Zakheim. Bado ilikuwa ikiifuata gari ya kina Mark the Sniper ambayo ilikuwa Mbagala Rangi Tatu. Simu ya Adrian iliita.

"IGP John Rondo anapiga" Adrian alisema huku akiipokea simu.

"Adrian mbona kimya sana. Hujanambia misheni yenu ya huko Kigamboni iliendaje? Na kwasasa mpo wapi?" IGP John Rondo aliuliza.

"Mkuu samahani sana sikukwambia juu ya ile misheni yetu. Ile misheni hatukufanikiwa mkuu. Tulikuta nyumba ambayo tuliamini Dr Luis alikuwepo imelipuliwa na Bomu mita chache kabla hatujaifikia!" Adrian alisema.

"Nimeipata hiyo taarifa ya mlipuko wa bomu huko Kigamboni. Na vijana wetu wapo huko wakifanya uchunguzi. Kumbe hiyo nyumba iliyolipuliwa na bomu ndiyo mliyokuwa mkienda ninyi?" IGP John Rondo aliuliza.

"Ndio mkuu. Ingawa hatukufanikiwa kufika pale lakini tunaamini Dr Luis alikuwa pale muda mchache kabla hilo bomu halijalipuliwa" Adrian alisema.

"Basi inawezekana walifahamu kama mnaenda pale?" IGP John Rondo alisema hisia zake.

"Aaah umeongea kitu ambacho mimi na wenzangu tulikuwa hatujawaza bado. Inawezekana mkuu walifaham kama tunaenda kuvamia pale nao wakaamua kuilipua ile nyumba" Adrian alisema. Daniel naye alimgeukia Adrian.

"Ni nani mwengine mlimjulisha kuwa mnaenda kuivamia hiyo nyumba ukiacha mimi?" IGP John Rondo aliuliza.

"Zaidi ya wewe, hakuna mwengine tuliyemjulisha" Adrian alijibu.

Ukapita ukimya kidogo. Kabla ya IGP Rondo hajaongea tena.

"Hapo kuna kitu hakipo sawa Adrian. Haiwezekani nyumba aliyokuwepo Dr Luis ilipuliwe muda mchache wakati mkienda kuichunguza. Huoni kwamba inawezekana kuna mtu aliwapa taarifa hao watu ndio wakaamua kuilipua?"

"Mwanzoni hatufikiria hivyo. Lakini sasa nauona ukweli katika maneno yako. Tutafanya uchunguzi pia juu ya hisia zako mkuu" Adrian alisema.

"Unaweza ukamuhisi mtu yoyote kuhusika katika kuvujisha siri?" IGP John Rondo aliuliza.

"Kwasasa hapana, hakuna tunayemuhisi, maana nd'o kwanza umetufumbua macho. Lakini naomba tupe muda. Tutamfahamu tu huyo Nyang'au. Je wewe kuna mtu yeyote yule uliyemwambia baada ya kukuambia juu ya operesheni tuliyokuwa tunataka tuifanye?"

IGP John alifikiri kidogo, kisha akasema " Hapana sikumwambia mtu"

"Basi sawa mkuu. Tutakujulisha baada ya kuwapata hawa watu tunaowafatilia kwenye gari" Adrian alisema.

Na simu ikakatwa.

IGP John Rondo akiwa kituo kikuu cha Polisi, simu yake ilipokata tu, hakukaa hata dakika nne. Simu yake ilipata uhai tena.Ilikuwa ni simu kutoka kwa mheshimiwa rais Mgaya.

"Habari za sahivi IGP?" Rais Mgaya alisalimu.

"Nzuri mheshimiwa rais. Sijui zako?"

"Huku Magogoni ni salama kabisa. IGP vipi watu wako walifanikiwa kuwapata wale watekaji?" Rais Mgaya aliuliza.

"Mheshimiwa rais hawakufanikiwa. Kulitokea tatizo kidogo"

"Tatizo gani hilo?"

"Nyumba waliyohisi kwamba Dr Luis alikuwemo ililipuliwa kwa bomu dakika chache kabla hawajawasiri!"

Kilipita kimya kidogo.

