Bilioni 230 zimetolewa kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa shule za msingi kupitia mradi wa kuimarisha ujifunzaji katika elimu ya awali na msingi

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Apr 18, 2017
2,813
11,991
BILIONI 230 ZIMETOLEWA KWA AJILI YA UJENZI NA UKARABATI WA SHULE ZA MSINGI KUPITIA MRADI WA KUIMARISHA UJIFUNZAJI KATIKA ELIMU YA AWALI NA MSINGI (BOOST)

Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa imepeleka kiasi cha shilingi 230,008,500,000 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya shule za msingi kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa mapema mwezi Aprili, 2023.

Kupitia fedha hizo kazi zitakazofanyika ni ujenzi wa shule mpya za msingi 302 ambazo zitakuwa na jumla ya madarasa ya awali 604, madarasa ya msingi 3,276, majengo ya utawala 302 pamoja na matundu ya vyoo 6,160.

Fedha hizi pia zitajenga madarasa kwenye baadhi ya shule za msingi zenye msongamano mkubwa wa wanafunzi unaosababishwa na upungufu wa madarasa ambapo jumla ya madarasa 2,929 yatajengwa katika shule mbalimbali. Lengo ni kupunguza msongamano na kuweka mazingira rafiki ya kujifunza na kufundishia.

Pamoja na shule mpya zitakazojengwa na ujenzi wa madarasa kwenye shule zenye msongamano, fedha hizi za awamu ya kwanza zitakarabatiwa shule za msingi zenye uchakavu 8, zitajenga madarasa ya awali 368, madarasa ya watoto wenye mahitaji maalumu 41 na mabweni 2, nyumba za walimu 41 pamoja na matundu ya vyoo 2,899.

Kwa ujumla ujenzi wa miundombinu mbalimbali ya elimu ya awali na msingi itakayojengwa kwenye awamu hii ya kwanza itahusisha shule za msingi 1,338.

Ikumbukwe kuwa fedha zilizopokelewa ni za mwaka wa kwanza tu wa utekelezaji wa mradi wa BOOST unaotekelezwa kwa kipindi cha miaka mitano kwa gharama ya shilingi trilioni 1.15 na unalenga kuimarisha ujifunzaji katika elimu ya awali na msingi.

Kufuatia upelekaji wa fedha hizo Mhe. Angela Kairuki, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI ametoa maelekezo kwa viongozi wote wa Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha kuwa:

I. Vigezo, masharti na miongozo ya matumizi ya fedha za mradi inazingatiwa ipasavyo ili kuwa na miradi yenye tija na iliyokidhi vigezo na matumizi sahihi ya fedha kwa kuwa mradi huu ni muendelezo wa Programu ya Lipa kulingana na Matokeo.

II. Taarifa za mapokezi ya fedha za ujenzi wa miundombinu hii zinafikishwa kwenye jamii inayonufaika na mradi.

III. Ushirikishwaji wa wadau wote kuanzia ngazi ya Mkoa mpaka kwenye Kijiji/mtaa unaimarishwa.

IV. Wananchi wote na jamii inayozunguka eneo la mradi wanashiriki kikamilifu katika utekelezaji wa mradi na ulinzi wa mali na vifaa vyote vya ujenzi.

V. Ujenzi wa miundombinu hii inakamilika ndani ya siku 90 tangu tarehe ya mapokezi ya fedha.

Imetolewa na:

Nteghenjwa Hosseah
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Ofisi ya Rais –TAMISEMI
30.04.2023
 
Back
Top Bottom