"IGP John, hiyo ni habari mbaya sana. Matukio ya milipuko ya mabomu yameshamiri sana hapa jijini. Hii sio Tanzania tuliyoizoea. Umefika muda wa kujipima sasa kama unastahili kukalia kiti hiko" Rais Mgaya alisema kwa sauti ya mamlaka.

"Mheshimiwa rais usiwe na shaka na mimi. Tunaenda kuwakamata hawa watu muda mfupi ujao. Kikosi changu kwa sasa kinawafukuzia kwa siri watu hao ambao bila shaka wanahusika na utekaji wa Dr Luis. Nitakupa majibu baada ya muda mfupi mafanikio yao" IGP John alisema.

"Ok sawa. Nasubiri matokeo ya ufatiliaji wao" Rais Mgaya alisema na kukata simu.

Rais Mgaya alipokata simu hiyo, simu yake ilipata uhai tena. Rais Mgaya alikuwa anampigia simu mzee Msangi.

"Mzee Msangi mambo gani mnafanya? Kwanini mmekosa umakini kiasi hiki?" Rais Mgaya alisema kwa hasira.

"Kuna nini mheshimiwa rais?" Mzee Msangi naye alirusha swali.

"Gari yenu moja inafatiliwa sasahivi na kikosi cha B1. Bila shaka ni ile inayokwenda kitaluni. Na unajua kwamba kitalu C ndipo mahali tulipohamishia makazi yetu kwa sasa" Rais Mgaya alisema.

"Inafatiliwa? Ngoja niwasiliane na kina Mark wajitoe mbele ya macho ya hao jamaa" Mzee Msangi alisema harakaharaka.

Na rais alikata simu.

Dakika ileile Mzee Msangi aliwapigia simu wakina Mark Sniper na kuwaeleza kwamba walikuwa wanafatiliwa.

***

Katika nyumba ya kulala wageni ya Platnumz huko Vikindu, Imma Ogbo, Felisia Nyenyembe na Dr Luis walikuwa na kikao kizito. Bado walikuwa wanapanga juu ya mpango wao wa siri wa kuulipua ubalozi wa Uganda nchini Tanzania ili kuharibu 'tension' ya polisi juu msako wao wa kumtafuta Dr Luis.

"Sasa nimeongea na rais Abayo. Ameubariki mpango wetu wa kuulipua ubalozi wa Uganda. Amesema hiyo ndiyo njia pekee rahisi inayoweza kumtoa Dr Luis nje ya nchi hii. Rais amesema tuulipue ubalozi wa Uganda haraka iwezekenavyo" Imma Ogbo alisema.

"Safi sana. Nafurahi sana kusikia kwamba rais kaubariki mpango huu. Hii imeonesha kiasi gani ananijari. Ila unajua huu ni mpango mgumu sana. Kuulipua ubalozi wa nchi nyingine si jambo la kitoto hata kidogo. Pamoja na ugumu wake lakini inabidi ufanywe kwa siri sana. Maana siri ikifichuka kama ni sisi ndio tuliolipua ubalozi huo kwa maagizo ya rais Abayo inaweza kuleta ugomvi ama vita hata nchi kwa nchi. Sijui tumejipanga vipi ili kuhakikisha siri hii inabaki kuwa siri milele na milele?." Dr Luis aliuliza.

"Kuhusu ugumu wa mpango huu msamiati huo ondoa Dr Luis. Rais Abayo ameahidi kuwaleta majasusi watano kutoka taasisi yetu ya ujasusi nchini Nigeria. Majasusi hao watatusaidia kutekekeza mpango huu. Maana nilimgusia rais Abayo juu ya kumuhitaji Mark the Sniper katika mpango huu wa kuulipua ubalozi wa Uganda. Alichosema rais ni kwamba tumwache Mark akae upande uleule ili aweze kuchota siri zao na mipango yao, na hivyo badala yake kaahidi kuleta majasusi hao watano kesho asubuhi.

Kuhusu suala la siri hilo usiwe na shaka nalo hata kidogo. Mpango huu utakuwa siri hadi kiama. Naamini si sisi wala hao majasusi hakuna atakayeweza kuutoa nje mpango huu" Imma Ogbo alisema kwa kirefu.

"Ni lini sasa tunaenda kuulipua ubalozi wa Uganda?" Felisia aliuliza.

"Hao majasusi watano wataingia kesho saa mbili asubuhi pale uwanja wa ndege wa Mwalimu Nyerere. Na kesho hiyohiyo usiku tunaenda kutekeleza shambulio letu, na usiku huohuo wakati Polisi wakihahaha kusaka wahusika wa shambulio hilo sisi tutaanza safari ya kutoroka hapa nchini" Imma Ogbo alisema.

"Tunaondoka kwa njia ipi sasa?" Dr Luis aliuliza.

"Rais Abayo amesema hao majasusi watakuja na ndege binafsi. Ambayo ndiyo tutakayoitumia kuondoka nayo" Imma Ogbo alisema.

"Good plan mtu mbaya Imma Ogbo. Hakika safari hii tutawaacha midomo wazi wapelelezi wa nchi hii wanaojiweka matawi ya juu katika mambo ya kipelelezi" Dr Luis alisema kwa furaha.

"Kwa hakika watajuta!" Felisia alisema kwa nguvu huku akimalizia kutuma ujumbe wake kwa mtu fulani kwa siri.

Kati yao, hakuna aliyejua kwamba alikuwa anawarekodi kwa siri...

Je mpango wa kulipua balozi ya Uganda utakamilika? Vipi kuhusu msako wakina Daniel na Mark the Sniper? Na je Felisia anatuma ujumbe kwa nani?

Tukutane hapahapa kesho kuisoma Bomu.

Pamoja na kusuasua ngoma tutaisoma hadi mwisho hii.
Tuvumiliane.
 
RIWAYA; BOMU
MWANDISHI; HALFANI SUDY
SIMU 0652212391

Sehemu ya Ishirini na Tatu

Wakati huohuo teksi iliyompakia Martin Hisia ilikuwa maeneo ya Buguruni. Pamoja na dereva teksi kujaribu kukimbiza kwa kasi kila apatapo nafasi, lakini foleni ya haja ilizizima mbio zake mara kwa mara.

Pindi walipokuwa katika foleni hapo Buguruni ndipo simu ya Martin Hisia ilipoingia meseji. Martin aliitoa simu yake mfukoni ili kuiangalia hiyo meseji. Ulikuwa ni ujumbe uliongia kwa njia ya mtandao wa Whatsapp. Martin alifungua whatsapp yake. Akaona ni ujumbe uliongia kutoka kwa mpenzi wake, Felisia. Lakini uliingia kwa mtindo wa 'voice note'. Martin alitoa 'earphone' kutoka katika mfuko wake mwengine wa suruali. Akazichomeka katika simu yake.

Akaanza kusikiliza.

Wakati huohuo kule katika nyumba ya kulala wageni ya Platnumz. Felisia aliomba kwenda kujisaidia chooni nakutoka mle chumbani ambapo walikuwepo wakina Imma Ogbo. Alinyanyuka bila kuomba ruhusa. Alitoka nje ya mlango wa chumba walichofikia. Akakata kushoto akiifuata korido ndefu ambapo ndipo kulikuwa na choo. Mara kwa mara alikuwa anageuka nyuma ili kuona kama kuna hatari yoyote ile ilikuwa inamfuata. Hakuiona hatari, wala harufu ya hatari. Aliingia moja kwa moja bafuni. Akafungulia bomba la maji, akiruhusu maji kutoa sauti wakati yakiingia katika ndoo ya chuma. Sekunde ileile alitoa simu yake mfukoni na kumpigia Martin Hisia. Alisikiliza kidogo, kwa bahati mbaya alikuta simu ya Martin Hisia ilikuwa inatumika. Martin Hisia alikuwa anaongea na simu nyingine.

Hofu dhahiri ilishamiri katika moyo wa Felisia. Aliujua uhatari uliopo kwa kitendo alichokuwa anakifanya. Alifahamu vizuri sana adhabu atakayopewa na Imma Ogbo pindi atakapogundua kwamba alikuwa anamsaliti. Lakini hakuwa na namna, kuungana na Imma Ogbo safari hii ilikuwa ni kuisaliti nchi yake Tanzania. Na yeye hakuwa tayari kwa hilo.

Akiwa anatetemeka kwa woga Felisia alipiga tena simu ya Martin Hisia. Lakini bado majibu yalikuwa yaleyale. Simu aliyokuwa anaipigia ilikuwa inatumika.

Hii ilimpa mawazo mengi sana Felisia. Maana hakujua kwamba Martin aliusikiliza ujumbe wake aliomtumia ama lah. Alitamani Martin apokee simu yake hata sekunde moja na kumjulisha kwamba aliusoma ujumbe wake.
Angejisikia amani..

Alipiga tena simu kwa mara ya tatu.

"Come on Martin pokea simu" Felisia alisema kwa sauti ndogo. Lakini majibu ya simu yalikuwa yaleyale, bado ilikuwa inatumika.

"Hapa sina jinsi. Yanipasa nitoke tu nje. Maana jamaa wasije wakanitilia shaka kwakuwa nimechelewa sana kutoka chooni" Felisia aliwaza. Akafunga lile bomba la maji na kuelekea mlangoni. Alipofika mlangoni na kufungua tu ule mlango, alikutana na jambo la kushtusha sana!!

Felisia alikuwa anatazamana na mdomo wa bastola nyeusi iliyoshikwa imara na mkono wa nguvu wa Immanuel Igbo!!

Kimbembe....

Wakati Felisia akitazamana na mdomo wa bastola, mpenzi wake, Martin Hisia alikuwa anaongea kwenye simu na Daniel Mwaseba. Alikuwa ameshamtumia ule ujumbe uliotoka kwa Felisia. Na Daniel aliituma ule ujjumbe pamoja na namba ya Felisia kwa Mwanasheria mlevi. Ndipo walipoweza kufanikiwa kupafahamu mahali alipo mtumaji wa ujumbe ule. Sasa safari yao ilibadilika, kwa kasi walikuwa wanaelekea Vikindu mahali ambapo waligundua kwamba ndipo alipokuwa Dr Luis.

"Kazi imekuwa rahisi sana. Sikutegemea kwamba tutampata Dr Luis kirahisi namna hii" Adrian alisema.

"Adrian, usiseme kazi ni rahisi. Hatujui Dr Luis yupo katika mazingira gani? Na hatujui tunaenda kupambana na watu wa aina gani? Hapa lazima tujipange kamili ili kuhakikisha tunampata Dr Luis" David alisema.

"Lakini jamani kuna mambo ya kushangaza kidogo juu ya hizi sauti alizotutumia Martin Hisia. Inaonesha kwamba Dr Luis hajatekwa, yupo na watu anaowafahamu kabisa huku naye akishiriki katika mpango wao wa kuulipua ubalozi wa Uganda. Hii ipo vipi?" Daniel aliuliza.

"Hata mimi nimekuwa nikijiuliza swali hilo kichwani mwangu. Lakini hatuna haja ya kuumiza kichwa. Dakika chache zijazo Tunaenda kukutana na hawa watu, na tutajua tu mbivu na mbichi" Adrian alisema.

"Hili swala limekuwa kubwa sana. Uhusika wa rais Abayo katika sakata hili ndo limezidi kulifanya kuwa kubwa. Lakini niahidi tu tutazifukia hila zote za watu hawa na kuziweka hadharani. Tutampata Dr Luis na kumfikisha kwa mheshimiwa rais, na lazima tuziseme hila zake. Pia lazima tuhakikishe ubalozi wa Uganda haulipuliwi abadaan, sambamba na kuwatia mikononi hao majasusi watano wanaokuja kutoka nchini Nigeria.

Pamoja na hayo lazima tuhakikishe tunamkomboa Hannan na familia ya David. Hizo ndio kazi zetu kuu, na nina hakika tutazikamilisha" Daniel alisema kipindi hiko gari yao ilikuwa Kongowe.

Walikuwa wameshapoteana na gari ya kina Mark ambao nao walihisi wanawakimbia wakina Daniel. Kumbe haikuwa hivyo, wakina Daniel walikuwa wamepata misheni ndani ya misheni.

Kwa mwendo wa gari la kina Daniel, Dakika saba tu ziliwafikisha Madafu kutokea Kongowe. Walipofika Madafu walimpigia simu Mwanasheria mlevi ili awape mwelekeo sahihi waliopo wakina Dr Luis.

"Mwanasheria, tupe mwelekeo, tupo Madafu hapa" Daniel alisema.

"Sasa Daniel ninavyoona hapa katika mtandao, hapo Madafu upande wenu wa kulia kuna kituo cha mafuta. Mita chache kutoka kituo cha mafuta upande huohuo wa kulia kuna nyumba ya kulala wageni. Hapo ndipo hiyo simu ilituma ile meseji" Mwanasheria alisema.

"Sawa Mwanasheria nd'o tupo katika kituo cha mafuta hapa, tunaelekea hilo eneo. Vipi hiyo namba iliwasiliana tena na mtu mwengine?" Daniel aliuliza.

"Hapana Daniel. Nimekuwa nikiichunguza namba hii muda wote. Ilijaribu kuwasiliana na namba moja ambayo nayo ilikuwa inaongea wakati akiipigia. Nilijaribu kuichunguza namba hiyo ikiyopigiwa nikagundua imesajiliwa kwa jina la Martin Hisia. Nikachunguza tena huyo Martin Hisia alikuwa anaongea na nani kwa muda huo? Nikagundua anawasiliana na simu iliyosajiliwa kwa majina ya Adrian Kaanan, hivyo nikagundua alikuwa anawasiliana nanyi" Mwanasheria mlevi alisema.

"Pengine huyo mtu alikuwa anataka kumpa taarifa nyingine Martin" Daniel alisema.

"Inawezekana. Maana alijaribu kupiga simu zaidi ya mara mbili"

"Sawa Mwanasheria. Sisi tunaingia kazini. Nitakupigia baada ya kutoka hapa. Tuna kazi kubwa sana kesho asubuhi kama ulivyosikia katika hizo records. Nitakuhitaji ili kuikamilisha hiyo kazi" Daniel alisema.

"Nipo tayari saa yoyote, sehemu yoyote. Mimi ni Mwanasheria..."

"Mwanasheria mlevi" Daniel alimalizia.

Na simu ikakatwa.

Daniel alimwangalia Adrian, kisha akamwangalia David.

"Wanaume, sasa tunaenda kuvamia hii nyumba ya kulala wageni ambayo tuna uhakika yupo mtu anayeitwa Imma Ogbo. Pengine hamumjui vizuri Imma Ogbo. Mimi nimemjua Imma Ogbo kupitia Mwanasheria pindi nilipomtumia zile record alizoturushia Martin Hisia. Katika record zile kuna sauti tatu, ya Dr Luis, mwanamke ambaye ndiye amevujisha siri hii na mwengine ni sauti ya Imma Ogbo. Sisi shabaha yetu ni Dr Luis, lakini tujue kwamba Dr Luis yupo sambamba na kiumbe hatari kinachoitwa Imma Ogbo.

Imma Ogbo ni nani?

Imma Ogbo ni jasusi namba mbili kutoka nchini Nigeria. Licha ya ujasusi Imma ni mlinzi namba mbili wa rais wa Nigeria, rais Abayo. Kupambana na jasusi namba mbili wa nchi kama Nigeria, nchi yenye maelfu ya majasusi na yeye kupewa namba mbili si jambo la kitoto. Kwa Afrika Imma Ogbo anashika namba sita. Mmeona uhatari wa huyu jamaa? Lazima tuwe makini sana ndugu zangu. Ukimwona Imma Ogbo cha kwanza mpige risasi ya kichwa kisha ndo umuhoji!! Nataka leo ndio uwe mwisho wa hila za hawa manyang'au!!!." Daniel alisema huku akiwaangalia wenzie kwa zamu.

Wote waliitikia. Sura zao zikionesha walikuwa na hamu kubwa ya kuingia katika mapambano haya magumu na ya hatari.

"Haya sasa...Twendeni tukaivamie hiyo nyumba ya kulala wageni. Iwe iweje..lazima tuhakikishe tunawatia mkononi Dr Luis na Imma Ogbo!!" Daniel alisema.

Wote watatu, walishuka kwenye gari, wakiwa tayaritayari, na kwa kutumia miguu yao walielekea katika nyumba ya kulala wageni ya Platnumz kuwatia mbaroni watu ambao waliwapachika jina la Manyang'au...

Je wataweza kuwatia mikononi wakina Imma Ogbo? Hili ni swali..wewe nipe jibu
 
Hongera mkuu sixman
Endelea kidogo kufidia maGap ya huko nyuma
 
RIWAYA; BOMU
IMEANDIKWA NA HALFANI SUDY
SIMU 0652 212391

Sehemu ya Ishirini na Nne

Daniel Mwaseba alipita upande wa nyuma kuelekea nyumba hiyo ya kulala wageni. Alikuwa ana bastola mbili kiunoni mwake zikizosubiri kutumika. Upande wa kulia na upande wa kushoto.

Bastola ya tatu ilikuwa katika mkono wa kulia ikiwa tayari imeondolewa usalama.

Tayari kuilipua hatari yoyote.

Mgongoni kwake, kulikuwa na begi dogo jeusi lenye zana kadhaa za kazi. Begi ambalo lilikuwa halikosekani mgongoni mwake akiwa katika misheni.

Daniel alikuwa ananyatia kimyakimya na kwa umakini mkubwa huku akijificha mara kwa mara katika mashina ya miti miarobaini iliyopandwa bila mpangilio maalum. Au pengine ilijiotea yenyewe.

Masikioni mwake, kulikuwa na kifaa kidogo cheusi. Hiki kilikuwa ni kifaa cha mawasiliano ambacho kilimwezesha kuwasiliana na wenzake. Sekunde na dakika yoyote.

Upande wa mbele wa nyumba ile ya kulala wageni alikuwepo Adrian Kaanan. Askari polisi imara ambaye alionesha umahiri mkubwa katika misheni mbalimbali.

Misheni yake ya kwanza aliifanyia huko maeneo ya Mkuranga. Misheni ambayo aliifanya kwa ufanisi mkubwa sana na kufumbua fumbo gumu, misheni hiyo ilipachikwa jina la Briefcase.

Adrian Kaanan akishirikiana na Martin Hisia pia walifanya kazi kubwa katika misheni ya kumsaka mwanamke muuaji mwenye kasi na shabaha ya ajabu. Kwa majina aliitwa Red Butterfly. Kutokana na kufanikisha misheni kadhaa hakuna mwenye kuhoji juu ya uwezo wa askari huyu kijana. Ambaye watu wengi wakimtazamia kuwa mrithi wa Daniel Mwaseba.

Sasa, alikuwa mbele ya nyumba ya kulala wageni ya Platnumz akiwa na bastola nyeusi katika mkono wake wa kuume. Dhamira yake kuu ilikuwa ni kummaliza kwa mkono wake mtoto wa kinigeria, wa kuitwa Imma Ogbo.

Pembeni ya nyumba hiyo alikuwepo David. Mwanajeshi imara ambaye ameshinda vita kadhaa huko msituni.

David alikuwa ni mtu katili na asiyekuwa na msamaha kwa wavunja amani. Alifanya kazi kadhaa chini ya mwamvuli wa umoja wa Afrika huko katika misitu ya Kongo na kuhakikisha waasi hawafurukuti. Kabla ya kwenda Sudan kwa mwamvuli wa umoja wa mataifa kwenda kupambana na kikundi cha kigaidi cha Al shabab. Mote alifanya kazi yake kwa usahihi na kutunukiwa tuzo mbalimbali. David hakuwa na mashara na wavunja amani. Lakini leo, David alikuwa katika misheni yake ya kwanza mjini. Misheni ambayo alianza kwa kufanya kosa, na sasa alikuwa anataka kusahihisha kosa.

Ataweza?

Sasa, alikuwa na bunduki aina ya SMG mkononi mwake. Kichwani alikuwa na wazo moja tu, la kuua tu...akiamini kwamba watu wanaowawinda hapo ndio wameiteka familia.

Misheni hii ya hatari ilikuwa inaongozwa na mpelelezi namba moja nchini Tanzania, kwa majina Daniel Mwaseba. Ndiye ambaye alikuwa anawaongoza wenzake kwa kupitia vile vifaa vyeusi walivyoweka masikioni mwao.

"Taratibu na kwa umakini mkubwa tusonge mbele. Kuweni makini kuhakikisha hawatutoroki hawa jamaa. Ama zao, ama zetu..." Daniel alisema kwa sauti ambayo ilisikiwa na kila mmoja.

"Tumekupata, tumekupata" David na Adrian waliitikia kwa pamoja.

Kule mbele Adrian aliingia ndani kwa kupitia mlango wa mbele. Alikutana na ukumbi mkubwa wa vinywaji uliokuwa unatazamana na mapokezi ya nyumba hiyo ya kulala wageni. Alipoingia tu, watu wote waliokuwa wanapata vinywaji mbalimbali huku wakiangalia mpira walimwangalia yeye. Nyuso za uwoga zikiwatamalaki.

Adrian hakujali.

Bastola yake bado ilikuwa mbele huku macho yake yakifanya kazi isivyo kawaida.

Kwa harakaharaka aliwaangalia wale watu waliokuwa wanakunywa vinywaji mle ndani. Walikuwa watu kama kumi na tano. Lakini hakumwona Imma Ogbo, hakumwona Dr Luis.

Moja kwa moja alielekea mapokezi. Ambapo kulikuwa na dada mmoja akihangaika kupanga vinywaji katika friji. Yule dada alipogeuka nyuma, alikutana na macho ya Adrian. Mtetemo ulionekana kwa yule mwanamke.

Kutazamana na mdomo wa bastola si kazi ndogo!

"Samahani kwa kuingia namna hii. Maneno mengi tutaongea baadae, kwasasa nielekeze chumba alichopanga Imma Ogbo" Adrian alisema.

Yule mhudumu alikaa kimya. Macho yake yakionesha kuwa hakumwelewa hata kidogo.

"We msichana sina siku nzima hapa!" Adrian aling'aka.

"Sijakuelewa kaka yangu..huyo Imma nani sijui mi simfaham. Na hatuna mteja mwenye jina hilo hapa" Yule mhudumu aliipata sauti yake.

Adrian akajipekua katika mfuko wa nyuma wa suruali yake. Akatoa picha na kumrushia yule msichana. Huku akisindikizwa na maneno...

"Namtaka huyo!!"

Yule mwanamke aliidaka ile picha na kuiangalia. Mstuko dhahiri ulionekana katika macho yake. Alikuwa anatazamana na mtu anayemjua.

"Yu..po ch..umba cha Li..on" Mtetemo dhahiri uliambatana na sauti yake.

"Nipeleke" Adrian alisema.

Yule mhudumu alitoka mle kaunta. Na kuongozana na Adrian kuelekea katika chumba cha Lion, kwenda kuwakamata wakina Imma Ogbo.

Upande wa Daniel Mwaseba alikuwa amekaribia kuingia nyumba ya kulala wageni ya Platnumz kwa kupitia mlango wa nyuma. Alikuwa na maelezo yote kuhusu chumba walipo wakina Dr Luis na Imma Ogbo. Kwa kupitia vile vifaa walivyoweka masikioni, wakati Adrian akimuhoji yule Mhudumu.

Chumba cha Lion...

Daniel aliingia ndani, akiongozwa na bastola yake ambayo ilikuwa tayari kwa lolote. Alipita uwani ambapo kulikuwa kumepandwa migomba kadhaa. Alitembea kidogo na kuingia sehemu ambapo kulikuwa na vyumba vya uwani vya 'guest' hiyo.

Akaanza kuhesabu vyumba..

Hali ilikuwa tulivu. Hakukuwa na pilikapilika katika vyumba hivyo vya uwani.

"Tiger" Alisoma moyoni.

"Elephant" Akasoma chumba kingine.

"Rabbit" Akasoma tena mlango mwingine.

"Rhino.." Akasoma tena.

Akapiga jicho mlango wa tano. Hapo ndipo alipokiona..

"LION!!" Alisoma kwa nguvu moyoni huku damu yake ikisisimka.

"Humu ndimo walimo wakina Imma Ogbo" Daniel alisema kimoyomoyo huku akiusogelea ule mlango. Mlango uliokolezwa kwa wino mwekundu. Maandishi yakisomeka..

LION.

Je nini kitatokea..
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom